Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja
Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao
Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii
Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm
Mwonekano wa korosho ikiwa kwenye mti kabla ya kudondoka (Picha na Musa Mtepa)
Wakulima wa korosho Nanyamba wamelalamikia tofauti kubwa ya bei ukilinganisha na Tandahimba, hali inayowalazimisha kuhamishia mazao yao Tandahimba
Na Musa Mtepa
Wakulima wa zao la korosho katika Halmashauri ya Mji Nanyamba wamehoji tofauti ya bei ya korosho inayojitokeza sokoni kati ya halmashauri hiyo na Wilaya ya Tandahimba, hali inayowalazimu baadhi yao kupeleka mazao yao Tandahimba ili kupata bei ya juu zaidi.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wakulima hao wamesema kuwa kwa takribani miaka kumi sasa bei ya korosho imekuwa hairidhishi, huku tofauti ya bei kati ya Nanyamba na Tandahimba ikiendelea kuwa kubwa.
Wamesema kuwa licha ya madai ya kuwepo kwa unyevu kwenye korosho zinazouzwa Nanyamba, korosho hizo hizo zikipelekwa Tandahimba hununuliwa kwa bei ya juu zaidi.
Sauti ya 1: Wakulima wa korosho Nanyamba
Wakizungumzia sababu za utofauti wa bei ndani ya mnada mmoja, wakulima hao wamesema kuwa mfumo wa ununuzi wa korosho kwa njia ya loti unaochangia tofauti ya bei kati ya Halmashauri ya Nanyamba na maeneo mengine ya Mtwara, Masasi pamoja na Nanyumbu.
Sauti ya 2: Wakulima wa korosho Nanyamba
Jamali Nalyogo, mkulima kutoka Mtimbwilimbwi, pamoja na Issa Kamkunje wa kijiji cha Njengwa wamesema hali hiyo imekuwa ikiwasababishia maumivu ya moyo, huku wakilaumu wawakilishi (Wabunge) na viongozi wanaosimamia zao la korosho katika Halmashauri ya Nanyamba,Mtwara,Masasi na Nanyumbu kutowatendea haki.
Sauti ya 3: Jamali Nalyogo na Issa Kamkunje – wakulima
Kwa upande wake, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Biadia Mtipa, amesema kuwa wakulima wa Nanyamba wako karibu na ukanda wa bahari hali inayosababisha korosho zao kuwa na unyevu mkubwa, jambo linalopunguza ubora na hatimaye kushusha bei sokoni.
Mrakibu msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Mtwara Ambros Ndunguru akiwa katika studio za jamii fm redio akitoa elimu ya matumizi sahihi ya Gesi ya kupikia majumbani(Picha na Amua Rushita)
Wananchi wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya gesi ya kupikia majumbani ili kuepuka madhara ikiwemo milipuko ya moto
Na Musa Mtepa
Wananchi wameshauriwa kuzingatia matumizi sahihi ya gesi ya kupikia majumbani ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwemo milipuko ya moto inayosababishwa na matumizi yasiyo salama ya nishati hiyo.
Ushauri huo umetolewa leo Disemba 24, 2025 na Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Ambros Ndunguru, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Redio.
Ndunguru amesema kuwa, mteja anaponunua gesi dukani, anatakiwa kwanza kuhakikisha anapima uzito wa mtungi wa gesi husika, pamoja na kuzingatia namna sahihi ya kuusafirisha. Ameongeza kuwa baada ya kuufikisha nyumbani, ni vyema kusubiri angalau dakika 30 kabla ya kuanza kuutumia.
Sauti ya 1: Ambros Ndunguru, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Aidha, Ndunguru amesema kuwa kutokana na kuimarika kwa kitengo cha huduma na mawasiliano, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limekuwa likipokea taarifa nyingi kutoka kwa wananchi kuhusu matukio mbalimbali yanayosababishwa na mitungi ya gesi.
Sauti ya 2: Ambros Ndunguru, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Akizungumzia hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo gesi itavuja au kulipuka, Ndunguru amesema kuwa ni muhimu kuepuka kuwasha au kuzima swichi za umeme, pamoja na kuto-buruta kitu chochote chenye uwezo wa kuzalisha cheche, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha mlipuko mkubwa zaidi.
Sauti ya 3: Ambros Ndunguru, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya gesi ya kupikia majumbani, sambamba na kuwasiliana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kupiga simu ya bure 114 kwa ajili ya kupata elimu zaidi au kutoa taarifa za matukio mbalimbali ya uokoaji.
Sauti ya 4: Ambros Ndunguru, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
Msafiri kipila akiwa na Fransis Chiwango katika mahojiano ya kipindi hiki. Picha na Mwandishi wetu
Ulemavu si jambo la hiari, na kwamba mtu yeyote anaweza kuwa mlemavu wakati wowote katika maisha yake.
