
Wananchi wa Kata ya Tangazo, Mtwara, wameishukuru serikali kwa kuwaletea kliniki tembezi ya uchunguzi wa kifua kikuu, hatua iliyowapunguzia gharama na kurahisisha upatikanaji wa matibabu, huku wakitaka kampeni hizo ziendelee vijijini.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Kata ya Tangazo, mkoani Mtwara, wameipongeza serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kupeleka kliniki tembezi ya uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu (TB) katika kijiji chao, hatua waliyoeleza kuwa imepunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu.
Wakizungumza na Jamii FM Radio, wakazi wa kata hiyo wamesema huduma hizo zimekuwa mkombozi kwao, hasa kwa kuzingatia hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili.
Wengine walioeleza shukrani zao ni pamoja na Mzee Mtalika Lilala na Abdala Salum Kibokotwe wa Kijiji cha Tangazo ambapo pamoja na yote wamependekeza kliniki tembezi hizo ziongezwe kwa magonjwa mengine
Kwa upande wake, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Mtwara, Dkt. Maikoadi Skoni, amesema kliniki tembezi hiyo ilizinduliwa rasmi Agosti 1, 2025, katika Viwanja vya Mkanaledi, Manispaa ya Mtwara Mikindani. Kampeni hiyo inalenga kufikia halmashauri zote tisa za mkoa wa Mtwara.
Amesisitiza kuwa huduma hizo zinatolewa bure, na wagonjwa wote watakaobainika huunganishwa moja kwa moja na vituo vya afya vya karibu ili kupata matibabu zaidi.

Naye Dkt. Boniface Jengela, Mratibu wa TB na Ukoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kuwafikia wananchi wanaoishi mbali na vituo vya afya na kuwatambua mapema wanaoonesha dalili za kifua kikuu.
Aidha Dkt Boniface amebainisha kuwa dalili wanazozinaglia ni pamoja na kukohoa zaidi ya wiki mbili,kutoka jasho wakati wa usiku na viashiria vingine huku akiwataka Wananchi kuitikia kwa uwingi maeneo yote yatakayopitia na kampeni hiyo.

Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za serikali kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu nchini ifikapo mwaka 2030.






No comments:
Post a Comment