Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi wa shule hiyo Gervas Mwanyila na kusema ni kweli tukio hilo limetokea katika shule yao japokuwa mpaka sasa hawajafahamu chanzo chake.#Moto wateketeza bweni la shule #Mbeya
Bweni la wasichana wa shule ya sekondari Kipoke mkoani Mbeya limeteketea kwa moto na kusababisha uharibifu mkubwa huku wanafunzi wawili wakijeruhiwa
Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi wa shule hiyo Gervas Mwanyila na kusema ni kweli tukio hilo limetokea katika shule yao japokuwa mpaka sasa hawajafahamu chanzo chake.
Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi wa shule hiyo Gervas Mwanyila na kusema ni kweli tukio hilo limetokea katika shule yao japokuwa mpaka sasa hawajafahamu chanzo chake.
"Ni bweni la wasichana kidato cha pili limeungua moto ambapo mpaka sasa hatujajua chanzo chake kama ni umeme au ni wanafunzi wenyewe tumeshindwa kufahamu. Tumefanya jitihada za kunusuru vitu vya wanafunzi na wao wenyewe lakini tumefanikiwa kwa kiasi kidogo kutokana na baadhi ya vitu ikiwemo magodoro na vitanda 68 kuteketea na moto", amesema Mwanyila.
Pamoja na hayo, Mwanyila ameendelea kwa kusema "ni vijana watano pekee waliojeruhiwa kidogo na moto huo baada ya wao kusaidia kukata bati ili moto usiweze kuenea katika maeneo mengine ya bweni".
Kwa upande mwingine, Mwanyila amesema bado hawajaweza kujuwa tathimini kamili ya mali za shule zilizoweza kuteketea na moto kutokana bado hawatulia tokea ajali hiyo ya moto ilipoanza
CHANZO :EATV
#UKIMWI upimwe kwa #lazima
Baraza la watu watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, Katika halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe wameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kutunga Sheria itakayopelekea watu kupima Ukimwi kwa lazima.
Hayo yamesemwa na watu wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Konga ya Mbozi wakati walipotembelewa na Kamati ya Bunge ya Ukimwi ambayo ipo ziarani mkoani humo.
Wamesema kuwa hatua hiyo itasaidia kwenye Mapambano ya Maambukizi na kuenea kwa ugonjwa huo ili kutimiza azma ya serikali ya 0.0.0 kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 hakuna Maambukizi Mapya ya Ukimwi.
Mmoja wa Waathirika hao Stephan Jonas alisema njia ya Mbadada ya kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ni kuweka sheria ya kulazimisha kila kaya kupima ugonjwa huo.
"hili suala inatakiwa liwe la lazima kwa sababu watu hawapimi, wanashindwa kujitambua hivyo wanaendelea kueneza kwa wengine sheria ikiwepo kila mtu apime kwa lazima itasaidia sana,"alisema
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Bunge, Dr Jasmini Bunga alikubalina na Ombi hilo na kueleza kuwa litasaidia mkakati wa serikali wa kukabiliana na Maambukizi mapya ya Ukimwi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la JSI linashughulika na Mifumo ya maisha na Ustawi wa Jamii Dr. Tulia Tuhuma alisema shirika lake litaendelea kufuatilia maendeleo ya Konga (Vikundi vya watu wanaoishi na Virusi vya ukimwi) pamoja na kusaidia utoaji wa huduma ya Ukimwi.
#CHADEMA yafunguka kuhusu kujitoa #uchaguzi wa kesho
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandaoni kuwa imejitoa katika uchaguzi mdogo wa marudio kwenye jimbo la #Kinondoni, Siha na kata nane nchini na kuwataka wananchi kuzipuuza taarifa hizo wazipatapo
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje- CHADEMA #John Mrema amesema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na kudai wanaofanya hivyo ni kundi cha watu wachache wenye lengo la kutaka kupotosha umma ili kesho wasiende kupigia kura.
Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje- CHADEMA #John Mrema amesema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na kudai wanaofanya hivyo ni kundi cha watu wachache wenye lengo la kutaka kupotosha umma ili kesho wasiende kupigia kura.
"Taarifa hizo ni za uongo n zinasambazwa na watu ambao wameshashindwa naomba watu wazipuuze. Tunapozungumza sasa hivi Mwenyekiti wa chama Mhe. Mbowe anahitimisha kampeni katika jimbo la Kinondoni na Mhe. Lowassa yupo kule Siha nae anahitimisha kampeni",amesema Mrema.
Pamoja na hayo, #Mrema ameendelea kwa kusema "tunaomba kuwaambia #wananchi na wanachama wa CHADEMA kuwa hiyo sio barua yetu na pia sio utaratibu kwa mujibu wa kanuni mwenyekiti wa chama kuandika barua ya kujitoa kama mtu mwenye haki ya kujitoa ni mgombea. Kwa hiyo hata hao watu walioandika hiyo barua hawajui sheria za #uchaguzi zinasemaje".
Kwa upande mwingine, Mrema amezidi kuwasisitizia wananchi kuzipuuza taarifa zozote zinazotoka sasa kuhusu kutoshiriki uchaguzi huku akiwaomba wananchi katika Jimbo la Kinondoni na Siha kujitokeza kwa wingi kesho kushiriki kupiga kura kwa sababu ni haki yao ya msingi.
CHANZO EATV
"MABAUNSA" WAPEWA ONYO
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa amewatadhahalisha watu kujiepusha na vitendo vya kihalifu ili waweze kuruhusu uchaguzi wa marudio ufanyike kwa amani na utulivu.
Kamanda Mambosasa ametoa wito huo leo (Ijumaa) wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Kinondoni Jijini Dar es Salaam na kusema Jeshi la Polisi wamepata taarifa za kiuchunguzi kuwa kuna kundi la watu wachache kutoka katika chama kimoja cha siasa ambao wamepanga kufanya vurugu kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho (Jumamosi) katika Jimbo la Kinondoni.
"Jeshi la Polisi limejipanga vizuri, uchaguzi uliopita 2015, tulikuwa na majimbo kadhaa ndani ya Dar es Salaam lakini kwa huu wa marudio tuna jimbo moja tu hili la Kinondoni na kwa sababu hiyo ni seme kwamba Jeshi la Polisi tumejipanga imara na kuhakikisha hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia na kufanya vurugu kwenye uchaguzi", amesema Kamanda Mambosasa
Pamoja na hayo, Kamanda Mambosasa ameendelea kwa kusema "nimeambiwa kwamba kuna mabaunsa lakini sijawahi kupata baunsa anayeweza kupambana na serikali halafu akabaki na ubansa wake. Namuonea huruma huyo baunsa aliyejiandaa kupambana na dola, niwashauri tu kuwa mtu haishi kwa kifua kikubwa bali anaishi kwa kutii sheria. Yeyote atakae fanya vinginevyo ajue hatobaki salama".
Kwa upande mwingine, Kamanda Mambosasa amesema ni vyema kwa mtu yeyote ambae ameshawishiwa kufanya vurugu katika zoezi la kupiga kura ni bora akijitoa mwenyewe kuliko kuingia katika matatizo kwa sababu hakuna atakayeachwa akafanya fujo kisha akaendelea kupiga hatua mbele.
CHANZO EATV
TANZANIA YASHINDA TUZO, DUBAI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshinda Tuzo za Kilele cha Serikali duniani (World Government Summit Awards) katika kundi la Tuzo ya Teknolojia bora inayoibuka Serikalini (Winner of the Best Government Emerging Technologies Award).
Tuzo hiyo ilitolewa na Mtukufu Shaikh Mansour Bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nchi, Ofisi ya Rais ya Umoja wa Falme za Kiarabu) (UAE) na kupokelewa na Balozi wa Tanzania, UAE, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk kwa niaba ya Serikali, wakati wa kilele cha Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Government Summit) uliohitimishwa jijini Dubai tarehe 13 Februari 2018.
