![]() |
| Amua Rushita akiendelea na mafunzo na Waandishi wa habari wa kituo cha Jamii fm redio yaliyofanyika leo August 15,2025 katika kituoni hapo (Picha na Musa Mtepa) |
Mafunzo kwa waandishi wa Jamii FM Redio yamewahimiza kuzingatia weledi, usalama kazini na kujikinga na uhalifu mtandaoni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025
Na Musa Mtepa
Waandishi wa habari wametakiwa kuwa makini na kuzingatia weledi wa taaluma yao, hususan kuelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 nchini.
Wito huo umetolewa leo, Agosti 15, 2025, na mkufunzi Amua Rushita wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa kituo cha Jamii FM Redio kuhusu ulinzi na usalama katika kipindi cha uchaguzi. Amesema kuwa waandishi wanapaswa kuchukua tahadhari wanapokuwa kazini ili kuepuka hatari zinazoweza kujitokeza.

Akifafanua, Amua amesema mafunzo hayo yamejikita katika maeneo matatu makuu: kuzingatia taratibu wakati wa kuhudhuria mikutano ya vyama vya siasa, kujikinga na uhalifu mtandaoni kupitia vifaa vya kidijitali, na kuimarisha ustawi wa kisaikolojia kwa waandishi wa habari wakiwa kazini.
Waandishi wa habari wa Jamii FM Redio, Shaibu Omari na Msafiri Kipila, wameeleza kufurahia mafunzo hayo, wakisema yamegusa moja kwa moja namna ya kuboresha usalama wao na kufuata taratibu sahihi wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Kwa upande wake, Mwanahamisi Chikambu, mwandishi wa habari wa kituo hicho, amesema ameongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuvaa mavazi yanayomtambulisha mwandishi wa habari, pamoja na kujitambulisha kwa viongozi wa usalama kwenye eneo la tukio ili kurahisisha utambuzi endapo changamoto itatokea

Mafunzo haya ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari ni sehemu ya mradi wa usalama wa mwandishi wa habari kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29,2025 nchini ambayo yanasimamiwa na umoja wa Klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC).







No comments:
Post a Comment