• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

MTWARA: (HABARI PICHA) Wazri Mkuu Kassim Majaliwa azindua kituo cha afya Chiwale

PMO_0269
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi wa jengo la wazazi katika kituo cha afya Chiwale, Wilayani Masasi, akiwa ameanza ziara yake ya kikazi ya siku tatu, Mkoani Mtwara  Februari 26, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO_0271
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe  wakati akiweka jiwe la msingi katika kituo cha afya Chiwale, akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu, Mkoani Mtwara  Februari 26, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO_0286
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua wodi ya wazazi katika kituo cha afya Chiwale, mara baada ya kuweka jiwe la msingi kituoni hapo, akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu, Mkoani Mtwara  Februari 26, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO_0320
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na wananchi wa Chiwale, Wilayani Masasi, mara baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo la wazazi katika kituo cha afya Chiwale. Februari 26, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Share:

DAR ES SALAAM: Wema Sepetu Alinambia anavuta Bangi kwa starehe

Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu imeendelea na kesi inayomkabili muigizaji Wema Sepetu ambapo Ofisa wa Polisi WP Mary ameieleza mahakama kuwa mnamo Februari 4, 2017 Wema alimwambia anatumia bangi kwa ajili ya starehe na si kuuza

WP Marry ambaye ni shahidi wa tatu ameyaeleza hayo wakati akiongozwa na Wakili wa serikali Costantine Kakula, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

WP Marry amedai kuwa Wema alimueleza maneno hayo wakati walipokuwa njiani kuelekea nyumbani kwake kumkagua.

Amedai kuwa February 4, 2017 aliagizwa kumtoa Wema Mahabusu na kwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwake akiwa na OC CID na Maofisa wengine wa Polisi.

Amedai kuwa wakiwa wanajiandaa kuondoka Central Polisi kuelekea kwa Wema Bunju Basihaya, wakiwa kwenye gari kuelekea huko alimuuliza Wema kuhusu tuhuma zinazomkabili kwamba anahusika na biashara ya Dawa za kulevya au kutumia.

Amedai kuwa Wema alijibu “Sijishughulishi na kuuza ila natumia bangi kama starehe”.

WP Marry amedai kuwa baada ya kumuuliza Wema alimwambia mara yake ya mwisho kuvuta Bangi ilikuwa Jumatatu ambapo swali hilo aliulizwa February 4,2017.

Alieleza kuwa walipofika nyumbani kwa Wema waligonga geti na kufunguliwa na mdada wa kazi ambapo walivyoingia ndani walikuta kuna mdada mwingine wa kazi.

WP Marry amedai kuwa kabla ya kuingia ndani Wema aliomba kumpigia simu dada yake ili awepo wakati wa kufanya ukaguzi ambapo dada yake alifika na kujitambulisha kwa jina la Nuru Sepetu.

WP Marry ameeleza kuwa wakati Wema anampigia simu dada yake alitoka dada mmoja wa kazi kumfuata mjumbe ambapo alikuja naye na kujitambulisha kwa jina la Steven Ndaho.

Amedai baada ya dada yake Wema kufika alitaka kuwapekua kabla ya kuingia ndani ambapo Nuru aliwapekuwa wote kabla ya kuingia ndani.

Amedai baada ya kumaliza upekuzi walirudi Central polis, February 8,2017 saa nne asubuhi alipewa maelekezo na Inspekta Wille kwamba aende na Wema kwa Mkemia Mkuu wa serikali kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli ya mkojo.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi March 12 na 13, 2018 kwaajili ya kuendelea na ushahidi.
Share:

MBEYA: Mawakilii wa Sugu Wajipanga Kukata Rufaa

Baada ya mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela, wakili wao Peter Kibatala amesema wanakusudia kukata rufaa.

Sugu na Masonga wamehukumiwa adhabu hiyo leo Februari 26,2018 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite.

Wawili hao wamehukumiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, kosa walilotenda kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Kibatala amesema baadaye watatoa taarifa ya nini kinaendelea ila wanakusudia kukata rufaa.

Baada ya hukumu kutolewa viongozi wa Chadema waliokuwepo mahakamani waliingia kwenye magari yao na kuelekea katika ofisi za chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Wakati wa usomwaji wa hukumu hiyo, nje ya jengo la mahakama ulinzi uliimarishwa kukiwa na askari waliotanda hadi maeneo ya jirani.

