Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja
Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao
Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii
Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm
Tofali zikiandaliwa kwa ajili ya ujezni wa Jengo la utawala la soko la kijiji cha Nanguruwe (Picha na Musa Mtepa)
Wananchi wa kijiji cha Nanguruwe wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kusaidia ujenzi wa soko la kisasa la bidhaa na vyakula ili kuboresha huduma za kibiashara. Ujenzi huo unafanywa kwa nguvu za wananchi na unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 70, huku wafanyabiashara zaidi ya 100 wakinufaika
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kijiji cha Nanguruwe wameiomba Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuchangia na kusaidia ujenzi wa soko la bidhaa na vyakula unaoendelea kujengwa katika kijiji hicho.
Wakizungumza na Jamii FM Redio Januari 17, 2026, wananchi hao wamesema kuwa kutokana na ukuaji wa kasi wa kijiji chao, viongozi wa kijiji wameamua kuanzisha ujenzi wa soko la kisasa ili kuwaondolea adha wakazi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kibiashara eneo la Barabarani.
Sauti ya wananchi wa kijiji cha NanguruweEneo linalotarajiwa kujengwa kwa soko la kijiji cha Nanguruwe (Picha na Musa Mtepa)
Akizungumza kuhusu ujenzi wa soko hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanguruwe, Bw. Saidi Mandova, amesema kuwa sababu kubwa ya uamuzi huo ni matumizi ya soko moja kwa vijiji vitatu kwa muda mrefu, hali iliyokuwa ikikisababishia kijiji kukosa mapato yatokanayo na shughuli za kibiashara.
Bw. Mandova ameongeza kuwa ujenzi wa soko hilo unatekelezwa kwa nguvu za wananchi wenyewe, huku akiomba wadau wa maendeleo kujitokeza kusaidia ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Sauti ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nanguruwe
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Nanguruwe, Bw. Saidi Hamisi, ameelezea hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo na kufafanua kuwa ujenzi unaendelea vizuri licha ya changamoto chache za upungufu wa rasilimali.
Ameongeza kuwa hadi kukamilika, ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 70, huku zaidi ya wafanyabiashara 100 wakitarajiwa kunufaika na huduma za soko hilo.
Sauti ya Afisa Kaimu Mtendaji wa kijiji cha NanguruweEneo lililopangwa kwa ajili ya kujenga vibanda vya Wafanyabiashara katika soko la kijiji cha Nanguruwe(Picha na Musa Mtepa)
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala akizungumza na wajumbe kwenye kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika Januari 8, 2026 katika ukumbi wa BoT Kanda ya Mtwara (Picha na Musa Mtepa)
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameitaka TANROADS kuongeza usimamizi kwa mkandarasi wa barabara ya Mnivata–Masasi baada ya mradi kusuasua. TANROADS imesema chanzo ni mkandarasi na hatua tayari zimechukuliwa kuharakisha ujenzi
Na Musa Mtepa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mtwara kuendelea kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya uchumi ya Mnivata–Tandahimba–Newala–Masasi yenye urefu wa kilomita 160 kwa kiwango cha lami, ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora unaotakiwa.
Kanali Sawala ametoa maelekezo hayo Januari 8, 2026, wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mtwara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Kanda ya Mtwara, Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Amesema utekelezaji wa mradi huo haujaenda kwa kasi ya kuridhisha, hali iliyomlazimu kuielekeza TANROADS kuongeza usimamizi kwa mkandarasi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa.
Sauti ya Kanali Patrick Sawala, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
Kwa upande wao, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdaa Dadi Chikota, pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Newala, Yusuf Kateule, wamehoji changamoto halisi inayomkabili mkandarasi huyo, wakitaka kufahamu iwapo kuchelewa kwa mradi kunasababishwa na ukosefu wa fedha au uzembe wa mkandarasi mwenyewe.
Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Newala na Mbunge Chikota
Akizungumzia kusuasua kwa mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara, Emil Zengo, amesema tayari wamemwondoa msimamizi mkuu wa mkandarasi na kumleta msimamizi mwingine, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo.
