• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Waziri wa Nishati ahimiza ushirikiano miradi ya CSR Mtwara

 

Power Plant ya kijiji cha Hiari ambapo Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi katika ziara yake alipata nafasi ya kutembelea na kujionea utendaji kazi wake(Picha na Musa Mtepa)

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ahimiza ushirikiano wa TPDC na viongozi wa Mtwara katika miradi ya CSR, huku akisisitiza ajira na uwezeshaji wa wananchi kwenye miradi ya gesi asilia

Na Musa Mtepa

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na kampuni zinazojihusisha na shughuli za gesi asilia mkoani Mtwara kushirikiana kwa karibu na viongozi wa maeneo husika wakati wa utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Ameyasema hayo Februari 27 na 28, 2026 alipokuwa katika ziara ya kikazi, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na viongozi wa vijiji, madiwani, wabunge na halmashauri ili miradi inayotekelezwa iendane na gharama halisi pamoja na thamani ya fedha inayowekezwa na Serikali.

Sauti ya Deogratius Ndejembi Waziri wa Nishati

Aidha, Mhe. Ndejembi ameagiza kuendelezwa kwa uwezo wa Watanzania, hususan wa maeneo yanayozunguka miradi ya gesi, ili waweze kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma hatua hiyo inayolenga kuongeza mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wa maeneo husika.

Sauti ya Deogratius Ndejembi Waziri wa Nishati

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya CSR, Mjiolojia Mwandamizi ambaye pia ni Meneja wa Mradi wa Utafutaji wa Mafuta na Gesi katika Kitalu cha Lindi–Mtwara, Shaidu Nuru, amesema kuwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo wamefanikiwa kurejesha faida kwa jamii kupitia miradi mbalimbali.

Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ununuzi wa mabati kwa ajili ya Soko la Kijiji cha Mkwajuni Juu, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya shule, uboreshaji wa barabara za kuunganisha vijiji, pamoja na kusaidia sekta ya afya katika maeneo yanayozunguka mradi.

Sauti ya Shaidu Nuru Meneja Mradi wa Utafutaji wa Gesi na Mafuta Kitalu cha Lindi–Mtwara

Shaidu Nuru amesema lengo kuu la mradi wa Lindi –Mtwara ni kutafuta rasilimali za mafuta na gesi asilia ili kuhakikisha taifa linakuwa na nishati ya kutosha, hatua itakayochochea maendeleo kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa mbali na manufaa ya moja kwa moja yatokanayo na upatikanaji wa nishati, pia kuna fursa mbalimbali kwa jamii zinazoguswa na mradi huo, ikiwemo ajira. Amesema waliendesha kampeni maalum kuhakikisha kazi zote zisizohitaji utaalamu wa hali ya juu zinafanywa na wakazi wa maeneo husika, kama ilivyotekelezwa wakati wa mradi huo.

Sauti ya Shaidu Nuru Meneja Mradi wa Utafutaji wa Gesi na Mafuta Kitalu cha Lindi–Mtwara

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Mhe. Arif Premji, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya gesi asilia mkoani Mtwara huku akibainisha kuwa miradi hiyo pamoja na ile ya CSR imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii na maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.

Sauti ya Arif Premji Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini

Share:

TAKUKURU Mtwara yadhibiti Milioni 15.3 za makato ya Korosho na ufuta

 

Kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara Mwanakombo Rajabu akitoa taarifa za mafanikio ya utendaji kazi kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2025 (Picha na Musa Mtepa)

TAKUKURU Mkoa wa Mtwara Region imedhibiti zaidi ya shilingi milioni 15.3 za makato ya korosho na ufuta, kupokea malalamiko 53 ya rushwa, na kusimamia marekebisho ya miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.03

Na Musa Mtepa

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) mkoa wa Mtwara imesaidia kurejesha na kudhibiti fedha zilizotokana na makato ya mauzo ya korosho na ufuta katika halmashauri tatu kati ya tisa zilizopo mkoani humu.

Akitoa taarifa ya mafanikio ya utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2025 kwa waandishi wa habari, Machi 3, 2026, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mwanakombo Rajabu, amesema kuwa zaidi ya shilingi milioni 15.3 zimedhibitiwa na kati ya fedha hizo, shilingi 11,896,000.00 zimerejeshwa katika Halmashauri ya Masasi, shilingi 2,571,500.00 Halmashauri ya Tandahimba, na shilingi 861,000.00 katika Halmashauri ya Newala.

Sauti ya Mwanakombo Rajabu Kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara

Aidha, katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Bi. Mwanakombo amesema TAKUKURU ilitoa mapendekezo ya kurekebisha mapungufu katika miradi minane yenye thamani ya jumla ya shilingi 2,035,825,000/=na kuelezea  kuwa mapungufu hayo yamerekebishwa kikamilifu baada ya taasisi hiyo kutembelea tena miradi husika kwa ajili ya uhakiki.