Sugu ni mbunge aliyeweka rekodi ya kupata kura nyingi kuwashinda wabunge wote wa majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika uchaguzi huo, Sugu alipata kura 108,566 akiwaacha wapinzani wake kugawana kura 57,690.

Hukumu imetolewa na hakimu Mteite aliyesikiliza shauri hilo baada ya upande wa mashtaka na wa utetezi kukamilisha ushahidi Februari 9,2018.

Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.

Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno waliyoshtakiwa kuyatoa.

Washtakiwa walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu kabla ya kujitoa na kazi hiyo kufanywa na Kibatala.

Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga  walifikishwa mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na usikilizaji.
CHANZO: MPEKUZI
Share:

IRINGA: Wahamiaji 83 wa Ethiopia wapandishwa kizimbani

Wahamiaji 83 raia wa Ethiopia na Mtanzania mmoja mkazi wa Tukuyu wamefikishwa Mahakama ya Mkoa Iringa huku wahamiaji hao wakituhumiwa kuingia nchini bila kibali.

Akisoma mashtaka hayo leo Februari 26, 2018, wakili wa Serikali, Godfrey Ngwijo amesema raia hao wanakabiliwa na shtaka la kuingia nchini kinyume na kifungu cha sheria namba 45(i) kifungu (1) ,(2) kilichofanyiwa marekebisho 2016.

Ngwijo amesema Februari 23, 2018 saa moja jioni katika kijiji cha Mazombe wilayani Kilolo, wahamiaji 83 wasio na vibali walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi kwa kuingia nchini kinyume na sheria ambapo dereva wa lori walilopanda  hakupatikana baada ya kukimbia.

Amesema wahamiaji hao walikamatwa wakiwa katika hali mbaya kutokana na kukaa sehemu ya nyuma ya lori hilo ambako hakuna hewa ya kutosha, joto kali na kutokula chakula kwa muda mrefu.

Baadhi ya wahamiaji hao leo wamefikishwa hospitali ya mkoa kupata matibabu.

Wakili huyo amesema kati ya waliofika mahakamani kusomewa mashtaka yao, watatu  walishindwa kufika kwa sababu bado wako hospitali wanaendelea na matibabu.

Mtanzania aliyekutwa katika gari hiyo, Hassan Mwalusanjo akituhumiwa kusafirisha wahamiaji hao kwa kutumia lori mali ya Gabriel Mwakyambiki mkazi wa Tukuyu kinyume na sheria, alikana kosa hilo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, David Ngonyani ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 2, 2018.
CHANZO: MPEKUZI
Share:

MBEYA: Mbunge Joseph Mbilinyi 'sugu' Kahukumiwa Miezi Mitano Jela

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imemuhukumu Miezi Mitano jela Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite ambapo amesema ameridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mteite amesema kuwa Mahakama imejikita katika sehemu kuu nne.

Amesema kuwa sehemu hizo ni kama washtakiwa walitamka Maneno ya fedheha, pia kama maneno waliyoyatoa yamebeba maudhui ya fedheha, pia kama maneno hayo yana mlenga Rais pamoja washtakiwa kama wana hatia ama lah.

Katika hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya saa moja Hakimu Mteite amesema amejiridhisha pasina kuacha shaka juu ya ushahidi wa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka.

Hakimu Mteite amesema Mahakama inakubaliana na hoja ya kwamba washtakiwa walitamka maneno ya fedheha dhidi ya Rais kutokana na ushahidi wa upande wa mashtaka ambao waliwasikia washtakiwa na kuwaona wakati wakitamka.

“Katika kesi hii mashahidi wengi ni askari, hivyo ni dhahiri wametoa maneno hayo,” -Hakimu Mteite

Pia kuhusu maneno hayo kumlenga Rais Magufuli, Hakimu Mteite amesema maneno hayo ya fedheha ni ya kitaifa, kwani masuala yanayogusa watu kuuawa ni ya kitaifa na ndio maana washtakiwa walitamka maneno (Rais Wetu).

“Tujiulize ni Rais yupi waliyemzungumzia ni wa Simba, Yanga ama Mbeya City hivyo Rais aliyezungumziwa hapa ni Magufuli kwani hakuna Magufuli mwingine anayetuongoza,”-Hakimu Mteite

Hakimu Mteite amesema kwa imani yake washtakiwa wana hatia.

“Kutokana na upande wa utetezi kuomba nafuu ya adhabu na upande wa mashtaka kutaka itolewe adhabu kali, nawahukumu miezi mitano jela,” -Hakimu Mteite.

