
“Kuruthumu amepatiwa msaada wa shilingi 300,000 kwa ajili ya gharama za ununuzi wa kiatu hicho maalumu. Huu ni mwanzo mpya kwa maisha yake, kwani sasa ataweza kushiriki ipasavyo katika shughuli za kila siku bila kikwazo kikubwa cha utembeaji”
Na Msafiri Kipila
Katika jamii yenye changamoto mbalimbali, watu wenye ulemavu mara nyingi hukumbwa na hali ngumu ya maisha, hususan kwa wale wanaohitaji vifaa maalumu ili kuweza kuendesha maisha yao ya kila siku. Hali hiyo imekuwa ikiwakwamisha katika kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi. Hata hivyo, kuna nuru ya matumaini kupitia moyo wa huruma kutoka kwa wadau na viongozi wa jamii.
Miongoni mwa walionufaika na msaada huo ni Bi. Kuruthumu Seifu Mohamed, mama mwenye ulemavu wa mguu ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihitaji kiatu maalumu ili aweze kutembea kwa urahisi. Kupitia juhudi za wadau wa haki na maendeleo ya watu wenye ulemavu, Kuruthumu amepatiwa msaada wa shilingi 300,000 kwa ajili ya gharama za ununuzi wa kiatu hicho maalumu. Huu ni mwanzo mpya kwa maisha yake, kwani sasa ataweza kushiriki ipasavyo katika shughuli za kila siku bila kikwazo kikubwa cha utembeaji.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake na Wasichana Wenye Ulemavu Mtwara Mikindani, amethibitisha kuwa fedha hizo zimepokelewa rasmi na kumfikia mhusika. Aidha, ametumia fursa hiyo kuhamasisha jamii iendelee kujitokeza kusaidia watu wenye ulemavu, kwani bado kuna changamoto nyingi zinazowakabili.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mtwara, Mhe. Anastazia Wambura, ameeleza kuguswa na hali wanayopitia watu wenye ulemavu. Amesema kuwa amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu hao wanapata usaidizi unaowasaidia kujikwamua kimaisha. “Nimekuwa nikifanya hivi mara kwa mara, lengo ni kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki katika shughuli za maendeleo kama watu wengine,” alisema Mhe. Wambura.
Msaada huu kwa Bi. Kuruthumu ni mfano hai wa jinsi mshikamano wa kijamii na uongozi wenye maono unavyoweza kuleta mabadiliko katika maisha ya watu wanaohitaji msaada. Ni wito kwa jamii nzima kuendelea kuwathamini, kuwaunga mkono na kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika nyanja zote za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.






No comments:
Post a Comment