
Uchongaji wa Barabara hiyo itarahisisha huduma kwa wakazi, hususan nyakati za dharura, Mwenyekiti wa mtaa, Bw. Kuladaku, ameunga mkono wazo hilo, akisisitiza mchango wake kwa maendeleo ya vijiji jirani
Na Musa Mtepa
Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya njia ya kutoka Mkunja Nguo kuelekea Namdohola, mdau wa maendeleo Bw. Ahmadi Issa Chihipu ameiomba Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kuiangalia kwa “jicho la tatu” na kuichonga rasmi kuwa barabara inayopitika kwa urahisi na usalama kwa wananchi.
Akizungumza na Jamii fm Redio, Bw. Chihipu amesema kuwa njia hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa Namdohola, pamoja na vijiji vya jirani vya Litumbo na Mnyengedi vya halmashauri ya Mtwara vijijini , na tayari ameanza kuchukua hatua binafsi kwa kujitolea kufanya usafi na kufyeka ili kuiandaa kwa ajili ya uchongaji, mara tu Halmashauri itakaporidhia.
Mbali na mchango wake binafsi, Bw. Chihipu ameeleza kuwa moja ya sababu kubwa zilizomsukuma kuibua umuhimu wa barabara hiyo ni changamoto za usafiri nyakati za dharura, hususan wakati wanawake wajawazito wanapopatwa na uchungu wa kujifungua usiku.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkunja Nguo, Bw. Musa Ali maarufu kama Kuladaku, ameunga mkono hoja hiyo na kubainisha kuwa barabara hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya jirani.
Mwenyekiti Kuladaku ametoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuifanyia kazi ombi hilo, akisisitiza kuwa barabara hiyo ni hitaji la muda mrefu linalogusa maisha ya watu moja kwa moja.
