Aidha, amesema kuwa kuhusu ujenzi wa barabara za mchepuko, amemuelekeza mhandisi mshauri kumkata mkandarasi malipo yanayohusiana na kazi ambazo hazijatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.
Sauti ya 1 Emil Zengo, Meneja TANROADS Mkoa wa MtwaraMeneja TANROADS Mkoa wa Mtwara Emil Zengo akiwasilisha hali ya Barabara na utekelezaji wa miradi Mbalimbali inayotekelezwa katika mkoa wa Mtwara(Picha na Musa)
Akijibu maswali kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Newala na Mbunge wa Nanyamba kuhusu iwapo chanzo cha kusuasua kwa mradi huo ni fedha au mkandarasi, Meneja wa TANROADS amesema chanzo kikuu ni mkandarasi, huku akisisitiza kuwa hatua stahiki tayari zimechukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Sauti ya 2 Emil Zengo, Meneja TANROADS Mkoa wa Mtwara
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Ibrahim Mjanakheri Ibrahim, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa, amesema CCM inaunga mkono azimio la kuitaka TANROADS kuharakisha kwa kasi zaidi ujenzi wa barabara hiyo ya uchumi kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara Ibrahim Mjanakheri Ibrahim akizungumza na wajumbe wa kikao cha Bodi ya barabara kilichofanyika Januari 8,2026 katika ukumbi wa BOT kanda ya Mtwara(Picha na Musa Mtepa)
Tanki la maji liliojengwa katika kijiji cha Makome B ambao ni mradi unaohusisha vijiji viwili vya Makome A na B ambao ujenzi wake umefikia asilimia 65(Picha na Musa Mtepa)
Wananchi wa Makome B wameiomba Serikali kupitia RUWASA kukamilisha mradi wa maji uliosimama ili kumaliza uhaba wa maji safi unaosababisha magonjwa na changamoto za kijamii.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kijiji cha Makome B kilichopo kata ya Mbawala,Halmashauri ya Mtwara vijijini, Mkoani Mtwara wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha mradi wa maji unaojengwa katika kijiji hicho ili kuondokana na adha ya uhaba wa maji safi na salama inayowakabili.
Wakizungumza na waandishi wa habari January 6 ,2026 wananchi hao wamesema kuwa kutokana na kukosekana kwa maji safi na salama, wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali za kiafya na kijamii, hali inayotokana na matumizi ya vyanzo vya maji vya asili ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu.
Wakazi wa kijiji hicho, Mwanahamisi Mitole na Sinani Kibwana, wamesema tatizo la maji limesababisha kuongezeka kwa magonjwa ya tumbo, hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali pamoja na migogoro ya kifamilia, hali inayohatarisha ndoa zao. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wameomba wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kukamilisha mradi wa maji uliosimama katika kijiji hicho.
Sauti ya Mwanahamisi Mitole na Sinana Kibwana, wakazi wa Makome BWananchi wa kijiji cha Makome B wakiteka Maji katika kisima cha asili kilichopo kijijini hapo(Picha na Musa Mtepa)
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Makome B, Ndugu Salumu Liwingu, amekiri kuwa hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho ni mbaya, kwani wananchi wanategemea maji yanayotiririka kutoka maeneo mbalimbali ambayo si salama, hali inayochangia wananchi kupata magonjwa ya tumbo mara kwa mara.
Sauti ya Salumu Liwingu, Mwenyekiti wa kijiji cha Makome BSalumu Liwingu, Mwenyekiti wa kijiji cha Makome B(Picha na Musa Mtepa)
Akizungumzia mradi wa maji unaojengwa kijijini hapo, Mwenyekiti huyo amesema mradi huo umeingia mwaka wa tatu tangu kuanza kwake. Ameeleza kuwa mradi huo ulizinduliwa rasmi mwaka 2024 wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, lakini maji yalitoka kwa takribani dakika tano pekee na tangu hapo hakuna maji yaliyowahi kutoka tena.
Sauti ya Salumu Liwingu, Mwenyekiti wa kijiji cha Makome B
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mtwara, Abdulaziz Hemedi, amesema mradi wa maji wa Makome umefikia asilimia 65 ya utekelezaji, huku asilimia 41 ya fedha za mradi zikiwa tayari zimeshalipwa kwa mkandarasi. Amesema changamoto mbalimbali zimejitokeza na kusababisha mradi huo kushindwa kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa Makome A na B, hali iliyopelekea RUWASA kufikiria kuvunja mkataba na mkandarasi husika.
