• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

CUF yaahidi maendeleo kwa Wananchi wa kata ya Madimba

 

Mgombea Ubunge katika Jimbo la Mtwara Vijijini Kupitia tiketi ya CUF Shamsia Azizi Mtamba akinadi sera mbele ya wananchi wa kata ya Madimba(Picha na Musa Mtepa)

Mgombea Ubunge wa Mtwara Vijijini kupitia CUF, Shamsia Azizi Mtamba, amewataka wananchi wa Kata ya Madimba kuendelea kumuamini na kumpa kura, akiahidi kuendeleza maendeleo na kulinda kura zao dhidi ya propaganda za kisiasa

Na Musa MtepaMtwara–Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini anaetetea nafasi hiyo kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Shamsia Azizi Mtamba, amewaomba wananchi wa Kata ya Madimba kutokufanya kosa la kumchagua mgombea mwingine zaidi yake.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, Oktoba 27, 2025, katika Kijiji cha Madimba, Shamsia amewataka wananchi hao kuendelea kumuamini ili aweze kuendeleza juhudi za kuleta maendeleo katika kata hiyo.

Sauti ya Shamsia Mtamba, Mgombea Ubunge Jimbo la Mtwara Vijijini

Aidha, Shamsia ametumia nafasi hiyo kuwatoa hofu wananchi wa Madimba akisema kuwa amejipanga kulinda kura zake, huku akiwataka wananchi kupuuza propaganda zinazoenezwa na baadhi ya wanasiasa ya kuwa hata akishinda hatotangazwa.

Sauti ya Shamsia Mtamba, Mgombea Ubunge Jimbo la Mtwara Vijijini

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Madimba kupitia tiketi ya CUF, Bashiru Mchamba, amewaomba wananchi wampe kura ili aweze kushirikiana nao katika kuleta maendeleo na ustawi wa kata hiyo.

Sauti ya Bashiru Mchamba, Mgombea Udiwani Kata ya Madimba

Wakizungumza kuhusu mwenendo wa kampeni, baadhi ya wananchi wa Kata ya Madimba wamesema baadhi ya wagombea wameonyesha kugusa changamoto zinazowakabili, zikiwemo miundombinu ya barabara, huduma za afya, elimu na upatikanaji wa maji safi.

Sauti ya Wananchi wa Kata ya Madimba
Share:

Hospitali ya kanda yaibua furaha Mtwara

 

Mwonekano wa mbele wa Hospitali ya Rufaa kanda ya Kusini iliyojengwa kata ya Mitengo Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa Mtwara wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, hatua iliyowapunguzia gharama na safari za kwenda Dar es Salaam kutafuta huduma za kibingwa, huku wakiiomba serikali kuendelea kuboresha huduma hizo kwa manufaa ya wananchi wa kusini

Na Musa Mtepa

Wananchi mkoani Mtwara wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuboresha huduma za afya kupitia Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyojengwa katika Kata ya Mitengo, Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

Wakizungumza Oktoba 25, 2025, wananchi hao wamesema kuwa kabla ya kujengwa kwa hospitali hiyo, walilazimika kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kufuata huduma za kibingwa. Wameeleza kuwa kwa sasa wanapata huduma hizo karibu, jambo lililopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu na usafiri.

Aidha, wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, hatua inayowanufaisha wakazi wa mikoa ya kusini pamoja na wananchi wa nchi jirani kupata huduma bora katika hospitali hiyo.

Sauti ya Wananchi wa Mtwara

Bi Hawa Mpai na Bi Hajrati Kuluthumu Mtonya, ambao ni miongoni mwa wagonjwa wanaopata matibabu katika hospitali hiyo, wameeleza kuridhishwa kwao na huduma zinazotolewa huku wakiiomba serikali kuendelea kuimarisha huduma za kibingwa ili kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Sauti ya Bi Hawa Mpai na Bi Hajrati Kuluthumu

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Benedect Ngaiza, amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini ina madaktari bingwa na madaktari bingwa wabobezi pamoja na vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo vifaa vinavyopatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema kuwa upatikanaji wa huduma hizo umewezesha wananchi wa mikoa ya kusini kupata matibabu bora bila kulazimika kusafiri hadi Dar es Salaam.

