
Familia ya Mzee Salumu Zomba, mwenye ulemavu wa macho, yamekabidhiwa nyumba mpya baada ya kuishi kwenye kibanda kibovu, juhudi zilizowezeshwa na viongozi wa kijiji cha Mnyengedi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Na Musa Mtepa
Baada ya kuishi katika mazingira hatarishi kwa muda mrefu, familia ya Mzee Salumu Ismail Zomba, ambaye ni mlemavu wa macho, mkazi wa Kijiji cha Mnyengedi kata ya Mkunwa mkoani Mtwara, hatimaye imekabidhiwa nyumba mpya yenye vyumba viwili na ukumbi, ikiwa ni matokeo ya juhudi za pamoja zilizoongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyengedi, Bi Lukia Mnyachi.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba hiyo, Mtendaji wa Kijiji cha Mnyengedi, Bi Ebby Hamisi, amesema kuwa familia ya Mzee Zomba hapo awali ilikuwa ikiishi katika kibanda kibovu ambacho hakikutoa hifadhi ya kutosha dhidi ya mvua na jua, hali iliyowaathiri hasa watoto waliokuwa wakiishi katika mazingira hayo.
Aidha, Bi Ebby ameeleza kuwa licha ya mafanikio ya ujenzi huo, familia hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaisha. Alitoa shukrani kwa wadau wote waliosaidia kufanikisha ujenzi huo, wakiwemo kituo cha redio cha Jamii FM kilichopo Naliendele, Mtwara.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Tarafa wa Mayanga, Bw. Marco Mapunda, amewapongeza wote waliojitolea katika kusaidia familia hiyo na kusema kuwa kitendo hicho ni mfano bora wa mshikamano wa kijamii na namna viongozi wanavyoweza kuwa chachu ya maendeleo kwa watu wenye uhitaji.

Pia afisa tarafa ameahidi kuzibeba na kuzifanyia kazi changamoto zote zilizowasishwa kupitia risala iliyosomwa na afisa mtendaji wa Kijiji cha Nyengedi Bi Ebby Hamisi kwa kuziwasilisha katika ofisi ya mkuu wa wilaya na kuona namna ya kuisaidia familia hiyo
Kwa upande wake, Bi Lukia Mnyachi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyengedi, alielezea jinsi alivyoguswa na hali ya maisha ya Mzee Zomba na kuamua kuanzisha juhudi za kutafuta msaada ili kumjengea nyumba.

Mzee Salumu Zomba, akizungumza kwa furaha, ameshukuru kwa jitihada kubwa zilizofanywa na viongozi na wadau waliomsaidia kupata makazi bora. Hata hivyo, ametumia nafasi hiyo kuomba msaada zaidi wa vitanda, magodoro, na mahitaji ya watoto wake wanaosoma.

Majirani wa Mzee Zomba pia wameelezea hali ngumu ya maisha anayopitia, wakisisitiza kuwa kwa kuwa ni mlemavu wa macho, anahitaji msaada wa mara kwa mara kutoka kwa jamii na serikali.







No comments:
Post a Comment