Sauti ya Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya MtwaraMwonekano wa kisima cha asili cha maji kinachotumiwa na wananchi wa Makome B kunywa,kuoshea na kuogea(Picha na Musa Mtepa)
Aidha, amesema mkataba wa ujenzi na ukamilishaji wa mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2025, na kufikia wakati wanapofikiria kuvunja mkataba, utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 65.
Sauti ya Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya MtwaraMwonekano wa baadhi ya Bomba zilizo telekezwa porini baada ya mkandarasi wa kutokamilisha ujenzi wa mradio huo(Picha na Musa Mtepa)
Hata hivyo, Kaimu Meneja huyo amesema pamoja na mchakato wa kuvunja mkataba na kumpata mkandarasi mpya wa kukamilisha mradi huo, wananchi wa vijiji vya Makome A na B wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Sauti ya Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mtwara
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Maji na ofisi mbalimbali za Serikali, hadi kufikia mwezi Julai 2025 upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya vijijini umefikia asilimia 83 na Sera ya Taifa ya Maji ikisisitiza upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa kuhusisha jamii, sekta binafsi pamoja na kulinda rasilimali za maji ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wote wa vijijini.
Wananchi wa kijiji cha Makome B wakiwa njiani kuelekea Nyumbani wakitokea Kisimani kuteka maji(Picha na Musa Mtepa)
Eneo linalotarajiwa kujenga Msikiti katika mtaa wa Shule ya msingi Majengo kata ya Tandandika Manispaa ya Mtwara Mikindani (Picha na Musa Mtepa)
Wanafunzi waliowahi kusoma Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi wamechangia shilingi 525,000/= kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo, Manispaa ya Mtwara
Na Musa Mtepa
Wanafunzi waliowahi kusoma Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi iliyopo Manispaa ya Mtwara ya Mikindani, wamechangia jumla ya shilingi laki tano na elfu ishirini na tano (525,000/=) kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa mtaa wa shule ya msingi Majengo.
Akizungumza leo Januari 5, 2026 mara baada ya kukabidhi mchango huo katika eneo linalotarajiwa ujenzi wa Msikiti huo, mwanajumuia wa wanafunzi hao, Hamdani Swalehe Amlima, amesema kuwa wao kama wadau waliamua kuwashirikisha wenzao waliowahi kusoma Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi ili kuona namna wanavyoweza kusaidia ujenzi huo, hatua iliyowezesha kupatikana kwa mchango huo.
Sauti ya Hamdani Swalehe Amlima – MwanajumuiaMwanajumuia ya wanafunzi waliowahi kusoma shule ya Sekondari Mtwara Ufundi akikabidhi fedha shilingi 525,000/= kwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Msikiti(Picha na Musa Mtepa)
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Msikiti huo, Mzee Musa Napinda, ameishukuru jumuia hiyo kwa mchango wao akisema kuwa fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa katika hatua za awali za ujenzi wa Msikiti huo.
Aidha, Mzee Napinda ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa maendeleo pamoja na waumini mbalimbali kujitokeza kuchangia ujenzi wa Msikiti huo ili kuwasaidia waumini wa Kiislamu katika eneo hilo kupata sehemu ya karibu ya kufanyia ibada.
Sauti ya Mzee Musa Napinda – Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Msikiti
Nao baadhi ya viongozi na waumini wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo wameishukuru jumuia hiyo pamoja na Diwani wa kata hiyo kwa kuhamasisha na kufanikisha upatikanaji wa mchango huo, huku wakiomba taasisi, wadau na waumini wengine kujitokeza ili kufanikisha ujenzi wa Msikiti huo.
