• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Wananchi walia na uchakavu wa Madarasa shule ya Msingi Mnyahi

 

Mwonekano wa ndani wa baadhi ya madarasa ya shule ya msingi Mnyahi iliyopo halmashauri ya mji Nanyamba mkoani Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa Mnyahi, Mtwara, wailalamikia Shule ya Msingi Mnyahi kuwa na majengo chakavu, wanafunzi kunyeshewa darasani,Wadai imepuuzwa licha ya ufaulu mzuri, viongozi waahidi hatua za ukarabati

Na Musa Mtepa

Wananchi wa Kijiji cha Mnyahi, kata ya Milangominne Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara, wameiomba serikali kuangalia kwa jicho la tatu hali ya Shule ya Msingi Mnyahi kufuatia uchakavu wa majengo ya shule hiyo.Hali hiyo imeelezwa kusababisha wanafunzi kunyeshewa na mvua wakiwa darasani.

Wakizungumza na Jamii FM Radio Machi 28, 2026, wananchi hao wamesema licha ya shule hiyo kufanya vizuri kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo katika mitihani ya Darasa la Saba, bado haijapatiwa ukarabati wala ujenzi wa majengo mapya.

Aidha, wameeleza kuwa shule hiyo imejengwa mwaka 1973, na mara ya mwisho kupata majengo mapya ilikuwa wakati wa utawala wa hayati Rais Benjamin Mkapa.

Sauti ya 1 Wananchi wa Mnyahi

Mkazi wa kijiji hicho, Abdulaaziz Bushiri Mjupa, amesema kutokana na serikali kutoipa kipaumbele shule hiyo katika ukarabati na ujenzi wa majengo, wananchi wamelazimika kuchangishana ili kupunguza baadhi ya changamoto, ikiwemo ujenzi wa matundu ya vyoo hali ambayo ni tofauti na ilivyo katika shule za vijiji jirani.

Sauti ya Abdulaaziz Bushiri mkazi wa Kijiji cha Mnyahi

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamisi Salumu Mpangu, amekiri kuwepo kwa majengo yanayohitaji ukarabati mkubwa kutokana na uchakavu uliopitiliza.

Amesema tayari amewasilisha taarifa za hali hiyo katika vikao vya maendeleo ya kata zaidi ya mara tatu bila mafanikio yoyote.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa halmashauri kufika kijijini hapo kujionea hali halisi na kuchukua hatua za haraka.

Sauti ya Hamisi Mpangu mwenyekiti wa Kijiji Mnyahi

Naye Diwani wa Kata ya Milangominne, Mhe. Sharifu Kapela, amesema kata hiyo ina shule mbili zenye changamoto ya majengo chakavu zinazohitaji ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya.

Amezitaja shule hizo kuwa ni Milangominne na Mnyahi, akibainisha kuwa tayari ameshawasilisha suala hilo halmashauri na ameahidiwa kuwa litafanyiwa kazi kuanzia mwezi Agosti.

Pia ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kujitokeza kusaidia kuboresha miundombinu ya shule hizo.

Sauti ya Mhe. Sharifu Kapela Diwani wa kata ya Milangominne

Akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Hassani Ali Mauji, amekiri kuwepo kwa shule chakavu katika halmashauri hiyo.

Amesema shule hiyo imeingizwa katika mpango wa BOOST unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka wa fedha wa serikali.

Sauti ya Hassani Ali Mauji mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Nanyamba

Share:

Daraja lakatika, Namuhi, Mnyija wakosa mawasiliano

 

Mwonekano wa Daraja baada ya maji yanayotokea Bwawa la kitere kupitia mto Mambi kulivunja na wananchi kuunganisha kwa kutumia miti (Picha na Salamu Nayaula)

Na Musa Mtepa

Wananchi wa vijiji vya Namuhi na Mnyija wamejikuta katika wakati mgumu wa mawasiliano kufuatia kukatika kwa daraja linalounganisha vijiji hivyo, baada ya kufurika kwa maji yanayotoka Bwawa la Kitere kupitia Mto Mambi unaotenganisha maeneo hayo.

