
CRDB Bank Foundation imekabidhi Pikipiki, Bajaji na Guta zenye thamani ya shilingi milioni 140 kwa vijana wa Mtwara, kuendeleza mikopo nafuu kwa ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Vijana
Na Musa Mtepa
Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, imekabidhi Pikipiki, Bajaji na Guta mkoani Mtwara ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mikopo inayotolewa kwa kushirikiana na wizara hiyo kwa vijana wa Kitanzania.
Akizungumza kuhusu mikopo hiyo Machi 2, 2026, Meneja Mwandamizi wa CRDB Bank Foundation anayesimamia mikopo yenye masharti nafuu ambaye pia ni msimamizi wa uhusiano na ubia na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, Baraka Kiyaro, amesema wamekabidhi Bajaji 5, Guta 5 na Pikipiki 15 zenye thamani ya shilingi milioni 140 kama sehemu ya mwendelezo wa mikopo inayotolewa kwa kushirikiana na Wizara ya Vijana.

Pamoja na hayo, Baraka Kiyaro amesema pia wameingia makubaliano na wizara mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu nchini. Amesema wanawasaidia kwa kuwajengea uwezo kupitia elimu ya fedha, kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali pamoja na kuwatafutia masoko ili kuwaondoa kwenye mikopo chechefu maarufu kama “kausha damu”.
Aidha, Baraka amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa vijana kujitokeza kupata mikopo hiyo, hali inayoonesha kuheshimu na kufurahia jitihada zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya vijana.
Naye meneja CRDB kanda ya kusini, Emmanuel Biganio, amesema tangu kuanzishwa kwa CRDB Foundation mwaka 2023, imeweza kuwafikia vijana laki saba na ishirini (720,000), huku zaidi ya shilingi bilioni 20.1 zikitolewa kama mikopo na mitaji wezeshi. Amesema makubaliano na wizara ni kuongeza kasi zaidi katika utekelezaji wa malengo yaliyowekwa na Wizara ya Vijana.

Mikopo hiyo imetolewa Machi 2, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) mkoa wa Mtwara uliofanyika katika Chuo cha Stella Maris Mtwara, ambapo zaidi ya vijana 25 wamenufaika na mikopo hiyo.


























