Katibu tawala wa wilaya ya NANYUMBU mkoani MTWARA, SALUM PALANGO
, March 10 mwaka huu 2018 katika Siku ya Mazoezi Kitaifa, amemuagiza Kaimu
Mkurugenzi wa wilaya hiyo NDG. HAMZA SEIF MNALIWA, kuwachukulia hatua za
Kinidhamu watumishi wapatao 50 wa Kata ya LIKOKONA, walioshindwa
kuhudhuria katika Mazoezi hayo yanayofanyika nchi nzima kila Jumamosi ya Wiki
ya pili ya mwanzo mwa Mwezi.NANYUMBU: wafanyakazi 50 kuchukuliwa hatua
Katibu tawala wa wilaya ya NANYUMBU mkoani MTWARA, SALUM PALANGO
, March 10 mwaka huu 2018 katika Siku ya Mazoezi Kitaifa, amemuagiza Kaimu
Mkurugenzi wa wilaya hiyo NDG. HAMZA SEIF MNALIWA, kuwachukulia hatua za
Kinidhamu watumishi wapatao 50 wa Kata ya LIKOKONA, walioshindwa
kuhudhuria katika Mazoezi hayo yanayofanyika nchi nzima kila Jumamosi ya Wiki
ya pili ya mwanzo mwa Mwezi.
PALANGO amebainisha hatua hizo za kinidhamu kuwa ni pamoja na
kuwapa barua za kujieleza wafanyakazi hao, za kwanini hatua za kinidhamu
zisichukuliwe dhidi yao.
Katika hatua nyingine Katibu tawala huyo kijana machachari pindi
awapo kazini, amemuagiza Mratibu Elimu KATA kuhakikisha MCHAKAMCHAKA kwa wanafunzi
unarudishwa kama zilivyo taratibu za kawaida .
“Wanafunzi wamenithibitishia Kuwa hawakimbii tena mchakamchaka,
ambao ni muhimu kwa ukuaji wa Afya ya mwili na akili zao na hivyo kuimarisha
taaluma zao, mratibu hakikisha mchakamchaka unarudi kama kawaida” amesema PALANGO
Ni utamaduni wa Wilaya ya NANYUMBU kufanya Mzunguko wa Mazoezi
katika Kila Kata za Wilaya hiyo na Mwezi huu ilikuwa ni Zamu ya KATA ya LIKOKONA.
Mazoezi hayo yamehudhuriwa na wakuu wa Idara, Wananchi, DIWANI
wa KATA, Kaimu Mkurugenzi,Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari LIKOKONA na
Shule mbili za Msingi na Mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Tawala Wilaya SALUM
PALANGO, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo Wilaya na Katibu
wake ni Afisa Utamaduni/ Afisa Michezo wa Wilaya.
TARIME: Nondo afananishwa na Viongozi
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche
amewataka watanzania kupiga kelele ili sheria ichukue mkondo wake hasa katika
masuala ya watu kubambikiwa kesi
Mh. Heche ameamua kusema hayo baada ya Mwanafunzi Abdul Nondo
kupotea jijini Dar es salaam kisha kupatikana huko Iringa na habari
tofauti zikiibuka kwamba alijiteka na kudaiwa kwamba alitoa taarifa za uongo.
Kutokana na taarifa hizo Mbunge wa Heche amesema kwamba "Kama viongozi wanabambikiziwa
kesi mchana kweupe sio ngumu kwao kumtengenezea huyu kijana kesi".
Ameongeza kuwa "Ni
wajibu wa Watanzania wote kupiga kelele sheria ifuatwe kwenye sakata
hili".
Nondo, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) aliripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu siku ya Machi
8 , ambapo amepatikana akiwa ametupwa barabarani Mafinga mkoani Iringa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, amesema Nondo
amepatikana akiwa salama bila jeraha lolote wala kupigwa lakini wamefungua
jalada hilo kwa ajili ya uchunguzi na mpaka sasa bado yupo kituoni hapo na
iwapo atabainika alidanganya atashughulikiwa kama wahalifu wengine.