Sauti ya Dkt. Benedect Ngaiza – Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
Chumba cha Dialysis kilichopo katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini (Picha na Musa Mtepa)
Share:

Dkt. Nanauka aahidi kuimarisha uchumi Mtwara

 

Mgombea Ubunge jimbo la Mtwara mjini Dkt Joel Nanauka akinadi sera zake mbele ya wananchi wa eneo la kokobichi ,kata ya Rahaleo Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Dkt. Joel Nanauka, mgombea ubunge Mtwara Mjini kwa tiketi ya CCM, ameahidi kuimarisha uchumi wa mji huo, kukuza ajira na kuwawezesha wajasiriamali endapo atachaguliwa. Pia amesisitiza utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa kushirikiana na Serikali

Na Musa Mtepa

Mtwara, Oktoba 20, 2025 – Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtwara Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Joel Nanauka, amewaahidi wananchi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge, atahakikisha anaweka kipaumbele katika kuimarisha uchumi wa mji huo ili kuongeza ajira na kipato kwa wakazi wake.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Kokobichi, Kata ya Rahaleo, Manispaa ya Mtwara Mikindani, Dkt. Nanauka amesema kuwa Ilani ya CCM inaelekeza utekelezaji wa miradi mikubwa inayotarajiwa kuifanya Mtwara kuwa kitovu cha uchumi wa ukanda wa kusini, na kusaidia hata nchi jirani kupitia huduma na bidhaa zitakazotokana na miradi hiyo.

Sauti ya Dkt. Joel Nanauka, mgombea ubunge Mtwara Mjini

Aidha, Dkt. Nanauka ameeleza kuwa akipewa dhamana ya kuwa Mbunge kwa miaka mitano ijayo, atahakikisha ofisi yake inakuwa na utaratibu maalum wa kuwawezesha wajasiriamali, hasa vijana na wanawake, kwa kuwapatia mafunzo, vifaa na elimu ya biashara ili kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.

Sauti ya Dkt. Joel Nanauka, mgombea ubunge Jimbo la Mtwara Mjini

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Rahaleo, Ndugu Edward Kapwapwa, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, bado kata hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo tatizo la mafuriko katika eneo la Nandope wakati wa masika, linalowasababishia wananchi usumbufu mkubwa.

Kapwapwa ameongeza kuwa tayari Serikali kupitia Manispaa ya Mtwara Mikindani imesaini mikataba ya TACTC kwa ajili ya ujenzi wa mifereji ya maji katika mitaa mbalimbali yenye changamoto, ikiwemo Nandope, ili kutatua tatizo hilo kwa njia ya kudumu.


Sauti ya Edward Kapwapwa, mgombea udiwani Kata ya Rahaleo

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mtwara, Ndugu Mohamedi Abdala (Mudy Ray), amewahakikishia wananchi kuwa Dkt. Nanauka ni kiongozi mwenye moyo wa unyenyekevu na atawajibika kwa bidii katika kuwahudumia wananchi wa Mtwara Mjini.

Sauti ya Mohamedi Abdala (Mudy Ray), Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Mkoa wa Mtwara
Mjumbe wa Halmashauri kuu CCM mkoa wa Mtwara Mohamed Abdala (Mudy Ray) akimnadi mgombea ubunge jimbo la Mtwara Mjini Dkt Joel Nanauka katika viwanja vya Kokobichi kata ya Rahaleo ,Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Katika hatua nyingine, baadhi ya vijana wa Mtwara Mjini wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi ili kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kwenda kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemwamini huku wakihimiza kuepuka upotoshaji unaosambazwa mitandaoni.

Sauti ya baadhi ya vijana wa Mtwara Mjini
Share:

CBT yatangaza ratiba rasmi ya minada ya Korosho 2025/2026

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania Brigadia Mstaafu Aloyce Mwanjile akizungumza na Waandishi wa habari Oktoba 18,2025 katika ofisi za kuu za Bodi ya Korosho mjini Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imetangaza kuwa minada ya korosho kwa msimu wa 2025/2026 itaanza Oktoba 31, 2025. Wakulima wametakiwa kuzingatia ubora wa korosho na kuepuka kuuza kwa kangomba, huku minada ikiendeshwa kwa njia ya mtandaoni chini ya usimamizi wa TMX

Na Musa Mtepa

Mtwara, Oktoba 18, 2025 — Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile, amesema kuwa msimu mpya wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2025/2026 unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 31 Oktoba 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 18 Oktoba 2025, Brigedia Jenerali Mwanjile amesema kuwa kwa mujibu wa historia ya misimu ya nyuma, minada ya korosho imekuwa ikianza katika wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba, kutokana na uwingi wa korosho na ukusanyaji wake kufikia hatua ya kuhifadhiwa ghalani.

Sauti ya 1 Brig. Aloyce Mwanjile mwenyekiti CBT

Aidha, ameongeza kuwa Bodi ya Korosho tayari imetoa ratiba ya minada kwa msimu huu, na kuwataka viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kuanza kupokea korosho za wakulima kuanzia tarehe 22 Oktoba 2025, kwa kuzingatia taratibu za ubora wa korosho kama ilivyoainishwa.

