Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja
Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao
Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii
Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm
Mmoja wa wadau akizungumza katika kipindi. Picha na mwandishi wetu
“Mtaa hauna mtoto ila watoto wanatoka kwenye jamii zetu wenyewe”
Jamii inapaswa kuzingatia malezi bora ya watoto na kupunguza au kuacha kabisa kutelekeza familia zao jambo ambalo linapelekea watoto wengi kushindwa kupata malezi bora na huduma stahiki katika ngazi ya familia na kupelekea watoto hao kukimbilia mitaani ili kujitafutia mahitaji na hapo ndipo linapozaliwa jina la Watoto wa mitaani.
Kiuhalisia mtaa hauna mtoto ila watoto wanatoka kwenye jamii zetu wenyewe na zipo sababu nyingi zinazopelekea tatizo hili ambalo limekuwa kubwa kwa baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo Mtwara,
Kwakuliona hilo Jamii FM Radio tumekuandalia kipindi kinachoangazia Mchango wa wazazi na walezi katika kupunguza watoto wa mtaani, Kipindi hiki kimekutanisha Teresia Ngonyani Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mtwara, Torai Kibit- Meneja miradi KIMAS, Martin Kasembe -Mzazi na Hamis Chikambu Kiongozi wa dini ya kiislamu
Washirika wa warsha iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Sport Development Aid (SDA) (Picha na Mwanahamisi Chikambu)
Ni warsha kujadili changamoto na fursa kwa watu wenye ulemavu, ikiwakutanisha viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo, lengo ni kuimarisha elimu jumuishi na kuondoa mitazamo potofu.
Na Mwanahamisi Chikambu
Katika juhudi za kuendeleza elimu jumuishi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, Shirika lisilo la Kiserikali la Sport Development Aid (SDA), linalojihusisha na kuwawezesha mabinti kupaza sauti, limeandaa warsha maalum ya siku moja iliyofanyika Mkoani Mtwara.
Warsha hiyo imelenga kujadili changamoto na fursa zinazohusu watu wenye ulemavu, ikiwakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (Mtwara DC), maafisa elimu, afisa michezo na utamaduni, afisa ustawi wa jamii, watendaji wa kata, wakuu wa shule za sekondari, pamoja na wawakilishi kutoka vyama vya watu wenye ulemavu na baadhi ya walemavu wenyewe.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Meneja wa Mradi kutoka SDA, Bi. Jacline Mpunjo, amesema kuwa licha ya watu wenye ulemavu kuwa sehemu ya jamii, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowazuia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Sauti ya… Meneja wa Mradi kutoka SDA, Bi. Jacline Mpunjo
Wadau wote walioshiriki warsha hiyo wameeleza umuhimu wa kuwatambua watu wenye ulemavu kama sehemu ya nguvu kazi ya taifa, wakisisitiza hitaji la kuwepo kwa sera jumuishi, pamoja na kuondoa mila na mitazamo potofu zinazowatenga.
Sauti ya washiriki
Warsha hiyo imehitimishwa kwa madhumuni ya pamoja ya kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa elimu jumuishi na upatikanaji wa huduma bora kwa watu wenye ulemavu, hususan katika sekta ya elimu na ustawi wa jamii.
Hali ya barabara ya Mtwara kuwelekea Dar es Salaam kabla ya kuharibika. Picha na Amua Rushita
“Tunatoa wito wa kuchukua hatua za pamoja, utunzaji wa miundombinu, kuboresha miundombinu, kuwahamisha watu kutoka maeneo hatarishi na kuimarisha elimu ya tabianchi“
Na Musa Mtepa,
Mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri maisha ya Watanzania, hasa katika mikoa ya Kusini kama Mtwara na Lindi, makala hii maalum inamulika madhara ya tabianchi ikiwemo mafuriko ya mara kwa mara, uharibifu wa makazi na kusimama kwa shughuli za kiuchumi na usafiri.
