
Mdahalo ulioandaliwa na Jamii FM umebainisha kuwa mimba mashuleni husababishwa na malezi duni, kutokuwepo kwa uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi, pamoja na ushiriki wa jamii hafifu katika kulinda watoto wa kike
Na Musa Mtepa
Inaelezwa kuwa ukosefu wa malezi na maandalizi bora kwa watoto kutoka kwa wazazi umeendelea kuwa moja ya sababu kuu zinazochangia wanafunzi wa kike kupata mimba wakiwa bado shuleni.
Hayo yamebainika katika mdahalo ulioandaliwa na Jamii FM Radio Oktoba 8, 2025, uliokuwa na kaulimbiu “Jamii Inashiriki Vipi Katika Kutokomeza Mimba Shuleni.
Maafisa usafirishaji (bodaboda) kutoka stendi ya Bajaji, kata ya Naliendele, wameeleza kuwa mimba nyingi zinazopatikana shuleni huchangiwa na wazazi kulega katika malezi, ikiwemo kuruhusu watoto kushiriki matukio ya usiku kama vile vigodoro, ambayo huwapeleka katika mazingira hatarishi.
Hata hivyo, baadhi ya wazazi wamepinga kauli hiyo wakisema si wazazi wote huruhusu watoto wao kwenda kwenye vigodoro. Shaibu Abdala Kupela na Brandina Chilumba, ambao ni wazazi, wamesema kuwa kuna sababu nyingine nyingi zinazochangia mimba shuleni, ikiwemo wazazi kutengana bila sababu za msingi, hali inayosababisha watoto kukosa uangalizi wa kutosha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pachoto “A”, Bw. Sadi Abdala Kombo, amesema kuwa ili kuondokana na tatizo la mimba mashuleni, ni lazima wazazi wasimame imara katika kulea watoto wao na kutambua wajibu wao kama walezi.
Aidha, Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa viongozi wa mitaa wana wajibu wa kukutana na wazazi mara kwa mara kwa ajili ya kujadiliana namna ya kuwasaidia watoto kuishi salama na kujitambua wakiwa shuleni.

Kwa upande mwingine, Judith Chitanda kutoka shirika la Nerio Paralegal pamoja na Sajenti Esta kutoka dawati la jinsia, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, wameitaka jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale mtoto anapopata ujauzito ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika na kusaidia kutokomeza mimba mashuleni.







No comments:
Post a Comment