• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Daraja lakatika, Namuhi, Mnyija wakosa mawasiliano

 

Mwonekano wa Daraja baada ya maji yanayotokea Bwawa la kitere kupitia mto Mambi kulivunja na wananchi kuunganisha kwa kutumia miti (Picha na Salamu Nayaula)

Na Musa Mtepa

Wananchi wa vijiji vya Namuhi na Mnyija wamejikuta katika wakati mgumu wa mawasiliano kufuatia kukatika kwa daraja linalounganisha vijiji hivyo, baada ya kufurika kwa maji yanayotoka Bwawa la Kitere kupitia Mto Mambi unaotenganisha maeneo hayo.

Wakizungumza na Jamii FM Radio Machi 28, 2026, wananchi hao wamesema kuwa uharibifu huo umetokana na maji mengi kufurika kutoka Bwawa la Kitere, hali ambayo imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii, ikiwemo kilimo, usafirishaji pamoja na elimu.

Aidha, wameeleza kuwa kutokana na ulazima wa kuvuka katika eneo hilo, wamelazimika kuweka miti juu ya mto huo ili iwe njia ya kupita, jambo linalohatarisha usalama wao.

Sauti ya 1 Wananchi wa Mnyija

Hata hivyo, wananchi hao wameiomba serikali kufika katika eneo hilo kujionea hali halisi na kutatua changamoto hiyo ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kujitokeza.

Sauti ya 2 Wananchi wa Mnyija

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Namuhi, Mwenyekiti wa kitongoji katika eneo lilipo daraja lililokatika, Bi. Suluhisho Nammanga, amesema athari zinazotokana na hali hiyo ni pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Namuhi na Shule ya Sekondari Libobe kushindwa kuhudhuria masomo. Pia, baadhi ya wakulima wameshindwa kufika mashambani kwa kuwa mashamba yao yapo upande wa pili wa mto.

Sauti ya Bi Suluhisho Nammanga kaimu mwenyekiti

Aidha, Bi. Suluhisho ametoa wito kwa serikali kutembelea eneo hilo na kuona umuhimu wa kujenga daraja hilo kwa haraka ili huduma muhimu kwa wananchi ziweze kuendelea kama kawaida.

Pia ameishauri serikali kwamba daraja litakapojengwa liwe refu zaidi kuliko lilivyokuwa awali, na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa kazi ya mkandarasi inakidhi matakwa ya mkataba husika wakati wa ukaguzi na makabidhiano.

Sauti ya Bi Suluhisho Nammanga kaimu mwenyekiti
Share:

Panda shuka za Mariam kuitumikia Chuno

 

Mariam Chibwalo akizungumza na muandaaji wa makala haya, Picha na Mwanaidi Kopakopa

Je, viongozi huzaliwa au hutengenezwa na mazingira? Makala hii inachunguza mjadala huo kupitia Mariam Chibwalo, mwanamke aliyethubutu kusimama pekee yake dhidi ya wanaume tisa katika kinyang’anyiro cha udiwani. Akiwa amesukumwa na changamoto na hamasa ya kuwa sauti ya wananchi wa Chuno, Mariam anaonesha kuwa uongozi si ndoto tu bali ni uamuzi wa kusimama na kuwatumikia wengine.

Na Mwanahamisi Chikambu na Mwanaidi Kopakopa.

Nadharia za uongozi duniani zimegawanyika katika makundi mawili makuu. Kuna wanaoamini kuwa viongozi huzaliwa na wengine wanaosisitiza kuwa viongozi hutengenezwa na mazingira au matukio wanayokutana nayo maishani.

Wanaodai viongozi huzaliwa huamini kuwa kipaji cha kuongoza kimo ndani ya damu ya mtu tangu kuzaliwa. Kwa upande mwingine, wanaoamini kuwa mazingira humjenga kiongozi wanasema kuwa changamoto, kero na dhuluma ndizo humsukuma mtu kusimama kidete na kusema ”Sasa basi, mimi nitakuwa sauti ya wenzangu”.