Wakizungumza na Jamii FM Radio Machi 28, 2026, wananchi hao wamesema kuwa uharibifu huo umetokana na maji mengi kufurika kutoka Bwawa la Kitere, hali ambayo imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii, ikiwemo kilimo, usafirishaji pamoja na elimu.

Aidha, wameeleza kuwa kutokana na ulazima wa kuvuka katika eneo hilo, wamelazimika kuweka miti juu ya mto huo ili iwe njia ya kupita, jambo linalohatarisha usalama wao.

Sauti ya 1 Wananchi wa Mnyija

Hata hivyo, wananchi hao wameiomba serikali kufika katika eneo hilo kujionea hali halisi na kutatua changamoto hiyo ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kujitokeza.

Sauti ya 2 Wananchi wa Mnyija

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Namuhi, Mwenyekiti wa kitongoji katika eneo lilipo daraja lililokatika, Bi. Suluhisho Nammanga, amesema athari zinazotokana na hali hiyo ni pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Namuhi na Shule ya Sekondari Libobe kushindwa kuhudhuria masomo. Pia, baadhi ya wakulima wameshindwa kufika mashambani kwa kuwa mashamba yao yapo upande wa pili wa mto.

Sauti ya Bi Suluhisho Nammanga kaimu mwenyekiti

Aidha, Bi. Suluhisho ametoa wito kwa serikali kutembelea eneo hilo na kuona umuhimu wa kujenga daraja hilo kwa haraka ili huduma muhimu kwa wananchi ziweze kuendelea kama kawaida.

Pia ameishauri serikali kwamba daraja litakapojengwa liwe refu zaidi kuliko lilivyokuwa awali, na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa kazi ya mkandarasi inakidhi matakwa ya mkataba husika wakati wa ukaguzi na makabidhiano.

Sauti ya Bi Suluhisho Nammanga kaimu mwenyekiti
Share:

Panda shuka za Mariam kuitumikia Chuno

 

Mariam Chibwalo akizungumza na muandaaji wa makala haya, Picha na Mwanaidi Kopakopa

Je, viongozi huzaliwa au hutengenezwa na mazingira? Makala hii inachunguza mjadala huo kupitia Mariam Chibwalo, mwanamke aliyethubutu kusimama pekee yake dhidi ya wanaume tisa katika kinyang’anyiro cha udiwani. Akiwa amesukumwa na changamoto na hamasa ya kuwa sauti ya wananchi wa Chuno, Mariam anaonesha kuwa uongozi si ndoto tu bali ni uamuzi wa kusimama na kuwatumikia wengine.

Na Mwanahamisi Chikambu na Mwanaidi Kopakopa.

Nadharia za uongozi duniani zimegawanyika katika makundi mawili makuu. Kuna wanaoamini kuwa viongozi huzaliwa na wengine wanaosisitiza kuwa viongozi hutengenezwa na mazingira au matukio wanayokutana nayo maishani.

Wanaodai viongozi huzaliwa huamini kuwa kipaji cha kuongoza kimo ndani ya damu ya mtu tangu kuzaliwa. Kwa upande mwingine, wanaoamini kuwa mazingira humjenga kiongozi wanasema kuwa changamoto, kero na dhuluma ndizo humsukuma mtu kusimama kidete na kusema ”Sasa basi, mimi nitakuwa sauti ya wenzangu”.

Safari ya uongozi wa Mariam Chibwalo haikuwa nyepesi. Katika kinyang’anyiro cha udiwani, alijitosa akiwa mwanamke pekee akishindana na wanaume tisa. Wengi waliutafsiri ujasiri wake kama ndoto isiyowezekana, lakini kwake yeye, haikuwa tu siasa bali ilikuwa ni wito wa dhati wa kuwatumikia wananchi wa Chuno.

Karibu usikilize makala hii ya kusisimua… Bonyeza hapa.

Share:

TMA yasisitiza wakulima kutumia vizuri mvua zinazonyesha

 

Kaimu meneja TMA kanda ya kusini Elewa Msomba akiwa katika mahojiano kwenye kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wamehimizwa kutumia vizuri mvua zinazonyesha kwa shughuli za maendeleo huku wakitakiwa kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa wataalam wa hali ya hewa na kilimo ili kupata tija

Na Musa Mtepa

Wananchi wameshauriwa kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo yao kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo, zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, ili kuwawezesha kupata tija.