Na Msafiri Kipila
Watu wenye ulemavu ni sehemu muhimu ya jamii na wana mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Licha ya uwezo na vipaji walivyonavyo, kundi hili limekuwa likikumbana na changamoto mbalimbali, nyingi zikiwa ni za kuepukika. Changamoto hizo ni pamoja na miundombinu isiyo rafiki, ukosefu wa mazingira jumuishi, pamoja na kukosekana kwa usawa wa fursa katika nyanja mbalimbali za maisha.
Kwa kutambua hali hiyo, wanachuo wa Chuo cha Utumishi wa Umma wametoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kuboresha mazingira yanayowazunguka watu wenye ulemavu. Wanachuo hao wamejadili pia namna bora za kutatua changamoto wanazokumbana nazo watu wenye ulemavu, wakisisitiza kuwa ulemavu si jambo la hiari, na kwamba mtu yeyote anaweza kuwa mlemavu wakati wowote katika maisha yake.
Maandalizi ya ujenzi wa ofisi za TARURA na Maabara ya kupimia vifaa na miradi ya ujenzi wilaya ya Mtwara(Picha na Musa Mtepa)
TARURA Wilaya ya Mtwara imeanza utekelezaji wa miradi ya TACTIC ikihusisha ujenzi wa ofisi, maabara ya kupima ubora wa miradi, barabara na mifereji ya maji, huku ikilenga kuboresha miundombinu na kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo
Na Musa Mtepa
TARURA Wilaya ya Mtwara imeanza utekelezaji wa miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) inayofadhiliwa na Serikali Kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia, kwa kuanza ujenzi wa jengo la ofisi ya usimamizi wa miradi pamoja na maabara ya kupima ubora wa vifaa vya ujenzi na miradi.
Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 22, 2025 katika eneo la mradi, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mtwara, Mhandisi Hatibu Nunu, amesema mradi huo unagharimu shilingi bilioni 27.4 na unatekelezwa na Mkandarasi Serengeti Limited. Amesema ujenzi huo umeanza rasmi Desemba 5, 2025 na utahusisha ujenzi wa ofisi tatu pamoja na chumba maalumu cha Maabara.
SAUTI: Mhandisi Hatibu Nunu – Meneja TARURA Wilaya ya Mtwara
Mhandisi Nunu ameongeza kuwa miradi ya TACTIC pia inahusisha ujenzi wa Barabara ya Pacha ya Mbae yenye urefu wa kilomita 2.4, Barabara ya stendi ya Chipuputa yenye urefu wa kilomita 2.4, Barabara ya kuzunguka soko la Chuno yenye urefu wa kilomita 3 pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua.
SAUTI: Mhandisi Hatibu Nunu – Meneja TARURA Wilaya ya Mtwara
Kwa upande wa ukarabati wa Barabara, amesema Wilaya ya Mtwara hutengewa shilingi bilioni 7 kwa mwaka kwa ajili ya halmashauri tatu, ambapo Manispaa ya Mtwara Mikindani hupata shilingi bilioni 3.8. Kwa mwaka huu, TARURA imesaini mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ukarabati wa Barabara na usafishaji wa mifereji, kazi ambazo tayari zinaendelea.
SAUTI: Mhandisi Hatibu Nunu – Meneja TARURA Wilaya ya Mtwara
Naye Mhandisi Mshauri Mkazi wa miradi ya TACTIC katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, Henry Moshi, amesema mkandarasi yupo katika hatua za maandalizi ya kazi (mobilization) na ameahidi kuwa vibarua wazawa watapewa kipaumbele katika ajira.
SAUTI: Mhandisi Henry Moshi – Mshauri wa Miradi ya TACTIC
Nao wananchi wakiwemo vijana na mama lishe wameeleza kufarijika na uwepo wa miradi hiyo wakisema italeta tija, kuongeza kipato na kuboresha mazingira ya biashara, huku wakiwahimiza vijana kutumia fursa zinazojitokeza.
Baadhi ya watoto na vijana wanaonufaika na kituo cha maendeleo ya mtoto na vijana cha FPCT Mtwara (Picha na Musa Mtepa)
Kituo cha Maendeleo ya Mtoto na Kijana FPCT Mtwara kimetoa zawadi za Krismasi kwa watoto wanaosoma kituoni hapo, ikiwa ni kuwapongeza na kumshukuru Mungu
Na Musa Mtepa
Kituo cha Maendeleo ya Mtoto na Kijana cha FPCT Mtwara kimetoa zawadi za Krismasi kwa watoto wanaosoma katika Kituo cha Huduma ya Mtoto, ikiwa ni sehemu ya kumshukuru Mungu na kuwapongeza watoto hao kwa juhudi zao katika masomo.
