• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Waziri Chongolo afanya ziara ya kikazi Mtwara

 

Waziri wa kilimo Daniel Chongolo akiwa katika ofisi za bodi ya korosho baada ya kuwasili mkoani Mtwara Disemba 11,2025 tayari kwa ziara ya siku moja (Picha na Musa Mtepa)

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alifanya ziara ya kikazi Mtwara kufuatilia msimu wa korosho 2025/2026, kuhimiza ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kuanzisha teknolojia ya ndege nyuki kupulizia dawa, na kuagiza TARI-Naliendele kufanya utafiti wa changamoto za korosho kutokana na mvua na hali ya hewa

Na Musa Mtepa

Mtwara, Disemba 11, 2025 – Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika mkoa wa Mtwara ili kufuatilia na kuangalia mwenendo wa msimu wa korosho wa mwaka 2025/2026.

Akiwa katika ofisi za Bodi ya Korosho Tanzania, Waziri Chongolo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka nguvu kuhakikisha wakulima wanapata ruzuku ya pembejeo wanazotumia ili kurahisisha shughuli zao za kilimo.

Sauti ya 1 Daniel Chongolo Waziri wa kilimo

Aidha, ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Korosho kuanza kutumia teknolojia mpya ya upuliziaji dawa kwa ndege nyuki (mikorošoni), teknolojia itakayosaidia wakulima kuongeza tija na kulinda zao katika eneo zima la mkorosho.

Sauti ya 2 Daniel Chongolo Waziri wa kilimo

Vilevile, Waziri Chongolo ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI–Naliendele) kufanya utafiti juu ya changamoto mtambuka zinazotokea kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, hususan mvua zinazoathiri maua ya mikorosho na kusababisha kupukutika kwa zao.

Sauti ya  2 Danile Chongolo waziri wa Kilimo

Akizungumzia hali na mwenendo wa uzalishaji wa korosho nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho, Frances Alfred, amesema kuwa uzalishaji ni mzuri, na katika miaka mitano iliyopita umeongezeka kutokana na uwepo wa pembejeo za bure zinazotolewa kwa wakulima.

Sauti ya Frances Alfred Mkurugenzi mkuu wa CBT
Mkurugenzi wa CBT ndugu Frances Alfred akielezea hali na mwenendo wa zao la korosho kwa waziri wa kilimo jana Disemba 11,2025 (Picha na Musa Mtepa)
Share:

Wakulima wataka ufumbuzi utofauti bei ya korosho

 

Mwonekano wa korosho zikiwa zimehifadhiwa kwenye ghala tayari kusubiria kwenda sokoni(Picha na Musa Mtepa)

Wakulima wa korosho Nanyamba wamelalamikia tofauti kubwa ya bei ukilinganisha na Tandahimba, hali inayowalazimisha kuhamishia mazao yao Tandahimba

Na Musa Mtepa

Baadhi ya wakulima wa zao la korosho wamehoji juu ya utofauti wa bei ya korosho unaojitokeza sokoni kati ya Halmashauri ya Nanyamba na Wilaya ya Tandahimba, hali inayosababisha wakulima kutoka Nanyamba kuhamishia mazao yao Tandahimba ili kupata bei ya juu.

Malalamiko hayo yametolewa jana, Desemba 11, 2025, wakati wa ziara ya Waziri wa Kilimo, Ndugu Daniel Chongolo, ambapo wakulima wameeleza kuwa kwa takribani miaka 10 sasa bei ya korosho imekuwa hairidhishi, sambamba na kuwepo kwa tofauti kubwa ya bei kati ya Tandahimba na Nanyamba.

Wamesema kuwa licha ya madai ya kuwepo kwa unyevu kwenye korosho zinazouzwa Nanyamba, mazao hayo hayo yakiuzwa Tandahimba hununuliwa kwa bei ya juu.