Safari ya uongozi wa Mariam Chibwalo haikuwa nyepesi. Katika kinyang’anyiro cha udiwani, alijitosa akiwa mwanamke pekee akishindana na wanaume tisa. Wengi waliutafsiri ujasiri wake kama ndoto isiyowezekana, lakini kwake yeye, haikuwa tu siasa bali ilikuwa ni wito wa dhati wa kuwatumikia wananchi wa Chuno.

Karibu usikilize makala hii ya kusisimua… Bonyeza hapa.

Share:

TMA yasisitiza wakulima kutumia vizuri mvua zinazonyesha

 

Kaimu meneja TMA kanda ya kusini Elewa Msomba akiwa katika mahojiano kwenye kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wamehimizwa kutumia vizuri mvua zinazonyesha kwa shughuli za maendeleo huku wakitakiwa kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa wataalam wa hali ya hewa na kilimo ili kupata tija

Na Musa Mtepa

Wananchi wameshauriwa kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo yao kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo, zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, ili kuwawezesha kupata tija.

Hayo yamesemwa Machi 23, 2026 na Kaimu Meneja wa TMA Kanda ya Kusini, Bw. Elewa Msomba, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio. Amesema kuwa kwa kuwa msimu wa mvua unaelekea mwishoni katika ukanda wa kusini, wananchi hawana budi kuzitumia ipasavyo ili kupata manufaa katika shughuli zao.

Sauti ya 1 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Aidha, Bw. Elewa Msomba amesema kuwa pamoja na msimu wa mvua kuelekea ukingoni katika ukanda wa kusini, hasa kwa wanaoishi maeneo ya bondeni na yenye unyevunyevu, wanapaswa kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kipindi hiki cha mwezi wa tatu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Sauti ya 2 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi kutoka Kituo cha Hali ya Hewa kilichopo katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI–Naliendele, Renatus Kapenda, amewataka wakulima kulima mazao kwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na TMA pamoja na ushauri wa wataalam wa kilimo waliopo katika maeneo yao, ili waweze kulima mazao yanayoendana na msimu husika.

Sauti ya 1 Renatus Kapenda Afisa TMA TARI–Naliendele

Sambamba na hilo, Renatus Kapenda amewataka wakulima kutambua kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili na mwanzoni mwa mwezi Mei. Hivyo, ni muhimu kwa wakulima kuzingatia ushauri na kushirikiana na wataalamu wa kilimo ili kuelekezwa mbegu zinazofaa kulingana na kiasi cha mvua kilichobaki.

Sauti ya 2 Renatus Kapenda Afisa TMA TARI–Naliendele
Afisa mfawidhi kutoka kituo cha hali ya hewa katika kituo cha utafiti wa kilimo Tanzania TARI-Naliendele Renatus Kapenda akiwa katika studio za jamii fm radio (Picha na Musa Mtepa)

Kwa mujibu wa TMA, msimu wa mvua kwa mikoa ya kusini ulianza mwezi Disemba 2025 na unatarajiwa kumalizika katika wiki ya nne ya mwezi Aprili hadi wiki ya kwanza ya mwezi Mei, huku mvua hizo zikiwa chini ya wastani kulingana na rekodi za mvua katika mikoa hiyo.

Sauti ya 3 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Kusikiliza kipindi Bonyeza hapa

Share:

Sekondari Naliendele na siku ya hali ya hewa duniani

 

Wanafunzi wa shule ya sekondari Naliendele wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka TMA kanda ya kusini (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wamehimizwa kuzingatia taarifa za hali ya hewa kutoka TMA ili kuboresha shughuli zao. Elimu imetolewa kwa wanafunzi Naliendele, wakihamasishwa kuwa mabalozi wa taarifa hizo kwa familia na jamii.

Na Musa Mtepa

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Kanda ya Kusini imeadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani katika Shule ya Sekondari Naliendele, huku ikiwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka hiyo ili kufanikisha shughuli zao za kila siku.

