• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Miili ya watu wawili yaokotwa katika mto Arusha

Watu wawili ambao ni wanandoa wamefariki dunia katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha baada ya kuchukuliwa na mafuriko katika mto Piyaya Kata ya Piyaya wilayani humo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Yusuph Ilembo amesema miili hiyo imeonekana leo majira ya asubuhi baada ya maji ya mto huo wa msimu kupungua.

Aidha, Kamanda Ilembo amewataja marehemu hao kuwa ni Ormins Sunguyo na mkewe Nembris Sunguyo ambao walikuwa na mtoto wa mdogo aliyefahamika kwa jina la Oloosukuta Sunguyo ambaye alinusurika kifo.

Kamanda Ilembo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi katika mkoa wa Arusha kuchukua tahadhari kipindi hiki cha mvua na kuepuka kuvuka mito wakati maji yanafurika.
Share:

BINA ameitaka TBS kuchunguza kemikali bandia wanazouziwa Wachimbaji wadogo

Serikali kupitia Shirika la Viwango nchini, TBS limetakiwa kuchunguza kemikali bandia zinazouzwa na wafanyabiashara wasio waaminifu kwa wachimbaji wadogo wa madini hali inayosababisha hasara kwa wachimbaji hao.

Rais wa Shirikisho la wachimbaji wadogo wa madini nchini, (FEMATA) Bw John Bina amesema hayo baada ya kikao kilichowakutanisha wachimbaji wadogo Mkoani Geita kwa lengo la kujadili namna Serikali inavyoweza kufanikisha ujenzi wa soko la madini kwa kanda ya ziwa.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiuza kemikali bandia kwa wachimbaji wadogo na hivyo kuwasababishia hasara.“Tunaomba serikali na TBS kuangalia sanaa haya madawa ambayo yanaingia nchini kuhakikisha wanachunguza kemikali hizi kwani kwa sasa uzalishaji unashuka kwa kiasi kikubwa wa madini ,na nyie wachimbaji niwaombe muwe mnachunguza kabla ya kununua kwani kweli mnaingia hasara kubwa sanaa”Alisisitiza Bina.

Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Bw Nuru Shabani alisema kwa kuuziwa Kemikali hizo bandia amekuwa akiathirika katika shughuli zake.“Kiukweli tunaathirika sanaa na hili halina ubisha sasa hivi unaweza kununua tani moja ya kaboni unakuta inapitisha bila ya kushika mali inamaana hadi iwe na pipim kuanzia mia saba hadi mia nane ,Ila kwa sasa nashukuru walau serikali imetambua mchango wetu na imetuthamini mimi nilikuwa naomba kupitia Kitengo chetu tuwe na wasimamizi ambao watatusaidia kubaini kemikali hizi”Alisema Nuru.

Bw John Bina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia kero za wachimbaji wadogo alisema pamoja na matatizo hayo lakini wachimbaji hao wamekubaliana kuanzishwa kwa soko la madini Mkoani Mwanza ili kudhibiti vitendo vya utoroshwaji wa madini.
Share:

DAR ES SALAAM: Hospitali ya Temeke yathibitisha kumpokea kijana aliyejeruhiwa kwa risasi

Siku moja baada ya Mwananchi kuripoti habari ya Alex Suke (18) anayedaiwa kupigwa risasi na polisi waliokuwa wakituliza vurugu eneo la Buguruni Relini Ijumaa iliyopita, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Temeke Dk Amani Malima, amethibitisha kumpokea kijana huyo.

Akizungumza jana na mwandishi wetu, Dk Malima alisema madaktari wanaendelea kumpatia matibabu na kubainisha kuwa juzi alishindwa kuthibitisha tukio hilo kwa maelezo kuwa hakuwepo ofisini, “Yupo wodi namba saba lakini kamuone Dk Mwita ambaye yuko zamu atakupa ushirikiano,”alisema.

Mwananchi lilipowasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula kwa njia ya simu alisema, “hilo suala ni la zamani sana wewe ndo unaulizia leo? Kwa sasa nipo nje ya ofisi nitakutafuta baadaye kidogo.”

Awali, mwandishi wetu alimtafuta Dk Mwita ambaye alikuwa zamu katika wodi namba saba alikolazwa kijana huyo.

Baada ya kufika wodini hapo saa saba mchana alishuhudia madaktari wakifanya maandalizi kwa ajili ya kumpeleka kijana huyo kwenye chumba cha upasuaji jambo lililozuia mahojiano wakati huo.

Mwandishi wetu aliweka kambi kwa muda hospitalini hapo kwa ajili ya kuzungumza na daktari huyo na kujibiwa na wasaidizi wake kuwa ana majukumu mengi, si rahisi kupata muda wa kuzungumza na mwanahabari.

Mama wa kijana huyo, Aghata Mwangamba alisema madaktari walimueleza kuwa mwanae atafanyiwa upasuaji wa mkono ambao ulijeruhiwa kwa risasi huku akilalamikia mzigo wa gharama za matibabu. “Leo (jana) analalamika sana mkono tofauti na jana (juzi) na madaktari wameniambia leo (jana) watamfanyia upasuaji mwingine wa mkono ambao ulijeruhiwa na risasi,” alisema.

Alisema wameiomba Serikali iwasaidie katika matibabu kwani hadi sasa ametumia Sh900,000 katika matibabu.

“Mtoto wangu hana bima na mimi ni mjane gharama ni kubwa na uwezo wangu kwa sasa umekuwa mdogo,” alisema mama huyo na kubainisha kuwa anategemea genge kuendesha maisha yake.

Bibi wa kijana huyo, Subira Mwakajila alisema familia imepata pigo kwa kujeruhiwa kijana huyo, “Sisi hatuoni haja ya kupelekana mahakamani lakini tunataka kujua hatma ya kijana wetu kiafya na kimasomo,”alisema.

Kijana huyo alipigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya watu maeneo ya Buguruni Relini Ijumaa iliyopita.

Juzi baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwamo Juma Liwanje walieleza kuwa kijana huyo alipigwa risasi kutokana na vurugu zilizotokea eneo la Buguruni Relini baada ya askari kufyatua risasi kuwatawanya watu wakiwamo madereva bodaboda.
Share:

DAR ES SALAAM: Mbarawa asema ujenzi reli ya kisasa kutoka Dar-Moro umefikia asilimia tisa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia tisa, utakamilka baada ya miezi 30.

Akizungumza leo Machi 14, 2018 katika uzinduzi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Morogoro hadi Makutopora mkoani Dodoma, Mbarawa amesema ujenzi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro utakamilika Novemba 2019.

“Reli iliyopo sasa ya upana wa mita moja miundombinu yake imechoka sana treni huenda kwa kasi ya Kilometa 30 kwa saa. Rais (John Magufuli) ninaomba nikuhakikishie kuwa wizara ya ujenzi itaendelea kuwasimamia wakandarasi,” amesema.

“Tutahakikisha wakandarasi wanamaliza kazi ya ujenzi wa reli hii kwa wakati na kuhakikisha ubora. Hivi ninavyokuambia wakandarasi wanafanya kazi usiku na mchana kwa siku saba kwa wiki.”
Chanzo: muungwana
Share:

DAR ES SALAAM: Rais Magufuli asema Wananchi kulipa kodi isiwe kero kwao

Rais John Magufuli amesema wananchi kulipa kodi isiwe kero kwao, bali heshima na kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa makini.

Akizungumza leo Machi 14, 2018 mjini eneo la Ihumwa nje kidogo ya Mkoa wa Dodoma wakati akizindua ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Morogoro hadi Makutopora, Rais Magufuli amesema baadhi ya kodi wananchi hukwepa kulipa kodi kutokana na namna zinavyotozwa na viwango kuwa juu.

“Kuna watu TRA siyo wazuri, Kamishna wa TRA na Waziri wa Fedha  shughulikieni hili. Mtu kulipa kodi isiwe ni kero bali heshima,” ameagiza.