CHANZO: MPEKUZI
Share:

MTWARA: Waziri Mkuu Aiagiza TAKUKURU Kuwakamata Aliiyekuwa Mkugenzi wa Halimashauri Masasi na Mweka Hazina

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara Bw. Stephen Mafipa  kumtafuta popote alipo na kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi Bw. Fortunatus  Kagoro  kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

Mbali na Bw. Kagoro pia Kaimu Mweka Hazina Bw. Heri Hamad Afisa Mipango Bi Teresia Nsumba  nao ameagiza wakamatwe na baada ya uchunguzi watakaobainika kwamba hawajahusika na ubadhilifu huo watarudishwa kazini. "Lazima fedha za Serikali zitumike kama ilivyokusudiwa."

Watendaji hao wanadaiwa kutumia sh. bilioni 1.8 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa kuchora mchoro na kujenga msingi katika maeneo mawili tofauti.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Februari 26, 2018) wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Masasi na Halmashauri ya wilaya ya Masasi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.

Amesema mwaka 2014  Serikali ilipeleka sh milioni 575 wilaya Masasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri hiyo na fedha hizo ziliishia kutumika  katika hatua za maandalizi ya awali ikiwa ni pamoja na kutengeneza michoro ya jengo.

Waziri Mkuu amesema 2016/2017 Serikali ilipeleka tena sh. bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo Halmashauri hiyo ilienda kutafuta eneo lingine na kufanya tena shughuli zilizokuwa zimefanyika na kuanza ujenzi ambao umeishia katika msingi na fedha zimeisha.

Pia amewataka watendaji hao kutotumia fedha za makusanyo ya ndani kwa ajili ya kuziba pengo la fedha za mradi huo ambazo baadhi yake hazijulikani zilipo na amewaagiza Madiwani kutoruhusu jambo hilo.

"Madiwani msikubali kutumia fedha za makusanyo ya ndani kupeleka kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo tayari Serikali ilishatoa fedha ya ujenzi wake.

Amesema Serikali inahitaji kuona fedha za maendeleo zinazopelekwa katika Halmashauri mbalimbali nchini zinatumika kama ilivyoelekeza na si vinginevyo na Serikai haitakuwa na mzaha kwa mtumishi atakayezitumia vibaya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 26, 2018.
Share:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha apata ajali

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo  amepata ajali  baada ya gari lake kupasuka tairi na kupinduka

Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo amesema ajali hiyo ilitokea kati ya eneo la Mdori na Minjingu wilayani Babati  jana  Februari 26  saa nane mchana.

Amesema Kamanda Mkumbo ambaye alikuwa anatoka mkoani Singida kurejea Arusha, ameumia kidole cha mkono wa kushoto na michubuko iliyotokana na kukatwa na vioo.

Amesema gari lilipata ajali baada ya kupasuka tairi la nyuma upande wa kushoto.

Ilembo amesema Mkumbo baada ya kufikishwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, aliingizwa chumba cha upasuaji moja kwa moja.

Pia, katika ajali hiyo dereva wa kamanda Mkumbo, Staff Sajent Silvanus aliumia maeneo ya paja.

Mganga mfawidhi wa Mkoa Arusha, Dk Omar Chande amesema  majeruhi wote wanapatiwa matibabu.

Hata hivyo, hakuwa tayari kuelezea hali za majeruhi hasa kwa maelezo kuwa uchunguzi wa kutabibu unaendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa pia wamefika  hospitali ya mkoa kumjulia hali Mkumbo na majeruhi wengine.
CHANZO: MPEKUZI
Share:

MTWARA: Waziri mkuu kuzuru MASASI, NANYUMBU, TANDAHIMBA, NANYAMBA, NA NEWALA


Waziri MKuu wa Jamhuri ya Muunganno wa Tanzania MHE KASSIM MAJALIWA anatarajia kufanya ziara ya kikazi Mkoani Mtwara kwa muda wa siku Tatu yaani tarehe 26-28 februari, 2018.
MHE MAJALIWA anatarajia kutembelea wilaya ya MASASI, NANYUMBU, TANDAHIMBA, NANYAMBA, NA NEWALA. Akiwa katika ziara yake anatarajia kupokea taarifa za miradi mbalimbali ya maendeleo, kuzindua jengo la wodi ya akina mama na watoto katika kituo cha afya cha CHIWALE, Ujenzi wa chuo cha ualimu KITANGALI na chanzo vya Maji vya Makonde na Mitema.
Ziara hii ni mwendelezo wa ziara za kikazi ambapo baada ya kuhitimisha katika mkoa wa MTWARA anatarajia kulekea mkoani LINDI



