
Mradi wa Kuwawezesha Mabinti Kupaza Sauti umepongezwa kwa kuleta mabadiliko chanya kwa wasichana Mtwara kwa kuwaongezea ujasiri, sauti na ushiriki katika maamuzi muhimu. Awamu ya tatu imezinduliwa Julai 2025, ikilenga kufikia mabinti wengi zaidi na kushirikisha jamii kwa upana.
Na Mwanahamisi Chikambu
Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Fatma Mtanda, amepongeza Shirika la Maendeleo ya Michezo (SDA) kwa mchango wao kupitia mradi wa Kuwawezesha Mabinti Kupaza Sauti, unaolenga kuimarisha nafasi ya mtoto wa kike katika jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi huo uliofanyika leo Julai 23, 2025 kwenye ukumbi wa TCCIA, Bi. Mtanda amesema mradi huo umeleta mabadiliko chanya kwa mabinti kwa kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujieleza na kushiriki kwenye maamuzi yanayohusu maisha yao.
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza jinsi elimu waliyoipata kupitia mradi huo ilivyowasaidia kuboresha mbinu za kushughulikia changamoto za kijinsia, hasa kwa wanafunzi wa kike. Wamesema mafunzo yamewasaidia kutambua njia bora za kuwasaidia wasichana kushinda vizingiti vya kijamii na kimfumo.
Kwa upande mwingine, baadhi ya makungwi walioshirikishwa katika utekelezaji wa mradi huo wameeleza namna walivyopokea elimu ya kutoa mafundisho chanya kwa mabinti, bila kuendeleza mila na desturi zinazowanyima haki au kuwawekea mipaka ya kimaendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya SDA, Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Thea Swai ameeeleza kuwa awamu hii ya tatu ya mradi itatekelezwa kuanzia mwaka 2025 hadi 2028, ikiwa na lengo la kufikia mabinti wengi zaidi, kuongeza idadi ya walimu na watendaji wanaopatiwa mafunzo pamoja na kushirikisha makundi mbalimbali ya jamii katika kuwawezesha wasichana kupaza sauti zao.






No comments:
Post a Comment