TEMEKE : DC ASHUSHA NEEMA KWENYE SEKTA YA AFYA, ULINZI NA ELIMU
Wakati akitoa ripoti ya utekelezaji wa ilani hiyo kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM- UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, Lyaniva amesema ofisi yake inahakikisha inaimarisha hali ya ulinzi na usalama, ambapo kwa sasa inajenga vituo vikubwa viwili vya Polisi maeneo ya Chamanzi na Toangoma, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Kwa upande wa sekta ya afya, Lyaniva amesema kuna vituo viwili vya afya vya kisasa vinajengwa katika Kata ya Yombo na Majimatitu ambapo vitakuwa na wodi ya kinamama na vyumba vya operesheni, ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali za Temeke na Zakhiem.
Kuhusu sekta ya elimu, Lyaniva amesema wanaongeza madarasa kwenye baadhi ya shule za msingi ili kupunguza msongamano wa wanafunzi hali iliyosababisha na utekelezwaji wa sera ya elimu bila malipo ambapo wazazi wengi wamekuwa na mwamko wa kuwaandikisha watoto wao shule.
“Suala la elimu bila malipo wananchi wameliitikia vizuri sana sababu wameweza kujitokeza wengi kuwaandikisha watoto wao shule, shule ya Majimatitu imeongoza kwa uandikishaji, ikifuati mbande. Palipokuwa na elimu ya malipo watu walikuwa majumbani wengi sana, nina uhakika hatutakuwa na watoto nyumbani, sasa hivi uhalifu umepungua hatuna kundi la kumi nje kumi ndani kwa kuwa watoto wanaenda shule,” amesema.
MWENYEKITI, AFISA MTENDAJI MBARONI KWA KUKODISHA RAIA WA BURUNDI HEKARI 100
Viongozi hao walikamatwa jana baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Kakonko kufanya operesheni ya ukaguzi wa usalama wa mipaka ya Tanzania.
Mkuu wa Wialaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala alisema awali walipata taarifa za tukio kutoka kwa raia wema kwamba kuna warundi wanaokuja kwenye mipaka ya nchi kinyume na sheria.
“Baada ya kukuta hali hiyo waliamua kumkamata Mwenyekiti wa Kijiji na Mtendaji na baadhi ya warundi waliokuwa katika mashamba hayo na wanaendelea na mahojiano na polisi baada ya hapo watafikishwa mahakamani,” alisema.
DAR ES SALAAM: Upande Wa Mashtaka Wafunga Ushaidi Kesi Ya Wema Sepetu
Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu na wenzake jana ulidai mahakamani kuwa umefunga ushahidi dhidi ya mashtaka kutumia na kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi kwa msanii huyo.
Madai hayo yalitolewa jana na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakati wa kusikiliza ushahidi wa shahidi wa nne na wa tano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Awali, shahidi wa nne, mjumbe wa nyumba 10, Steven Ndonde alidai mahakamani hapo kuwa siku ya tukio aliitwa kushuhudia upekuzi nyumbani kwa Sepetu.
Alidai kuwa wakati upekuzi unaendelea walikuta kipisi cha msokoto katika chumba cha nguo na viatu cha msanii huyo na chumba cha mfanyakazi wake walikuta kipisi kingine.
Hata hivyo, shahidi huyo alipohojiwa na wakili wa utetezi Albart Msando alikana kuwakuta washtakiwa wote wakiwa na dawa za kulevya aina ya bangi katika upekuzi huo.
Shahidi wa tano, Koplo wa Polisi Robert (31), alidai kuwa Februari 4, 2017 alipokea maagizo kutoka kwa bosi wake ya kupeleka vielelezo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ikiwamo msokoto mmoja na vipisi viwili vya dawa za kulevya idhaniwayo kuwa bangi.
"Nilipeleka, vilipokelewa ofisi ya mkemia mkuu, baada ya kupokelewa niliandika barua kuhusu vielelezo hivyo," alidai Koplo Robert.
Kakula alidai baada ya kuita mashahidi watato dhidi ya washtakiwa upande wa Jamhuri imefunga kesi yao.
"Mheshimiwa hakimu tunaiachia mahakama iamue sisi upande wa Jamhuri tumefunga kesi yetu..." Alidai Kakula.
Wakili Msando aliomba upande wa utetezi kuwasilisha hoja za kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la ndani ya siku 10.
Upande wa Jamhuri ulidai utawasilisha majibu Aprili 3, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.
Mbali na Sepetu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Angelina Msigwa na Matrida Abbas.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.
Inadaiwa kuwa Februari 4, mwaka jana katika makazi ya Wema huko Kunduchi Ununio, washtakiwa hao walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Ilidaiwa kuwa Februari mosi, mwaka jana katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam, Sepetu alitumia dawa za kulevya aina ya bangi. Washtakiwa walikana mashitaka.
ARUSHA: Mwakyembe Kuwashitaki kwa Waziri Mkuu Maofisa Habari Wazembe
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema atawasilisha kwa Waziri Mkuu majina ya maofisa habari wazembe, ili watumbuliwe.