Hayo yamesemwa Machi 23, 2026 na Kaimu Meneja wa TMA Kanda ya Kusini, Bw. Elewa Msomba, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio. Amesema kuwa kwa kuwa msimu wa mvua unaelekea mwishoni katika ukanda wa kusini, wananchi hawana budi kuzitumia ipasavyo ili kupata manufaa katika shughuli zao.

Sauti ya 1 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Aidha, Bw. Elewa Msomba amesema kuwa pamoja na msimu wa mvua kuelekea ukingoni katika ukanda wa kusini, hasa kwa wanaoishi maeneo ya bondeni na yenye unyevunyevu, wanapaswa kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kipindi hiki cha mwezi wa tatu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Sauti ya 2 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi kutoka Kituo cha Hali ya Hewa kilichopo katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI–Naliendele, Renatus Kapenda, amewataka wakulima kulima mazao kwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na TMA pamoja na ushauri wa wataalam wa kilimo waliopo katika maeneo yao, ili waweze kulima mazao yanayoendana na msimu husika.

Sauti ya 1 Renatus Kapenda Afisa TMA TARI–Naliendele

Sambamba na hilo, Renatus Kapenda amewataka wakulima kutambua kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili na mwanzoni mwa mwezi Mei. Hivyo, ni muhimu kwa wakulima kuzingatia ushauri na kushirikiana na wataalamu wa kilimo ili kuelekezwa mbegu zinazofaa kulingana na kiasi cha mvua kilichobaki.

Sauti ya 2 Renatus Kapenda Afisa TMA TARI–Naliendele
Afisa mfawidhi kutoka kituo cha hali ya hewa katika kituo cha utafiti wa kilimo Tanzania TARI-Naliendele Renatus Kapenda akiwa katika studio za jamii fm radio (Picha na Musa Mtepa)

Kwa mujibu wa TMA, msimu wa mvua kwa mikoa ya kusini ulianza mwezi Disemba 2025 na unatarajiwa kumalizika katika wiki ya nne ya mwezi Aprili hadi wiki ya kwanza ya mwezi Mei, huku mvua hizo zikiwa chini ya wastani kulingana na rekodi za mvua katika mikoa hiyo.

Sauti ya 3 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Kusikiliza kipindi Bonyeza hapa

Share:

Sekondari Naliendele na siku ya hali ya hewa duniani

 

Wanafunzi wa shule ya sekondari Naliendele wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka TMA kanda ya kusini (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wamehimizwa kuzingatia taarifa za hali ya hewa kutoka TMA ili kuboresha shughuli zao. Elimu imetolewa kwa wanafunzi Naliendele, wakihamasishwa kuwa mabalozi wa taarifa hizo kwa familia na jamii.

Na Musa Mtepa

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Kanda ya Kusini imeadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani katika Shule ya Sekondari Naliendele, huku ikiwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka hiyo ili kufanikisha shughuli zao za kila siku.

Wito huo umetolewa leo Machi 23, 2026 na Tamimu Masai, afisa wa TMA Kanda ya Kusini, wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kikanda katika shule hiyo. Amesema lengo la maadhimisho ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa hali ya hewa, ili waweze kufikisha ujumbe huo katika familia zao.

Tamimu amesema wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuzitumia ipasavyo, kwa kuwa zinamhusu kila mtu na kila shughuli ya maisha ya kila siku.

Sauti ya Tamimu Masai afisa wa TMA Kanda ya Kusini

Aidha, amesema kuchagua Shule ya Sekondari Naliendele kumechangiwa na nia ya kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, pamoja na kuwaandaa kuwa mabalozi wa kueneza ujumbe wa umuhimu wa kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

Sauti ya Tamimu Masai afisa wa TMA Kanda ya Kusini

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameeleza kufurahishwa na maadhimisho hayo, wakisema yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu hali ya hewa huku wakiwataka wazazi na wakulima kuzingatia taarifa zinazotolewa na wataalamu wa TMA kupitia vyombo vya habari.