Wito huo umetolewa leo Machi 23, 2026 na Tamimu Masai, afisa wa TMA Kanda ya Kusini, wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kikanda katika shule hiyo. Amesema lengo la maadhimisho ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa hali ya hewa, ili waweze kufikisha ujumbe huo katika familia zao.

Tamimu amesema wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuzitumia ipasavyo, kwa kuwa zinamhusu kila mtu na kila shughuli ya maisha ya kila siku.

Sauti ya Tamimu Masai afisa wa TMA Kanda ya Kusini

Aidha, amesema kuchagua Shule ya Sekondari Naliendele kumechangiwa na nia ya kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, pamoja na kuwaandaa kuwa mabalozi wa kueneza ujumbe wa umuhimu wa kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

Sauti ya Tamimu Masai afisa wa TMA Kanda ya Kusini

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameeleza kufurahishwa na maadhimisho hayo, wakisema yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu hali ya hewa huku wakiwataka wazazi na wakulima kuzingatia taarifa zinazotolewa na wataalamu wa TMA kupitia vyombo vya habari.

Sauti ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Naliendele
Share:

TAKUKURU Mtwara yaandaa Iftar kuimarisha ushirikiano na Jamii

 

Baadhi ya washiriki wa Iftar iliyoandaliwa na TAKUKURU mkoa wa Mtwara wakiwa katika ukumbi uliondaliwa iftar hiyo(Picha na Musa Mtepa)

TAKUKURU Mtwara yaandaa Iftar kuimarisha uhusiano na jamii, viongozi wakisisitiza umoja, mshikamano na ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa wakati wa mwezi wa Ramadhani

Na Musa Mtepa

Ikiwa katika juhudi za kuimarisha uhusiano na utendaji wake pamoja na jamii inayoizunguka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara imejumuika na makundi mbalimbali katika kuandaa Iftar, huku ujumbe wa umoja na mshikamano ukitawala katika hafla hiyo.

Hafla hiyo iliyowakutanisha viongozi na wananchi wa kada mbalimbali imefanyika Machi 17, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin Mkapa uliopo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (tawi la Mtwara), zamani Chuo cha Ualimu (TTC).

Akizungumza katika Iftar hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara, Wakili Richard Mwalingo, amewakumbusha wananchi umuhimu wa kuchukia vitendo vya rushwa na kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vya vitendo hivyo na kusisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni silaha muhimu katika vita dhidi ya rushwa.

Sauti ya Richard Mwalingo Katibu Tawala Wilaya ya Mtwara

Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mashauri Elisante, amewashukuru wote waliojitokeza, akisema kuwa hafla hiyo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya TAKUKURU na jamii, kwani taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii katika utekelezaji wa majukumu yake.

Sauti ya Mashauri Elisante Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Mtwara, ambaye pia ni Askofu na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki, Yeriko Nguema, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania bila kujali rangi, kabila au imani ya mtu.

Sauti ya Askofu, Mchungaji Yeriko Nguema

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Sheikh Jamaldin Chamwi, amesema huruma, upendo na mshikamano ndivyo vinavyoimarisha misingi mikuu ya mwezi wa Ramadhani na kuongeza kuwa miongoni mwa mambo yanayokamilisha saumu ni pamoja na kufuturisha, kama ambavyo TAKUKURU imefanya.

Sauti ya Sheikh Jamaldin Chamwi, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
Share:

Jamii Africa yawajengea uwezo Waandishi wa habari Mtwara

 

Waandishi wa habari wakiwa katika mafunzo ya utambuzi na uthibitishaji wa taarifa yaliyotolewa na Jamii Africa yaliyofanyika March 17,2026 mjini Mtwara(Picha na Hery Abdala)

Waandishi wa habari 25 mkoani Mtwara wamepata mafunzo ya uhakiki wa taarifa kutoka Jamii Africa, yakilenga kuwasaidia kutambua taarifa sahihi na potofu ili kuboresha utoaji wa habari kwa wananchi

Na Musa Mtepa

Jumla ya waandishi wa habari 25 kutoka vyombo mbalimbali mkoani Mtwara wamepatiwa mafunzo ya uhakiki na uthibitishaji wa taarifa, yaliyotolewa na Jamii Africa chini ya taasisi mama ya Jamii Forums, kwa lengo la kuwawezesha kutambua taarifa potofu na zisizo sahihi katika jamii.

