• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Wanasalamu Kanda ya Kusini wamsaidia mwenye ulemavu

 

Mwakilishi wa Wanasalamu Kanda ya Kusini akikabidhi godoro na daftari kwa Mzee Somba ikiwa ni mchango wa umoja huo (Picha na Musa Mtepa)

Wanasalamu Kanda ya Kusini kwa kushirikiana na Jamii FM wametoa msaada wa godoro na vifaa vya shule kwa Mzee Salumu Somba, mlemavu wa macho na mkazi wa Mnyengedi, baada ya kuguswa na hali yake kupitia kipindi cha Sikika. Wametoa wito kwa jamii kushirikiana kusaidia wenye uhitaji.

Na Musa Mtepa

Umoja wa Wanasalamu Kanda ya Kusini kwa kushirikiana na wadau wa Jamii FM Radio, leo Oktoba 15, 2025, wametoa msaada wa godoro na vifaa vya shule kwa familia ya Mzee Salumu Somba, mkazi wa Kijiji cha Mnyengedi,Mzee Somba ni mlemavu wa macho na anaishi katika mazingira ya kipato duni.

Akizungumza kwa niaba ya umoja huo wakati wa kukabidhi msaada, Bi Mwanahawa Nayopa (Mrs. Machela) amesema kuwa walipata taarifa za hali ngumu ya maisha ya Mzee Somba kupitia kipengele cha Sikika, kinachorushwa hewani na Jamii FM Radio kupitia kipindi cha Dira ya Asubuhi.

Kupitia taarifa hiyo, waliguswa na hali ya familia hiyo, hasa watoto wa Mzee Somba wanaosoma katika Shule ya Msingi Mwenge, na wakaamua kuchangishana fedha kwa ajili ya kununua godoro pamoja na vifaa vya shule.

Sauti ya Mwanahawa Nayopa – Mwakilishi wa Wanasalamu Kanda ya Kusini

Aidha, Bi Nayopa ameishukuru Jamii FM Radio kwa mchango wake mkubwa wa kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hususan watu wenye uhitaji maalum. Ametoa wito kwa jamii nzima kuendeleza moyo wa kusaidiana kwani kusaidia wenye uhitaji si jukumu la mtu mmoja bali ni la jamii nzima.

Sauti ya Mwanahawa Nayopa – Mwakilishi wa Wanasalamu Kanda ya Kusini

Kwa upande wake, Mzee Salumu Somba amewashukuru Wanasalamu kwa msaada waliompatia, huku akiwaombea baraka tele kutoka kwa Mungu huku akisema kuwa msaada huo umempa faraja kubwa na kuwaomba waendelee kuwa na moyo huo wa huruma kwa wengine wenye mahitaji kama yake au hata zaidi.

Sauti ya Mzee Salumu Somba – Mlemavu wa Macho

Naye Ebby Hamisi, Mtendaji wa Kijiji cha Mnyengedi, ametoa shukrani zake kwa Umoja wa Wanasalamu kanda ya kusini kwa kuguswa na hali ya Mzee Somba na kutoa rai kwao kwa kutokata tamaa kutokana na maneno ya kubezwa au kudhihakiwa, bali waendelee kufanya mema kwa jamii.

Sauti ya Ebby Hamisi – Mtendaji wa Kijiji cha Mnyengedi

Share:

Kijiji chaingiwa hofu ya ushirikina mkoani Mtwara

 

Kitu kinachodahniwa kuwa ni cha kishirikina kikiwa kimezungushiwa hirizi(Picha na Musa Mtepa)

Taharuki yatanda Magomeni Nyasi baada ya kugunduliwa kifaa kisichojulikana chenye hirizi, kinachodhaniwa kuhusika na imani za kishirikina. Wakazi wataka uchunguzi wa kina kufuatia ongezeko la matukio ya aina hiyo kijijini

Na Musa Mtepa

Mtwara –Wakazi wa kijiji cha Magomeni Nyasi, kilichopo kata ya Tangazo, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Oktoba 12,2025 wameamka na taharuki kubwa  baada ya kukutwa kwa kifaa kisichojulikana kilichozungushiwa hirizi, tukio linalodhaniwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Wakizungumza na Jamii FM, baadhi ya wananchi wameelezea mshangao wao juu ya tukio hilo, wakikitaja kuwa cha kutisha na kisicho cha kawaida.

