Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja
Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao
Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii
Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm
Hali ya barabara ya Mtwara kuwelekea Dar es Salaam kabla ya kuharibika. Picha na Amua Rushita
“Tunatoa wito wa kuchukua hatua za pamoja, utunzaji wa miundombinu, kuboresha miundombinu, kuwahamisha watu kutoka maeneo hatarishi na kuimarisha elimu ya tabianchi“
Na Musa Mtepa,
Mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri maisha ya Watanzania, hasa katika mikoa ya Kusini kama Mtwara na Lindi, makala hii maalum inamulika madhara ya tabianchi ikiwemo mafuriko ya mara kwa mara, uharibifu wa makazi na kusimama kwa shughuli za kiuchumi na usafiri.
Kupitia ushuhuda wa wananchi na kauli za viongozi wa serikali, makala inaonyesha hatua zilizochukuliwa kama ujenzi wa madaraja makubwa lakini pia inaibua maswali kuhusu ufanisi wake wa muda mrefu. Je, tuna mikakati ya kweli ya kukabiliana na mabadiliko haya?
Tunatoa wito wa kuchukua hatua za pamoja, utunzaji wa miundombinu, kuboresha miundombinu, kuwahamisha watu kutoka maeneo hatarishi, na kuimarisha elimu ya tabianchi. Ustawi wa mikoa ya kusini na mustakabali wa taifa uko mikononi mwetu sote.
Mwonekano wa nje wa nyumba anayoishi mzee Salumu Somba mlemavu wa macho katika kijiji cha Nyengedi Mtwara Vijijini (Picha na Musa Mtepa)
Mzee Salumu Somba mkazi wa Mnyengedi, Mtwara, mlemavu wa macho, anaomba msaada wa makazi, mavazi, na mahitaji ya msingi kwa ajili ya familia yake kutokana na hali ngumu ya maisha.
Na Musa Mtepa
Mzee Salumu Somba, mkazi wa Kijiji cha Mnyengedi kata ya Mkunwa katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini, anaomba msaada kutoka kwa wadau na wasamaria wema ili apate makazi bora na mahitaji ya msingi ya kibinadamu.
Mzee Somba ni mlemavu wa macho ambaye anaeleza kuwa maisha anayopitia kwa sasa ni magumu mno kutokana na hali yake ya ulemavu, ukosefu wa makazi bora, mavazi na upatikanaji wa chakula cha uhakika kwa familia yake.
Sauti ya 1 mzee Salumu Somba Mlemavu wa macho
Mzee huyo mwenye mke mmoja na watoto wawili wanaosoma darasa la kwanza na la tatu, anasema kwa sasa nyumba yake imeharibika kiasi kwamba wakati wa mvua hunyeshewa akiwa ndani na familia yake, hali inayowaweka kwenye mazingira hatarishi kiafya na kimaisha.
Sauti ya 2 mzee Salumu Somba Mlemavu wa machoMzee Salumu Somba akiwa ameketi barazani mwa nyumba yake (Picha na Musa Mtepa0
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyengedi, Bi Lukia Mnyachi, amesema alifahamishwa kuhusu hali ya Mzee Somba na mwanakijiji mmoja. Baada ya kutembelea eneo analoishi mzee huyo na kujionea mazingira halisi, aliamua kuanzisha jitihada za kumsaidia.
Sauti ya 1 Lukia Mnyachi mwenyekiti wa Kijiji
Aidha Bi Lukia amesema baada ya kupata mchango kutoka kwa umoja wa wenyeviti akaanza mchakato rasmi wa kujenga nyumba kwa ajili ya Mzee Somba kwa kuendelea kushirikisha viongozi wengine wa juu ambao kwa namna moja au nyingine wameendelea kumuunga mkono katika kulifanikisha hilo.