Wakizungumza baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika Machi 17, 2026 mjini Mtwara, waandishi hao wameishukuru Jamii Africa kwa kuwapatia mafunzo hayo, wakisema yatawasaidia katika kazi zao za kila siku za kuhabarisha wananchi.

Aidha, waandishi hao wamesema kutokana na kukua kwa teknolojia, kumekuwa na changamoto ya watu kuzalisha maudhui ambayo kwa namna moja au nyingine husababisha mkanganyiko wa kutambua taarifa sahihi na zisizo sahihi hivyo, kupitia mafunzo hayo, wataweza kubaini ipi ni taarifa sahihi na ipi si sahihi.

Sauti ya Waandishi wa habari Mtwara

Naye Afisa Programu kutoka Jamii Africa, Edward Chaina, amesema mafunzo ya uhakiki na uthibitishaji wa taarifa ni muhimu kwa waandishi wa habari kwa kuwa yatawawezesha kuwa na uelewa wa kutambua na kuthibitisha taarifa hizo, ili kuwasaidia wananchi kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi.

Sauti ya Edward Chaina Afisa Programu Jamii Africa
Share:

Mtoto ahofiwa kupoteza maisha mto mambi Mtwara

Mwonekano wa Mto Mambi unaomwaga maji Bahari ya Lindi (Likonde Namahyavi kijiji cha Ndumbwe) ukiwa umefurika maji( Picha na Musa Mtepa)

Mtoto Yasri Hamisi (14) wa kijiji cha Ndumbwe, Mtwara, anahofiwa kufariki baada ya kutumbukia mtoni alipoteleza akijaribu kugusa maji wakati akiwa na wenzake. Wananchi na vikosi vya uokoaji wanaendelea na juhudi za kumtafuta

Na Musa Mtepa

Mtoto Yasri Hamisi, mwenye umri wa miaka 14, mkazi wa kijiji cha Ndumbwe, wilaya na mkoa wa Mtwara, anahofiwa kupoteza maisha baada ya kutumbukia katika mto unaopita kijijini hapo ukitokea Bwawa la Kitere kuelekea Bahari ya Hindi upande wa Ndumbwe.

Inaelezwa kuwa Yasri aliambatana na wenzake watatu mnamo March 7, 2026 kwenda katika mto huo kwa ajili ya kufanya shughuli za uvuvi. Hata hivyo, walipofika mtoni walibadili maamuzi ya kuvua samaki na kuamua kuoga. Mmoja wao aliwaonya wenzake kuwa maji yalikuwa mengi na yana kasi hivyo yeye hangeweza kuoga.

Inadaiwa kuwa Yasri alipokuwa akijaribu kugusa maji kwa mguu ndipo alipoteleza na kutumbukia mtoni na kuzama.

Wakizungumzia tukio hilo jana, March 9, 2026, wakazi wa kijiji cha Ndumbwe wamesema wanaendelea na juhudi za kumtafuta kijana huyo kwa kufuata mwelekeo wa maji yanakoelekea kuchanganyika na maji ya Bahari ya Hindi.

Sauti ya wananchi wa kijiji cha Ndumbwe
Wananchi wa kijiji cha Ndumbwe wakiendelea na utafutaji wa Mtoto Yasri Hamisi katika eneo la Mikoko mwelekeo wa maji yanatoka Mto Mambi(Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, mwenyekiti wa kijiji cha Ndumbwe Ali Mshamu amekiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa baada ya kupata taarifa alitoa taarifa kwa wananchi wa kijiji kizima ili kuanza jitihada za kumtafuta kijana huyo. Hata hivyo hadi kufikia jana, March 9, 2026, bado hawajafanikiwa kumpata.