Sauti ya waumini na viongozi wa mtaa unaojengwa MsikitiMhe; Diwani wa kata ya Tandika Al-Hajji Haroun Selemani Haroun akiwa na baadhi ya viongozi wa kamati ya ujenzi wa Msikiti wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo(Picha na Musa Mtepa)
Naye Diwani wa Kata ya Tandika, ambako Msikiti huo unatarajiwa kujengwa, Al-Hajji Haroun Selemani Haroun maarufu kama Chai Jaba, amewashukuru wakazi wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo pamoja na wanajumuia wa Mtwara Ufundi kwa moyo wao wa kujitolea na kushiriki katika kutoa sadaka hiyo (Swadakati Jaria).
Sauti ya Al-Hajji Haroun Selemani Haroun – Diwani wa Kata ya Tandika
Mkurugenzi wa jamii fm radio Ndug Swallah Saidi Swallah akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa tuzo,wasikilizaji wa vipindi na wafanyakazi wa kituo hicho(Picha na Mohamedi Masanga)
Jamii FM Redio imetangaza wasikilizaji na wachangiaji bora wa vipindi vyake kwa mwaka 2025. Washindi walichaguliwa na wasikilizaji kupitia SMS na kukabidhiwa tuzo katika hafla iliyofanyika katika studio za kituo hicho
Na Musa Mtepa
Jamii FM Redio imetangaza wasikilizaji na wachangiaji bora wa vipindi vyake kwa mwaka 2025, katika hafla iliyofanyika Jumatano Desemba 31, 2025, katika kituo cha kurushia matangazo cha Jamii FM Redio kilichopo Mtwara.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio, Bw. Swallah Said Swallah, alimtangaza Ndg. Mambo Katani, mtoto wa Fatu Mohamedi Kumbuko kutoka kijiji cha Rondo Ntene, Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi, kuwa msikilizaji na mchangiaji bora wa kiume. Aidha, Bi. Amina Mkanjima, binti wa Mkanjima maarufu kama Mama wa Yanga (Mama Bakari Kitemwe) kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani, alitangazwa kuwa msikilizaji na mchangiaji bora wa kike.
Sauti ya Swallah Said Swallah, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio
Bw. Swallah amesema kuwa utaratibu wa kutambua na kuwazawadia wasikilizaji na wachangiaji bora ulianza rasmi mwaka 2024 na utaendelea kila mwaka, huku kituo kikiendelea kuboresha mifumo ya upatikanaji wa washindi pamoja na thamani ya zawadi zitakazotolewa kadri miaka inavyoendelea.
Sauti ya Swallah Said Swallah, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio
Akizungumzia malengo ya kituo hicho, Bw. Swallah ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Jamii FM chini ya MTUKWAO Community Media kunalenga kuibua, kuchakata na kurusha taarifa za kijamii ambazo mara nyingi hazipewi nafasi katika vyombo vingine vya habari na kubainisha kuwa lengo la MTUKWAO COMMUNITY MEDIA kuwa na kituo hicho cha redio na televisheni ya kijamii (Community Television – CTV).
Sauti ya Swallah Said Swallah, Mkurugenzi wa Jamii FM Redio
Uchaguzi wa washindi ulifanyika kwa kuwashirikisha wasikilizaji wenyewe kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), ambapo walipiga kura kumchagua msikilizaji na mchangiaji bora wa kike na wa kiume.
Nao baadhi ya washiriki waliofanikiwa kufika hatua ya washiriki 15 bora wameipongeza Jamii FM Redio kwa kuandaa tuzo hizo, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza hamasa ya ushiriki wa vipindi na kuwapongeza washindi waliopata tuzo kwa mwaka 2025.
Sauti ya washiriki wa tuzo za uchangiaji na usikilizaji bora
Kwa upande wao, Bi. Amina Mkanjima na Ndg. Mambo Katani, washindi wa tuzo za msikilizaji na mchangiaji bora kwa mwaka 2025, wameishukuru Jamii FM Redio pamoja na wasikilizaji wote kwa kuwaamini na kuwachagua. Pia wametoa wito kwa wasikilizaji wengine kuendelea kufuatilia na kuchangia vipindi vya redio hiyo kwa kuzingatia maadili, utaratibu na kuheshimu haki za wengine bila kumdhuru mtu yeyote.