Kuhusu ujenzi wa reli hiyo, Rais Magufuli amesema katika awamu zote za ujenzi itagharimu Sh15 trilioni.

“Ukiachilia mbali mradi huu, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mingine ya miundombinu. Hapa Dodoma tunajenga barabara za mizungumko, kazi ya designing (usanifu) inafanyika na itakuwa kwa kiwango cha lami ili kweli Dodoma ionekane makao makuu ya nchi,” amesema.
Chanzo: muungwana
Share:

Wafuasi Chadema waliokamatwa msibani kupandishwa Mahakamani

Wafuasi zaidi ya 10  wa Chadema waliokamatwa wakiwa nyumbani kwa mwanachama mwenzao kuhani msiba wanatarajiwa kupandishwa kizimbani muda mfupi ujao.

Watu hao, leo Machi 14, 2018 tayari wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza na kuwekwa katika mahabusu mahakamani hapo kusubiri kukamilika kwa taratibu za kimahakama ili wasomewe mashtaka dhidi yao.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi watu hao walikamatwa eneo la Mabatini Machi 13, 20018  baada ya kutokea kutoelewana kati yao na askari polisi.

Amesema askari hao walikuwa wakifuatilia nyendo za wafuasi hao  tangu walipokuwa wakikusanyika kutoka sehemu mbalimbali za Jiji la Mwanza kwenda nyumbani kwa wanachama mwenzao kwa kile kinachodaiwa ni kuhani msiba.

Katika tukio hilo, polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya kundi la watu zaidi ya 500 waliokuwa kwenye eneo hilo.
Share:

Sakata la Nondo Polisi watofautiana

Jeshi la polisi nchini limetofautiana katika taarifa zake kuhusu kupatikana kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ambapo RPC wa Iringa alisema kijana huyo alifika mwenyewe kituo cha polisi huku Mambosasa akipinga hilo.

Katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire Machi 8, 2018 imeonyesha kutofautiana na kauli iliyotolewa jana Machi 13, 2018 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kamanda Juma Bwire alisema haya.

"Jana tarehe 7 mwezi wa tatu majira ya saa moja Abdul Nondo alifika katika kituo cha polisi Mafinga wilaya ya Mufindi na kuelezea kuwa ametekwa na watu wasiofahamika, jeshi la polisi mkoa wa Iringa limefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama alikuwa ametekwa na kama kweli alikuwa ametekwa tunaahidi kwamba sisi jeshi la polisi tukiwapata watuhumiwa sheria itachukua mkondo wake" alisema kamanda Bwire

Taarifa ya RPC wa Iringa imeonyesha kukinzana na taarifa aliyotoa jana Kamanda Mambosasa ambaye amedai kuwa Abdul Nondo hakuripoti sehemu yoyote ile na kudai kuwa walimkuta akiendelea na shughuli zake.

"Mnamo tarehe 7 Machi mwaka huu jeshi la polisi kanda Malaamu ya Dar es Salaam lililetewa taarifa kutoka polisi mkoa wa Iringa kwamba mwanafunzi huyo aliyekuwa amedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana alipatikana mkoani humo wilaya ya Mafinga akiwa na afya njema na mwenye kujitambua akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio lolote kabla ya kukamatwa ili kuthibitisha kile kilichokuwa kikisemwa ametekwa na watu wasiojulikana. Hakuripoti mahali popote si kwa Mwenyekiti wa Mtaa, si kwa Afisa Mtendaji wa Kata, wala kituo chochote cha polisi mkoani Iringa bali alikamatwa akiwa Mafinga akiendelea na shughuli zake" alisisitiza Mambosasa 

Mpaka sasa jeshi la polisi linaendelea kumshikilia Abdul Nondo, kwani kwa mujibu wa wakili wa mwanafunzi huyo anasema kwamba mpaka jana Machi 14, 2018 hajafanikiwa kukutana wala kuongea na mteja wake.
Share:

ZANZIBAR: Nyama kutoka Afrika Kusini yateketezwa na ZFDA

Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), imeteketeza  kilo 48 za nyama kutoka Afrika Kusini baada ya Serikali kusitisha uingizaji nyama kutoka nchini humo kutokana na mlipuko wa bakteria wa listeria.

