Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Bi. Gemma Akilimali
Na Mwandishi wetu
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umekanusha vikali tuhuma za mitandaoni kuhusu uvunjifu wa kiuongozi na matumizi mabaya ya fedha, na umesisitiza kuwa uwajibikaji na uwazi ndio nguzo kuu za kazi zake.
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Bi. Gemma S. Akilimali, alisema hatua ya kuteua Kaimu Mkurugenzi Mtendaji imefanywa kwa mujibu wa Katiba ya TGNP ya mwaka 2021, Ibara ya 19 (viii).
“Uteuzi huu ulikuwa wa lazima ili kuhakikisha mwendelezo wa taasisi wakati mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya ukiendelea,” alisema Akilimali.
Akizungumzia madai ya ubadhirifu, aliongeza:“Tuhuma hizi hazina msingi wowote. TGNP ina mfumo madhubuti wa usimamizi wa fedha unaokaguliwa mara kwa mara na wakaguzi wa ndani na wa nje. Tunabaki thabiti katika uwazi na uwajibikaji.”
Pia alitoa onyo kwa wanaosambaza taarifa za kupotosha:“Tutachukua hatua za kisheria chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao kwa yeyote anayeeneza taarifa za uongo na za kashfa. Kazi ya TGNP inaendelea bila kusimama na hatutavunjwa moyo na upotoshaji.”
Licha ya upotoshaji huo, mafanikio ya TGNP yanaonekana kupitia zaidi ya Vituo 90 vya Taarifa na Maarifa (Knowledge Centres – KCs) vilivyoanzishwa katika zaidi ya halmashauri 80 nchini. Vituo hivi vimekuwa chachu ya kupunguza umasikini, kupambana na ukatili wa kijinsia (GBV), kuongeza uelewa wa sera, na kuwaunganisha wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye maamuzi ya maendeleo.
Amesisitiza kwamba, TGNP itaendelea kujenga uwezo kwa jamii kupitia mbinu shirikishi, na kuwajengea uwezo wananchi namna ya kuibua changamoto zao, na kuziwasilisha kwa viongozi na wafanya maamuzi ili wazifanyie kazi, lakini pia jamii ijitambue, itambue nafasi yao, na kushirikiana na uongozi ili wabadilishe mifumo kandamizi hasa ya mila na desturi na kuhakikisha rasilimali zinasogezwa karibu na wananchi kwa usawa bila ubaguzi wa kijinsia.
Bi. Akilimali alisema:“Uwajibikaji wa TGNP unadhihirika vijijini na mitaani — pale ambapo wanawake hawatembei tena kilomita nyingi kutafuta huduma za afya, pale watoto wanapopata elimu bora, na pale jamii inapopaza sauti kudai haki zao. Huo ndio ushahidi wa kweli wa TGNP.”
Kwa mujibu wa Bi. Sabina Mwaliego wa Kituo cha Mshewe, Mbeya DC:“Kupitia TGNP, huduma za afya ya mama zimeimarika Mshewe. Wanawake wanajifungua salama karibu na makazi yao. Mbinu ya ‘Triple A’, Kutathmini, Kuchambua na Kuchukua Hatua, imetusaidia kuibua changamoto na kusukuma mabadiliko. Viongozi wetu wametuelewa na wamechukua hatua”
Afisa wa Halmashauri ya Kishapu , ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema: “Ushirikiano na TGNP umetusaidia kupanga bajeti kwa kuzingatia sauti za wananchi, hususan wanawake na vijana. Huduma za maji, elimu na afya zimeboreshwa kutokana na ushirikishwaji huu, Mfano kata zetu tisa zimenufaika, Ukienda Kata ya Ukenyenge, Mondo, Kishapu, Kiloleli, Songwa utaona kazi za TGNP kwenye jamii.”
Mwanachama wa TGNP, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema:“Mbinu za uhamasishaji wa TGNP zinawafanya wananchi kuchukua hatua na kutumia rasilimali walizo nazo. Jamii zinakuwa na ujasiri wa kupinga ukatili na kudai mabadiliko.”
Ufanisi wa KCs umevutia hata Halmashauri ambazo hazipo moja kwa moja kwenye miradi ya TGNP. Baadhi, zikiwemo Mtwara DC, Mtwara MC, Lindi MC, Kisarawe DC, Ilala MC, Chalinze DC, Kibaha MC, Ruangwa DC na Nachingwea DC, zimeomba mwongozo kutoka TGNP ili kuanzisha KCs zao wenyewe baada ya kuona matokeo chanya kwa wenzao.
Zaidi ya kazi za ngazi ya jamii, TGNP imekuwa mshirika muhimu wa Serikali Kuu katika kusukuma mbele marekebisho ya sera na sheria zinazohusu afya, elimu na bajeti za kitaifa, kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika sera zote.