Tuzo hiyo ilitokana na juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Kilimo ya Mikocheni (Mikocheni Agricultural Research Institute kufanikiwa kulipatia ufumbuzi tatizo la maradhi ya zao la muhogo “Cassava Brown Creek Disease,” na “Cassava Mosaic Disease,” kwa kutumia chombo cha kisasa kinachoitwa “Portable DNA Sequencer”. Maradhi hayo yanasumbua sana zao la muhogo ambalo ni zao muhimu kwa Tanzania na nchi mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla.
Kwa kutumia teknolojia hii mpya wataalamu wanaweza kugundua magonjwa mbalimbali ya zao la muhogo yanayosababishwa na wadudu, virusi, bacteria na fangasi (pathogens) kwa muda wa siku 2 tu kulinganisha na teknolojia ya zamani ambayo huchukua miezi kadhaa na ina gharama kubwa.
Zao la muhogo ni zao muhimu la chakula na biashara linalotegemewa sio tu na Tanzania bali na nchi nyingine nyingi duniani. Inakadiriwa kuwa watu wapatao millioni 800 duniani wanategemea zao la muhogo kwa chakula na biashara. Hivyo, teknolojia hii mpya itanufaisha nchi mbalimbali duniani katika kusaidia na kuendeleza zao hilo.
Nchi nyingine zilizopata Tuzo hiyo ni India na Australia.
Wakati huo huo, Watanzania wenye sifa wanahimizwa kuomba nafasi ya kazi iliyotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya mazingira (UNEP). Nafasi inayotakiwa kujazwa ni ya Chief Biodiversity Unit. Maelezo kuhusu nafasi hiyo yanapatikana katika mawasiliano http://careers.un/bw/jobdetail.aspx?id=88749 na siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni tarehe 25 Februari 2018.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Februari
2018.
POLISI KUIMARISHA ULINZI KATIKA UCHAGUZI WA KINONDONI
Jeshi la Polisi limesema siku ya uchaguzi wa mdogo wa ubunge kwa jimbo la Kinondoni kutakuwa na ulinzi mkali ili kuhakikisha mchakato wote wa masuala ya uchaguzi unafanyika katika misingi ya sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, RPC Jumanne Mlilo wakati akizungumza na wanahabari.
“Rai ya Jeshi la Polisi kwa wananchi ni kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili wawekutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kufuata sheria na taratibu watakazoelekkezwa siku hiyo na wahusika wa uchaguzi bila kuleta vurugu au wao kuwa chanzo cha vurugu,” amesema.
RPC Mlilo amesema, siku hiyo kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na polisi wa kawaida na wa FFU, kutakuwa na maji ya washawasha, huku doria ikifanyika kila sehemu itayoongozwa na askari maalumu wa kushughulikia waleta fujo.
“Jeshi halitasita kuchukua hatua za haraka za kisheria kwa mtu yeyote au kikundi chochote chenye nia ya kufanya vitendo vyovyote ambavyo ni kinyume na kanuni au sheria ya uchaguzi,” amesema.
WANANCHI WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA MVUA ZA WASTANI NA ZA MASIKA
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema mwanzoni mwa mwezi machi hadi mei mwaka huu, mvua za wastani na za masika zinatarajiwa kunyesha.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza mwelekeo wa mvua katika kipindi cha msimu wa masika.
Ametaja maeneo ambayo mvua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha mwanzoni mwa mwezi Machi, ikiwemo Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Unguja, Pemba na Uakanda wa Pwani ya Kaskazini.
Dkt. Kijazi amezitaka sekta mbalimbali kuchukua tahadhari kwa kujiandaa vyema na kuutumia utabiri huo, kwa kuwa mvua hizo zitaleta athari kutokana na vipindi vifupi vya mvua kubwa vinavyoweza kusababisha mafuriko.
