
Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imetangaza kuwa minada ya korosho kwa msimu wa 2025/2026 itaanza Oktoba 31, 2025. Wakulima wametakiwa kuzingatia ubora wa korosho na kuepuka kuuza kwa kangomba, huku minada ikiendeshwa kwa njia ya mtandaoni chini ya usimamizi wa TMX
Na Musa Mtepa
Mtwara, Oktoba 18, 2025 — Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile, amesema kuwa msimu mpya wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2025/2026 unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 31 Oktoba 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari tarehe 18 Oktoba 2025, Brigedia Jenerali Mwanjile amesema kuwa kwa mujibu wa historia ya misimu ya nyuma, minada ya korosho imekuwa ikianza katika wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba, kutokana na uwingi wa korosho na ukusanyaji wake kufikia hatua ya kuhifadhiwa ghalani.
Aidha, ameongeza kuwa Bodi ya Korosho tayari imetoa ratiba ya minada kwa msimu huu, na kuwataka viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kuanza kupokea korosho za wakulima kuanzia tarehe 22 Oktoba 2025, kwa kuzingatia taratibu za ubora wa korosho kama ilivyoainishwa.

Vilevile, Brigedia Mwanjile amewaonya wakulima dhidi ya kuuza korosho kwa wanunuzi wa mitaani maarufu kama kangomba, akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kinahatarisha maslahi ya mkulima mwenyewe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Ndg. Frances Alfred, amesema kuwa msimu huu kutakuwa na usimamizi madhubuti kuanzia ngazi ya vyama vya msingi (AMCOS), ambapo vijana wa mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora watasimamia ubora na kiasi cha korosho zinazopelekwa kwenye maghala makuu.

Katika kuhakikisha uwazi na ufanisi, msimu wa korosho wa mwaka 2025/2026 utaendelea kuendeshwa kwa mfumo wa minada ya mtandaoni chini ya usimamizi wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).






No comments:
Post a Comment