Sauti ya washindi wa tuzo
Naye Meneja wa Jamii FM Redio, Bw. Amua Rushita, amewashukuru wasikilizaji wa Jamii FM Redio kwa kuendelea kuisikiliza redio hiyo kwa mwaka 2025, huku akiukaribisha mwaka 2026 kwa kauli mbiu isemayo “Mtaa kwa Mtaa.”
Jumla ya washiriki kumi na tano (15) walichaguliwa kufikia hatua ya mwisho ya mashindano, ambapo wawili kati yao waliibuka washindi.
Washindi wamekabidhiwa zawadi ya redio aina ya Subwoofer yenye thamani ya shilingi laki moja na elfu hamsini (Tshs 150,000/=) kila mmoja.
Watumiaji wa kivuko cha Mv Kilambo wakilazimika kuvuka kwa kutumia Boti ndogo kulekea nchi jirani ya Msumbiji(Picha na Musa Mtepa)
Wananchi wa Kilambo na maeneo ya mpakani na Msumbiji wanaiomba Serikali kurejesha kivuko cha MV Kilambo kilichosimama kufanya kazi, Serikali imesema matengenezo yanaendelea
Na Musa Mtepa
Wananchi na watumiaji wa kivuko cha Kilambo kinachounganisha Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji wamehoji ni lini kitarejea na kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kurejesha huduma ya feri ya MV Kilambo, ili kuondoa usumbufu na gharama kubwa wanazokumbana nazo kwa sasa.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wakazi wa eneo hilo wamesema hali ya usafiri si ya kuridhisha, kwani wanalazimika kutumia viboti vidogo kuvuka mpaka wa maji, ambavyo si salama na vina gharama kubwa ikilinganishwa na huduma ya awali ya feri.
Ahamadi Hassani na Ahamadi Fuka, wakazi wa Kijiji cha Kilambo katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini, wanasema kutokuwepo kwa feri hiyo kunawalazimu kutumia vyombo vya majini visivyo salama, hali inayohatarisha maisha yao na kuongeza gharama za usafiri.
Sauti: Ahamadi Hassani na Ahamadi Fuka – Wakazi wa Kijiji cha Kilambo
Kwa upande wake, Rajabu Athumani Salumu, dereva wa bodaboda kutoka kijiji hicho, amesema ukosefu wa chombo cha uhakika cha usafiri umesababisha mlundikano wa abiria na mizigo, huku baadhi ya wasafiri wakilazimika kulala eneo hilo kwa zaidi ya siku tatu wakisubiri usafiri.
Sauti: Rajabu Athumani Salumu – Bodaboda, Kijiji cha KilamboBaadhi ya bidhaa zinazovushwa kupitia kivuko cha Kilambo kuelekea Palma na vijiji jirani vya Msumbiji(Picha na Musa Mtepa0
Naye Fatuma Bakari, mkazi wa Kijiji cha Singa kilichopo nchini Msumbiji, amesema ucheleweshaji unaotokana na kutokuwepo kwa kivuko hicho ni changamoto kubwa kwa wakazi wa pande zote mbili za mpaka, hasa kwa shughuli za kibiashara na kijamii.
Sauti: Fatuma Bakari – Mkazi wa Kijiji cha Singa, Msumbiji
Akitoa ufafanuzi kwa njia ya simu, Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini, Abdulrahman Amir, amesema feri ya MV Kilambo ilipelekwa kufanyiwa matengenezo, lakini baada ya kukamilika ilirejeshwa Mtwara Mjini kutokana na changamoto za kiusalama na miundombinu katika eneo la Kilambo–Namoto kwa kipindi hicho.
Sauti: Abdulrahman Amir – Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na KusiniViroba vya unga vya wafanyabiashara wa Msumbiji wakisubiria Boti ili waweze kuvusha kuelekea nchini Msumbiji( Picha na Musa Mtepa)
Ameongeza kuwa kutokana na kivuko hicho kukaa muda mrefu bila kufanya kazi, kinahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu ya kuegeshea feri katika eneo la Kilambo.
Aidha, amesema TEMESA inatarajia kuingia mkataba kwa ajili ya matengenezo hayo makubwa, huku matarajio ya kurejea kwa huduma ya kivuko cha MV Kilambo kwa wananchi yakiwa ni kuanzia mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2026.
Sauti: Abdulrahman Amir – Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini