
Mdondoko wa wanafunzi na ukatili wa kijinsia vyatajwa kuchangia ongezeko la vitendo vinavyohatarisha amani katika jamii , huku wazazi wakilaumiwa kwa kulegeza majukumu ya malezi na ufuatiliaji wa watoto wao
Na Musa Mtepa
Mtwara, Septemba 24, 2025 – Ukatili wa kijinsia pamoja na mdondoko wa wanafunzi mashuleni vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea viashiria vya uvunjifu wa amani katika jamii.
Akizungumza katika kipindi Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM radio tarehe 24 Septemba, 2025, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Safety Alliance (TASA), Bw. Hamisi Mwinshekhe, amesema wanafunzi wanaokumbwa na changamoto ya kuacha shule hukosa mwelekeo wa maisha, hali inayowafanya kuwa rahisi kushawishika kujiingiza kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani.
Bw. Mwinshekhe ameongeza kuwa chanzo kikuu cha mdondoko wa wanafunzi ni kulegalega kwa wazazi katika jukumu la malezi. Ameeleza kuwa baadhi ya wazazi huacha watoto wao kulelewa na mazingira ya mitaani, jambo linalowapelekea vijana hao kujiunga na makundi hatarishi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi kutoka shirika la TASA, Bi. Betty Chenge, amesema wazazi wengi wamekuwa wakiwaachia walimu jukumu la malezi na ufuatiliaji wa watoto wao, badala ya kushirikiana nao kikamilifu. Hali hiyo, amesema, imekuwa chanzo cha ongezeko la utoro na mdondoko mashuleni.
Aidha, Bi. Chenge ameisisitiza jamii kutambua kuwa malezi ya mtoto si jukumu la mtu mmoja pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha mtoto anapata mahitaji yake ya msingi. Ameongeza kuwa jamii inapaswa kuwasaidia watoto wanaoonesha viashiria vya mienendo hatarishi kwa kuwaelimisha na kuwaongoza katika njia sahihi.
Katika mjadala huo, baadhi ya wasikilizaji waliopiga simu kushiriki kipindi wamelishukuru shirika la TASA kwa elimu waliyopatiwa, huku wakikiri kuwa uzembe wa malezi kutoka kwa baadhi ya wazazi umekuwa chanzo kikuu cha mdondoko wa wanafunzi na kushiriki kwao katika vitendo vinavyohatarisha amani ya jamii.
Shirika la Tanzania Safety Alliance (TASA) kwa sasa linatekeleza mradi wa “Amani Yetu Kesho Yetu” , unaotekelezwa katika kata tano za Halmashauri ya Mtwara Vijijini ambazo ni Madimba, Tangazo, Nalingu, Msimbati, na Mahurunga.






No comments:
Post a Comment