Sauti ya wananchi wa kijiji cha Magomeni Nyasi

Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Alfani amedai kuwa tukio hilo lina uhusiano na ujio wa waganga wa kienyeji waliotembelea kijiji hicho siku za nyuma kwa lengo la kutoa uchawi.

Sauti ya Alfani, kijana mkazi wa Magomeni Nyasi

Mzee Abdala Yusuf Nammandila, ambaye ndiye mmiliki wa nyumba iliyokutwa na kifaa hicho chenye hirizi, amesimulia jinsi alivyokigundua na hatua alizochukua mara baada ya kukikuta.

Sauti ya Mzee Nammandila

Tukio hili limezua hofu miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho, wengi wao wakitoa wito kwa mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio ya kishirikina ambayo yanaonekana kuongezeka kwa kasi maeneo ya vijijini.

Share:

Malezi duni yatajwa sababu ya mimba mashuleni Mtwara

 

Baadhi ya wananchi wa kata ya Naliendele wakishiriki mdahalo huo(Picha na Mohamed Masanga)

Mdahalo ulioandaliwa na Jamii FM umebainisha kuwa mimba mashuleni husababishwa na malezi duni, kutokuwepo kwa uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi, pamoja na ushiriki wa jamii hafifu katika kulinda watoto wa kike

Na Musa Mtepa

Inaelezwa kuwa ukosefu wa malezi na maandalizi bora kwa watoto kutoka kwa wazazi umeendelea kuwa moja ya sababu kuu zinazochangia wanafunzi wa kike kupata mimba wakiwa bado shuleni.

Hayo yamebainika katika mdahalo ulioandaliwa na Jamii FM Radio Oktoba 8, 2025, uliokuwa na kaulimbiu “Jamii Inashiriki Vipi Katika Kutokomeza Mimba Shuleni.

Maafisa usafirishaji (bodaboda) kutoka stendi ya Bajaji, kata ya Naliendele, wameeleza kuwa mimba nyingi zinazopatikana shuleni huchangiwa na wazazi kulega katika malezi, ikiwemo kuruhusu watoto kushiriki matukio ya usiku kama vile vigodoro, ambayo huwapeleka katika mazingira hatarishi.

Sauti ya maafisa usafirishaji – kata ya Naliendele

Hata hivyo, baadhi ya wazazi wamepinga kauli hiyo wakisema si wazazi wote huruhusu watoto wao kwenda kwenye vigodoro. Shaibu Abdala Kupela na Brandina Chilumba, ambao ni wazazi, wamesema kuwa kuna sababu nyingine nyingi zinazochangia mimba shuleni, ikiwemo wazazi kutengana bila sababu za msingi, hali inayosababisha watoto kukosa uangalizi wa kutosha.

Sauti za wazazi wakichangia mjadala

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pachoto “A”, Bw. Sadi Abdala Kombo, amesema kuwa ili kuondokana na tatizo la mimba mashuleni, ni lazima wazazi wasimame imara katika kulea watoto wao na kutambua wajibu wao kama walezi.

Sauti ya Sadi Kombo – 1 Mwenyekiti wa Mtaa wa Pachoto A

Aidha, Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa viongozi wa mitaa wana wajibu wa kukutana na wazazi mara kwa mara kwa ajili ya kujadiliana namna ya kuwasaidia watoto kuishi salama na kujitambua wakiwa shuleni.

Sauti ya Sadi Kombo – 2 Mwenyekiti wa Mtaa wa Pachoto A

Kwa upande mwingine, Judith Chitanda kutoka shirika la Nerio Paralegal pamoja na Sajenti Esta kutoka dawati la jinsia, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, wameitaka jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale mtoto anapopata ujauzito ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika na kusaidia kutokomeza mimba mashuleni.

Sauti ya Judith Chitanda na Sajent Esta – Dawati la Jinsia, Jeshi la Polisi
Share:

CUF yasisitiza umuhimu wa kupiga kura,Octoba 29,2025

 

Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo akizungumza na waanishi wa habari mkoani Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Mgombea urais wa CUF, Gombo Samandito Gombo, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akiahidi huduma bora za jamii na maendeleo ya kweli endapo chama chake kitaunda serikali

Na Musa Mtepa

Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kwa kuchagua viongozi wanaowataka ili kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa.

