
Dkt. Joel Nanauka, mgombea ubunge Mtwara Mjini kwa tiketi ya CCM, ameahidi kuimarisha uchumi wa mji huo, kukuza ajira na kuwawezesha wajasiriamali endapo atachaguliwa. Pia amesisitiza utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa kushirikiana na Serikali
Na Musa Mtepa
Mtwara, Oktoba 20, 2025 – Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtwara Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Joel Nanauka, amewaahidi wananchi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge, atahakikisha anaweka kipaumbele katika kuimarisha uchumi wa mji huo ili kuongeza ajira na kipato kwa wakazi wake.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Kokobichi, Kata ya Rahaleo, Manispaa ya Mtwara Mikindani, Dkt. Nanauka amesema kuwa Ilani ya CCM inaelekeza utekelezaji wa miradi mikubwa inayotarajiwa kuifanya Mtwara kuwa kitovu cha uchumi wa ukanda wa kusini, na kusaidia hata nchi jirani kupitia huduma na bidhaa zitakazotokana na miradi hiyo.
Aidha, Dkt. Nanauka ameeleza kuwa akipewa dhamana ya kuwa Mbunge kwa miaka mitano ijayo, atahakikisha ofisi yake inakuwa na utaratibu maalum wa kuwawezesha wajasiriamali, hasa vijana na wanawake, kwa kuwapatia mafunzo, vifaa na elimu ya biashara ili kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Rahaleo, Ndugu Edward Kapwapwa, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, bado kata hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo tatizo la mafuriko katika eneo la Nandope wakati wa masika, linalowasababishia wananchi usumbufu mkubwa.
Kapwapwa ameongeza kuwa tayari Serikali kupitia Manispaa ya Mtwara Mikindani imesaini mikataba ya TACTC kwa ajili ya ujenzi wa mifereji ya maji katika mitaa mbalimbali yenye changamoto, ikiwemo Nandope, ili kutatua tatizo hilo kwa njia ya kudumu.
Sauti ya Edward Kapwapwa, mgombea udiwani Kata ya Rahaleo

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mtwara, Ndugu Mohamedi Abdala (Mudy Ray), amewahakikishia wananchi kuwa Dkt. Nanauka ni kiongozi mwenye moyo wa unyenyekevu na atawajibika kwa bidii katika kuwahudumia wananchi wa Mtwara Mjini.

Katika hatua nyingine, baadhi ya vijana wa Mtwara Mjini wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi ili kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kwenda kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemwamini huku wakihimiza kuepuka upotoshaji unaosambazwa mitandaoni.






No comments:
Post a Comment