Pia, ametaka wananchi kutumia kipindi hicho vizuri kwa kufanya kilimo na usalama wa mifugo, wanayammapori na chakula.
SERIKALI YAAHIDI KUREKEBISHA MAPUNGUFU KATIKA SHERIA YA MADINI
Serikali imesema iko tayari kurekebisha mapungufu yatakayobainika katika Sheria au Kanuni za Madini ili kuhakikisha wadau wote wa sekta hiyo wananufaika ipasavyo hivyo kukuza Pato la Taifa.
Hayo yalisemwa Februari 14 jijini Arusha na Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Doto Biteko wakati wa Mkutano wao na wadau wa sekta ya madini wakiwemo Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA).
Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini haitasita kufanya marekebisho katika sheria au kanuni za madini zitakazobainika kuwa kikwazo katika biashara ya madini nchini.
Akiunga mkono maneno hayo, Naibu Waziri Biteko alisema, “Sheria au Kanuni siyo Msahafu ambao hauwezi kubadilishwa hivyo pale tutakapojiridhisha kuna mapungufu, tutarekebisha kusudi mambo yaende vizuri.”
Biteko na Nyongo walisema kuwa, dhamira ya Serikali ni kuona sekta ya madini inalinufaisha Taifa ipasavyo kwa kukuza vipato vya wananchi wanaojishughulisha na shughuli za madini lakini kubwa zaidi ni kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
“Mchango wa Madini katika Pato la Taifa bado kwa sasa ni asilimia 4.2 tu. Hii ni ndogo sana. Tunaamini kuwa ikiwa sekta hii itasimamiwa vizuri, mchango wake unaweza kufikia asilimia 10 na kuendelea,” alisema Nyongo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Biteko alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuhakikisha madini yanayopatikana Tanzania, hususan Tanzanite, yanawanufaisha watanzania zaidi kuliko nchi nyingine yoyote kwani yanapatikana nchini tu. “Tumechoka kuona madini yetu wenyewe yananufaisha mataifa mengine zaidi yetu, nasi kuambulia kipato kidogo sana kisichostahili. Hili tutalisimamia kwa nguvu zetu zote na tunaamini inawezekana,” alisema.
Kauli hiyo ya Naibu Mawaziri ilikuja kufuatia vyama hivyo vya wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kuwasilisha taarifa zao katika mkutano huo; ambapo walieleza kuwa moja ya changamoto kubwa wanayoomba Serikali ifanyie kazi ni kubadili kanuni katika Sheria ya Madini inayoelekeza kuongeza thamani ya madini hapa nchini kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.
Akiwasilisha taarifa husika kwa niaba ya wanachama wa TAMIDA, Mwenyekiti wake, Sammy Mollel alisema kuwa kumekuwa na mkanganyiko kuhusu maelezo ya kanuni hiyo inayohusu uongezaji thamani madini nchini.
“Sisi tunaamini Kanuni hiyo inalenga madini ya metali na ya viwanda lakini siyo madini ya vito. Madini ya vito yakikatwa, yanapungua thamani hivyo tunaomba Serikali itufikirie katika hili.”
Hata hivyo, Naibu Mawaziri Biteko na Nyongo, wakitolea ufafanuzi zaidi suala hilo, walisema kuwa Wizara iko katika hatua za mwisho kukamilisha Mwongozo maalum utakaobainisha kila aina ya madini yanapaswa kuwa katika hali gani au kuongezwa thamani kwa kiasi gani kabla hayajatolewa kibali cha kuyasafirisha nje ya nchi. “Mwongozo huo tutautoa hivi karibuni maana kwa sasa tunaukamilisha.”
Katika hatua nyingine, Nyongo na Biteko walisisitiza ushirikiano baina ya Serikali na wadau hao wa sekta ya madini katika kufanikisha udhibiti wa utoroshaji wa madini hivyo kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki kutokana na biashara hiyo.
