
“Hamisi Bakari anakiri kuwa changamoto kubwa anayokumbana nayo ni ukosefu wa eneo maalum la kufanyia biashara, kama angepata sehemu hiyo rasmi basi angeweza kupiga hatua zaidi za kimaendeleo kwa kuwa angeendesha biashara yake kwa utulivu na kujiimarisha zaidi kiuchumi”
Na Msafiri Kipila
Katika harakati za kujikwamua na umasikini, watu wenye ulemavu wameendelea kuonyesha juhudi na uthubutu mkubwa wa kushiriki katika shughuli za maendeleo kama walivyo watu wengine katika jamii. Licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili, bado wengi wao wamejiajiri na kufanya biashara ndogondogo ili kujitegemea kiuchumi na kuondoa dhana potofu kuwa ulemavu ni mwisho wa uwezo wa mtu.
Hamisi Mshamu Bakari ni miongoni mwa watu hao. Ni mlemavu wa mguu ambaye amejikita katika biashara ya kuuza viatu na nguo za mtumba kwa zaidi ya miaka 20. Akiwa na azma ya kubadili maisha yake, Hamisi hutembea umbali mrefu kila siku kutoka Mtawanya Juu hadi Magomeni, ambako huchukua bidhaa zake kabla ya kuzitembeza mitaani kwa ajili ya kuziuza. Safari hizo ndefu, licha ya hali yake ya ulemavu, zinadhihirisha kiwango kikubwa cha uvumilivu, bidii na kujituma alichonacho.

Hata hivyo, Hamisi anakiri kuwa changamoto kubwa anayokumbana nayo ni ukosefu wa eneo maalumu la kufanyia biashara. Anasema kama angepata sehemu hiyo rasmi, basi angeweza kupiga hatua zaidi za kimaendeleo kwa kuwa angeendesha biashara yake kwa utulivu na kujiimarisha zaidi kiuchumi. Anaeleza kuwa msaada wa aina hiyo ungekuwa chachu kubwa ya mafanikio kwa watu wenye ulemavu, ambao mara nyingi hukosa fursa za msingi zinazoweza kuwainua kiuchumi.
Kupitia simulizi hii, jamii inapaswa kutambua kuwa watu wenye ulemavu hawahitaji huruma, bali wanahitaji fursa, mazingira rafiki na msaada wa kweli utakaowawezesha kujitegemea. Kama jamii itawekeza kwao, kwa kuwapatia maeneo ya biashara, mikopo au mafunzo ya ujasiriamali, basi watakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa letu. Kisa cha Hamisi kinatoa somo la matumaini, lakini pia changamoto inayohitaji hatua za haraka.






No comments:
Post a Comment