• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

SIDO Mtwara yawataka wajasiriamali kukuza biashara kidijitali

 

Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdalla Mwaipaya akizungumza wakati ya mafunzo ya uingezaji thamani uliofanyika february 24,2026 mjini Mtwara(Picha na Gregory Milanzi)

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewahimiza wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa na kutumia teknolojia, ikiwemo akili mnemba, kukuza biashara zao. Mafunzo hayo yaliandaliwa na SIDO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwawezesha kibiashara

Na Gregory Millanzi

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewataka wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuongeza kipato, pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kujitangaza na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Mwaipaya ameyasema hayo Februari 24, 2026, wakati akifungua semina ya utambuzi wa bidhaa, viwanda na matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence), iliyofanyika katika Ukumbi wa Benjamini Mkapa, Chuo Kikuu cha MUST Mtwara (zamani Chuo cha Ualimu TTC Kawaida).

Sauti ya Abdallah Mwaipaya – Mkuu wa Wilaya ya Mtwara

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mtwara, Merina Mkuchu, amesema lengo la semina hiyo ni kuwatambua wajasiriamali wa Manispaa ya Mtwara na kuwapatia elimu ya kufanya biashara kidijitali badala ya kufanya biashara kwa mazoea.

Mkuchu ameongeza kuwa kwa sasa wanaandaa kanzidata ya kuwatambua wajasiriamali hao ili kuwaunganisha na wadau mbalimbali wanaofika Mtwara kutafuta washirika wa biashara. Pia, SIDO inaandaa kongani la viwanda katika kila wilaya kwa lengo la kuwaunganisha wajasiriamali na kukuza ushirikiano miongoni mwao.

Sauti ya Merina Mkuchu – Meneja SIDO Mkoa wa Mtwara

Naye Afisa Uhusiano kwa Umma kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Feisal Abdul, amewahimiza wajasiriamali kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Uendelezaji Ubunifu (Samia Fund), unaolenga kuwajengea uwezo na kuwapatia ruzuku za kuendeleza bunifu zao.

Sauti ya Feisal Abdul – Afisa Uhusiano COSTECH

Aidha, kampuni ya Scan Code imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wa Mtwara kuhusu matumizi ya Scan Code na akili mnemba katika kujitangaza na kupanua masoko ya biashara zao.

Abdulwahid Khamis, mkufunzi kutoka Scan Code, ameeleza faida za teknolojia hiyo na namna inavyoweza kuwasaidia wajasiriamali kuongeza wigo wa soko na mapato.

Sauti ya Abdulwahid Khamis – Mtaalamu wa Mafunzo kutoka Scan Code
Share:

Vijana Mtwara wahimizwa maadili kulinda amani nchini

 

Vijana wa Skauti wakiwa katika maandamano ya kuadhimisha siku ya Skauti Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Vijana wamehimizwa kutumia mitandao kwa maadili na kulinda amani wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani yaliyofanyika Mtwara , yakikumbuka miaka 160 ya Robert Stephenson Baden-Powell

Na Musa Mtepa

Vijana wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia maadili, tamaduni na mila za Kitanzania, na kuitumia kwa manufaa yao binafsi pamoja na taifa kwa ujumla. Pia wametakiwa kuachana na maudhui yanayoharibu maadili, utu, tunu za taifa, pamoja na yale yanayochochea uvunjifu wa amani.

Nasaha hizo zimetolewa leo Februari 22, 2026 na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara , ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Bi. Telack amewataka vijana kutumia teknolojia kwa hekima na busara, pamoja na kupambanua maudhui yanayopatikana kwenye mitandao ya kijamii, na kuachana na yale yote yanayoharibu imani za dini, maadili na tamaduni za Kitanzania.

Sauti ya Bi. Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Lindi

Aidha, Bi. Telack ameendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kuipenda na kuilinda amani iliyopo nchini kwa kuwa na uzalendo wa kweli kwa Tanzania. Alisema hakuna nchi nyingine kwao zaidi ya Tanzania, hivyo ni wajibu wa kila kijana kuhakikisha anailinda na kuipambania nchi yake.

