
Watanzania wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, kuchagua viongozi watakaosimamia maendeleo ya taifa. Wito umetolewa na Nabii Nicolous Suguye wakati wa ziara yake kwenye vituo vya watoto wenye mahitaji maalum, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kulinda amani na kuchochea maendeleo ya jamii.
Na Musa Mtepa
Watanzania wamehimizwa kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025, kushiriki katika uchaguzi kwa ajili ya kuchagua viongozi watakaosimamia miradi ya maendeleo na maslahi ya wananchi na kuachana na dhana potofu ya kutoshiriki kupiga kura.
Wito huo umetolewa Oktoba 1, 2025, na kiongozi wa kiroho, Nabii Nicolous Suguye, alipotembelea kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalum cha Upendo pamoja na kitengo cha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia katika Shule ya Msingi Rahaleo.
Amesema kuwa, kama kiongozi wa kiroho na raia Tanzania, ana jukumu la kuhakikisha anachangia kulinda amani ya nchi yake.
Aidha, Nabii Suguye amesema kuwa uchaguzi huu ni Watanzania wote, hivyo kila mwenye sifa ya kupiga kura anapaswa kuwajibika kwa kuchagua viongozi bora watakaoweka vipaumbele kwenye miundombinu na huduma muhimu kwa jamii.
Katika hatua nyingine, Nabii Suguye ameeleza kuwa oparesheni yake iitwayo “Komboa Misukule” inalenga kuwaokoa watu kiakili, kihisia, kiafya na kiroho, kwani wengi wamepoteza dira na fursa muhimu za maisha kutokana na vifungo vya kiakili na kiroho.
Nabii Suguye anatarajia kufanya mkutano mkubwa wa injili kuanzia Oktoba 2 hadi Oktoba 6, 2025, katika viwanja vya Sabasaba, vilivyopo Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara ambapo katika mkutano huo, huduma mbalimbali za kiroho zinatarajiwa kutolewa kwa wananchi.






No comments:
Post a Comment