Ilibainika kuwa nyama hizo ziliingizwa nchini kinyume cha sheria, Nyama hizo ni mali ya kampuni ya Qamar ya Vingunguti jijini Dar es Salaam, ilikamatwa Uwanja wa wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza leo Machi 14 wakati wa zoezi hilo, mkuu wa kitengo cha uchambuzi wa hatari zinazotokana na chakula wa ZFDA, Aisha Suleiman amesema kilichosababisha kuteketezwa kwa nyama hiyo ni katazo lililotolewa na ZFDA baada ya kutokea mlipuko wa ugonjwa wa listeriosis.

Amesema ZFDA ndiyo yenye majukumu ya kuhakikisha wananchi wanapata chakula salama, Aisha amesema uamuzi ya katazo hilo umetokana na uwapo wa maradhi ya Listeriosis nchini Afrika Kusini, hivyo ofisi yao imepiga marufuku uingizwaji nyama, maziwa na samaki kutoka nchi hiyo.

 Bakteria wa listeria, wanaosababisha maradhi ya listeriosis, wamesababisha vifo vya watu zaidi ya 180 Afrika Kusini.

Amesema katazo hilo si kwa Zanzibar pekee bali na Tanzania bara na nchi nyingine kutokana na utaratibu wa biashara kimataifa.

“Hili katazo siyo sisi tu, ni utaratibu wa kimataifa kwamba kutokana na maradhi ya listeriosis bidhaa za nyama, samaki, maziwa ni marufuku kuingizwa nchini sasa hii kampuni ya Qamar LTD ya Dar es Salaam wao waliamua kuingiza nyama hiyo, tumeikamata na kuiangamiza.” amesema Aisha.
Chanzo Muungwana
Share:

Rais Magufuli: Mimi nasema tuzaliane tu

Rais John Magufuli amesema idadi kubwa ya watu nchini haina budi kuendana na maendeleo kwani watu wanapokuwa wengi wanakuwa na sauti na hivyo akawataka Watanzania waendelee kuzaliana.

“Juzi tuliambiwa kwa sasa tumefikia watu milioni 55, watu wanasema kwa nini tunazaliana, mimi nasema tuzaliane tu,” amesema.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Machi 14, wakati wa uzinduzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), Makutupora, Dodoma.

“Lakini idadi hiyo ya watu ni lazima wachape kazi, mfano Denmark ina watu milioni tano lakini wana maendeleo mpaka wanazisaidia nchi nyingine zenye watu milioni 55 kama Tanzania,” amesema.

Amesema ujenzi wa reli utatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 30,000 na zisizo za moja kwa moja 600,000.
Share:

Wafariki kwa kusombwa na maji mtoni wakijinadi wanajeshi

Picha kwa mujibu wa mtandao
WATU watatu wakiwamo wawili ambao walijinadi kuwa wana mafunzo ya kijeshi, wamefariki dunia mkoani Dodoma katika matukio mawili tofauti ya kusombwa na mafuriko.

Vifo hivyo vimesababishwa na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa juzi.

Katika tukio la kwanza lililotokea Nzuguni Manispaa ya Dodoma, Diwani wa Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhega, alisema kuwa katika eneo hilo watu wawili waliojinadi kuwa na mafunzo ya kijeshi walisombwa na mafuriko wakati wakitoka katika majukumu yao ya kazi majira ya jioni.

Alisema kuwa wakati wakirudi nyumbani, watu hao walifika katika eneo lenye kivuko ambapo pamejengwa daraja la chini ambalo lilikuwa limejaa maji kutoka na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha juzi jioni.