Sauti ya Bi. Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Lindi

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Sarah Vanessa, mwakilishi wa Skauti Mkoa wa Mtwara, amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia Skauti bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo ufinyu wa bajeti ya kusaidia vijana wa skauti kutekeleza miradi ya uzalishaji mali, pamoja na ukosefu wa vifaa vya uokoaji kwa timu za maafa katika wilaya na mikoa.

Sauti ya Sarah Vanessa, Mwakilishi wa Skauti Mkoa wa Mtwara

Akitoa salamu kwa niaba ya Bodi ya Skauti Tanzania, mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ndugu Lazaro Mkeni, amesema wizara itaendelea kusimama pamoja na Chama cha Skauti Tanzania kuhakikisha misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho inalindwa na kuimarishwa. Ameongeza kuwa wizara ipo tayari kutoa msaada pale inapobidi ili kuhakikisha misingi hiyo inasimamiwa ipasavyo.

Sauti ya Lazaro Mkeni, Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Komredi Ibrahim Mjanaheri Ibrahim, amewapongeza waandaaji wa maadhimisho hayo,huku akitoa rai kwa vijana kuendelea kudumisha amani na kuachana na mtu yeyote anayetaka kuivuruga amani ya nchi.

Sauti ya Ibrahim Mjanaheri Ibrahim, Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara

Maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani Kitaifa kwa mwaka 2026 yamefanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Elimu Bunifu na Stadi za Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu ya Vijana.”

Maadhimisho hayo ni kumbukizi ya miaka 160 tangu kuzaliwa kwa mwanzilishi wa Skauti Duniani, Robert Stephenson Baden-Powell, mzaliwa wa Uingereza, aliyezaliwa Februari 22, 1857. Alianzisha Skauti mwaka 1907 na baadaye mwaka 1908 akaandika kitabu maarufu kiitwacho Scouting for Boys.

Baden-Powell alianza kwa kufanya kambi ya majaribio mwaka 1907 katika Kisiwa cha Brownsea, Uingereza, ambapo alitoa mafunzo kwa vijana yenye lengo la kuwafundisha uongozi, kujitegemea, uzalendo na huduma kwa jamii. Harakati hizo zilisambaa duniani kote, kama ambavyo leo zimeadhimishwa mkoani Mtwara na Tanzania kwa ujumla.

Share:

AGCOT yataka mageuzi ya kilimo mikoa ya Kusini

 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi Zainab Telack akizungumza na wadau wa kilimo katika mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara (picha na Musa Mtepa)

“Kama tunaweza uzalisha zaidi ya bilioni 260 kwa zao moja, tunashindwa nini kutegemewa”

Na Musa Mtepa

Wadau wa kilimo wametakiwa kushirikiana kwa umoja katika kumsaidia mkulima kuzalisha kilimo chenye tija kwa kuwawezesha kulima kwa njia za kisasa, ikiwemo kuwapatia vitendea kazi bora vya kilimo.

Hayo yamesemwa Februari 20, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, wakati akifungua Warsha ya Wadau wa Kilimo ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo kwa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara, iliyofanyika mjini Mtwara.

Bi. Telack amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika zao la korosho, ambapo wakulima wamezalisha zaidi ya shilingi bilioni 260, yanaonesha kuwa inawezekana pia kuongeza uzalishaji wa mazao mengine endapo wakulima watawezeshwa kulima kisasa. Amesisitiza matumizi ya matrekta na zana bora za kilimo ili kuwawezesha wakulima kulima mashamba makubwa zaidi na kuongeza tija.

Sauti ya Bi Zainab Telack mkuu wa mkoa wa Lindi

Aidha, amewataka wakuu wa wilaya, wakuu wa idara za kilimo na sekta binafsi kutumia warsha hiyo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati imara ya utekelezaji wa mageuzi ya sekta ya kilimo kwa mikoa ya kusini na taifa kwa ujumla.