Sauti ya Mwanakombo Rajabu Kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara

Akizungumzia masuala ya uchunguzi na mashitaka kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Disemba pamoja na mikakati ya Januari hadi Machi, Bi. Mwanakombo amesema jumla ya malalamiko 53 yamepokelewa, ambapo 33 kati yake yanahusu tuhuma za rushwa na kubainisha kuwa uchunguzi wa malalamiko hayo unaendelea katika hatua mbalimbali.

Sauti ya Mwanakombo Rajabu kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara

Bi. Mwanakombo Rajabu ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa miradi ya serikali inayotekelezwa mkoani Mtwara, ikiwemo ujenzi wa stendi mpya ya mabasi ya Mkanaledi.

Sauti ya Mwanakombo Rajabu kaimu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara
Share:

CRDB Foundation na serikali yawawezesha vijana Mtwara

 

Pikipiki,Guta na Bajaji zilikabidhiwa March 2,2026 na waziri wa vijana Dkt Joel Nanauka kwa vijana 25 mkoani Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

CRDB Bank Foundation imekabidhi Pikipiki, Bajaji na Guta zenye thamani ya shilingi milioni 140 kwa vijana wa Mtwara, kuendeleza mikopo nafuu kwa ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Vijana

Na Musa Mtepa

Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, imekabidhi Pikipiki, Bajaji na Guta mkoani Mtwara ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mikopo inayotolewa kwa kushirikiana na wizara hiyo kwa vijana wa Kitanzania.

Akizungumza kuhusu mikopo hiyo Machi 2, 2026, Meneja Mwandamizi wa CRDB Bank Foundation anayesimamia mikopo yenye masharti nafuu ambaye pia ni msimamizi wa uhusiano na ubia na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, Baraka Kiyaro, amesema wamekabidhi Bajaji 5, Guta 5 na Pikipiki 15 zenye thamani ya shilingi milioni 140 kama sehemu ya mwendelezo wa mikopo inayotolewa kwa kushirikiana na Wizara ya Vijana.

Sauti ya Baraka Kiyaro Mwandamizi CRDB benk Foundation

Pamoja na hayo, Baraka Kiyaro amesema pia wameingia makubaliano na wizara mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu nchini. Amesema wanawasaidia kwa kuwajengea uwezo kupitia elimu ya fedha, kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali pamoja na kuwatafutia masoko ili kuwaondoa kwenye mikopo chechefu maarufu kama “kausha damu”.

Sauti ya Baraka Kiyaro Mwandamizi CRDB benk Foundation

Aidha, Baraka amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa vijana kujitokeza kupata mikopo hiyo, hali inayoonesha kuheshimu na kufurahia jitihada zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya vijana.

Sauti ya Baraka Kiyaro Mwandamizi CRDB benk Foundation

Naye meneja  CRDB kanda ya kusini, Emmanuel Biganio, amesema tangu kuanzishwa kwa CRDB Foundation mwaka 2023, imeweza kuwafikia vijana laki saba na ishirini (720,000), huku zaidi ya shilingi bilioni 20.1 zikitolewa kama mikopo na mitaji wezeshi. Amesema makubaliano na wizara ni kuongeza kasi zaidi katika utekelezaji wa malengo yaliyowekwa na Wizara ya Vijana.

Sauti ya Emmanuel Biganio meneja wa CRDB kanda ya kusini.

Mikopo hiyo imetolewa Machi 2, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) mkoa wa Mtwara uliofanyika katika Chuo cha Stella Maris Mtwara, ambapo zaidi ya vijana 25 wamenufaika na mikopo hiyo.

Share:

Vijana 25 Mtwara wapokea mikopo ya serikali

 

Baadhi ya pikipiki zilizotolewa kwa mkopo wa masharti nafuu kwa vijana 25 mkoani Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Zaidi ya vijana 25 Mtwara wamenufaika na mikopo nafuu, wakiwemo wapokeaji wa pikipiki, bajaji na guta, iliyokabidhiwa na Waziri wa Vijana kwa lengo la kukuza biashara na ajira

Na Musa Mtepa

Vijana 25 mkoani Mtwara wamenufaika na mikopo yenye masharti nafuu inayosimamiwa na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana. Mikopo hiyo imetolewa leo, March 2, 2026, na Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, baada ya kuzinduliwa kwa jukwaa la Vijana (Vijana Platform) mkoani Mtwara.

Waziri Nanauka amesema kuwa amewakabidhi vijana pikpiki 15, bajaji 5 na guta 5 vyenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 140, vyote ikiwa na bima zao, huku wakipewa muda wa miezi mitatu kuanza kulipa marejesho.