Kupitia ushuhuda wa wananchi na kauli za viongozi wa serikali, makala inaonyesha hatua zilizochukuliwa kama ujenzi wa madaraja makubwa lakini pia inaibua maswali kuhusu ufanisi wake wa muda mrefu. Je, tuna mikakati ya kweli ya kukabiliana na mabadiliko haya?
Tunatoa wito wa kuchukua hatua za pamoja, utunzaji wa miundombinu, kuboresha miundombinu, kuwahamisha watu kutoka maeneo hatarishi, na kuimarisha elimu ya tabianchi. Ustawi wa mikoa ya kusini na mustakabali wa taifa uko mikononi mwetu sote.
Mwonekano wa nje wa nyumba anayoishi mzee Salumu Somba mlemavu wa macho katika kijiji cha Nyengedi Mtwara Vijijini (Picha na Musa Mtepa)
Mzee Salumu Somba mkazi wa Mnyengedi, Mtwara, mlemavu wa macho, anaomba msaada wa makazi, mavazi, na mahitaji ya msingi kwa ajili ya familia yake kutokana na hali ngumu ya maisha.
Na Musa Mtepa
Mzee Salumu Somba, mkazi wa Kijiji cha Mnyengedi kata ya Mkunwa katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini, anaomba msaada kutoka kwa wadau na wasamaria wema ili apate makazi bora na mahitaji ya msingi ya kibinadamu.
Mzee Somba ni mlemavu wa macho ambaye anaeleza kuwa maisha anayopitia kwa sasa ni magumu mno kutokana na hali yake ya ulemavu, ukosefu wa makazi bora, mavazi na upatikanaji wa chakula cha uhakika kwa familia yake.
Sauti ya 1 mzee Salumu Somba Mlemavu wa macho
Mzee huyo mwenye mke mmoja na watoto wawili wanaosoma darasa la kwanza na la tatu, anasema kwa sasa nyumba yake imeharibika kiasi kwamba wakati wa mvua hunyeshewa akiwa ndani na familia yake, hali inayowaweka kwenye mazingira hatarishi kiafya na kimaisha.
Sauti ya 2 mzee Salumu Somba Mlemavu wa machoMzee Salumu Somba akiwa ameketi barazani mwa nyumba yake (Picha na Musa Mtepa0
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyengedi, Bi Lukia Mnyachi, amesema alifahamishwa kuhusu hali ya Mzee Somba na mwanakijiji mmoja. Baada ya kutembelea eneo analoishi mzee huyo na kujionea mazingira halisi, aliamua kuanzisha jitihada za kumsaidia.
Sauti ya 1 Lukia Mnyachi mwenyekiti wa Kijiji
Aidha Bi Lukia amesema baada ya kupata mchango kutoka kwa umoja wa wenyeviti akaanza mchakato rasmi wa kujenga nyumba kwa ajili ya Mzee Somba kwa kuendelea kushirikisha viongozi wengine wa juu ambao kwa namna moja au nyingine wameendelea kumuunga mkono katika kulifanikisha hilo.
Sauti ya 2 Lukia Mnyachi mwenyekiti wa Kijiji
Licha ya hatua hizo, bado kuna uhitaji mkubwa wa msaada zaidi kwa familia hiyo — hasa vifaa vya msingi kama kitanda, magodoro, mashuka na mavazi kwa watoto wake.
Sauti ya 3 Lukia Mnyachi mwenyekiti wa Kijiji
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamejitokeza kwa moyo mmoja kushiriki katika jitihada za kumjengea Mzee Somba banda la muda, huku wakiendelea kuomba msaada zaidi kutoka kwa wadau wa maendeleo na mashirika ya kijamii.