Sauti ya 2 Brig. Aloyce Mwanjile mwenyekiti CBT

Vilevile, Brigedia Mwanjile amewaonya wakulima dhidi ya kuuza korosho kwa wanunuzi wa mitaani maarufu kama kangomba, akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kinahatarisha maslahi ya mkulima mwenyewe.

Sauti ya 3 Brig. Aloyce Mwanjile mwenyekiti CBT

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Ndg. Frances Alfred, amesema kuwa msimu huu kutakuwa na usimamizi madhubuti kuanzia ngazi ya vyama vya msingi (AMCOS), ambapo vijana wa mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora watasimamia ubora na kiasi cha korosho zinazopelekwa kwenye maghala makuu.

Sauti ya Frances Alfred Mkurugenzi CBT
Mkurugenzi mkuu wa CBT ndug Frances Alfred akizungumza katika mkutano na waandishi habari uliofanyika Oktoba 18,2025 katika ofisi za bodi hiyo mjini Mtwara( picha na Musa Mtepa)

Katika kuhakikisha uwazi na ufanisi, msimu wa korosho wa mwaka 2025/2026 utaendelea kuendeshwa kwa mfumo wa minada ya mtandaoni chini ya usimamizi wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).

Share:

Wanasalamu Kanda ya Kusini wamsaidia mwenye ulemavu

 

Mwakilishi wa Wanasalamu Kanda ya Kusini akikabidhi godoro na daftari kwa Mzee Somba ikiwa ni mchango wa umoja huo (Picha na Musa Mtepa)

Wanasalamu Kanda ya Kusini kwa kushirikiana na Jamii FM wametoa msaada wa godoro na vifaa vya shule kwa Mzee Salumu Somba, mlemavu wa macho na mkazi wa Mnyengedi, baada ya kuguswa na hali yake kupitia kipindi cha Sikika. Wametoa wito kwa jamii kushirikiana kusaidia wenye uhitaji.

Na Musa Mtepa

Umoja wa Wanasalamu Kanda ya Kusini kwa kushirikiana na wadau wa Jamii FM Radio, leo Oktoba 15, 2025, wametoa msaada wa godoro na vifaa vya shule kwa familia ya Mzee Salumu Somba, mkazi wa Kijiji cha Mnyengedi,Mzee Somba ni mlemavu wa macho na anaishi katika mazingira ya kipato duni.

Akizungumza kwa niaba ya umoja huo wakati wa kukabidhi msaada, Bi Mwanahawa Nayopa (Mrs. Machela) amesema kuwa walipata taarifa za hali ngumu ya maisha ya Mzee Somba kupitia kipengele cha Sikika, kinachorushwa hewani na Jamii FM Radio kupitia kipindi cha Dira ya Asubuhi.

Kupitia taarifa hiyo, waliguswa na hali ya familia hiyo, hasa watoto wa Mzee Somba wanaosoma katika Shule ya Msingi Mwenge, na wakaamua kuchangishana fedha kwa ajili ya kununua godoro pamoja na vifaa vya shule.

Sauti ya Mwanahawa Nayopa – Mwakilishi wa Wanasalamu Kanda ya Kusini

Aidha, Bi Nayopa ameishukuru Jamii FM Radio kwa mchango wake mkubwa wa kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hususan watu wenye uhitaji maalum. Ametoa wito kwa jamii nzima kuendeleza moyo wa kusaidiana kwani kusaidia wenye uhitaji si jukumu la mtu mmoja bali ni la jamii nzima.

Sauti ya Mwanahawa Nayopa – Mwakilishi wa Wanasalamu Kanda ya Kusini

Kwa upande wake, Mzee Salumu Somba amewashukuru Wanasalamu kwa msaada waliompatia, huku akiwaombea baraka tele kutoka kwa Mungu huku akisema kuwa msaada huo umempa faraja kubwa na kuwaomba waendelee kuwa na moyo huo wa huruma kwa wengine wenye mahitaji kama yake au hata zaidi.

Sauti ya Mzee Salumu Somba – Mlemavu wa Macho

Naye Ebby Hamisi, Mtendaji wa Kijiji cha Mnyengedi, ametoa shukrani zake kwa Umoja wa Wanasalamu kanda ya kusini kwa kuguswa na hali ya Mzee Somba na kutoa rai kwao kwa kutokata tamaa kutokana na maneno ya kubezwa au kudhihakiwa, bali waendelee kufanya mema kwa jamii.

