
Bandari ya Mtwara imeongeza usafirishaji wa mizigo kwa asilimia 49 kati ya 2023/2024, ikihusisha korosho na makaa ya mawe, huku idadi ya makampuni ya meli ikiongezeka
Na Gregory Milanzi
Mtwara-September 29,2025 – Ukusanyaji na usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Mtwara umeongezeka kwa asilimia 49 katika mwaka wa fedha 2023/2024 ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hatua inayodhihirisha ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika ukanda wa kusini.
Akizungumza September 29, 2025 kwenye mkutano wa wadau wa bandari hiyo unaoendelea mkoani Mtwara, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi amesema bandari hiyo imesafirisha tani milioni 2.5 za mizigo kwa mwaka 2024/2025 kutoka tani milioni 1.7 kwa mwaka uliopita wa fedha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Meli Tanzania (TASAA), Daniel Mallongo amesema Bandari ya Mtwara ni muhimu sana kwa usafirishaji wa zao la korosho, na kwamba idadi ya makampuni ya usafirishaji wa meli imeongezeka kutoka mawili hadi sita katika misimu mitatu iliyopita.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Emanuel Mrutu amesema Bandari ya Mtwara haifanyi kazi msimu wa korosho pekee, bali imekuwa ikihudumia pia bidhaa nyingine kama makaa ya mawe.

Mkutano huo wa wadau wa bandari unalenga kuangazia fursa na changamoto katika kuendeleza shughuli za usafirishaji kupitia Bandari ya Mtwara.

