Sauti ya baadhi ya wakulima wakiwasilisha changamoto zao kwa waziri wa kilimo

Akizungumzia changamoto zinazolikabili zao la korosho katika Halmashauri ya Nanyamba na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Mhe. Abdala Chikota, amesema Serikali imeamua kujenga kongani ya viwanda vya ubanguaji wa korosho ili kuongeza thamani ya zao hilo na kupunguza changamoto za bei pamoja na changamoto nyingine zinazowakabili wakulima.

Sauti ya Abdala Chikota Mbunge wa Nanyamba
Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdala Chikota akizungumzia hali ya zao la korosho katika jimbo hilo mbele ya waziri wa kilimo(Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema Nanyamba ni miongoni mwa halmashauri zinazozalisha korosho kwa wingi, hivyo ni wakati muafaka wa kuanza na kuendelea kujenga maghala makubwa yatakayosaidia kupanga na kupima viwango vya ubora wa korosho. Amesema hatua hiyo itamwezesha mnunuzi kutambua thamani ya korosho anayoenda kuinunua.

Sauti ya1 Daniel Chongolo waziri wa Kilimo
Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo akizungumza mara baada ya kutembelea Kongani ya viwanda iliyopo katika kijiji cha Maranje Halmashauri ya mji Nanyamba (Picha na Musa Mtepa)

Aidha, Mhe. Chongolo amesema ili kufikia dhamira ya mwaka 2030 ya kuhakikisha korosho zinazozalishwa nchini zinabanguliwa hapa hapa nchini, ni lazima kuonesha matokeo ya ujenzi wa viwanda hivyo ili kuongeza thamani ya zao hilo.

Sauti ya 2 Daniel Chongolo waziri wa Kilimo
Share:

Waziri wa Kilimo aagiza mazao yanayolimwa kusini yapitie bandari ya Mtwara

 

Waziri wa kilimo Daniel Chongolo akitoa agizo la mazao yanayolimwa mikoa ya kusini kupitia Banadari ya Mtwara.(Picha na Musa Mtepa)

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amemuagiza Mkurugenzi wa COPRA kuhakikisha mazao ya Ruvuma, Lindi na Mtwara yapitie Bandari ya Mtwara ili kuongeza tija, kurahisisha upakiaji na kuhakikisha fursa zinabaki kwa wakazi wa mikoa hiyo

Na Musa Mtepa

Waziri wa kilimo Mhe.Danieli Chongolo amemuagiza mkurugenzi wa COPRA  kusimamia mazao yote ya kibiashara yanayozalishwa katika mikoa mitatu ya Ruvuma,Lindi na Mtwara yapitie katika Bandari ya Mtwara ili kuongeza tija na kuwarahisishia wanunuzi  uhakika wa muda mfupi wa kusubirisha Meli,kupakia na kuondoa bidhaa.

Hayo amesema Disemba 11,2025 wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika mkoa wa Mtwara ambapo akiwa Bandari ya Mtwara amesema  kitendo hicho kitaifanya Bandari kufanyakazi muda wote na kusaidia kuongeza tija kwa Wanamtwara na taifa kwa ujumla.

Sauti ya 1 Daniel Chongolo Waziri wa Kilimo
Mizigo ya korosho ikipakiwa kwenye Meli tayari kusafirishwa kwenda nje ya nchi(Picha na Musa Mtepa)

Aidha Waziri Chongolo amesema kuwa lengo kuu sio kuzihamisha fursa kuzipeleka sehemu nyingine ni katika kuhakikisha zinabakia kwa wanamtwara,Lindi na vijana wanaozunguka ukanda wa kusini kujitafutia fedha kupitia bandari hiyo.

Sauti ya 2 Daniel Chongolo Waziri wa Kilimo

Kwa upande wake meneja wa Bandari ya Mtwara Ferdinandi Nyathi amesema hakuna haja ya kutoa Korosho kutoka mikoa ya kusini kwenda kusafirishia Dar es salaam kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vinavyoweza kufanyakazi kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa wakati.