Akizungumza leo Disemba 20, 2025 wakati wa zoezi la utoaji wa zawadi hizo, Mchungaji Kiongozi Msaidizi wa Kanisa la FPCT Mtwara, Frank Mchihama, amesema pamoja na utoaji wa zawadi, kituo hicho kimezindua utaratibu mpya wa ufadhili wa ndani, utakaosaidia kukusanya fedha kwa ajili ya kuwafikia watoto wengine waliopo katika mazingira magumu ambao bado hawajapata fursa ya kuhudumiwa na kituo hicho.
Sauti ya 1: Frank Mchihama, Mchungaji Kiongozi Msaidizi FPCT MtwaraMchungaji Kiongozi Msaidizi wa Kanisa la FPCT Mtwara, Frank Mchihama akielezea juu ya uzinduzi wa ufadhili wa ndani (Picha na Musa Mtepa)
Kwa upande wake, Afisa mawasiliano na fedha wa Kituo hicho, Bi Dorcas Mlawa, amesema zawadi zilizotolewa zimegharimu jumla ya shilingi milioni sita. Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya uendeshaji wa kituo, wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuwasaidia watoto kufikia viwango mbalimbali vya elimu kama vile kidato cha sita, vyuo vya kati pamoja na vyuo vikuu.
Sauti ya 1: Dorcas Jackson, Meneja wa KituoAfisa mawasiliano na fedha Bi Dorcas Mlawa akielezea juu ya mafanikio ya kituo (picha na Musa Mtepa)
Aidha, Bi Dorcas amesema kituo hicho hakibagui watoto, kwani kinapokea watoto kutoka jamii zote bila kujali imani, rangi au kabila, akisisitiza kuwa kigezo kikubwa ni mtoto kutoka katika mazingira magumu.
Sauti ya 2: Dorcas Jackson, Meneja wa Kituo
Akizungumzia umuhimu wa kufadhili watoto wenye uhitaji, Mchungaji Enoshi Aloyce wa FPCT Mtwara ameitaka jamii kuwa na amani na furaha kwa kushika mkono wa mtoto mwenye uhitaji ili aweze kupata elimu na kujikwamua katika umasikini.
Sauti: Mchungaji Enoshi Aloyce, FPCT Mtwara
Nao baadhi ya wazazi pamoja na watoto wanufaika wa kituo hicho wamekishukuru uongozi wa kituo kwa kuendelea kuwapatia msaada na zawadi mbalimbali. Wametoa wito kwa wazazi na walezi wanaoishi katika mazingira magumu kuwapeleka watoto wao katika kituo hicho ili waweze kunufaika na huduma na misaada inayotolewa.
Sauti za baadhi ya wazazi na watoto wanufaika wa kituo hichoMmoja ya miongoni mwa wazazi waliojitokeza wakati wa upokeaji wa zawadi za watoto katika kituo cha maendeleo ya mtoto na vijani FPCT Mtwara(picha na Musa Mtepa)
Waziri wa kilimo Daniel Chongolo akipata maelezo kutoka kwa moja ya wafanyakazi wa kituo na kiwanda cha kubangua Korosho Mahuta wilayani Tandahimba (Picha na Musa Mtepa)
Ujenzi wa kiwanda cha Tells One General Supply Mahuta wilayani Tandahimba mkoani Mtwara umeleta faraja kwa akina mama na wabanguaji wadogo wa korosho. Kiwanda hicho kimewezesha upatikanaji wa soko, ajira na kuboresha maisha ya wananchi hususan wanawake wa eneo hilo
Na Musa Mtepa
Vikundi vya akina mama na wabanguaji wadogo wa korosho Mahuta wilayani Tandahimba mkoani Mtwara vimeeleza kufurahishwa kwao na ujenzi wa kiwanda pamoja na kituo cha kuwasaidia kupata soko na ajira cha Tells One General Supply.
Wakizungumza kuhusu manufaa wanayoyapata kutokana na uwepo wa kiwanda hicho, Bi Amina Mande na Bi Amina Makwangu, ambao ni wafanyakazi wa kiwanda hicho, wamesema kuwa kiwanda kimekuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto zao za kimaisha ikiwemo kusomesha watoto na kujikimu katika mahitaji ya kila siku.
Sauti ya Bi Amina Mande, mfanyakazi wa kiwanda cha Tells One General SupplyBaadhi ya wafanyakazi wa Tells One wakichambua Korosho karanga zilizopokelewa kutoka kwa vikundi vya wabangauaji wadogo Mahuta (Picha na Musa Mtepa)
Kwa upande wake, msimamizi wa kiwanda hicho, Bi Mariamu Chilongo, amesema dhamira ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni kuwasaidia wabanguaji wadogo wa korosho, hususan akina mama, ambao hapo awali walikuwa wakikumbana na changamoto ya upatikanaji wa masoko. Amesema kiwanda hicho hupokea korosho zilizobanguliwa, kuziboresha na kuzisafirisha kwenda sokoni.