Akizungumza na Waandishi wa habari Oktoba 8, 2025, mjini Mtwara, Gombo amesema kuwa fikra za baadhi ya wananchi kutoshiriki kupiga kura haziwezi kuwasaidia Watanzania kwa namna yoyote ile na kusisitiza kuwa ni muhimu kila mmoja kutumia haki na nguvu yake ya kikatiba kwa kumpigia kura mgombea wa CUF.

Sauti ya 1 Gombo Samandito Gombo Mgombea Urais CUF

Aidha, Gombo ameongeza kuwa chama hicho hakikatishwi tamaa na idadi ya watu wanaojitokeza kwenye mikutano ya kampeni, kwani CUF inaamini kuwa uungwaji mkono kutoka kwa wananchi ni mkubwa na unaendelea kuimarika kila siku.

Sauti ya 2 Gombo Samandito Gombo Mgombea Urais CUF

Akizungumzia sera za chama chake, Gombo amesema kuwa endapo CUF itashinda uchaguzi na kuunda serikali, itahakikisha wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla wanapata huduma bora za kijamii, ikiwemo matibabu bure na miundombinu ya kisasa.

Sauti ya 3 Gombo Samandito Gombo Mgombea Urais CUF

Chama cha Wananchi (CUF) ni miongoni mwa vyama vinavyowania nafasi ya kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo wagombea mbalimbali wameendelea na kampeni zao katika maeneo mbalimbali nchini.

Share:

Mkaa wenye moto waunguza nyumba Mangamba chini

 

Sehemu ya Nyumba ya Bw Roboti iliyoteketea kwa Moto Oktoba 8,2025 (Picha na Grace Khamisi)

Nyumba ya mkazi wa Mangamba Chini, Bw. Roboti, imeteketea kwa moto asubuhi ya Oktoba 8, 2025, kutokana na mkaa uliokuwa bado una moto. Jeshi la Zimamoto lilifika kwa haraka kuzima moto huo, huku viongozi na majirani wakitoa pole na elimu ya tahadhari dhidi ya moto majumbani

Na Grace Khamisi

Mkazi mmoja wa mtaa wa Mangamba Chini, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, anayefahamika kwa jina la Roboti, amejikuta katika wakati mgumu baada ya nyumba yake kuteketea kwa moto. Tukio hilo limetokea majira ya saa tatu asubuhi, Oktoba 8, 2025.

Wakizungumza na Jamii fm redio, majirani wa Bw. Roboti, Bi. Mariamu Yusufu na Mohamedi Moa ,wamesema kuwa wakati moto huo ulipoanza walikuwa nyumba ya jirani, karibu na nyumba ya Roboti, ndipo walipoona moshi na kuwajulisha majirani wengine ili kusaidia kuzima moto huo.

Sauti ya Mariamu Yusufu – Jirani wa Bw. Roboti

Kwa upande wake, Bw. Roboti ambaye ni muathirika wa tukio hilo, amesema kuwa alipata taarifa za kuungua kwa nyumba yake kupitia simu alipokuwa kazini, na alilazimika kukatisha kazi ili kufika nyumbani haraka kwa ajili ya kuokoa mali na kusaidia kuuzima moto huo.

Sauti ya Bw. Roboti – Muathirika wa Moto

Naye Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Ambros Ndunguru, amesema chanzo cha moto huo ni kiroba cha mkaa kilichowekwa na Bw. Roboti bila kuchunguza kama mkaa huo ulikuwa bado una moto.

Aidha, Mrakibu Ndunguru ametumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya majiko ya mkaa, huku akitoa onyo dhidi ya tabia ya kuzima mkaa wa moto kwa kutumia majivu, akisema ni hatari kwa usalama wa makazi.

Sauti ya Ambros Ndunguru – Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Mrakibu msaidizi wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Ambrosi Ndunguru akizungumza na wakazi wa mtaa wa Mangamba chini jinsi ya matumizi sahihi ya majiko ya mkaa(Picha na Grace Khamisi)

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mangamba Chini, Bw. Abdala Abdala, amempa pole Bw. Roboti kwa tukio hilo, huku akilishukuru Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kufika kwa haraka na kuzuia madhara makubwa zaidi.

