
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amemuagiza Mkurugenzi wa COPRA kuhakikisha mazao ya Ruvuma, Lindi na Mtwara yapitie Bandari ya Mtwara ili kuongeza tija, kurahisisha upakiaji na kuhakikisha fursa zinabaki kwa wakazi wa mikoa hiyo
Na Musa Mtepa
Waziri wa kilimo Mhe.Danieli Chongolo amemuagiza mkurugenzi wa COPRA kusimamia mazao yote ya kibiashara yanayozalishwa katika mikoa mitatu ya Ruvuma,Lindi na Mtwara yapitie katika Bandari ya Mtwara ili kuongeza tija na kuwarahisishia wanunuzi uhakika wa muda mfupi wa kusubirisha Meli,kupakia na kuondoa bidhaa.
Hayo amesema Disemba 11,2025 wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika mkoa wa Mtwara ambapo akiwa Bandari ya Mtwara amesema kitendo hicho kitaifanya Bandari kufanyakazi muda wote na kusaidia kuongeza tija kwa Wanamtwara na taifa kwa ujumla.

Aidha Waziri Chongolo amesema kuwa lengo kuu sio kuzihamisha fursa kuzipeleka sehemu nyingine ni katika kuhakikisha zinabakia kwa wanamtwara,Lindi na vijana wanaozunguka ukanda wa kusini kujitafutia fedha kupitia bandari hiyo.
Kwa upande wake meneja wa Bandari ya Mtwara Ferdinandi Nyathi amesema hakuna haja ya kutoa Korosho kutoka mikoa ya kusini kwenda kusafirishia Dar es salaam kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vinavyoweza kufanyakazi kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa wakati.

Hii ni ziara yake ya kwanza ya kikazi ya Waziri wa kilimo Mhe.Daniel Chongolo tangu alipoteuliwa na Mh. Rais ,ambapo alifanikiwa kutembelea katika ofisi za Bodi ya Korosho,Bandari ya Mtwara,kituo cha utafiti wa Kilimo cha TARI-Naliendele,Kongani ya Viwanda Maranje –Nanyamba Mtwara,Maghali ya kuhifadhiwa Korosho ,kituo cha wajasiliam mali wadogo wa ubanguaji Korosho Mahuta na kiwanda cha Kubangua Korosho cha TANECU kilichojengwa katika kijiji cha Mmova Kitangari Newala vijijini.
























