
Nabii Ncolous Suguye ametoa msaada wa viti mwendo na chakula kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Kituo cha Upendo na Shule ya Msingi Rahaleo, Mtwara, kabla ya kuanza mkutano wa Injili utakaofanyika Oktoba 2, 2025, katika viwanja vya Sabasaba.
Na Musa Mtepa
Oktoba 1, 2025 – Nabii Nicolous Suguye ametembelea na kutoa msaada wa viti mwendo pamoja na chakula kwa watoto wenye mahitaji maalum katika Kituo cha Upendo na kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia katika Shule ya Msingi Rahaleo, iliyopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza baada ya kutoa msaada huo, Nabii Suguye amesema kuwa ziara yake Mtwara inalenga kufanikisha mkutano wa Injili, na kwamba ana utaratibu wa kuwatembelea na kuwasaidia watu wenye uhitaji kila anapofika katika maeneo tofauti kwa ajili ya huduma ya kiroho.

Aidha, Nabii Suguye ametoa wito kwa jamii kutowatenga watu wenye ulemavu, bali kuendelea kuwaonesha upendo na kuwahudumia kwa moyo wa furaha.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Rahaleo na mlezi wa kitengo cha wanafunzi viziwi, Bi. Hilda Mapunda, amemshukuru Nabii Suguye kwa mchango wake, akisema kuwa msaada huo umeleta faraja na matumaini kwa watoto hao.

Naye Meneja wa Kituo cha Upendo, Faustini Keha, ametoa wito kwa jamii kuwa na moyo wa upendo kwa watoto wenye changamoto ya usonji, huku akimshukuru Nabii Suguye kwa msaada wa viti mwendo vinne na chakula.

Nabii Suguye anatarajia kuendesha mkutano mkubwa wa Injili kuanzia Oktoba 2, 2025, katika viwanja vya Sabasaba, Manispaa ya Mtwara Mikindani, ukiwa na ujumbe maalum: ‘Tokomeza Misukule.’






No comments:
Post a Comment