Sauti ya Dkt. Joel Nanauka, Waziri wa Vijana

Akizungumza kwa niaba ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dolnad Msengi, amewashauri vijana kuchangamkia fursa hiyo na kuachana na hoja za masharti magumu ya mikopo, huku akiunga mkono jitihada za Rais wa nchi katika kuwasaidia vijana kupata uchumi.

Sauti ya Dolnad Msengi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara

Katibu wa chama cha waendesha boda boda na bajaji mkoa wa Mtwara, Mshamu Ali, amesema kuwa hatua ya serikali kukopesha chombo baada ya fedha italeta tija kubwa kwa vijana ikilinganishwa na ukopeshaji wa fedha pekee.

Sauti ya Mshamu Ali, Katibu wa Dereva Boda Boda na Bajaji Mtwara

Vijana wanufaika wamesema wanashukuru kwa jitihada za serikali na kueleza kuwa mikopo hiyo itawasaidia kusogeza mbele maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Sauti ya vijana wanufaika na mikopo ya vijana
Share:

Waziri Nanauka azindua Jukwaa la vijana Mtwara

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Dkt. Joel Nanauka,akiwa katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha SAUT tawi la Mtwara tayari kwa uzinduzi wa jukwaa la vijana kwa mkoa wa Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Waziri  Nanauka amewahimiza vijana kujiandaa kuchangamkia fursa za maendeleo wakati wa uzinduzi wa Vijana Platform Mtwara

Na Musa Mtepa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Dkt. Joel Nanauka, amewataka vijana kuwa na maandalizi madhubuti ili kuchangamkia fursa zinazotolewa na wadau mbalimbali pamoja na wizara hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 2, 2026 wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) mkoani Mtwara, uliofanyika katika viwanja vya Chuo cha Stella Maris, Mtwara.

Waziri Nanauka amesema jukwaa hilo linalenga kufungua ndoto za vijana na kuwawezesha kuchangamkia fursa za maendeleo, akisisitiza kuwa maandalizi ni msingi wa mafanikio.

Sauti ya Dkt Joel Nanauka waziri wa vijana

Akizungumzia shilingi bilioni 200 zilizotolewa na serikali kwa Wizara ya Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya kusimamia mikopo ya vijana na wanawake, Waziri Nanauka amewataka vijana kufuatilia taarifa sahihi kupitia ngazi za kata hadi halmashauri ili kufahamu taratibu za mikopo hiyo.

Sauti ya Dkt Joel Nanauka waziri wa vijana

Aidha, Dkt. Nanauka amezielekeza halmashauri zote nchini kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele katika utoaji wa tenda za huduma mbalimbali za kiserikali, ikiwemo shughuli za Mwenge.

Sauti ya Dkt Joel Nanauka waziri wa vijana

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amesema mkoa umejipanga kuhakikisha vijana wanachangamkia fursa za kiuchumi zikiwemo kilimo, uchumi wa bluu na miradi mingine ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo.

Sauti ya Dolnad Msengi mkuu wa mkoa wa Mtwara
Share:

Trilioni moja kukuza gesi asilia Mtwara

 

Mtambo wa uchimbaji Gesi Ardhini ukifanyakazi katika kitalu cha Mnazi Bay Msimbati ikiwa miongoni mwa visima vitatu vinavyotarajiwa kuchimba katika eneo hilo(Picha na Musa Mtepa)

Serikali yawekeza zaidi ya trilioni moja kwenye miradi ya gesi Mtwara, ikilenga kuimarisha upatikanaji wa umeme na kukuza viwanda nchini

Na Musa Mtepa

Zidi ya shilingi trilioni moja za Kitanzania zimewekezwa katika sekta ya gesi asilia kupitia miradi ya uchimbaji katika visima vya Mnazi Bay, Ntorya pamoja na mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Ntorya hadi bomba kuu la Madimba, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.

Hayo yamesemwa Februari 27, 2026 na Waziri wa Nishati,  Mhe. Deogratius Ndejembi, alipofanya ziara na kuzindua uchimbaji wa kisima kipya cha gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay, kata ya Msimbati, wilayani na mkoani Mtwara.

Waziri Ndejembi amesema fedha hizo za Serikali, zaidi ya trilioni moja, zinalenga kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa umeme unaotokana na gesi pamoja na kukuza sekta ya viwanda na uzalishaji nchini.

Sauti ya Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Aidha, Waziri Ndejembi amesisitiza kuongeza kasi ya uchimbaji katika maeneo mengine ili vitalu vilivyopo vianze kuzalisha badala ya kubaki kwenye hatua za maandalizi pekee.