Sauti ya Abdala Abdala – Mwenyekiti wa Mtaa wa Mangamba Chini
Share:

Viongozi Mkunwa wagusa maisha ya mzee Somba

 

Afisa mtendaji wa kata ya Mkunwa Bi Rachael Pether wa pili kutokea kulia akiwa katika picha ya pamoja wakati wa kukabidhi msaada wa Godoro kwa familia ya Mzee Salamu Somba (Picha na Musa Mtepa)

Viongozi wa Kata ya Mkunwa wametoa msaada wa godoro, sabuni na taa kwa familia ya Mzee Salumu Somba ili kusaidia kupunguza changamoto za maisha zinazoikabili familia hiyo.

Na Musa Mtepa

Viongozi na watendaji wa vijiji katika Kata ya Mkunwa wametoa msaada wa godoro, sabuni na taa kwa familia ya Mzee Salumu Somba, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za mwenyekiti wa Kijiji cha Nyengedi katika kusaidia familia hiyo inayokabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Akizungumza na Jamii FM Radio leo Oktoba 9, 2025 wakati wa kukabidhi msaada huo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mkunwa, Bi Rechal Bernadater Pether, amesema kuwa uongozi wa Kijiji cha Nyengedi uliwasilisha taarifa juu ya hali ya familia hiyo katika ofisi ya kata, na baada ya kutembelea familia hiyo walijiridhisha kuhusu uhitaji wa msaada.

Aidha, Bi Rechal ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kusaidia familia hiyo ambayo inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

Sauti ya Bi Rechal Bernadater Pether, Mtendaji wa Kata ya Mkunwa

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyengedi, Bi Ebby Hamisi, ameushukuru uongozi wa kata kwa kuguswa na changamoto zinazowakabili wananchi wao, akibainisha kuwa msaada huo utasaidia kupunguza kwa kiasi fulani matatizo yanayoikumba familia hiyo.

Hata hivyo, Bi Ebby amesema kuwa pamoja na msaada huo, familia ya Mzee Somba bado inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo watoto wake wa shule ya msingi kukosa mahitaji muhimu ya shule, na hali ya kulala chini kwa kutumia matambala ardhini.

Sauti ya Bi Ebby Hamisi, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyengedi

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyengedi, Bi Lukia Mnyachi, ameushukuru uongozi wa kata kwa msaada huo, akisema umeleta faraja na kupunguza changamoto kwa familia ya Mzee Somba.

Sauti ya Bi Lukia Mnyachi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyengedi

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mzee Salumu Somba ameushukuru uongozi wa kata pamoja na mwenyekiti wa kijiji kwa jitihada zao za kuwafikia na kuwasaidia, akieleza kuwa hali yao kwa sasa imeimarika ukilinganisha na kipindi cha nyuma.

Sauti ya Mzee Salumu Somba, mlemavu wa macho

Mzee Salumu Somba ni mkazi wa Kijiji cha Nyengedi kilichopo Kata ya Mkunwa, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, mkoani Mtwara. Hapo awali alikuwa akiishi katika nyumba chakavu isiyo na paa imara, hali iliyosababisha yeye na watoto wake watatu wenye umri kati ya miaka 5 hadi 8 kulala wakiwa wazi kwa mvua na jua.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Kijiji cha Nyengedi, kupitia kwa Mwenyekiti wake Bi Lukia Mnyachi, ulijitahidi na kufanikisha ujenzi wa nyumba mpya kwa familia hiyo. Hata hivyo, familia hiyo iliendelea kukosa vitanda na kulazimika kulala chini, hali iliyowalazimu viongozi hao kuandaa msaada wa godoro na mahitaji mengine ya msingi.

Share:

Wanafunzi DIS waitembelea Jamii FM Mtwara

 

Amua Rushita meneja na mtaalamu wa TEHAMA akitoa maelekezo jinsi redio inavyofanya kazi kutokea studio hadi kufikia kwa wasikilizaji(Picha na Musa Mtepa)

Wanafunzi wa Kidato cha Pili wa Dar es Salaam Independent School wametembelea Jamii FM Radio Mtwara kujifunza kuhusu vyombo vya habari na athari za mitandao ya kijamii , ikiwa ni sehemu ya somo la Mtazamo wa Kidunia (Global Perspective).

Na Musa Mtepa

Mtwara —-Wanafunzi wa Kidato cha Pili kutoka Dar es Salaam Independent School (DIS) leo, Oktoba 7, 2025, wametembelea kituo cha kurushia matangazo cha Jamii FM Radio kilichopo Mtwara, kwa lengo la kujifunza kwa vitendo kuhusu vyombo vya habari, hususan redio na mitandao ya kijamii.

