
Door of Hope Tanzania imewasilisha mrejesho wa mradi wa “Pinga Ukatili, Jenga Amani na Kizazi Chenye Usawa” mkoani Mtwara, ukilenga kupinga ukatili wa kijinsia na kutoa msaada wa kisheria. Viongozi wamesifu mafanikio, ikiwemo kupungua kwa funga nyumba na talaka holela
Na Musa Mtepa
Shirika lisilo la Kiserikali la Door of Hope Tanzania, linalojihusisha na utetezi, uwezeshaji na usaidizi kwa vijana na wanawake nchini kupitia huduma za msaada wa kisheria bila malipo,limewasilisha mrejesho wa utekelezaji wa mradi wake wa “Pinga Ukatili, Jenga Amani na Kizazi Chenye Usawa” kwa wadau mbalimbali mkoani Mtwara.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TCCIA, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mheshimiwa Abdalla Mwaipaya, amesema kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia, hususan vitendo vya “funga nyumba” vinavyofanywa na baadhi ya wanaume, vimepungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Door of Hope Tanzania, Clemence Mwombeki, amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kutoa mrejesho wa shughuli zilizotekelezwa kama sehemu ya mwendelezo wa mradi huo, sambamba na kuishauri serikali kuchukua hatua stahiki juu ya changamoto zilizobainika.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Bi. Athmini Mapalilo, amesema serikali imeanza kutoa mafunzo kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya mapato yanayotokana na zao la korosho. Aidha, ametoa rai kwa taasisi za kidini na mashirika ya kiraia kuendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya talaka holela na vitendo vya funga nyumba.
Akichangia katika kikao hicho, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata ya Mahurunga, Bi. Asmini Liwowa, pamoja na Bi. Fatuma Shaibu, mkazi wa Chikongola, walisisitiza umuhimu wa wadau kutoa elimu kwa familia kuhusu athari za talaka holela na namna zinavyowaathiri watoto na jamii kwa ujumla.




