Sauti ya baadhi ya wananchi wa NyengediMwenyekiti wa kijiji cha Nyengedi Bi Lukia Mnyachi akiwa na mzee Salumu Somba mlemavu wa macho baada ya kutembelea nyumbani kwake(Picha na Musa Mtepa)
Kwa wale wanaotaka kuchangia au kumsaidia Mzee Somba na familia yake, wanaombwa kuwasiliana na uongozi wa Kijiji cha Mnyengedi au kupitia kituo cha Jamii FM Radio kwa maelekezo zaidi.
Mariamo Chibwalo (Pichani) akizungumza na Mwanaidi kopakopa (aliyeshika kinasa sauti) kuhusu kuwania nafasi ya uongozi katika kata ya Chuno iliyopo Mkoani Mtwara nchini Tanzania. Picha na Mpiga Picha wetu
Kata ya Chuno iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani yenye jumla ya watia nia 10 wanaowania nafasi ya udiwani, Mariam Chibwalo ndiye mwanamke pekee aliyejitokeza kuomba ridhaa ya chama.
Na Mwanaidi Kopakopa
Kujiamini na uzoefu katika siasa ni miongoni mwa silaha kuu anazozitumia Mariam Chibwalo, mkazi wa Kata ya Chuno katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara. Mariam ni mmoja wa watia nia kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo katika kata hiyo yenye jumla ya watia nia 10 wanaowania nafasi ya udiwani, yeye ndiye mwanamke pekee aliyejitokeza kuomba ridhaa ya chama.
Dhamira yake ni kutimiza ndoto na maono aliyojiwekea kwa ajili ya ustawi wa jamii yake, Kwa mujibu wa Mariam, moja ya ndoto zake ni kuiona Kata ya Chuno ikipiga hatua mpya katika nyanja mbalimbali hasa za uchumi, elimu na maendeleo ya kijamii yanayoonekana wazi.
Analenga kuhakikisha makundi ya wanawake na vijana yanashiriki kikamilifu katika maamuzi pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha hakuna kundi linalobaki nyuma katika safari ya maendeleo ya kata hiyo.
Mkurugenzi wa SDA Thea Swai akizungumza mbele ya washiriki wakati wa utambulisho wa mradi wa Girls Speak Out season three katika ukumbi TCIA mjini Mtwara (Picha na Mwanahamisi Chikambu)
Mradi wa Kuwawezesha Mabinti Kupaza Sauti umepongezwa kwa kuleta mabadiliko chanya kwa wasichana Mtwara kwa kuwaongezea ujasiri, sauti na ushiriki katika maamuzi muhimu. Awamu ya tatu imezinduliwa Julai 2025, ikilenga kufikia mabinti wengi zaidi na kushirikisha jamii kwa upana.
Na Mwanahamisi Chikambu
Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Fatma Mtanda, amepongeza Shirika la Maendeleo ya Michezo (SDA) kwa mchango wao kupitia mradi wa Kuwawezesha Mabinti Kupaza Sauti, unaolenga kuimarisha nafasi ya mtoto wa kike katika jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi huo uliofanyika leo Julai 23, 2025 kwenye ukumbi wa TCCIA, Bi. Mtanda amesema mradi huo umeleta mabadiliko chanya kwa mabinti kwa kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujieleza na kushiriki kwenye maamuzi yanayohusu maisha yao.
Sauti ya Bi Fatma Mtanda Afisa Utamaduni Mkoa wa Mtwara
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza jinsi elimu waliyoipata kupitia mradi huo ilivyowasaidia kuboresha mbinu za kushughulikia changamoto za kijinsia, hasa kwa wanafunzi wa kike. Wamesema mafunzo yamewasaidia kutambua njia bora za kuwasaidia wasichana kushinda vizingiti vya kijamii na kimfumo.
Sauti ya washiriki wa mafunzo
Kwa upande mwingine, baadhi ya makungwi walioshirikishwa katika utekelezaji wa mradi huo wameeleza namna walivyopokea elimu ya kutoa mafundisho chanya kwa mabinti, bila kuendeleza mila na desturi zinazowanyima haki au kuwawekea mipaka ya kimaendeleo.