Sauti ya Ali Mshamu mwenyekiti wa kijiji

Akizungumzia tukio hilo, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Ambrosi Ndunguru amesema kuwa baada ya kupokea taarifa ya tukio hilo, timu ya uokoaji ya jeshi hilo ilifika katika kijiji cha Ndumbwe na kuanza operesheni ya kumtafuta kijana huyo, lakini hadi sasa hawajafanikiwa kumpata baada ya juhudi za siku mbili huku akisema kuwa zoezi la utafutaji litaendelea kwa siku ya tatu.

Aidha, Mrakibu Ndunguru ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuepuka kusogelea mto huo kwa shughuli za uvuvi au kilimo kwa sasa, kutokana na kufurika kwa maji yenye kasi yanayotoka katika Bwawa la Kitere pamoja na vijiji vya pembezoni.

Sauti yaAmbrosi Ndunguru mrakibu msaidizi wa zimamoto
Share:

Makala: siku ya wanawake duniani 2026

 

Merina Mkuchu Meneja wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo SIDO Mkoa wa Mtwara (Picha na Gregory Millanzi)

Kupitia maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani (IWD), jamii inapata fursa ya kutafakari mchango, changamoto na mafanikio ya wanawake.

Gregory Millanzi na Mwanahamis Chikambu.

Katika mwanzo wa historia ya mwanadamu, kabla ya ustaarabu kujengeka na kabla jamii haijaweka mifumo ya maisha tunayoijua leo, kulikuwepo mwanamke. Mwanamke ndiye aliyebeba tumaini la uhai, mlezi wa kizazi na nguzo ya familia. Kupitia mikono yake jamii imekua, kupitia hekima yake maadili yamefundishwa, na kupitia uvumilivu wake maisha yameendelea. Tangu zamani, uwepo wa mwanamke umeendelea kuwa msingi muhimu katika kujenga na kuendeleza maisha ya binadamu.

Kwa mwaka huu, maadhimisho yamebeba kauli mbiu “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.

Katika kila zama, mwanamke amekuwa kama mwanga unaoangaza njia ya maisha ya binadamu. Akiwa mama, mlezi, mwalimu na wakati mwingine kiongozi wa kimya kimya ndani ya jamii, mchango wake umeendelea kuandika sura muhimu katika historia ya maendeleo ya dunia. Ni nguvu ambayo mara nyingi haionekani wazi kwa macho, lakini athari yake imekuwa kubwa katika kujenga kizazi, kuimarisha familia na kusimika misingi imara ya jamii.

Debora Didi afisa ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (picha na Gregory Millanzi)

Hata hivyo, kwa miaka mingi wanawake na wasichana wamekumbana na changamoto na vikwazo mbalimbali katika nyanja tofauti za maisha. Baadhi walinyimwa fursa sawa za kupata elimu, wengine hawakupewa nafasi katika uongozi, na wengi hawakushirikishwa kikamilifu katika maamuzi muhimu yanayoathiri maisha ya jamii. Hali hii ilisababisha sauti ya mwanamke kutosikika ipasavyo licha ya mchango mkubwa aliokuwa akiutoa kila siku katika maendeleo ya familia na taifa.

Licha ya changamoto hizo, dunia inaendelea kubadilika. Leo hii, sauti ya mwanamke inazidi kusikika na nafasi yake katika jamii inaendelea kutambuliwa. Kupitia maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani (IWD), jamii inapata fursa ya kutafakari mchango, changamoto na mafanikio ya wanawake. Kwa mwaka huu, maadhimisho yamebeba kauli mbiu “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.” Makala haya yameandaliwa na Gregory Millanzi akishirikiana na Mwanahamis Chikambu.

Ili kusikia makala haya, bonyeza hapa

Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>