Sauti ya Ferdinand Nyathi Meneja wa Bandari ya Mtwara.
Meneja wa Bndari ya Mtwara akitoa maelekezo kwa Waziri wa kilimo ya utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara katika msimu huu wa Korosho.(Picha na Musa Mtepa)

Hii ni ziara yake ya kwanza ya kikazi ya Waziri wa kilimo Mhe.Daniel Chongolo tangu alipoteuliwa na Mh. Rais ,ambapo alifanikiwa kutembelea katika ofisi za Bodi ya Korosho,Bandari ya Mtwara,kituo cha utafiti wa Kilimo cha TARI-Naliendele,Kongani ya Viwanda Maranje –Nanyamba Mtwara,Maghali ya kuhifadhiwa Korosho ,kituo cha wajasiliam mali wadogo wa ubanguaji Korosho Mahuta na kiwanda cha Kubangua Korosho cha TANECU kilichojengwa katika kijiji cha Mmova Kitangari Newala vijijini.

Share:

Wananchi kuchangia 2,000 kumleta mganga wa asili kijijini

 

Wananchi wa kitongoji cha Nunu wakiwa katika mkutano wa kujadili changamoto ya mlipuko wa moyo (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa Kitongoji cha Nunu, Msakala, wameamua kuchangia shilingi 2,000 kwa kila nyumba ili kumleta mganga wa jadi baada ya hofu ya “mlipuko wa ugonjwa wa moyo.” suluhisho

Na Musa Mtepa

Katika hali ya kushangaza, wananchi wa kitongoji cha Nunu kilichopo katika Kijiji cha Msakala, Kata ya Ziwani, Halmashauri ya Mtwara vijijini wamekubaliana kuchangia shilingi 2,000 kwa kila nyumba ili kufanikisha kuletwa kwa mganga wa asili (Jadi) atakayesaidia kutafuta na kutatua changamoto ya wananchi kukumbwa na kile wanachokieleza kuwa ni “mlipuko wa ugonjwa wa moyo.”

Wakizungumza katika mkutano wa kitongoji ulioitishwa Desemba 10, 2025 kwa lengo la kujadili namna ya kukabiliana na tatizo hilo, wananchi wamesema kuwa  hali hiyo imeleta taharuki kubwa na kuchochewa na imani za kishirikina kwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo.

Sauti ya Wananchi wa kitongoji cha Nunu

Cornel Caspari, ambaye ni muhanga na mkazi wa kitongoji hicho, amesema kijana wake alipokumbwa na tatizo hilo alianza kuhisi maumivu ya mwili na baadaye kupata matatizo ya moyo yaliyomsababisha kuanguka chini na baadae kuinuka na kuanza kukimbia kusikojulikana huku akitamka majina ya watu wasiojulikana ( kuweweseka).

Sauti ya Cornel Caspari Muhanga wa tukio

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nunu, Bw. Matias Poolu, amesema ukubwa wa changamoto hiyo ndiyo uliowalazimu kuitisha mkutano wa wananchi ili kujadili na kutafuta suluhisho, ambapo kwa kauli moja walikubaliana kuchangia shilingi 2,000 kwa kila nyumba.

Sauti ya Matias Pool Mwenyekiti wa kitongoji cha Nunu

Hamisi Salumu Namngwangula, Mwenyekiti wa kijiji cha Msakala ambacho kinahudumia Kitongoji cha Nunu, amekiri kuwepo kwa matukio ya wananchi kukumbwa na changamoto hiyo na kupongeza hatua ya wananchi kuitisha mkutano ili kujadiliana na kufikia muafaka.

