
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgao ameishukuru Halmashauri ya Mtwara Vijijini kwa kulipa fidia ya ujenzi wa bandari Kisiwani Mgao, huku akitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za kiafya kutokana na ongezeko la wageni.
Na Musa Mtepa
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mgao, kilichopo Kata ya Naumbu, Mzee Shahame, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini kwa hatua ya kuwalipa fidia wakulima waliopisha ujenzi wa Bandari ya bidhaa chafu katika eneo la Kisiwa cha Mgao.
Akizungumza na Jamii FM Radio, Mzee Shahame amesema kuwa baada ya msuguano wa muda mrefu kati ya wananchi wa Kijiji cha Mgao, Kisiwa, na Halmashauri, hatimaye malipo ya fidia yamekamilika kwa wakulima husika. Aidha, amesema kuwa hadi sasa hakuna mwananchi yeyote kutoka kijijini kwake aliyefika kwake kulalamikia malipo hayo.
Aidha, Mzee Shahame amesema kuwa ujio wa bandari hiyo umepokelewa kwa mtazamo chanya kutokana na manufaa yake kwa taifa kwa ujumla. Hata hivyo, ameeleza kuwa bado ana mashaka juu ya wananchi wa kijiji chake kunufaika moja kwa moja kwa kupata ajira za muda (vibarua) katika mradi huo.

Pamoja na hayo, Mzee Shahame amesema kuwa maandalizi ya ujenzi wa bandari hiyo yameanza kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na ongezeko la wageni wanaofika kijijini hapo na kupanga kwenye nyumba za wenyeji, jambo linaloongeza mzunguko wa fedha katika kijiji hicho.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za kiafya na kimazingira kutokana na ongezeko la wageni wanaoendelea kufika kijijini hapo.






No comments:
Post a Comment