DAR ES SALAAM: SERIKALI YAONGEZA HUDUMA ZA MATIBABU YA UGONJWA WA FIGO
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati wa matembezi ya Siku ya figo duniani ambayo yamefanyika mapema leo katika viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar es salaam.
“Wataalamu tunao 13 kwa upande wa madaktari, tumeiona hiyo changamoto kama Serikali, tumeongeza wigo wakufanya mafunzo kwa madaktari bingwa, na hivi karibuni tutatangaza ufadhili kupitia Serikali, vile vile tumetenga fedha kwaajili ya kuwafundisha madaktari ili kuweza kufanya matibabu ya figo” alisema Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile aliendelea kusema kwamba Serikali imeongeza wigo wa usafishaji damu kwa kuongeza vituo Zaidi ya 17 ambavyo vinatoa huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa Figo katika hospitali binafsi na Hospitali za Serikali.
“Tumeongeza wigo wa usafishaji damu hadi tunavyoongea, tunavituo Zaidi ya 17 ambavyo vinatoa huduma ya kusafisha damu katika hospitali binafsi pamoja na hospitali zetu za Serikali , Muhimbili kuna vitanda 42, Mloganzira kuna vitanda 12, Bugando vitanda 6, KCMC vitanda 6, Mbeya vitanda 6, bila kusahau Regency, TMJ, Agakhan, Hindumandal, na tunaendelea kuimarisha huduma”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Vile vile Dkt. Ndugulile alisema kuwa Serikali imeanza upandikizaji wa Figo na imeshafanikisha kwa mgonjwa mmoja mpaka sasa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na matarajio ni kufanya upasuaji kwa mgonjwa mmoja kila mwezi mmoja.
Aliendelea kusema mgonjwa mmoja anahitaji wastani wa shilingi milioni 37 kwa mwaka kwa ajili ya kulipia gharama ya kusafisha damu. Aidha, anahitaji kusafiri na kufika kwenye huduma kwa wastani wa safari 126 kwa mwaka sawa na wastani wa safari 3 hadi 4 kwa wiki.
Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile aliendelea kuwa kukumbusha kuwa Serikali ya awamu ya tano imeongeza Bajeti ya Dawa kutoka Bilioni 30 ilipokuwa ikiingia madarakani hadi sasa ni Bilioni 270 kwaajili ya Dawa, vifaa na vifaa tiba kwaajili ya magonjwa yakiwemo magonjwa ya Figo.
“Tumeongeza bajeti kwaajili ya Vifaa, Dawa na Vifaa Tiba kutoka Bilioni 30 wakati Serikali hii inaingia madarakani mbaka Bilioni 270, yaani mara tisa Zaidi, kwahiyo Dawa na Vifaa Tiba kwaajili ya matibabu ya Figo tunazo” alisema Dkt. Ndugulile.
Mwisho Dkt.Ndugulile alitoa wito kwa wananchi kubadili jinsi ya kuandaa vyakula nyumbani, mfano kwa kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na kiasi cha mafuta kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza magonjwa shinikizo la damu (hypertension), kisukari na unene wa kupindukia, vile vile kuhamasisha familia kufanya mazoezi.
“Watanzania hatujui kula, tunakula bora chakula kuliko chakula bora, Matumizi ya vyakula vya mafuta, matumizi ya chumvi nyingi, matumizi ya vilevi, matumizi ya sigara kama hayana ulazima basi tupunguze, tutumie vyakula vilivyochemshwa na vilivyochomwa, bila kusahau kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi angalau mara 3 kwa wiki kwa lisaa limoja inatosha” alisema Dkt. Ndugulile.
CHANZO: WIZARA YA AFYA - WAMJW
Tundu Lissu Kufanyiwa Upasuaji Wa 19 March 14
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu Machi 14,2018 atafanyiwa upasuaji wa 19 katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji.
Upasuaji huo ni mwendelezo wa ambazo amekuwa akifanyiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikokuwa amelazwa baada ya kushambuliwa kwa risasi akiwa katika makazi yake mjini Dodoma Septemba 7,2017.