“Tunaomba sana mtupe ushirikiano. Tukishirikiana tutafanikiwa. Tuleteeni majina ya wanaotorosha madini pamoja na taarifa nyingine mbalimbali zinazohusu sekta hii ambazo mnahisi zinaweza kutusaidia kudhibiti suala husika.”
Akizungumzia kuhusu mabadiliko yanayoendelea kufanywa katika sekta ya madini ili kudhibiti mianya ya wizi na utoroshwaji wa madini, Naibu Waziri Biteko aliwataka wafanyabiashara na wachimbaji wa madini kuachana na dhana potofu kuwa Serikali inawachukia.
“Mkiona tunashughulika katika kipindi hiki cha mpito msidhani Serikali inawachukia. Naomba niwahakikishie kuwa Rais John Magufuli anawapenda sana wachimbaji. Lakini anachukia sana anapoona wachimbaji wanasaidia kufanya haya madini yanufaishe nchi nyingine. Sasa mtusaidie.”
Aidha, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko waliwahakikishia wachimbaji na wafanyabiashara hao wa madini kuwa, hoja zote walizoziwasilisha zitafanyiwa kazi na Serikali.
“Tumesikia hoja zote mlizowasilisha. Ni nzuri. Tumezichukua. Hii ni pamoja na suala la ushirikishwaji ambalo mmeliongelea. Sisi tutaendelea kushirikiana nanyi.”
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Gabriel Daqarro, Mbunge wa Simanjiro James Ole Millya, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Adam Juma pamoja na wataalam mbalimbali wa Wizara ya Madini.
Chanzo: Veronica Simba – Arusha
NAIBU WAZIRI SHONZA AHIDI KUSIMAMIA MAADILI YA MTANZANIA
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ameahidi kushirikiana na Watendaji wa Wizara, wadau pamoja na wananchi kwa ujumla kusimamia maadili ya Mtanzania ili kuendelea kuwa na taifa bora.
Mhe. Shonza ameyasema hayo alipowasili katika ofisi za Wizara leo mjini Dodoma ambapo alipokelewa na Waziri mwenye dhamana Dkt. Harrison Mwakyembe, viongozi wa Wizara pamoja na watumishi.
“Wizara hii ni muhimu sana kwa kuwa inajenga taswira ya taifa kupitia sekta zake ambazo ni Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo hivyo ntahakikisha tunashirikiana kwa karibu katika kuwatumikia wananchi,”alisema Naibu Waziri Shonza.
Aliongeza kwa kueleza kuwa atahakikisha suala la maadili bora kwa jamii linazingatiwa ili kuendelea kujenga taifa imara kwa kuzingatia mavazi yenye heshima na nyimbo zenye kujenga.
Aidha, Naibu Waziri Shonza amesema ni wajibu wetu kama watumishi wa umma kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya chama tawala ambacho kiliahidi kuwatumikia watanzania ili kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa kwa wakati.
Naye aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo Anastazia Wambura amempongeza Naibu Waziri Shonza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na amemshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini kuwatumikia Watanzania.
Akizungumzia utendaji kazi, Mhe. Wambura ameufananisha utumishi wa umma na chombo cha usafiri ambapo abiria hushuka kituo mara baada ya kufika na dereva kuendelea na safari.
“Mhe.Waziri, viongozi wenzangu na ndugu zangu watumishi wa Wizara, mimi nimefika kituoni, Naibu Waziri nakukabidhi kijiti endelea na safari, endelea kuwatumikia Watanzania kama ambavyo ilani ya chama tawala inavyoeleza,” alisema Mhe.Wambura
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amemuahidi Naibu Waziri Shonza ushirikiano wa hali na mali katika kuwahudumia wananchi kupitia sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Chanzo: Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma
MADINI YA RUBY KUENDELEA KUWANUFAISHA WANANCHI WA LONGIDO
Serikali imewaahidi wakazi wa Kata ya Mundarara katika Wilaya ya Loliondo kuwa itahakikisha madini ya Ruby ambayo yanapatikana katika eneo hilo yanaendelea kuwanufaisha na siyo kuwadidimiza.