Akizungumza kuhusiana na ujio huo, Meneja na Mtaalamu wa Masuala ya TEHAMA kutoka Jamii FMAmua Rushita, amesema kuwa wanafunzi hao wamefika kituoni hapo ili kujifunza namna mitandao ya kijamii inavyoathiri vyombo vya habari (Traditional Media), pamoja na jinsi jamii inavyoweza kupata taarifa sahihi kupitia vyombo vya habari.


Sauti ya Amua Rushita – Meneja wa Jamii FM

Amua ameongeza kuwa moja ya sababu zilizowavutia wanafunzi kutembelea Jamii FM ni kutokana na namna vipindi vya redio hiyo vinavyogusa makundi yote ya jamii moja kwa moja.

Sauti ya Amua Rushita – Meneja wa Jamii FM

Kwa upande wake, Mwalimu, Donald kutoka Dar es Salaam Independent School, ameishukuru Jamii FM kupitia kwa Amua Rushita kwa kutoa elimu ya kina kuhusu aina mbili za vyombo vya habari   faida na changamoto zake kwa jamii .

Pia amesema kuwa moja ya mambo waliokuja kujifunza Mtwara ni somo la Mtazamo wa Kidunia (Global Perspective), ambalo limejikita katika kueleza jinsi mitandao ya kijamii inavyoathiri Jamii hususani kwa upande wa vyombo vya habari.

Sauti ya Mr. Donald – Mwalimu, Dar es Salaam Independent School

Nao wanafunzi wa DIS wamesema kuwa ziara hiyo imewasaidia kuelewa kwa undani namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi, na nafasi ya redio kama chanzo cha habari kinachoaminika katika jamii.

Sauti ya Wanafunzi wa Dar es Salaam Independent School
Share:

Nabii Suguye atoa msaada kwa watoto maalum Mtwara

 

Nabii Nicolous Suguye akizungumza na Wanafunzi baada ya kutoa msaada katika shule ya Msingi Rahaleo (Picha na Musa Mtepa)

Nabii Ncolous Suguye ametoa msaada wa viti mwendo na chakula kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Kituo cha Upendo na Shule ya Msingi Rahaleo, Mtwara, kabla ya kuanza mkutano wa Injili utakaofanyika Oktoba 2, 2025, katika viwanja vya Sabasaba.

Na Musa Mtepa
Oktoba 1, 2025 – Nabii Nicolous Suguye ametembelea na kutoa msaada wa viti mwendo pamoja na chakula kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Kituo cha Upendo na kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia katika Shule ya Msingi Rahaleo, iliyopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Akizungumza baada ya kutoa msaada huo, Nabii Suguye amesema kuwa ziara yake Mtwara inalenga kufanikisha mkutano wa Injili, na kwamba ana utaratibu wa kuwatembelea na kuwasaidia watu wenye uhitaji kila anapofika katika maeneo tofauti kwa ajili ya huduma ya kiroho.

Sauti 1: Nabii Ncolous Suguye
Nabii Suguye akiwa na Mtoto mwenye ulemavu katika kituo cha upendo kilichopo mtaa wa Mdenga ,Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Aidha, Nabii Suguye ametoa wito kwa jamii kutowatenga watu wenye ulemavu, bali kuendelea kuwaonesha upendo na kuwahudumia kwa moyo wa furaha.

Sauti 2: Nabii Ncolous Suguye

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Rahaleo na mlezi wa kitengo cha wanafunzi viziwi, Bi. Hilda Mapunda, amemshukuru Nabii Suguye kwa mchango wake, akisema kuwa msaada huo umeleta faraja na matumaini kwa watoto hao.

Sauti: Hilda Mapunda, Mwalimu Mkuu Msaidizi

Naye Meneja wa Kituo cha Upendo,   Faustini Keha, ametoa wito kwa jamii kuwa na moyo wa upendo kwa watoto wenye changamoto ya usonji, huku akimshukuru Nabii Suguye kwa msaada wa viti mwendo vinne na chakula.

Sauti: Fautini Kayeka, Meneja wa Kituo cha Upendo

Nabii Suguye anatarajia kuendesha mkutano mkubwa wa Injili kuanzia Oktoba 2, 2025, katika viwanja vya Sabasaba, Manispaa ya Mtwara Mikindani, ukiwa na ujumbe maalum: ‘Tokomeza Misukule.’

Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>