Kufanya mapenzi na ng'ombe kwamponza
Kijana Joseph Koech Alias Mnandi (25) wa Baringo huko Kenya ameuawa kwa kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali baada ya kukutwa akifanya mapenzi na ng'ombe
Habari kutoka katika vyombo vya habari nchini humo zinadai kwamba Kijana huyo alijitetea kuwa alilazimika kufanya mapenzi na ng'ombe kutokana na ukweli kwamba wasichana wengi wameathirika na virusi vya UKIMWI
Wakati akipokea kipigo Bw. Mnandi aliwasihi watu hao wasimuue, wamuache alipe gharama za kosa hilo kwa kutoa kipande chake cha ardhi.
Vijana wenye hasira walimshambulia kwa makofi, mawe na vijiti na kumwacha na majeraha makubwa ambayo yalipelekea kifo chake alipokuwa amefikishwa katika hospitali ya Eldama-Ravine.
Kiongozi wa eneo la Torongo Edwin Ronoh amesema huyo mtu anafanya kazi kama mfanyakazi wa kawaida kwa miller mtaa wa eneo la msitu wa Sawich ambapo ameongeza kwamba familia (wamiliki wa ng'ombe) huyo ilikuwa na wakati mgumu wa kumtafuta ng'ombe wao aliyepotea katika misitu ya Sawich.
Amedai kuwa mtuhumiwa huyo alifunga pembe za ng'ombe juu ya mti na na miguu ya nyuma juu ili kuzuia mtafaruku.
Chanzo: eatv
Askari Magereza waendelea kusota rumande
ASKARI Magereza 11 Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wanaodaiwa kumuua mwanakijiji, Aloys Makalla, wanaendelea kusota mahabusu, baada ya kesi yao kuahirishwa.Kesi hiyo iliahirishwa tena jana kwa mara ya nne na Mahakama ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Askari hao wanaotuhumiwa kumuua Makalla, mkazi wa Kijiji cha Kerenge, Kata ya Kerenge, Wilaya ya Korogwe.Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Albert Nyang’ali, ambaye alisoma shtaka hilo la mauaji kama mlinzi wa amani, alisema sababu ya kuendelea kutajwa shauri hilo bila kupangiwa kusikilizwa ni kutokana na baadhi ya vipengele kufanyiwa marekebisho.
Nyang’ali aliwataja askari hao ambao wapo mahabusu ya Gereza la Wilaya ya Korogwe ni P. 5377 Inspekta Makere, A. 4921 RSM (Mkuu wa Nidhamu) Mokiwa Shadrack Lugendo, A. 7367 Sajenti Mussa Mdoe Seif, B. 5919 Koplo Lazaro Stephen Nyato, B. 5486, Koplo Ramadhan Yusuph, B. 7087 WDR Robert Alfred, B. 7980 Fidirishi Cosmas Joseph, B. 7248 WDR Alphonce Revocatus, B. 8911 WDR Mbesha Naftari, B. 9747 WDR Michael Elias Michael na B. 8533 WDR Hamis Halfa Msola.Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa watuhumiwa wote kwa pamoja Januari 22, 2018 katika Kijiji cha Kerenge wilayani Korogwe walimuua Aloyce Makalla maarufu kama Mapi.Katika kesi hiyo namba 2 P I ya mwaka 2018, watuhumiwa wote walikana shtaka, lakini hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.Shauri hilo limepangwa kutajwa tena Machi 26, mwaka huu. Hii ni mara ya nne kesi hiyo kutajwa huku, watuhumiwa wote wakirejeshwa rumande.
Fahamu chanzo cha watu kupata upofu wa maisha
Daktari bingwa wa upasuaji wa macho kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt.Neema Daniel Kanyaro amedai ugonjwa wa presha ya macho ni moja kati ya magonjwa yanayopelekea mtu kupata upofu wa maisha endapo hatopata tiba mapema.Dkt. Kanyaro amebainisha hayo kupitia kipindi cha Supamix kinachorushwa kupitia East Africa Radio baada ya kuwepo wimbo kubwa la watu kupata ugonjwa huo, huku wengine wakidhani unatokana na magonjwa ya kurithi kifamilia kama yalivyo mengine yanayojulikana.
"Shinikizo la jicho au presha ya jicho ni moja kati ya magonjwa yanayoleta upovu wa kudumu. Hili tatizo linawaathiri watu wote nikiwa namaanisha kwamba mtoto anaweza akazaliwa nalo kama ile sehemu yake ya kutolea machozi haitakuwa vizuri. Tunasisitiza sana jamii kufahamu ugonjwa huu wa presha ya macho ni lazima upime", amesema Dkt. Kanyaro.
Orodha ya wenyekiti na makamu wenyekiti kamati ya kudumu ya bunge 2018-2020
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametoa orodha ya majina ya Wabunge mbalimbali ambao wameteuliwa katika kamati mbalimbali za kudumu za Bunge ambao wataongoza kwa kipindi cha mwaka 2018-2020.