Sauti ya Bi Mariamu Chilongo, Msimamizi wa KiwandaMariamu Chilongo Msimamizi wa kituo na kiwanda cha kuwasaidia wabanguaji wadogo Mahuta wilayani Tandahimba (Picha na Musa Mtepa)
Aidha, Bi Mariamu amesema kuwa pamoja na kupokea korosho kutoka katika vikundi mbalimbali, kiwanda hicho tayari kimeajiri wafanyakazi wa kike wasiopungua 50, huku matarajio yakiwa ni kuongeza idadi hiyo hadi kufikia wafanyakazi 500 siku za usoni.
Sauti ya Bi Mariamu Chilongo, Msimamizi wa Kiwanda
Kituo na kiwanda cha Tells One General Supply (TOGS) kimejengwa katika kijiji cha Mahuta wilayani Tandahimba mkoani Mtwara, kikiwa na lengo la kusaidia upatikanaji wa soko la korosho kwa vikundi vidogo vya ubanguaji pamoja na kutoa ajira kwa akina mama wa eneo hilo.
Kaimu mkurugenzi wa TARI-Naliendele Bakari Kidunda akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa kujadili changamoto na mafanikio ya msimu wa kilimo wa 2025/2026(Picha na Musa Mtepa)
Taassisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele imefanya mkutano wa mwaka na wadau wa kilimo kuwasilisha matokeo ya tafiti na kujadili mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, huku ikilenga kuongeza uzalishaji wa zao la korosho msimu ujao wa kilimo
Na Musa Mtepa
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Naliendele, mkoani Mtwara, imeendelea na utaratibu wake wa kila mwaka wa kukutana na wadau wa kilimo kwa lengo la kuwasilisha matokeo ya tafiti zilizofanyika kwa kipindi cha mwaka mzima pamoja na kueleza matarajio ya msimu ujao wa kilimo.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Desemba 12, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa TARI–Naliendele, Bakari Kidunda, amesema mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali wa kilimo kutoka mikoa tofauti, huku ukitoa fursa kwa wadau hao kusikiliza na kujadili kazi zilizofanywa na watafiti pamoja na mipango ya tafiti zitakazofanyika katika msimu mpya wa kilimo.
Sauti ya Bakari Kidunda, Kaimu Mkurugenzi TARI–Naliendele
Aidha, Kidunda amesema miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka uliopita ni utafiti wa teknolojia ya matumizi ya mbolea kwenye zao la korosho. Amesema utafiti huo umefikia hatua ya mwisho na matokeo yake yanakwenda moja kwa moja kwa wakulima ili yaweze kutumika kuongeza uzalishaji wa korosho.
Sauti ya pili ya Bakari Kidunda, Kaimu Mkurugenzi TARI–Naliendele
Pamoja na mafanikio hayo, Kidunda ameainisha mabadiliko ya hali ya hewa kuwa changamoto kubwa inayokwamisha uzalishaji wa mazao kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026. Amesema TARI–Naliendele inaendelea kufanya tafiti mahsusi zitakazosaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Sauti ya tatu ya Bakari Kidunda, Kaimu Mkurugenzi TARI–NaliendeleBaadhi ya washiriki wa mkutano wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mafunzo ya kujadili changamoto na mafanikio ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na TARI-Naliendele kwa msimu wa kilimo 2024/2025(Picha na Musa Mtepa)
Kwa upande wake, Lazaro Maliganya, Afisa Kilimo Msaidizi kutoka Halmashauri ya Songwe, akimwakilisha Mkuu wa Idara, amesema mkutano huo umempa maarifa mapya yatakayosaidia halmashauri yao kuboresha uzalishaji, hususan katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa iliyojitokeza katika msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.
Maliganya amesema mabadiliko hayo yameathiri uzalishaji wa zao la korosho na kusababisha halmashauri kushindwa kufikia lengo la kuzalisha tani nane, huku wakilenga kufikia tani 15 katika msimu ujao wa kilimo.
Sauti ya Lazaro Maliganya, Afisa Kilimo Msaidizi Halmashauri ya Songwe
Naye George Mbaga, Afisa Kilimo kutoka Mkoa wa Tanga, amesema mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa zao la korosho katika mkoa huo. Hata hivyo, amesema kupitia uwasilishaji wa tafiti uliofanywa na TARI–Naliendele, wamepata mwanga wa namna ya kukabiliana na changamoto za tabianchi ili kuongeza uzalishaji.
Sauti ya George Mbaga, Afisa Kilimo Mkoa wa TangaGeorge Mbaga, Afisa Kilimo kutoka Mkoa wa Tanga akizungumza na waandishi wahabari (Picha na Musa Mtepa)