Alipatiwa huduma za awali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Taarifa ya Lissu aliyoitoa jana usiku Machi 10,2018 akielezea afya yake amesema licha ya sasa kuweza kusimama bila msaada, amejuzwa na timu ya madaktari wanaomtibu kuwa kasi ya mfupa wa juu ya goti kuunga ni ndogo.
"Madaktari wangu wamesema wasipoingilia kati na kurekebisha mfupa huo itachukua muda mrefu sana kuunga," amesema.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) amesema madaktari wamemweleza hata mfupa huo ukiunga baada ya muda mrefu, hautaunga kwa namna utakaoondoa hatari ya kuvunjika baadaye.
"Kwa sababu hizi, madaktari wangu wamependekeza kufanya operesheni nyingine kwenye mfupa wa juu ya goti la kulia Machi 14,2018, nitarudi Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg, kwa ajili ya kufanyiwa operesheni hiyo," amesema.
Amesema yuko katika mikono salama ya kitabibu chini ya madaktari Profesa Stefa Nijs na Profesa Willem-Jan Mertsemakers ambao amesema ni madaktari bingwa wa mifupa wanaosifika barani Ulaya.
"Hivyo, msiwe na hofu. Mungu wetu aliyeniwezesha kuwa hai sasa, ataendelea kutenda miujiza kupitia kwa madaktari bingwa hawa," amesema.
Lissu amesema ataendelea kutoa taarifa za maendeleo ya afya yake kwa kadri itakavyohitajika akiwaomba Watanzania kumuunga mkono yeye na familia yake katika kipindi anachopitia.
Lissu yupo Ubelgiji tangu Januari 6,2018 alikopelekwa akitokea Hospitali ya Nairobi, Kenya.
DAR ES SALAAM: Mamlaka ya hali ya hewa Yatoa Tahadhari
Mamlaka ya hali ya hewa iliyopo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania imewatahadharisha wananchi kuwepo kwa hali mbaya ya hewa katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara ndani ya saa 24 kuanzia leo.
Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na mamlaka hiyo na kudai kutakuwepo vipindi vifupi vya mvua kubwa ambazo zinatarajiwa kunyesha katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro, Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Kilimanjaro, Manyara na Arusha
Mbali na hilo, TMA imesema kutakuwepo upepo mkali unaofikia kilomita 30 kwa saa kutoka Kaskazini- Mashariki kwa Pwani ya Kaskazini na kutokaa Kaskazini-Magharibi kwa Pwani ya Kusini huku hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi.
SHINYANGA: Rais Mkuu Ataka Viwanda Viajiri Wazawa
Rais John Magufuli amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha wamiliki wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.
Ametoa agizo hilo leo Jumapili Machi 11,2018 akizindua kiwanda cha kufua vyuma cha Kahama Oil Mill mjini Kahama mkoani Shinyanga.
Rais amesema wananchi wazawa ndio waliompigia kura, hivyo wapewe kipaumbele cha ajira katika viwanda hivyo.
“Kama wewe ni waziri nimekuteua mimi, unaacha kuwaajiri wazawa walionipigia kura unaenda kuchukua watu wa nje hii hakubaliki,” amesema.
Rais Magufuli amesema, “Nitoe wito kwa mawaziri wangu na wakurugenzi, hakikisheni viwanda mnavyovianzisha nchini mnaajiri Watanzania, hawa ndio walionipigia kura.”
Amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanatumia malighafi za ndani kutengeneza bidhaa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
“Mwaka huu pamba nyingi imelimwa, Kahama Oil Mill pia mnatengeneza mafuta, hakuna haja ya kuagiza pamba kutoka nje wakati tuna pamba ya kutosha hapa,” amesema.
Kuhusu kiwanda cha chuma amesema malighafi inapatikana nchini, hivyo iwapo mkurugenzi wa Kahama Oil Mill anahitaji yupo tayari kumpa bure badala ya kuagiza nje.
Pia, amewataka Watanzania kununua bidhaa za ndani, huku akiwataka wamiliki wa viwanda kutengeneza zenye ubora ili kuhimili ushindani.