Sauti ya Ebby Hamisi – Mtendaji wa Kijiji cha Mnyengedi

Share:

Kijiji chaingiwa hofu ya ushirikina mkoani Mtwara

 

Kitu kinachodahniwa kuwa ni cha kishirikina kikiwa kimezungushiwa hirizi(Picha na Musa Mtepa)

Taharuki yatanda Magomeni Nyasi baada ya kugunduliwa kifaa kisichojulikana chenye hirizi, kinachodhaniwa kuhusika na imani za kishirikina. Wakazi wataka uchunguzi wa kina kufuatia ongezeko la matukio ya aina hiyo kijijini

Na Musa Mtepa

Mtwara –Wakazi wa kijiji cha Magomeni Nyasi, kilichopo kata ya Tangazo, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Oktoba 12,2025 wameamka na taharuki kubwa  baada ya kukutwa kwa kifaa kisichojulikana kilichozungushiwa hirizi, tukio linalodhaniwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Wakizungumza na Jamii FM, baadhi ya wananchi wameelezea mshangao wao juu ya tukio hilo, wakikitaja kuwa cha kutisha na kisicho cha kawaida.

Sauti ya wananchi wa kijiji cha Magomeni Nyasi

Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Alfani amedai kuwa tukio hilo lina uhusiano na ujio wa waganga wa kienyeji waliotembelea kijiji hicho siku za nyuma kwa lengo la kutoa uchawi.

Sauti ya Alfani, kijana mkazi wa Magomeni Nyasi

Mzee Abdala Yusuf Nammandila, ambaye ndiye mmiliki wa nyumba iliyokutwa na kifaa hicho chenye hirizi, amesimulia jinsi alivyokigundua na hatua alizochukua mara baada ya kukikuta.

Sauti ya Mzee Nammandila

Tukio hili limezua hofu miongoni mwa wakazi wa kijiji hicho, wengi wao wakitoa wito kwa mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio ya kishirikina ambayo yanaonekana kuongezeka kwa kasi maeneo ya vijijini.

Share:

Malezi duni yatajwa sababu ya mimba mashuleni Mtwara

 

Baadhi ya wananchi wa kata ya Naliendele wakishiriki mdahalo huo(Picha na Mohamed Masanga)

Mdahalo ulioandaliwa na Jamii FM umebainisha kuwa mimba mashuleni husababishwa na malezi duni, kutokuwepo kwa uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi, pamoja na ushiriki wa jamii hafifu katika kulinda watoto wa kike

Na Musa Mtepa

Inaelezwa kuwa ukosefu wa malezi na maandalizi bora kwa watoto kutoka kwa wazazi umeendelea kuwa moja ya sababu kuu zinazochangia wanafunzi wa kike kupata mimba wakiwa bado shuleni.

Hayo yamebainika katika mdahalo ulioandaliwa na Jamii FM Radio Oktoba 8, 2025, uliokuwa na kaulimbiu “Jamii Inashiriki Vipi Katika Kutokomeza Mimba Shuleni.

Maafisa usafirishaji (bodaboda) kutoka stendi ya Bajaji, kata ya Naliendele, wameeleza kuwa mimba nyingi zinazopatikana shuleni huchangiwa na wazazi kulega katika malezi, ikiwemo kuruhusu watoto kushiriki matukio ya usiku kama vile vigodoro, ambayo huwapeleka katika mazingira hatarishi.

Sauti ya maafisa usafirishaji – kata ya Naliendele

Hata hivyo, baadhi ya wazazi wamepinga kauli hiyo wakisema si wazazi wote huruhusu watoto wao kwenda kwenye vigodoro. Shaibu Abdala Kupela na Brandina Chilumba, ambao ni wazazi, wamesema kuwa kuna sababu nyingine nyingi zinazochangia mimba shuleni, ikiwemo wazazi kutengana bila sababu za msingi, hali inayosababisha watoto kukosa uangalizi wa kutosha.

Sauti za wazazi wakichangia mjadala

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pachoto “A”, Bw. Sadi Abdala Kombo, amesema kuwa ili kuondokana na tatizo la mimba mashuleni, ni lazima wazazi wasimame imara katika kulea watoto wao na kutambua wajibu wao kama walezi.

Sauti ya Sadi Kombo – 1 Mwenyekiti wa Mtaa wa Pachoto A

Aidha, Mwenyekiti huyo amesisitiza kuwa viongozi wa mitaa wana wajibu wa kukutana na wazazi mara kwa mara kwa ajili ya kujadiliana namna ya kuwasaidia watoto kuishi salama na kujitambua wakiwa shuleni.

Sauti ya Sadi Kombo – 2 Mwenyekiti wa Mtaa wa Pachoto A

Kwa upande mwingine, Judith Chitanda kutoka shirika la Nerio Paralegal pamoja na Sajenti Esta kutoka dawati la jinsia, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, wameitaka jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale mtoto anapopata ujauzito ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika na kusaidia kutokomeza mimba mashuleni.

Sauti ya Judith Chitanda na Sajent Esta – Dawati la Jinsia, Jeshi la Polisi
Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>