Sauti ya 2 Lukia Mnyachi mwenyekiti wa Kijiji
Licha ya hatua hizo, bado kuna uhitaji mkubwa wa msaada zaidi kwa familia hiyo — hasa vifaa vya msingi kama kitanda, magodoro, mashuka na mavazi kwa watoto wake.
Sauti ya 3 Lukia Mnyachi mwenyekiti wa Kijiji
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamejitokeza kwa moyo mmoja kushiriki katika jitihada za kumjengea Mzee Somba banda la muda, huku wakiendelea kuomba msaada zaidi kutoka kwa wadau wa maendeleo na mashirika ya kijamii.
Sauti ya baadhi ya wananchi wa NyengediMwenyekiti wa kijiji cha Nyengedi Bi Lukia Mnyachi akiwa na mzee Salumu Somba mlemavu wa macho baada ya kutembelea nyumbani kwake(Picha na Musa Mtepa)
Kwa wale wanaotaka kuchangia au kumsaidia Mzee Somba na familia yake, wanaombwa kuwasiliana na uongozi wa Kijiji cha Mnyengedi au kupitia kituo cha Jamii FM Radio kwa maelekezo zaidi.
Mariamo Chibwalo (Pichani) akizungumza na Mwanaidi kopakopa (aliyeshika kinasa sauti) kuhusu kuwania nafasi ya uongozi katika kata ya Chuno iliyopo Mkoani Mtwara nchini Tanzania. Picha na Mpiga Picha wetu
Kata ya Chuno iliyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani yenye jumla ya watia nia 10 wanaowania nafasi ya udiwani, Mariam Chibwalo ndiye mwanamke pekee aliyejitokeza kuomba ridhaa ya chama.
Na Mwanaidi Kopakopa
Kujiamini na uzoefu katika siasa ni miongoni mwa silaha kuu anazozitumia Mariam Chibwalo, mkazi wa Kata ya Chuno katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara. Mariam ni mmoja wa watia nia kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo katika kata hiyo yenye jumla ya watia nia 10 wanaowania nafasi ya udiwani, yeye ndiye mwanamke pekee aliyejitokeza kuomba ridhaa ya chama.
Dhamira yake ni kutimiza ndoto na maono aliyojiwekea kwa ajili ya ustawi wa jamii yake, Kwa mujibu wa Mariam, moja ya ndoto zake ni kuiona Kata ya Chuno ikipiga hatua mpya katika nyanja mbalimbali hasa za uchumi, elimu na maendeleo ya kijamii yanayoonekana wazi.
Analenga kuhakikisha makundi ya wanawake na vijana yanashiriki kikamilifu katika maamuzi pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha hakuna kundi linalobaki nyuma katika safari ya maendeleo ya kata hiyo.
Mkurugenzi wa SDA Thea Swai akizungumza mbele ya washiriki wakati wa utambulisho wa mradi wa Girls Speak Out season three katika ukumbi TCIA mjini Mtwara (Picha na Mwanahamisi Chikambu)
Mradi wa Kuwawezesha Mabinti Kupaza Sauti umepongezwa kwa kuleta mabadiliko chanya kwa wasichana Mtwara kwa kuwaongezea ujasiri, sauti na ushiriki katika maamuzi muhimu. Awamu ya tatu imezinduliwa Julai 2025, ikilenga kufikia mabinti wengi zaidi na kushirikisha jamii kwa upana.
Na Mwanahamisi Chikambu
Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Fatma Mtanda, amepongeza Shirika la Maendeleo ya Michezo (SDA) kwa mchango wao kupitia mradi wa Kuwawezesha Mabinti Kupaza Sauti, unaolenga kuimarisha nafasi ya mtoto wa kike katika jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi huo uliofanyika leo Julai 23, 2025 kwenye ukumbi wa TCCIA, Bi. Mtanda amesema mradi huo umeleta mabadiliko chanya kwa mabinti kwa kuwajengea uwezo wa kujiamini, kujieleza na kushiriki kwenye maamuzi yanayohusu maisha yao.
