 |
| Mwenyekiti wa mtandao wa redio za jamii Tanzania (TADIO) ndugu Baptist akizungumza katika mafunzo hayo |
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inaendesha semina kwa wamiliki na wahariri wa redio za kijamii zipatazo 50 ikiwemo Jamii FM Radioo ya Mtwara toka Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia tarehe 23 hadi 25,Mei 2026, Lengo kuu likiwa ni kukuza uelewa juu ya majukumu ya TADB pamoja na kuonesha fursa zinazopatikana katika benki hiyo.
Aidha, washiriki wamejengewa uwezo wa kuripoti masuala ya maendeleo ya sekta ya kilimo, fedha za kilimo, na nafasi ya taasisi za kifedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa kilimo nchini.
Mafunzo hayo yataimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari vya kijamii na TADB katika kuhamasisha uelewa wa umma kuhusu fursa za uwezeshaji wa kifedha kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengine wa mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.
Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Jengo la Mkandarasi Jijini Dodoma na kufunguliwa rasmi na Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi TADB, ndugu Mkani Waziri, ambaye amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu mchango wa sekta ya fedha kwenye maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Mbali na elimu hiyo wanahabari hao wamepatiwa vyeti ikiwa ni njia ya kutambua mchango wao katika jamii pamoja na materials mbalimbali yatakayosaidia kutangaza fursa zinazopatikana TADB ili wakulima wote nchini waweze kunufaika nazo.