CHANZO: MPEKUZI
KUWANIA UONGOZI TLS KWAZUA KIZAAZAA
Mabadiliko ya kanuni za uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) zimewagonganisha viongozi wake na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) baada ya kudaiwa kuongezwa masharti yanayowanyima fursa watumishi wa umma na wanasiasa kuwania uongozi ndani ya chama hicho.
Kanuni hizo zimechapishwa juzi katika Gazeti la Serikali (GN) namba 116, jambo ambalo limekifanya chama hicho kuitisha kikao cha dharura kujadili mabadiliko hayo kwa maelezo kuwa hakikuyapitisha katika kikao cha baraza la uongozi.
Kipengele hicho kinacholalamikiwa na TLS ni cha (8)(e) kinachoeleza masharti ya mwanachama anayetaka kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho kuwa asiwe mtumishi wa umma, mbunge, diwani au kiongozi wa chama cha siasa kilichosajiliwa.
Pia, Rais wa TLS, Tundu Lissu aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu amedai kuwa saini yake imeghushiwa katika kanuni hizo inayoonyesha alisaini Februari 9.
Jana, Makamu Mwenyekiti wa TLS, Godwin Ngwilimi alisema, “Hiki kipengele hakikupitishwa katika kanuni za kikao cha baraza la uongozi ambazo zilikwenda kwa AG, lakini zimerudi kikiwa kimeongezwa, kwa nini aliweka muulize AG.”
Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu kuzungumzia madai hayo, AG Dk Adelardus Kilangi alijibu kwa kifupi “sorry (samahani) sizungumzi katika magazeti.”
Kuhusu hatua ambazo TLS itachukua kutokana na utata huo, Ngwilimi alisema, “Kwanza tayari ishakuwa katika gazeti la Serikali, mimi siwezi kutoa uamuzi wangu, tumeitisha kikao cha dharura cha kujadili suala hilo. Hatujajua AG ametumia mamlaka gani kuweka hayo mabadiliko.”
Kuhusu madai ya Lissu kwamba saini yake imeghushiwa, Ngwilimi alisema saini hiyo haijaghushiwa kwani iliyotumika ni saini ya kielektroniki ambayo baada ya kikao cha baraza la uongozi kumaliza kupitisha kanuni, mmoja wa watumishi wa TLS aliiweka.
“Hata Lissu analijua hilo, lakini kwa kuwa kipengele hicho kimeongezwa ndiyo anasema imeghushiwa lakini kama isingeongezwa kipengele hicho sidhani kama angeongea, lakini hili nalo la saini ni moja ya mambo tutakayojadili kwenye kikao hicho cha dharura.”
Kwa upande wake, Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki na mwanasheria mkuu wa Chadema alisema, “Vita ya mwaka jana inaendelea...”
“Wanajua hawaniwezi kwenye sanduku la kura za mawakili... Mimi sijashiriki kikao au shughuli yoyote ya TLS tangu wanaoitwa ‘watu wasiojulikana’ waliponipiga risasi nyingi mwaka jana,” alisema Lissu.
“Nitasaini vipi kanuni za uchaguzi zilizopitishwa na kikao ambacho sikukiendesha wala kukihudhuria?”
Ngwilimi alipoelezwa kuhusu Lissu kupinga saini yake kutumika wakati hakuwapo kwenye kikao alisema “Hilo sasa siwezi kulisemea lakini muulize yeye ni mjumbe wa baraza la uongozi, alipowauliza walimjibu nini.”
Hata hivyo, Lissu alipoulizwa swali hilo alisema “Walifanya hivyo kwa idhini ya nani? Mimi sikuwepo kwenye kikao husika, sikushiriki kwenye kufanya maamuzi haya na sikusaini au kutoa idhini ya sahihi yangu kutumika kwenye maazimio ya kikao husika.