Sauti ya Bi Fatma Mtanda Afisa Utamaduni Mkoa wa Mtwara
Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza jinsi elimu waliyoipata kupitia mradi huo ilivyowasaidia kuboresha mbinu za kushughulikia changamoto za kijinsia, hasa kwa wanafunzi wa kike. Wamesema mafunzo yamewasaidia kutambua njia bora za kuwasaidia wasichana kushinda vizingiti vya kijamii na kimfumo.
Sauti ya washiriki wa mafunzo
Kwa upande mwingine, baadhi ya makungwi walioshirikishwa katika utekelezaji wa mradi huo wameeleza namna walivyopokea elimu ya kutoa mafundisho chanya kwa mabinti, bila kuendeleza mila na desturi zinazowanyima haki au kuwawekea mipaka ya kimaendeleo.
Sauti ya Makungwi walioshiriki mafunzo hayo
Akizungumza kwa niaba ya SDA, Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Thea Swai ameeeleza kuwa awamu hii ya tatu ya mradi itatekelezwa kuanzia mwaka 2025 hadi 2028, ikiwa na lengo la kufikia mabinti wengi zaidi, kuongeza idadi ya walimu na watendaji wanaopatiwa mafunzo pamoja na kushirikisha makundi mbalimbali ya jamii katika kuwawezesha wasichana kupaza sauti zao.
Omari Bakari Hidobelele (35), mkazi wa Madangwa, Lindi, amekutwa amejinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali. Polisi wamesema marehemu alikuwa na msongo wa mawazo. Familia imeshangazwa na tukio hilo, ikieleza kuwa hakuwa na matatizo yoyote. Polisi wamehimiza jamii kusaidia wenye changamoto za afya ya akili
Na Musa Mtepa
Mtu mmoja aliefahamika kwa jina Omari Bakari Hidobelele(35) mkazi wa Kijiji Cha madangwa kata ya Sudi halmashauri ya Mtama mkoani Lindi amekutwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia mkanda wa suruali yake.
Akitihibitisha tukio hilo Daktari wa Zahanati ya kijiji cha Mtegu Jackine Joseph Sita amesema kwa mujibu wa vipimo vilivyofanyika inonekana kuwa na alama zinazo thibitisha kujinyonga kupitia kifo chake .
Sauti ya Jackline Joseph Sita Daktari wa Zahanati ya Mtegu
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Salumu Hassani Kuku, kijana huyo alitoweka tangu saa tatu asubuhi ya Julai 21, 2025. Jitihada za kumtafuta zilianza mara moja bila mafanikio hadi siku iliyofuata, Jumanne ya Julai 22, ambapo alikutwa akiwa amejinyonga kwenye mti wa mkorosho majira ya saa mbili asubuhi.
Sauti ya Salumu Hassani Kuku Mwenyekiti wa kijiji cha Madangwa
Bibi wa marehemu, Bi. Fatuma Ahmadi Liyai, amesema familia imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo, lakini wamelazimika kuikubali kama sehemu ya maisha.
Aidha, Bi. Fatuma amesema tangu Omari aliporejea kutoka Kilwa, hakuwa na matatizo yoyote wala migogoro na mtu yeyote, jambo linaloendelea kuwashangaza.
Sauti ya Bi Fatuma Liyai Bibi wa Marehemu
Kwa upande wake, Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa anapitia hali ya msongo wa mawazo kwa kipindi cha muda mrefu, jambo linalodhaniwa kuwa chanzo cha uamuzi huo wa kujiua.
Jeshi la Polisi pia limetoa wito kwa jamii kuhakikisha wanaimarisha usaidizi wa kisaikolojia kwa watu wanaoonesha dalili za msongo wa mawazo au matatizo ya afya ya akili, na kutoa taarifa mapema kwa wataalamu husika ili kusaidia kuzuia matukio ya aina hii.