Sauti ya Bi Zainab Telack mkuu wa mkoa wa Lindi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa utaratibu wa Shoroba Tanzania (AGCOT), Geoffrey Kirenga, amesema lengo la warsha hiyo ni kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma pamoja na kuongeza ukaribu baina yao ili kukuza sekta ya kilimo.

Sauti ya Geoffrey Kirenga mkurugenzi wa AGCOT

Kirenga ameongeza kuwa katika warsha hiyo ameguswa na hoja zilizotolewa na sekta binafsi pamoja na viongozi wa halmashauri kwamba mwaka 2026 huenda malengo ya uzalishaji yasifikiwe kama ilivyotarajiwa kutokana na uhaba wa mbegu bora za ufuta. Amesema hali hiyo inaashiria kuongezeka kwa idadi ya wakulima wa zao hilo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Sauti ya Geoffrey Kirenga mkurugenzi wa AGCOT

Kwa upande wao, Mkuu wa Idara ya Kilimo Halmashauri ya Masasi, James Chitumbi, pamoja na Mkuu wa Idara ya Kilimo Halmashauri ya Nachingwea, Rafael Magetu, wamesema warsha hiyo imewapa manufaa makubwa, ikiwemo namna ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mbegu bora za mazao ya chakula na biashara kwa kuongeza juhudi za uzalishaji ili kufikia kilimo chenye tija.

Wakuu wa Idara ya Kilimo halmashauri ya Nachingwea na Masasi

Akifunga warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brig Jenerali ,Ahmed Abbas, ametoa wito kwa wakuu wa wilaya kwenda kujifunza mbinu za kilimo-biashara zinazotekelezwa mkoani Lindi ili kukuza kilimo mseto na biashara katika Mkoa wa Ruvuma.

Sauti ya Brig Ahmed Abbasi mkuu wa mkoa wa Ruvuma

Warsha hiyo ya siku moja imewakutanisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakuu wa idara za kilimo, sekta binafsi pamoja na wadau wa kilimo kutoka mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara. Lengo kuu lilikuwa kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo katika mikoa hiyo.

Share:

Mtwara kuadhimisha kitaifa siku ya Skauti Duniani

 

Kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara ambae pia mkuu wa mkoa wa Lindi Bi Zainab Telack akizungumza na vyombo vya habari leo ofisini kwake mjiniMtwara(Picha na Musa Mtepa)

Mkoa wa Mtwara utaadhimisha Siku ya Skauti Duniani Februari 22, 2026, kumuenzi Robert Baden-Powell. Maadhimisho hayo yatajumuisha mafunzo, huduma za jamii na kampeni za uzalendo, huku vijana 400 wakitarajiwa kunufaika na elimu mbalimbali. Wananchi wamealikwa kushiriki katika viwanja vya Nangwanda Sijaona

NA Musa Mtepa

Mkoa wa Mtwara unatarajia kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Skauti Duniani yatakayofanyika Februari 22, 2026, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi mwanzilishi wa harakati za Skauti Duniani, Robert Baden-Powell.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack, amesema kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya historia ya zaidi ya miaka 100 ya Skauti, yenye lengo la kuwajenga vijana katika misingi ya uzalendo, uwajibikaji na kuipenda nchi yao.

Bi. Telack ameeleza kuwa katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, tayari shughuli mbalimbali zimeanza kufanyika kupitia vijana wa Skauti, ikiwemo kambi za mafunzo ya ukakamavu, utoaji wa huduma za jamii pamoja na shughuli za utunzaji wa mazingira. Aidha, Februari 21, 2026, vijana hao wanatarajiwa kushiriki mafunzo yanayohusu uwajibikaji, uzalendo na masuala ya usalama.

Sauti ya 1 Bi Zainab Telack kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara

Katika hatua nyingine, Bi. Telack ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wote wa Mtwara kushiriki kwa pamoja katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika Viwanja vya Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.

Sauti ya 2 Bi Zainab Telack kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara

Kwa upande wake, Naibu Kamishina wa Skauti Mkoa wa Mtwara, Sofia Malandi, amesema kuwa kufanyika kwa maadhimisho hayo kumeleta fursa mbalimbali kwa vijana na kwa mkoa kwa ujumla. Amefafanua kuwa elimu tofauti zinaendelea kutolewa, ikiwemo elimu ya kupinga rushwa na kuimarisha uzalendo, ambapo jumla ya vijana 400 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo.