Sauti ya Makungwi walioshiriki mafunzo hayo
Akizungumza kwa niaba ya SDA, Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Thea Swai ameeeleza kuwa awamu hii ya tatu ya mradi itatekelezwa kuanzia mwaka 2025 hadi 2028, ikiwa na lengo la kufikia mabinti wengi zaidi, kuongeza idadi ya walimu na watendaji wanaopatiwa mafunzo pamoja na kushirikisha makundi mbalimbali ya jamii katika kuwawezesha wasichana kupaza sauti zao.
Omari Bakari Hidobelele (35), mkazi wa Madangwa, Lindi, amekutwa amejinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali. Polisi wamesema marehemu alikuwa na msongo wa mawazo. Familia imeshangazwa na tukio hilo, ikieleza kuwa hakuwa na matatizo yoyote. Polisi wamehimiza jamii kusaidia wenye changamoto za afya ya akili
Na Musa Mtepa
Mtu mmoja aliefahamika kwa jina Omari Bakari Hidobelele(35) mkazi wa Kijiji Cha madangwa kata ya Sudi halmashauri ya Mtama mkoani Lindi amekutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia mkanda wa suruali yake.
Akitihibitisha tukio hilo Daktari wa Zahanati ya kijiji cha Mtegu Jackine Joseph Sita amesema kwa mujibu wa vipimo vilivyofanyika inonekana kuwa na alama zinazo thibitisha kujinyonga kupitia kifo chake .
Sauti ya Jackline Joseph Sita Daktari wa Zahanati ya Mtegu
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Salumu Hassani Kuku, kijana huyo alitoweka tangu saa tatu asubuhi ya Julai 21, 2025. Jitihada za kumtafuta zilianza mara moja bila mafanikio hadi siku iliyofuata, Jumanne ya Julai 22, ambapo alikutwa akiwa amejinyonga kwenye mti wa mkorosho majira ya saa mbili asubuhi.
Sauti ya Salumu Hassani Kuku Mwenyekiti wa kijiji cha Madangwa
Bibi wa marehemu, Bi. Fatuma Ahmadi Liyai, amesema familia imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo, lakini wamelazimika kuikubali kama sehemu ya maisha.
Aidha, Bi. Fatuma amesema tangu Omari aliporejea kutoka Kilwa, hakuwa na matatizo yoyote wala migogoro na mtu yeyote, jambo linaloendelea kuwashangaza.
Sauti ya Bi Fatuma Liyai Bibi wa Marehemu
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa anapitia hali ya msongo wa mawazo kwa kipindi cha muda mrefu, jambo linalodhaniwa kuwa chanzo cha uamuzi huo wa kujiua.
Jeshi la Polisi pia limetoa wito kwa jamii kuhakikisha wanaimarisha usaidizi wa kisaikolojia kwa watu wanaoonesha dalili za msongo wa mawazo au matatizo ya afya ya akili, na kutoa taarifa mapema kwa wataalamu husika ili kusaidia kuzuia matukio ya aina hii.
Serikali ya wilaya ya
Mtwara, mkoani Mtwara imepiga marufuku matumizi ya msumeno wa
Mnyonyoro(chainsaw)ambayo inadaiwa kuwa chanzo cha uvunaji holela wa miti
Wilayani humo.
