
Ni warsha kujadili changamoto na fursa kwa watu wenye ulemavu, ikiwakutanisha viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo, lengo ni kuimarisha elimu jumuishi na kuondoa mitazamo potofu.
Na Mwanahamisi Chikambu
Katika juhudi za kuendeleza elimu jumuishi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, Shirika lisilo la Kiserikali la Sport Development Aid (SDA), linalojihusisha na kuwawezesha mabinti kupaza sauti, limeandaa warsha maalum ya siku moja iliyofanyika Mkoani Mtwara.
Warsha hiyo imelenga kujadili changamoto na fursa zinazohusu watu wenye ulemavu, ikiwakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (Mtwara DC), maafisa elimu, afisa michezo na utamaduni, afisa ustawi wa jamii, watendaji wa kata, wakuu wa shule za sekondari, pamoja na wawakilishi kutoka vyama vya watu wenye ulemavu na baadhi ya walemavu wenyewe.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Meneja wa Mradi kutoka SDA, Bi. Jacline Mpunjo, amesema kuwa licha ya watu wenye ulemavu kuwa sehemu ya jamii, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowazuia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Wadau wote walioshiriki warsha hiyo wameeleza umuhimu wa kuwatambua watu wenye ulemavu kama sehemu ya nguvu kazi ya taifa, wakisisitiza hitaji la kuwepo kwa sera jumuishi, pamoja na kuondoa mila na mitazamo potofu zinazowatenga.

Warsha hiyo imehitimishwa kwa madhumuni ya pamoja ya kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa elimu jumuishi na upatikanaji wa huduma bora kwa watu wenye ulemavu, hususan katika sekta ya elimu na ustawi wa jamii.






No comments:
Post a Comment