2 August 2025, 15:18 pm
![]() |
| Coletha Chiponde na Zaituni Selemani Namkola wakizungumza na Mwanaidi Kopakopa (hayupo pichani) Picha na mwandishi wetu |
Na Mwanaidi Kopakopa
Walizunguka kwa miguu, walikutana na wananchi, wakahamasisha, na walipambana kwa hali na mali kuhakikisha sauti ya mwanamke inasikika katika uongozi wa ngazi ya chini
Na Mwanaidi Kopakopa
Katika miaka ya karibuni, Tanzania imeanza kushuhudia mwamko mpya wa wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi, hasa kwenye siasa za mitaa. Katika mazingira ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitawaliwa na wanaume, wanawake sasa wanasimama kidete kudai nafasi zao za uongozi si kwa maneno tu, bali kwa vitendo.
Katika kona ya kusini mwa Tanzania, mabadiliko haya yanaanza kuchipua, si kwa baraka za kisiasa, bali kwa sauti zenye uthubutu na dhamira ya kweli kutoka kwa wanawake. Katika kata za Mkunwa na Libobe, wanawake wawili jasiri Coletha Chiponde na Zaituni Selemani Namkola waliamua kuvunja ukimya. Walichukua fomu na kujitokeza kuwania nafasi za udiwani katika kata zao. Walizunguka kwa miguu, walikutana na wananchi, wakahamasisha, na walipambana kwa hali na mali kuhakikisha sauti ya mwanamke inasikika katika uongozi wa ngazi ya chini.
Hata hivyo, licha ya jitihada kubwa walizofanya, majina yao hayakufanikiwa kupenya katika hatua ya kura za maoni. Lakini huu si mwisho wa safari. Ushiriki wao umeacha alama, umeleta majadiliano, umeibua matumaini mapya kwa wanawake na wasichana wengine katika jamii zao. Ni ushahidi wa wazi kuwa demokrasia ya kweli huanza kwa ujasiri wa mtu mmoja au wawili kusimama na kusema: “Naweza.”
Coletha na Zaituni wametoa mfano wa kuigwa. Safari yao ni mwanga kwa kizazi kijacho cha viongozi wanawake walioshikilia imani kuwa uongozi bora huanzia mtaani, kijijini, na katika vikao vya kata. Ni wajibu wa jamii sasa kuenzi jitihada hizi, kuunga mkono usawa wa kijinsia, na kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa ya kushiriki katika maamuzi yanayoathiri maisha yao ya kila siku.







No comments:
Post a Comment