Sauti ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Naliendele
Share:

TAKUKURU Mtwara yaandaa Iftar kuimarisha ushirikiano na Jamii

 

Baadhi ya washiriki wa Iftar iliyoandaliwa na TAKUKURU mkoa wa Mtwara wakiwa katika ukumbi uliondaliwa iftar hiyo(Picha na Musa Mtepa)

TAKUKURU Mtwara yaandaa Iftar kuimarisha uhusiano na jamii, viongozi wakisisitiza umoja, mshikamano na ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa wakati wa mwezi wa Ramadhani

Na Musa Mtepa

Ikiwa katika juhudi za kuimarisha uhusiano na utendaji wake pamoja na jamii inayoizunguka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara imejumuika na makundi mbalimbali katika kuandaa Iftar, huku ujumbe wa umoja na mshikamano ukitawala katika hafla hiyo.

Hafla hiyo iliyowakutanisha viongozi na wananchi wa kada mbalimbali imefanyika Machi 17, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin Mkapa uliopo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (tawi la Mtwara), zamani Chuo cha Ualimu (TTC).

Akizungumza katika Iftar hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara, Wakili Richard Mwalingo, amewakumbusha wananchi umuhimu wa kuchukia vitendo vya rushwa na kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vya vitendo hivyo na kusisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni silaha muhimu katika vita dhidi ya rushwa.

Sauti ya Richard Mwalingo Katibu Tawala Wilaya ya Mtwara

Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mashauri Elisante, amewashukuru wote waliojitokeza, akisema kuwa hafla hiyo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya TAKUKURU na jamii, kwani taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii katika utekelezaji wa majukumu yake.

Sauti ya Mashauri Elisante Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Mtwara, ambaye pia ni Askofu na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki, Yeriko Nguema, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania bila kujali rangi, kabila au imani ya mtu.

Sauti ya Askofu, Mchungaji Yeriko Nguema

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Sheikh Jamaldin Chamwi, amesema huruma, upendo na mshikamano ndivyo vinavyoimarisha misingi mikuu ya mwezi wa Ramadhani na kuongeza kuwa miongoni mwa mambo yanayokamilisha saumu ni pamoja na kufuturisha, kama ambavyo TAKUKURU imefanya.

Sauti ya Sheikh Jamaldin Chamwi, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
Share:

Jamii Africa yawajengea uwezo Waandishi wa habari Mtwara

 

Waandishi wa habari wakiwa katika mafunzo ya utambuzi na uthibitishaji wa taarifa yaliyotolewa na Jamii Africa yaliyofanyika March 17,2026 mjini Mtwara(Picha na Hery Abdala)

Waandishi wa habari 25 mkoani Mtwara wamepata mafunzo ya uhakiki wa taarifa kutoka Jamii Africa, yakilenga kuwasaidia kutambua taarifa sahihi na potofu ili kuboresha utoaji wa habari kwa wananchi

Na Musa Mtepa

Jumla ya waandishi wa habari 25 kutoka vyombo mbalimbali mkoani Mtwara wamepatiwa mafunzo ya uhakiki na uthibitishaji wa taarifa, yaliyotolewa na Jamii Africa chini ya taasisi mama ya Jamii Forums, kwa lengo la kuwawezesha kutambua taarifa potofu na zisizo sahihi katika jamii.

Wakizungumza baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika Machi 17, 2026 mjini Mtwara, waandishi hao wameishukuru Jamii Africa kwa kuwapatia mafunzo hayo, wakisema yatawasaidia katika kazi zao za kila siku za kuhabarisha wananchi.

Aidha, waandishi hao wamesema kutokana na kukua kwa teknolojia, kumekuwa na changamoto ya watu kuzalisha maudhui ambayo kwa namna moja au nyingine husababisha mkanganyiko wa kutambua taarifa sahihi na zisizo sahihi hivyo, kupitia mafunzo hayo, wataweza kubaini ipi ni taarifa sahihi na ipi si sahihi.

Sauti ya Waandishi wa habari Mtwara

Naye Afisa Programu kutoka Jamii Africa, Edward Chaina, amesema mafunzo ya uhakiki na uthibitishaji wa taarifa ni muhimu kwa waandishi wa habari kwa kuwa yatawawezesha kuwa na uelewa wa kutambua na kuthibitisha taarifa hizo, ili kuwasaidia wananchi kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi.

Sauti ya Edward Chaina Afisa Programu Jamii Africa
Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>