Hayo yamebainishwa na
Mkuu wa wilaya ya Mtwara,Evod Mmanda wakati akizungumza katika uzinduzi wa
zoezi la upandaji wa Miti katika wilaya hiyo ambapo pia amezitaka halmashauri
zote katika wilaya ya Mtwara kuzuia na kudhibiti uvunaji holela wa miti kwani
hali hiyo inasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
"Mtu anayemiliki
Chainsaw hana tofaut na mtu anayemiliki mtambo wa gongo" alisema Mmanda na
kulngezea "utaratibu wa kuvuna miti unafahamika lazima uombe kibali
kuanzia ngazi ya kijiji na kijiji waandike muhtsari walete wilayani hata kama
ni mwembe wako lazima ufuate utaratibu huo" Mmanda amesema
kuwa utaratibu huo si
wake bali utaratibu wa kisheria na hivyo atakayekiuka atachukuliwa hatua Kali
za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani. Awali kaimu katibu tawala wa
Wilaya ya Mtwara,Fransis Mkuti akisoma taarifa ya upandaji miti katika wilaya
hiyo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2017 had machi mwaka huu amesema kuwa jumla
ya miti 594876 imepandwa.
Mkuu wa Mkoa
wa Mtwara Mh Gelasius Byakanwa ameamuru kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya
ya Tandahimba kuwakamata viongozi wote wa vyama 35 vya msingi waliosababisha kulipa
malipo hewa kwa wakulima ambao hawajauza korosho, yenyethamani ya Shilingi Milioni 395.
Mh Byakanwa
amesema hayo wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mkoa hapa,
baada ya kukabidhiwa ripoti ya kamati ya uchunguzi wa zao la korosho Wilaya ya
Tandahimba, na kuibaini madudu mengi kwenye wilaya hiyo, na kuakikisha wote
waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria na mkulima mmoja mmoja analipwa pesa
yake.
Mkuu wa Mkoa
amesema, pia kamati ya uchunguziwamebaini takribani Bilioni 3 hazijalipwa kwa wakulima zimecheleweshwa
na wameamuru ndani ya wiki ijayo vyama hivyo viakikishe vinawalipa wakulima
wote kwa pesa zilizopo kwenye akaunti husika.
Pia Mh
Byakanwa ameamuru kamati ya ulinzi na usalama kumkamataMeneja wa Chama kikuu cha ushirika cha
Tandahimba na Newala(TANECU) Mohamed Nassoro na mtunza ghala wa chama hicho
Msafiri Zombe kutokana na upotevu korosho kwenye ghala kuu ambazo ni mali ya
vyama 5 vya ushirika ambazo ni takribani tani 194.
Kamati hiyo
ya uchunguzi wa zao la korosho Wilayani Tandahimba, iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa
ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Jackline Kasondela ambae ni Afisa Maendeleo ya
Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.
Walimu za shule za
Msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya MASASI Mkoani MTWARA wameamua kutumia
muda wao wa likizo fupi kujengeana uwezo wa mada ngumu kwa masomo ya Sayansi,
Hisabati na Kiingereza lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi wa ufundishaji wa masomo
hayo na hivyo kuinua ufaulu katika Mitihani ya Kitaifa.
Akiongea wakati wa
mafunzo hayo katika Tarafa ya LULINDI wilayani humo, AFISA ELIMU Msingi wa
Halmashauri ya Wilaya ya MASASI Ndugu ELIZABETH MLAPONI amesema kuwa mafunzo
hayo ni kati mikakati ya kuongeza ufaulu kwa matokeo ya darasa la NNE na la SABA
kwa mwaka 2018.
Walimu wamefikia hatua hiyo baada ya kuona
baadhi ya walimu hawana uwezo wa kufundisha baadhi ya mada kutokana
kutokuzielewa vizuri hivyo mafunzo hayo yatawasaidia walimu hao kuwa na uwezo
wa kufundisha masomo hayo kwa ufanisi na hivyo kuongeza ufaulu wa masomo hayo.
MLAPONI amesema kuwa kwa matokeo ya mwaka 2017
masomo ya Kiswahili na Maarifa ya Jamii ufaulu ulikuwa asilimia 50 wakati Masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza
ufaulu ulikuwa chini ya asilimia 40 ambapo somo la Kiingereza ufaulu ulikuwa
chini ikifuatiwa na Hisabati.