Alisema hayo kufuatia uzembe unaofanywa na baadhi yao huku wakibweteka kukaa maofisini bila kufanya kazi.
Alisema maofisa habari wasiojituma ni sawa na kuwa na maofisa habari hewa, ambao wanakula mishahara wasioifanyia kazi, jambo ambalo hakubaliani nalo.
Dk. Mwakyembe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa kazi wa siku tano wa maofisa habari, mawasiliano na uhusiano serikalini, unaofanyika jijini Arusha, aliwataka kubadilika na kutekeleza malengo waliojiwekea.
"Kweli naangalia tovuti za halmashauri zipo tisa tu zinazofanya vizuri, zingine wahusika wamelala; na mikoa 18 tu inafanya vizuri kuhabarisha, sasa hawa wengine wajitathmini vinginevyo nitapeleka majina yao kwa Waziri Mkuu, ili watumbuliwe, tutoe ajira kwa wengine," alisema.
Aliwataka wafanye kazi ya kuhabarisha wananchi kazi zinazofanywa na serikali, ili wasitumbuliwe.
Alisema hata wizara husika pia wapo wazembe nao atapeleka taarifa ngazi ya juu ili wachukuliwe hatua, lengo kazi nzuri zinazofanywa na serikali zitambulike kwa wananchi na kuziba mianya kwa wapotoshaji wa taarifa za serikali.
Dk. Mwakyembe aliwataka maofisa habari hao kujituma na kutoa taarifa za kazi zinazofanyika kila siku kwenye mitandao ya kijamii na endapo watazuiwa na mtu yeyote, wawafichue hata kwa siri ili wizara ishughulike na muhusika.
Naye Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez, aliwataka maofisa habari hao kubadilika na kuleta tija kwa taifa baada ya mkutano huo kuisha.
Alisema dunia sasa imeunganishwa kwa teknolojia, hivyo ni vema jamii ikapata taarifa zilizo sahihi kwa wakati.
Aidha, alisema serikali pia inahitaji kusikiliza jamii na sauti za wananchi, ili kupiga hatua katika kufikia Tanzania ya Viwanda.
“Sisi kama wadau tunahitaji kusikia zaidi habari za wananchi wa vijijini, ili tuone jinsi wanavyobadilika katika hali walizonazo,” alisema.
DAR ES SALAAM: Sababu za mashahidi Kutofika Mahakamani kesi ya Mfanyakazi wa TRA anaemiliki magari 19
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imesema itaanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri dhidi ya kesi inayomkabili Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Jennifer Mushi anayekabiliwa na tuhuma za kumiliki magari 19 na kuishi maisha ya juu kuliko kipato chake kama mtumishi yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 530.8.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa kuwa mashahidi hawajapatikana kutokana na kuwa na majukumu mengine.
Wakili wa Serikali Vitalis Peter alidai kuwa kutokana na mashahidi kuwa na majukumu mengine ya serikali wameshindwa kuwapata kwenda kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa huyo.
Hakimu alisema mahakama yake itaanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri Aprili 9.
Katika kesi ya msingi, Peter alidai kati ya Machi 21, 2016 na Juni 30 mwaka huo mahali tofauti jijini Dar es Salaam, akiwa mtumishi wa TRA, mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki mali zisizolingana na kipato chake, kinyume na sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Alitaja mali hizo kuwa ni magari 19 ya Toyota Rav4, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark II, Toyota Regius, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Passo na Suzuki Carry, yote yakiwa na thamani ya Sh. milioni 197.6.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kati ya Machi 21, 2012 na Machi 30, 2016 jijini Dar es Salaam akiwa mwajiri wa TRA aliishi maisha ya hali ya juu tofauti na kipato chake, yenye thamani ya Sh. 333,255,556.24.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yatahadharisha mvua kubwa mikoa 11
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya vipindi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa kuendelea katika maeneo ya mikoa 11 nchini.
TMA imetaja mikoa itakayoathirika na mvua hizo ni Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe.
Taarifa iliyotolewa leo na mamlaka hiyo inabainisha kuwa kuanzia leo Machi 12 hadi 13 ,2018 kunatarajiwa vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24.
“Hali hii inatokana na kuendelea kuimarika kwa ukanda wa mvua, wakazi wa maeneo yaliyotajwa wanatakiwa kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa na tahadhari zinazotolewa, TMA inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejesho kila itakapobidi,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Rais Magufuli kuongoza mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC)
Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limeandaa Mkutano wa 11 wa Baraza ambao utaongozwa na Rais John Magufuli wiki hii.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Raymond Mbilinyi, Amesema kuwa mkutano huo unaonyesha dhamira iliyonayo serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli ya kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.
“Mkutano huu wa Baraza ni muhimu sana sekta za umma na binafsi kwani unatoa fursa kwa pande mbili hizi kujadiliana namna bora ya kujenga mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji zaidi kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Mbilinyi.