Share:

MASASI: WAUZA MKAA ZINGATIENI SHERIA

Wafanyabiashara wa mazao ya Misitu hasa Mkaa, Kuni na Mbao wilayani MASASI wametakiwa kufuata sheria wakati wa kuvuna  mazao hayo kwa kupata vibali vitakavyowawezesha kufanya biashara hiyo

Akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kutoa elimu juu ya sheria zinazotakiwa kufuatwa, AFISA MISITU MBWANA MILANZI amesema kuwa idara ya misitu inapita kutoa elimu juu ya sheria na taratibu za kufanya biashara ya misitu kwa mara ya mwisho na baada ya Elimu hii sheria itafuata mkondo wake.

MILLANZI  amefafanua kuwa "Sio mara ya Kwanza kwa wakala wa misitu wilani Masasi kutoa elimu hii kwa wananchi, hivyo watu wanafahamu ndio maana wakikutana na watu wa maliasili wanakimbia. Hivyo kwa anayetaka kuendelea kufanya biashara ya misitu ni lazima afuate sheria ili kulipa kodi ya serikali na kulinda misitu yetu ambayo ina faida kubwa kwa maisha ya binadamu".


Kutokana na changamoto hiyo Wakala wa Misitu Wilayani MASASI inawakumbusha wafanyabiashara wote kutambua sheria na kanuni zilizowekwa na idara hiyo ili waweze kutambulika lakini pia kuzuia uvunaji holela wa mazao Hayo hali inayopelekea uharibifu mkubwa wa misitu.
Share:

DAR ES SALAAM: TRA SASA UNAWEZA KULIPA KODI YA MAJENGO KIELEKTRONIKI

TRWito umetolewa kwa wananchi wote kuanza kulipa Kodi ya Majengo ya mwaka 2017/18 mapema kwa kuwa ulipaji wa kodi hiyo umerahisishwa  ambapo wanaweza kulipa kwa kutumia njia ya kielektroniki.

Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere alisema hakuna muda utakao ongezwa ifikapo Juni 30, mwaka huu na badala yake faini itatozwa kwa kila mmiliki wa jengo atakayechelewa kulipa kodi hiyo.

“Kama mamlaka hatuoni sababu ya kuongeza muda wa kulipa Kodi ya Majengo ifikapo tarehe 30 Juni 2018 kwasababu tumewarahisishia wananchi ulipaji wa Kodi hii ambapo wanaweza kupata ankara ya malipo kwa majengo yaliyosajiliwa kwenye tovuti ya TRA au simu ya mkononi na kufanya malipo katika tawi lolote la Benki ya NMB au CRDB popote nchini au kwa njia ya mitandao ya simu ya Mpesa, Tigopesa au Halopesa”, alisema Kichere.

Kamishna Mkuu Kichere alisema kuwa, wananchi wafuatilie matangazo ya namna ya kulipa Kodi ya Majengo kwa njia ya kielektroniki katika mitandao ya kijamii na kwenye vyombo mbalimbali vya habari au wafike katika ofisi za TRA zilizo karibu na maeneo yao nchi nzima wapate utaratibu wa kulipa kodi hiyo kielektroniki.

Kichere aliongeza kuwa Kodi ya Majengo inalipwa kwa mujibu wa Sheria hivyo, ni muhimu wananchi walipe mapema kodi hiyo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza mwishoni ikiwa ni pamoja na msongamano wa watu.

“Natoa wito kwa wananchi kwamba, wasisubiri mpaka mwisho ndio waanze kupanga foleni kwenye ofisi za TRA, wanatakiwa kulipa kuanzia sasa hivi katika ofisi zetu na wanaweza kulipa kwa kutumia njia ya kielektroniki kama nilivyoeleza hapo awali, kinyume na hapo itatubidi tutoze faini kwa atakayechelewa kulipa kodi hii ya majengo,” alisisitiza Kichere.

Kodi ya Majengo hulipwa kuanzia mwezi Julai mosi ya mwaka wa fedha husika hadi Juni 30 ya mwaka unaofuatia kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu,  hivyo, muda huu ni muafaka kwa wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo mpaka ifikapo tarehe 30 Juni, 2018.


Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>