Sauti ya Sofia Mlandi naibu kamishina wa Skauti mkoa wa Mtwara
kamishina wa Skauti mkoa wa Mtwara Sofia Mlandi akizungumzia shughuli zinazofanyika kuelekea maadhimisho hayo(Picha na Musa Mtepa)

Naye Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mratibu wa maadhimisho hayo, Bi. Fatuma Mtanda, amesema kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na wageni kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Lindi, Ruvuma, Mbeya, Mjini Magharibi na Pwani. Ameongeza kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Zainab Telack.

Sauti ya Fatuma Mtanda mratibu wa maadhimisho
Mratibu wa maadhimisho ya siku ya Skauti Duniani , Bi. Fatuma Mtanda akitolea ufafanuzi juu ya wageni watarajiwa na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo(Picha na Musa Mtepa)
Share:

Paka wa ajabu aibua taharuki Mtwara vijijini

 

Paka wa ajabu aliyekutwa amekufa baada ya kudhaniwa kujipiga kwenye nyumba ya Bi Maimuna Abilahi mkazai wa kijiji cha Nangumi(Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa kitongoji cha Shangani, Nangumi, wamekumbwa na taharuki baada ya paka kupatikana amekufa na kuvalishwa hirizi katika nyumba ya mkazi mmoja. Tukio hilo limeibua hofu na maswali, huku viongozi wa kijiji wakieleza kusikitishwa na hali hiyo isiyo ya kawaida

Na Musa Mtepa

Wananchi wa kitongoji cha Shangani, kijiji cha Nangumi, kata ya Mayanga wilayani Mtwara Vijijini, wamekumbwa na taharuki baada ya kuonekana kwa paka aliyekufa huku mwilini mwake akiwa amevalishwa hirizi.

Tukio hilo limetokea alfajiri ya leo, Februari 17, 2026, katika nyumba ya Maimuna Abilahi, mchuuzi wa samaki na mkazi wa kijiji hicho.

Wakizungumza na Jamii FM Radio, baadhi ya wananchi wa Nangumi wameeleza kushangazwa na tukio hilo, huku wakilihusisha na imani za kishirikina. Wamedai kuwa paka huyo alionekana akiwa amejitupa katika eneo la nyumba hiyo, na baada ya kuchunguzwa alikutwa na hirizi shingoni na kiunoni.

Sauti ya wananchi wa Nangumi

Akizungumzia tukio hilo, Maimuna Abilahi, mmiliki wa nyumba hiyo, amesema alipata taarifa za tukio hilo kupitia simu alipokuwa feri kununua samaki kwa ajili ya biashara yake. Ameeleza kuwa aliondoka nyumbani mapema asubuhi akitumia mlango wa nyuma, ambao ni tofauti na eneo alikokutwa paka huyo.

Sauti ya Maimuna Abilahi, mmiliki wa nyumba

Kwa upande wake, baba mzazi wa Maimuna, mzee Abilahi Issa Mohamedi, amesema baada ya kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na kisha kumpigia simu mwanawe kumjulisha. Ameeleza kuwa walikubaliana kumchoma moto paka huyo majira ya saa kumi jioni.

Alipoulizwa sababu ya kusubiri hadi saa kumi jioni, mzee Abilahi amesema ni maagizo ya wataalamu, akidai kuwa paka huyo ni wa aina ya kipekee.

Sauti ya mzee Abilahi Issa Mohamedi

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Nangumi, Musa Salumu Nassoro, ameeleza kusikitishwa na tukio hilo, akisema linaweza kujenga taswira mbaya kwa kijiji hicho. Ameongeza kuwa katika kipindi chote cha uongozi wake hajawahi kushuhudia wala kusikia tukio la aina hiyo katika kijiji cha Nangumi.

Sauti ya Musa Salumu Nassoro, mwenyekiti wa kijiji cha Nangumi
Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>