Alisema mkutano utafanyika tayari kukiwa na mafanikio makubwa chini ya awamu ya Tano ambapo viwanda zaidi 3,500 vikiwa vimeshaanzishwa katika kipindi kifupi tu cha uongozi wa Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza.
“Huu utakuwa ni mkutano wake wa pili kuuongoza kama Mwenyekiti wa Baraza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Mkutano wake wa kwanza umeleta mafanikio mengi katika sekta za umma na binafsi,” alisema na kuwa utafanyika Jumapili.
Mbilinyi alisema serikali ya awamu ya tano imesimamia mabadiliko mbalimbali yaliyolenga kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda.
GEITA: Mwili wa marehemu watelekezwa nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Nyakabale wilayani Geita wametelekeza mwili wa marehemu nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa huu, Elias Ndarawa.
Ndarawa anatuhumiwa kutoshughulikia tukio la Zacharia Shaban kupigwa na polisi jamii hadi kufa.
Wananchi hao waliubeba mwili wa Zacharia na kuulaza kwenye kitanda cha mwenyekiti huyo.
Majaliwa Shaban ambaye ni ndugu wa marehemu Zacharia amesema leo Machi 12,2018 kwamba nduguye alipigwa Machi 5,2018 akiwa eneo la Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) akiokota mabaki ya mawe ya dhahabu maarufu magwangala.
Amesema Zacharia alipelekwa polisi alikokaa kwa siku sita na aliporudi uraiani hali yake ilikuwa mbaya.
Majaliwa amesema nduguye alipelekwa hospitali alikofariki dunia Jumamosi Machi 10,2018 na hadi sasa hakuna kiongozi aliyefika kwenye msiba huo wala kutoa kauli yoyote.
Mkazi wa mtaa huo, Johnson John amesema hawapo tayari kuzika hadi Serikali itakapotoa kauli kuhusu hatima ya maisha yao kwa kuwa polisi jamii wamekuwa wakiwapiga na kuwajeruhi.
Jana, Machi 11,2018 wananchi walivamia eneo la kituo cha polisi jamii kilichopo mtaa wa Manga na kukichoma moto kwa madai kwamba wamempiga na kumuua Zacharia
CHANZO: MPEKUZI
DODOMA: Spika Job Ndugai apangua kamati za Bunge
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Machi 12,2018 inasema Spika amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa Ibara ya 96 ya Katibu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa hiyo imesema ibara hiyo imeweka wazi kwamba, Kanuni za Kudumu za Bunge zinafafanua muundo wa shughuli za Kamati za Bunge.
“Kwa msingi huo Kanuni ya 118 ya Kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 imeweka Kanuni za Kudumu za Bunge zenye muundo na majukumu mbalimbali kama yanavyofafanuliwa katika nyongeza ya nane. Uteuzi wa wabunge kwenye kamati mbalimbali unaonekana utaratibu katika Kanuni ya 116.”
“Kanuni ya 116(1) inaweka utaratibu kwamba, ujumbe kwenye Kamati za Kudumu za Bunge utadumu mpaka mwisho wa Mkutano wa Kumi wa Bunge ambao ni nusu ya kwanza ya maisha ya Bunge,” anasema Spika Ndugai.
Katika uteuzi huo, wajumbe mbalimbali wamerejea katika kamati zao, wengine wakibadilishwa huku baadhi ya wenyeviti waliokuwa wakiongoza baadhi ya kamati wameondolewa.
“Kwa mamlaka niliyopewa na Kanuni ya 115(3) na kwa kuzingatia vigezo vilivyoanishwa katika Kanuni ya 116(5) nimefanya uteuzi mpya wa ujumbe katika Kamati za Kudumu za Bunge. Wajumbe wa kila kamati wanawajibika kuchagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti kwa mujibu wa Kanuni ya 116(10) kuwa viongozi wao,” amesema.
DAR ES SALAAM: Maria Tsarungi kumburuza mahakamani mhariri wa gazeti la Tanzanite
Mjasiriamali/Mwanahabari na
Mkurugenzi wa Compass Communications, Maria Sarungi amefungua kesi ya madai
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya Mhariri wa Gazeti la Tanzanite
na Mwanasheria Cyprian Musiba kwa kumkashifu na kuchafua jina lake kupitia
mkutano wake na Waandishi wa Habari uliyofanyika tarehe 25 Februari, 2018.Barua hiyo iliyotolewa na Mwanasheria wa Maria Sarungi, Benedict Alex Ishabakaki imeeleza kuwa mteja wake alitajwa na gazeti la Tanzanite toleo Namba 50 lililotoka Februari 26, 2018 kuwa ni moja ya watu hatari kwenye usalama wa taifa.
Kwa upande mwingine, barua hiyo imeitaka Blog ya Dar24 kufuta habari hiyo na kuomba radhi hadharani kwa kitendo cha kuandika habari hiyo yenye lengo la kumfedhehesha mteja wao.

CHANZO: MUUNGWANA