Sauti ya Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja Mradi Mhandisi Coletha Selsi amesema kitalu hicho kinatarajiwa kuongeza zaidi ya futi za ujazo milioni 55 za gesi asilia kwa siku.

Sauti ya Coletha Selsi, Mradi uchimbaji kitalu cha Mnazi Bay

Ameongeza kuwa katika kitalu hicho, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linamiliki asilimia 40 huku M & P ikimiliki asilimia 60. Makubaliano yao yanahusisha uchimbaji wa visima vitatu — viwili vya nyongeza na kimoja cha utafutaji katika shapu jipya la Kasa.

Sauti ya Coletha Selsi, Mradi uchimbaji kitalu cha Mnazi Bay

Ziara hiyo ya siku mbili ya Waziri Ndejembi mkoani Mtwara ilianza Februari 27 na kuhitimishwa Februari 28, 2026. Katika ziara hiyo, alizindua uchimbaji wa kitalu kipya cha Mnazi Bay, kuweka jiwe la msingi mradi wa bomba la gesi kutoka Ntorya kwenda bomba kuu la Madimba, pamoja na kutembelea mradi wa utafutaji wa vyanzo vipya vya gesi katika kijiji cha Hiari (Dangote), unaotekelezwa katika vijiji 40 vya mikoa ya Mtwara na Lindi.

Share:

Waziri Ndejembi ataka mradi wa Gesi Ntorya ukamilike kwa wakati

 

Picha na Mchoro wa mradi wa uchimbaji na ujenzi wa bomba la Gesi asilia kutoka Ntorya kuelekea Bomba kuu la Madimba (Picha na Musa Mtepa)

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi wa bomba la gesi Ntorya–Madimba ifikapo Septemba 2026

Na Musa Mtepa

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa uchimbaji na ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Ntorya kwenda Madimba mkoani Mtwara kukamilisha mradi huo kwa wakati, ili kuendana na mahitaji ya Watanzania.

Rai hiyo ameitoa Februari 27, 2026, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa uchimbaji na usambazaji wa bomba la gesi asilia uliofanyika katika eneo la Ntorya, lililopo kijiji cha Namahyakati Barabarani, kata ya Nanguruwe, mkoani Mtwara.

Ndejembi amesema lengo la wizara ni kuhakikisha kuwa ifikapo Septemba 2026, visima hivyo vinaanza kuzalisha gesi na kuungwa katika bomba kuu la Madimba. Amesisitiza kuwa mkandarasi hana budi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

Sauti ya Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Aidha, Ndejembi amesema ili kufanikisha hilo kunahitajika usimamizi wa hali ya juu kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kuwepo eneo la mradi muda wote, ili wakati utakapofika mradi huo uweze kuanza kama ilivyopangwa.

Sauti ya 2 Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Akizungumzia hali ya utekelezaji wa mradi huo, Mjiolojia Mwandamizi ambaye pia ni Meneja wa Mradi wa Ntorya kwa upande wa mkondo wa juu, Patrick Kabwe, amesema utekelezaji ulianza mwaka 2005 baada ya kusainiwa kwa mkataba kati ya TPDC, Ndovu Resources ya Uingereza pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa wakati huo.

Amesema mwaka 2010 walichimba kisima cha Ntorya namba moja na kufanikiwa kugundua gesi ambayo sasa inatarajiwa kuchimbwa na kuungwa katika bomba kuu la Madimba.

Sauti ya Patrick Kabwe, Meneja wa Mradi wa Ntorya

Akimkaribisha Waziri wa Nishati, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. James Mataragio, amesema kitalu cha gesi cha Ntorya ni kitalu kipya kitakachoongeza upatikanaji wa gesi, huku mahitaji yake yakiendelea kuongezeka siku hadi siku kutoka kwa wananchi.

Ameongeza kuwa Wizara ya Nishati kupitia TPDC imejipanga kuhakikisha inachimba na kuzalisha gesi ya kutosha kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kukidhi mahitaji ya viwanda na matumizi ya wananchi.

Sauti ya Dkt. James Mataragio, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati

Kukamilika kwa visima vitatu vya gesi vinavyochimbwa katika eneo la Ntorya — Ntorya namba moja, Ntorya namba mbili na Ntorya namba tatu — kunatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa takribani futi za ujazo milioni 60 kwa siku katika uzalishaji wa gesi nchini.

Baada ya uzinduzi huo, Waziri wa Nishati alitembelea eneo la Mnazi Bay, ambapo kuna uchimbaji wa kisima kipya ambacho kikikamilika kitaongeza takribani futi za ujazo milioni 45 za gesi asilia kwa siku. Kwa sasa, uzalishaji wa gesi kutoka Mnazi Bay ni takribani futi za ujazo milioni ni 90 – 100 za gesi asilia kwa siku (Million Standard Cubic Feet per Day) MMscf/d).

Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>