
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alifanya ziara ya kikazi Mtwara kufuatilia msimu wa korosho 2025/2026, kuhimiza ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kuanzisha teknolojia ya ndege nyuki kupulizia dawa, na kuagiza TARI-Naliendele kufanya utafiti wa changamoto za korosho kutokana na mvua na hali ya hewa
Na Musa Mtepa
Mtwara, Disemba 11, 2025 – Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika mkoa wa Mtwara ili kufuatilia na kuangalia mwenendo wa msimu wa korosho wa mwaka 2025/2026.
Akiwa katika ofisi za Bodi ya Korosho Tanzania, Waziri Chongolo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka nguvu kuhakikisha wakulima wanapata ruzuku ya pembejeo wanazotumia ili kurahisisha shughuli zao za kilimo.
Aidha, ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Korosho kuanza kutumia teknolojia mpya ya upuliziaji dawa kwa ndege nyuki (mikorošoni), teknolojia itakayosaidia wakulima kuongeza tija na kulinda zao katika eneo zima la mkorosho.
Vilevile, Waziri Chongolo ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI–Naliendele) kufanya utafiti juu ya changamoto mtambuka zinazotokea kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, hususan mvua zinazoathiri maua ya mikorosho na kusababisha kupukutika kwa zao.
Akizungumzia hali na mwenendo wa uzalishaji wa korosho nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho, Frances Alfred, amesema kuwa uzalishaji ni mzuri, na katika miaka mitano iliyopita umeongezeka kutokana na uwepo wa pembejeo za bure zinazotolewa kwa wakulima.







No comments:
Post a Comment