Wabunge mbalimbali wameteuliwa kuongoza kamati hizo za kudumu kwa kipindi hiko cha mwaka ambapo baadhi ya wabunge walioteuliwa ni Mhe. Nnape Nnauye, Mhe. Andrew J. Chenge, Mhe. Emmanuel Mwakasaka na wengine.
Kufahamu wabunge hao na kamati zao angalia chati iliyopo hapa chini ikibainisha majina ya wenyekiti na makamu wao.

Wazee CHADEMA Waomba Kukutana na Rais Magufuli
Baraza la Wazee wa Chadema limemuomba Rais John Magufuli kukutana na wazee ili kubadilishana nao mawazo sambamba na kumpa ushauri wa masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.
Akizungumza leo Jumanne Machi 13, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, katibu mkuu wa baraza hilo, Roderick Lutembeka amesema kumekuwa na mambo mengi yanayopigiwa kelele, ni vyema rais akakutana na wazee ili wamueleza mambo hayo.
“Ni lazima kama Taifa tuchukue hatua mapema kabla hatujachelewa. Rais Magufuli akubali kuitikia wito wa kukutana na wazee ambao watakuwa na ujasiri wa kumshauri ili kuepusha Taifa kuingia kwenye majanga,” amesema.
Amesema suala la wazee kukutana na rais, kimekuwa ni kilio cha muda mrefu na kwamba nchini Kenya viongozi wameweza kukaa meza moja na kumaliza tofauti zao.
“Lazima tukae tujue mustakabali wa Taifa hatuwezi kusema hakuna tatizo. Tunamtaka akutane na wazee, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa tuzungumze kwa kuwa hii ni nchi yetu wote na si ya chama kimoja,” amesema.
Amesema mambo yanayopaswa kuzungumziwa ni suala la Katiba Mpya, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Amesema pia matukio ya watu kutekwa na kuuawa yameongezeka, “miezi sita iliyopita tulizungumzia mambo haya lakini naona ndio yanaongezeka.”
“Wazee tumeumizwa mno kuhusu suala la Abdul Nondo hasa pale Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba) alipotoa kauli kuwa kijana huyu alijiteka. Tulitegemea polisi wafanye uchunguzi, sasa kama waziri mhusika tayari ameshatoa hukumu tutegemee nini kwa hawa polisi. Tunajenga nini ndani ya mioyo ya hawa vijana ambao walijitoa kumtetea kijana mwenzao kama si chuki.”
Bajeti ya Mwaka 2018/19 ni Trilioni 32.476
Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango cha ukomo wa bajeti kwa mwaka 2018/19, waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema ukomo wa bajeti umezingatia upatikanaji wa mapato.
Dk Mpango amesema katika mwaka huo Serikali imepanga kutumia Sh20.468 trilioni kwenye matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti yote.
Matumizi hayo amesema yanajumuisha Sh10 trilioni zitakazolipa deni la Taifa na Sh7.369 trilioni mishahara ya watumishi wakati Sh3.094 trilioni zikielekezwa kwenye matumizi mengine.
Dk Mpango amesema Serikali itatumia Sh12 trilioni sawa na asilimia 37 kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kiasi hicho, amesema kinajumuisha Sh9.876 trilioni sawa na asilimia 82.3 kutoka vyanzo vya ndani na Sh2.13 trilioni sawa na asilimia 17.7 kutoka nje.
Jumla ya mapato ya ndani pamoja na makusanyo ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh20.894 trilioni ambayo ni sawa asilimia 64 ya bajeti yote.
“Kati ya mapato hayo yatokanayo na kodi yanatarajiwa kuwa Sh18 trilioni sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa,” amesema.
Amesema mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufika Sh2.158 trilioni wakati vyanzo vya halmashauri vikikusanya Sh735.6 bilioni.
Mpango amesema vyanzo vingine vinavyotarajiwa kufanikisha utekelezaji wa bajeti hiyo ni misaada na mikopo yenye masharti nafuu kiasi cha Sh2.676 trilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo ambazo ni sawa na asilimia nane ya bajeti hiyo.
Katika mwaka ujao, amesema Serikali inatarajia kukopa Sh5.793 trilioni kutoka soko la ndani ambazo kati ya hizo, Sh4.6 trilioni zitatumika kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva.
Sh1.193 trilioni zinazozidi kwenye mikopo hiyo ya ndani ambazo ni sawa na asilimia 0.9 ya Pato la Taifa, amesema ndilo deni jipya.
“Ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa Sh3.111 trilioni kutoka soko la nje,” amesema.
Serikali yasema deni la Taifa ni himilivu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hadi Desemba 2017, deni la Taifa lilikuwa limefikia Sh47.756 trilioni na tathmini zinaonyesha bado ni himilivu.
Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19 mjini hapa leo Machi 13, 2018, Dk Mpango amesema deni la nje lilikuwa Sh34.148 trilioni sawa na asilimia 71.5 na deni la ndani ni Sh13.607 trilioni sawa na asilimia 28.5.
Hata hivyo amesema uwiano wa deni hilo na Pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo ambao ni asilimia 56.
“Uwiano wa deni la nje na mauzo ya nje ni asilimia 81.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150. Hii inamaanisha kuwa uwezo wetu wa kulipa deni bado ni imara,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kwa kukopa kwenye vyanzo vyenye masharti nafuu kuhakikisha mikopo hiyo inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Rais wa Ufaransa apongeza utendaji kazi wa serikali ya Tanzania
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan jana amekutana na kuzungumza na Balozi mpya wa Ufaransa nchini Mhe. Frederic Clavier ambaye aliongozana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bw. Emmanuel Baudran.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi Clavier aliwasilisha salaam za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kusema, “Rais wa Ufaransa ana uhakika na Tanzania ijayo na anaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli.”
Balozi huyo mpya wa Ufaransa nchini ambaye amekutana na kuzungumza na Mheshimiwa Makamu wa Rais aliipongeza Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala mbali mbali ya Kimataifa na kusema “Tanzania ni nchi yenye utulivu na Amani kitu ambacho kinaipa taswira nzuri Umoja wa Mataifa”.
Mhe. Balozi alimjulisha Makamu wa Rais kwamba Ufaransa imekusudia kuimarisha uhusiano zaidi na Tanzania wa Uchumi na Siasa na kuanzisha majadiliano mbali mbali katika masuala ya Mazingira,Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Balozi Clavier alimjulisha Makamu wa Rais kuwa mwezi ujao kutakuwa na ugeni wa wafanya biashara kati ya 30 au 40 kutoka nchi ya Ufaransa ambao watakuja kujionea fursa mbali mbali za kibiashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.
Mhe. Balozi alimuelezea Makamu wa Rais azma ya Ufaransa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Tanzania katika kuanzisha na kuendesha kozi mbali mbali kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mwisho aliipongeza Serikali kwa mapambano dhidi ya rushwa na urasimu jambo litakalo wavutia wawekezaji wengi nchini.
Aidha, Bw. Emmanuel Baudran Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa alisema Shirika lao linakusudia kuanzisha kiwanda cha vifaa vya umeme wa jua (solar) mkoani Shinyanga pia shirika hilo limeshafanya miradi ya uboreshaji maji taka katika manispaa ya Temeke na wanaendelea na mikakati ya uanzishwaji wa miradi mingine.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alimshukuru na kumpongeza Balozi wa Ufaransa kwa kazi nzuri wanazofanya hapa nchini.
Alimhakikishia kwamba Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano kwa mambo yote muhimu yenye maslahi kwa wananchi.
Wakati huohuo Makamu wa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Mhe. Michael Danford.
Serikali ya Nigeria yatamani kufanya mazungumzo na Boko Haram
Serikali ya Nigeria imesema ina mpango wa kutumia njia ya mazungumzo badala ya kutumia nguvu za kijeshi ili kuwaokoa wasichana 110 waliotekwa katika mji wa Daptch hivi karibuni pamoja na wale waliotekwa mjini Chibok mwaka 2014.
Ofisi ya Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari imesema ingependa kuwapata wasichana waliotekwa Chibok na Daptch wakiwa hai.
Utekaji huo ndio mkubwa zaidi kufanywa na kundi la wanamgambo la Boko Haram lenye itikadi kali ya Jihadi, tangu lilipowateka wasichana wa shule 270 katika mji wa chibok mwaka 2014.
Hata hivyo, taarifa iliyowahi kutolewa na vyombo vya habari vya kiusalama ilidai kuwa takribani wasichana 100 waliachiliwa huru na Boko Haram baada ya kulipwa fidia na serikali.
Viongozi Watatu Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) Waitwa Polisi
Viongozi watatu wa nafasi za juu katika Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP) wameitikia wito wa kufika kwa mpelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) Jijini Dar es Salaam leo asubuhi kwa lengo la kuhojiwa kutokana na tukio la Abdu Nondo.
Hayo yamebainishwa na taarifa iliyotolewa na Afisa Habari- TSNP, Hellen Sisya baada ya kupita siku moja tokea Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuwataka viongozi hao kufika katika ofisi za DCI.
"Tumepokea taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inatofautiana kabisa na ile ya Iringa juu ya kuonekana kwake. Hata hivyo, kabla ya taarifa ya uchunguzi kulitanguliwa na matamko ya viongozi wa juu waliodai kuwa Abdul Nondo alijiteka mwenyewe jambo ambalo kwa vyevyote lingeathiri uchunguzi wa jeshi la polisi", amesema Hellen.
Pamoja na hayo, Hellen ameendelea kwa kusema "pamoja na mapungufu yote tunaamini Nondo atatendewa haki atakapofikishwa mahakamani".
Chanzo: mpekuzi