Alieleza kuwa watu hao ambao bado hawajajulikana majina yao, walipofika katika eneo hilo watu waliwashauri wasivuke hadi maji yatakapopungua, lakini walikaidi na kudai kuwa wanaweza kuvuka.

“Walikwenda hadi katikati wakarudi kama mara tatu hivi, lakini mwisho wake wakasema wao wanaweze kuvuka kwa kuwa walishapitia jeshi, lakini wakati wakielekea kuvuka nguvu ya maji iliwashinda na kuwasomba huku tukiwaangalia,” alisema na kuongeza:

“Hatukuwa na la kufanya, tukawafuatilia, lakini kutokana na giza hatukuweza kuwapata hadi leo hii (jana) asubuhi ndipo tumeweza kuwapata wote wawili.”

Alisema miili ya marehemu polisi wameichukua kwa ajili ya hatua nyingine, ikiwamo waliopotelewa na ndugu zao kuitambua.

“Sasa hivi polisi wanalishughulikia suala hili, sisi kama serikali ya kata tumetoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuitafuta miili hiyo hadi kuipata, hatua nyingine wenzetu wa polisi wataifanyia kazi, nitoe wito kwa wananchi wakati huu wa mvua kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari,” alisema Luhega.

Katika tukio jingine, mkazi mmoja wa Kijiji cha Chibwegele Kata ya Mtera Wilaya Mpwapwa, aliyetambulika kwa jina moja la Martha, amefariki dunia baada ya nyumba yake kumwangukia kutokana na mvua iliyonyesha.

Mvua hiyo pia imesababisha kaya 40 za Kitongoji cha Chungu kukosa mahali pa kuishi, baada ya nyumba zao kusombwa.

Diwani wa kata hiyo, Amoni Kodi, alisema mkazi huyo aliyepoteza maisha alikutwa na mkasa huo akiwa ndani ya nyumba yake.

Alisema baada ya kuangukiwa na nyumba majirani walifanikiwa kwenda kumuokoa, lakini walimkuta amefariki dunia huku akiwa amevunjika miguu.

Diwani huyo alisema waathirika wamehifadhiwa na majirani huku serikali ya kata kwa kushirikiana na kamati ya maafa ya wilaya ikijipanga jinsi ya kuwasaidia.

“Waathirika wote wamepatiwa hifadhi na majirani  na kwa upande wa serikali ya kata na wilaya tunajipanga jinsi ya kuzisaidia kaya hizo kama vile chakula, maturubai na mabati hatua ambayo tunaamini itawasaidia, “alisema Kodi .

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alipoulizwa alisema hana taarifa za kutosha juu ya matukio hayo na kuahidi kutoa taarifa rasmi baadaye.

Vifo hivyo ni mwendelezo wa matukio ya majanga ya mvua za mafuriko zinazoendelea katika maeneo kadhaa nchini.

Watu watano wameripotiwa wamepoteza maisha wakiwamo ndugu wawili ndani ya siku tatu katika matukio ya kufa maji katika mvua za mafuriko wilaya za Handeni na Lushoto mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, juzi alithibitisha kutokea kwa vifo vinne vilivyotokana na mafuriko na cha mtu mmoja aliyepigwa na radi.

Bukombe alisema Jumamosi 10 jioni wilayani Lushoto watu wawili ambao ni ndugu, Kassim Yahaya na Awadh Yahaya, wakazi wa Kitongoji cha Mbugui Chini walikufa maji wakivuka mto Lukundo.

Naye Mwamini Ally (46), mkazi wa Kijiji cha Rangwi alikufa kwa kusombwa na maji ya mto Ngurumo.Tukio lingine lilitokea Ijumaa jioni katika Kijiji cha Zavuza Kata ya Kiva wilayani Handeni ambapo Mwanahawa Rajab (60) alikufa kwa kusombwa na maji katika bonde la Bangala na Shaban Juma (30), mkazi wa Kijiji cha Mwamgodi Kata ya Msasa wilayani humo alikufa kwa kupigwa na radi. 
Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>