Sauti ya Hamisi Namngwangula Mwenyekiti wa kijiji cha Msakala
Share:

Jamii yahimizwa kuepuka hisia katika kutatua migogoro

 

Afisa ufuatiliaji na tathmini kutoka shirika la TASA Hamisi Mwinshehe akiwa katika studio za Jamii fm Mtwara

Afisa wa TASA, imeitaka  jamii kutenga muda wa kufikiria na kutoa maamuzi sahihi katika kutatua migogoro, ikisisitiza kuepuka hisia na kutoegemea upande wowote

Na Musa Mtepa

Jamii imetakiwa kutenga muda wa kufikiria, kuchakata na kutoa maamuzi sahihi katika kutatua migogoro inayowakabili katika maeneo yao.

Hayo yamesemwa na Afisa Tathmini na ufuatiliaji kutoka shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Safety Alliance (TASA) linalofanya kazi katika Manispaa ya Mtwara–Mikindani, Hamisi Rashidi Mwinshekhe, kupitia kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na kituo cha redio cha Jamii FM Mtwara.

Amesema kuwa mgogoro ni hali ya kuwepo kwa mivutano ya kimawazo au kimtazamo, hivyo ni muhimu jamii kutenga muda wa kutosha wakati wa mchakato wa utatuzi ili kuhakikisha kila upande unaridhika na maamuzi yatakayofikiwa.

Sauti ya 1: Hamisi Mwinshekhe – Afisa Tathmini na Ufuatiliaji, TASA

Aidha, Mwinshekhe amesema kuwa kumekuwa na sababu mbalimbali zinazosababisha kuibuka kwa migogoro katika jamii, ambazo kwa namna moja au nyingine ni muhimu kuepukika ili kujenga jamii imara na yenye amani.

Sauti ya 2: Hamisi Mwinshekhe – Afisa Tathmini na Ufuatiliaji, TASA

Ameongeza kuwa kuna mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kutatua migogoro, ikiwemo kuepuka matumizi ya hisia, kuonesha huruma, pamoja na kutoegemea upande wowote katika mgogoro unaoendelea.

Sauti ya 3: Hamisi Mwinshekhe – Afisa Tathmini na Ufuatiliaji, TASA

Shirika la TASA kwa sasa linatekeleza mradi wa “Amani Yetu, Kesho Yetu” katika kata tano za Halmashauri ya Mtwara Vijijini, ambazo ni Nalingu, Madimba, Msimbati, Tangazo na Mahurunga.

Mradi huu unalenga kuelimisha jamii, hususan vijana, kuhusu athari za uvunjifu wa amani na umuhimu wa kudumisha utulivu katika maeneo yao.

Share:

Wakulima wa mwani Naumbu walia na soko

 

Mwonekano wa zao la Mwani likiwa limeanikwa baada ya kuvunwa kutoka shambani (Baharini) Picha na Musa Mtepa

Serikali imeombwa kuongeza wanunuzi wa zao la mwani ili kuboresha ushindani wa soko huku wakulima wakilalamikia bei ya shilingi 800 ambayo haiendani na gharama za uzalishaji na usafirishaji kutoka baharini

Na Musa Mtepa

Wakulima wa mwani kutoka Kijiji cha Naumbu, Kata ya Naumbu, Halmashauri ya Mtwara Vijijini wameiomba Serikali pamoja na wadau wa zao hilo kuhakikisha kunakuwepo na ongezeko la wanunuzi ili kuongeza ushindani wa soko.

Wakizungumza na Jamii FM Radio , wakulima hao wamesema kuwa bei ya mwani inayofikia shilingi 800 kwa kilo haiendani na gharama pamoja na mahitaji yao ukilinganisha na uzalishaji wanaoufanya.

Wamesisitiza kuwa ongezeko la wanunuzi litaongeza ushindani na hivyo kusaidia kupandisha bei ili waweze kunufaika zaidi na zao hilo.

Aidha, wameeleza kuwa ili kuzalisha na kufikisha mwani nchi kavu, hulazimika kugharamia usafirishaji kutoka baharini, hivyo kwa bei ya shilingi 800 kwa kilo hawawezi kupata kipato kinachokidhi mahitaji yao.