Ahadi hiyo ilitolewa na Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Dotto Biteko baada ya kufanya ziara katika Mgodi unaojishughulisha na uchimbaji wa madini hayo na kisha kuzungumza na wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Nyongo na Biteko waliwataka wananchi wa Mundarara kuondoa hofu kuwa neema ya madini hayo yanayopatikana katika maeneo yao haitawanufaisha tena kutokana na kile wanachodai kuwa sheria mbalimbali zilizowekwa na Serikali zinasababisha kupungua kwa Soko lake.
Akizungumza na wananchi hao, Naibu Waziri Biteko aliwaambia kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaandaa mwongozo maalum utakaobainisha utaratibu unaopaswa kutumika katika biashara ya kila aina ya madini hapa nchini ili yaweze kuwanufaisha wananchi na Taifa ipasavyo.
“Nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha rasilimali zote zinazopatikana nchini yakiwemo madini, zinalinufaisha Taifa kwa kiwango kinachostahili. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiibiwa sana na watu wengine kunufaishwa na rasilimali zetu wenyewe ilhali sisi tunazidi kuwa maskini. Sasa tumeamua kuwa hatutaki kuibiwa tena,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi, Biteko alisema kwamba, mwongozo huo unaoandaliwa na Serikali utasaidia hata wananchi wanaozungukwa na Migodi ya Madini kunufaika zaidi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wananchi hao wa Mundarara kuwa na subira wakati Serikali ikishughulikia hoja zao walizoziwasilisha.
Hata hivyo, alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuziba mianya yote ya wizi wa rasilimali madini hivyo alitoa wito kwa wote waliozoea kufanya biashara hiyo kwa udanganyifu kuacha mara moja vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
“Mnapaswa kufanya biashara iliyo safi. Msiiibie Serikali maana tunahitaji kodi na tozo stahiki kutoka biashara hiyo ili zituwezeshe kuwaletea wananchi maendeleo ikiwemo kujenga barabara, hospitali, shule, huduma za maji safi na nyinginezo.” alisema Biteko.
Awali, akiwasilisha taarifa kwa Naibu Mawaziri kwa niaba ya wananchi wa Mundarara, Diwani wa Kata hiyo, Alais Mushao alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kadhaa, kubwa ikiwa ni kushuka kwa soko la madini ya Ruby, hali inayosababisha kushuka kwa kipato chao hivyo kurudisha nyuma maendeleo.
“Kutokana na idadi ya wanunuzi wa Ruby kuzidi kupungua siku hadi siku, inasababisha wao kujipangia bei wanayoitaka na hivyo sisi kutonufaika,” alisema Mushao.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali ya uasili wa madini ya Ruby kuwa madogomadogo husababisha kupasuka na kupukuchika. Kufuatia hali hiyo, madini hayo yanapokatwa ili kuyaongezea thamani, yanazidi kupoteza uasili na ubora wake hivyo kushusha zaidi thamani yake.
“Kwa hivyo, tunaiomba Serikali iondoe madini haya katika orodha ya madini yanayotakiwa kukatwa ili turuhusiwe kuyauza kama yalivyo, Soko lake lipande nasi tuendelee kunufaika,” alisema Diwani Mushao.
Wakihitimisha Mkutano huo, Naibu Mawaziri Nyongo na Biteko, walipongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Mwekezaji wa Mgodi na wananchi hao ambao walisema ni wa mfano wa kuigwa.
Ilielezwa kuwa pamoja na kusaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Kata husika, Mwekezaji huyo amewaruhusu wananchi kuchukua na kuchekecha udongo kutoka Mgodini pasipo kuwalipisha chochote.
chanzo: Veronica Simba, Longido















