
TAKUKURU Mkoa wa Mtwara Region imedhibiti zaidi ya shilingi milioni 15.3 za makato ya korosho na ufuta, kupokea malalamiko 53 ya rushwa, na kusimamia marekebisho ya miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.03
Na Musa Mtepa
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mtwara imesaidia kurejesha na kudhibiti fedha zilizotokana na makato ya mauzo ya korosho na ufuta katika halmashauri tatu kati ya tisa zilizopo mkoani humu.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya utendaji kazi wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2025 kwa waandishi wa habari, Machi 3, 2026, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mwanakombo Rajabu, amesema kuwa zaidi ya shilingi milioni 15.3 zimedhibitiwa na kati ya fedha hizo, shilingi 11,896,000.00 zimerejeshwa katika Halmashauri ya Masasi, shilingi 2,571,500.00 Halmashauri ya Tandahimba, na shilingi 861,000.00 katika Halmashauri ya Newala.
Aidha, katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Bi. Mwanakombo amesema TAKUKURU ilitoa mapendekezo ya kurekebisha mapungufu katika miradi minane yenye thamani ya jumla ya shilingi 2,035,825,000/=na kuelezea kuwa mapungufu hayo yamerekebishwa kikamilifu baada ya taasisi hiyo kutembelea tena miradi husika kwa ajili ya uhakiki.

Akizungumzia masuala ya uchunguzi na mashitaka kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Disemba pamoja na mikakati ya Januari hadi Machi, Bi. Mwanakombo amesema jumla ya malalamiko 53 yamepokelewa, ambapo 33 kati yake yanahusu tuhuma za rushwa na kubainisha kuwa uchunguzi wa malalamiko hayo unaendelea katika hatua mbalimbali.
Bi. Mwanakombo Rajabu ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa miradi ya serikali inayotekelezwa mkoani Mtwara, ikiwemo ujenzi wa stendi mpya ya mabasi ya Mkanaledi.







No comments:
Post a Comment