Sauti ya wakulima wa mwani Naumbu Kusini

Akizungumzia hali ya uzalishaji wa mwani katika kijiji hicho, mkulima Bi Bibie Ali Kitenge amesema kuwa wamekuwa wazalishaji wakubwa wa zao hilo, huku wakizalisha kila baada ya siku 45.

Sauti ya Bi Bibie Kitenge mkulima wa Mwani

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Naumbu Kusini, Bw. Selemani Shineni, amesema soko la mwani bado ni changamoto kubwa, hali inayosababisha kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wakulima wanaoomba watafutiwe soko lenye tija.

Sauti ya 1 – Selemani Shineni, Mwenyekiti Naumbu Kusini

Aidha, Shineni ameiomba halmashauri, kupitia maafisa uvuvi, kutowazuia wanunuzi wengine wanaojitokeza kununua mwani. Amesema kuwa kama kuna vigezo wanunuzi wanashindwa kuvifuata, wanapaswa kuelezwa ili wavifuate na hatimaye waweze kununua, jambo litakalowezesha wakulima kunufaika na zao lao.

Sauti ya 2 – Selemani Shineni, Mwenyekiti Naumbu Kusini
Share:

SDA yaadhimisha IDPWD kwa usafi wa mazingira

 

Shirika la SDA wakiwa pamoja na watu wenye ulemavu katika zoezi la usafi wa mazingira. Picha na Msafiri kipila

Ikiwa leo ni Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani, siku hii imeambatana na mabadiliko ya tabianchi na uwepo wa mabadiliko hayo kuna athari kwa watu wenye ulemavu.

Na Grace Hamisi

Shirika lisilo la kiserikali Sports Development Aids (SDA) kupitia mradi wake wa mazingira leo tarehe  03/12/2025, wameadhimisha siku ya watu wenye ulemavu duniani kwa kushirikiana na watu wenye ulemavu kufanya usafi eneo la fukwe ya bahari na kutoa elimu namna ya kutunza takataka mkoani Mtwara.

Akizungumza mkurugenzi wa shirika hilo Tea Swai, ameelezea namna walivyoshirikiana na watu wenye ulemavu kufanya usafi huo na kutoa elimu jinsi ya kutunza mazingira pamoja namna ya  kupunguza ukatili kwa watu wenye ulemavu.

Sauti ya Tea Swai – Mkurugenzi wa SDA

Nae Afisa afya Mazingira Salome Mayala, amepongeza kwa kile ambacho kimefanyika kwani kinahamasisha watu kuweza kutunza mazingira na kujikinga na madhara yanayopatikana kwa kuchafua mazingira.

Sauti ya Afisa afya Mazingira Salome Mayala

Kwa upande wake mtaalamu wa masuala ya walemavu na saikolojia, mwalimu Chris Mkwela amesema ikiwa leo ni siku ya watu wenye ulemavu imeambatana na mabadiriko ya tabia ya nchi na uwepo wa mabadiliko hayo kuna athari kwa watu wenye ulemavu kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la umoja wa mataifa ambalo linahusika kupunguza hatari na majanga.

Sauti ya mwalimu Chris Mkwela – mtaalamu wa masuala ya walemavu na saikolojia

Hata hivyo Amani Danfod Kazumari ambae ni mtu mwenye ulemavu ameshukuru shirika la SDA kwa kuwakutanisha pamoja na kufanya usafiri eneo la fukwe ya bahari ambapo alikuwa mazingira sio mazuri.

Sauti ya Amani Danfod Kazumari

Fatuma Mpondomoka mkazi wa likombe ameomba taasisi nyingine pia kuwaweka karibu watu wenye ulemavu katika shughuli mbalimbali ikiwemo siku hizi muhimu na kuwapa taarifa mapema ili wa wao waweze kujiandaa na kuonyesha vile ambavyo wanavifanya kwani wanaweza.

Sauti ya Fatuma Mpondomoka
Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>