
Wanachama zaidi ya 150 wa CCM Msimbati wamelalamikia kuondolewa kwa jina la Rashidi Linkoni aliyeshinda kura za maoni, wakitishia kurudisha kadi zao, huku viongozi wa wilaya wakisisitiza maamuzi ya kamati ya siasa
Na Musa Mtepa
Zaidi ya wanachama 150 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Msimbati, wilayani Mtwara Vijijini, wameonesha kutoridhishwa na kitendo cha kuondolewa jina la Rashidi Omari Linkoni, aliyeshinda kura za maoni kwa kura 116, na kurejeshwa jina la Abrehemani Hamisi aliyeshika nafasi ya pili kwa kura 101.
Wanachama hao, wakizungumza na Jamii FM Agosti 17, 2025, wamesema hatua hiyo ni dharau kwa maamuzi ya wajumbe na kutishia kurudisha kadi za chama.

Mzee Musa Ali maarufu kama Mzee Chituka, muasisi wa CCM kata ya Msimbati, amesema kitendo hicho kimekwenda kinyume na maamuzi ya wajumbe na akashauri uongozi wa wilaya kufika Msimbati kufanya mazungumzo na wanachama waliomchagua Linkoni.

Kwa upande wake, Salumu Uchumi, mwenyekiti wa CCM tawi la Liumo, alithibitisha kuwa hadi kufikia Agosti 17, zaidi ya wanachama 150 walikuwa tayari wamerudisha kadi zao za uanachama kutokana na uamuzi huo.
Rashidi Omari Linkoni, diwani mstaafu aliyeenguliwa licha ya kuongoza kura za maoni, amesema amepokea kwa namna yake maamuzi ya viongozi wa wilaya, lakini hana budi kuyakubali.

Naye Shahame Masudi Ahmadi, katibu wa CCM kata ya Msimbati, amekiri jina la Abrehemani Hamisi kurudi badala ya Linkoni na kueleza kuwa ni maamuzi ya Kamati ya Siasa ya Wilaya, huku akiwataka wanachama kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya viongozi wa juu.

Akizungumzia hali hiyo, Hamisi Wanyama, katibu wa siasa na uenezi CCM Mtwara Vijijini, amesema wajumbe walimteua Linkoni kwenye kura za maoni, lakini kamati ya siasa wilaya ina mamlaka ya kubadili jina endapo itaona inafaa. Aidha, ameongeza kuwa malalamiko ya wanachama ni ishara ya utovu wa nidhamu na kutoifuata itikadi ya chama.
Wanyama amebainisha kuwa taarifa za wanachama kurudisha kadi ameziona mitandaoni na hajapokea rasmi, lakini endapo zitafikishwa watazipokea, huku akiahidi kufika Msimbati kuzungumza na wanachama husika.







No comments:
Post a Comment