“Sahihi yangu imetumika huko nyuma kwenye kikao gani ambacho sikukihudhuria? Hakuna, kwa kadri ninavyofahamu hii ni hoja ya ajabu kabisa. Maana yake ni kwamba wanaweza kutumia sahihi yangu ya kielektroniki kutolea pesa benki na ikawa sawa tu.”
DODOMA: Waziri Kigwangalla Amsimamisha Kazi Mkuu Wa Kanda - Pori La Akiba Rukwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amemsimamisha kazi mkuu wa kanda Pori la Akiba Rukwa lililopo wilayani Mlele mkoani Katavi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu, Dk Aloyce Nzuki iliyotolewa jana Machi 10,2018 inasema waziri amemsimamisha kazi Emmanuel Barabara ambaye pia ni mhifadhi wanyamapori mkuu.
Dk Kigwangalla amefikia uamuzi huo kutokana na taarifa za raia wema kuwa Barabara amekuwa akishirikiana na majangili kuhujumu rasilimali za misitu nchini.
Waziri Kigwangalla katika taarifa hiyo ameagiza iundwe kamati ya uchunguzi kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
Amesema iwapo mtuhumiwa atatiwa hatia, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma ili iwe fundisho kwa wengine.
“Tunatoa onyo kali kwa watumishi wa wizara wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu wa rasilimali za misitu, wanyamapori na mali kale. Tunawataka waache mara moja kwa kuwa hatutosita kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo, ikiwemo kufukuzwa kazi,” amesema.
Amewataka watumishi wa wizara kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na miongozo iliyowekwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya uhifadhi wa rasilimali za nchi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

DAR ES SALAAM: KUBENEA "DC HAPI KADANGANYA UMMA, NIMEONDOKA MWENYEWE OFISINI"
Akizungumza na wanahabari asubuhi ya leo Jumamosi Machi 10, 2018, Mhe. Kubenea amesema mkuu wa wilaya hiyo ameamua kutumia jina lake (Kubenea) ili kujipatia umaarufu maana taarifa ya mkuu wa wilaya imekuja ikiwa tayari yeye ameshahama kwenye ofisi hizo.
Katika hatua nyingine Mhe. Kubenea amewataka vijana walioaminiwa na Mhe. Rais, na kupewa madaraka, wasilewe madaraka hayo na kujiona wao miungu watu, huku akisema vyeo walivyonavyo kwasasa ni vya kupita tuu maana walikuwepo waliokuwa navyo kabla yao, hivyo wawatumikie wananchi kwa kuzingatia utawala wa sheria bila kuwabagua wapinzani.
Mhe. Kubenea amehitimisha mkutano wake na wanahabari kwa kumsihi Mhe. Rais Magufuli atazame yale yanayofanyika kwa majirani zetu Kenya, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alikutana na mpinzani wake Raila Odinga, na kufanya mazungumzo naye kwa maslahi ya wakenya wote, hivyo kumuomba Rais Magufuli asiwachukulie wapinzani kama maadui, bali watu wanaompa changamoto ili kulisaidia taifa, na hivyo hanabudi kushirikiana nao.
CHANZO: DARMPYA
BERLIN: TANZANIA YAJITANGAZA KITALII UGHAIBUNI
Lengo la Maonesho hayo ni kutangaza fursa za utalii zilizopo nchini hapa Tanzania katika masoko mbalimbali ya utalii barani Ulaya na duniani kote.
Maonesho hayo yalianza tarehe 7 mwezi huu na yanatarajiwa kufikia tamati hapo keshokutwa tarehe 11 Machi, 2018. Ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo umehusisha Sekta ya Umma na Sekta mbalimbali Binafsi.
Ambapo washiriki kutoka sekta ya umma ni pamoja na idara ya utalii kutoka wizara ya maliasili na utalii,bodi ya utalii Tanzania,shirika la hifadhi za taifa,mamlaka ya hifadhi Ngorongoro na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania.
Kwa upande mwingine sekta binafsi jumla ya kampuni zipatazo 60 zimeshiriki maonyesho hayo ikiwemo kampuni moja inayoshughulika na uratibu wa matukio (Events and Exhibitions management),kampuni tatu zinazoshughulika na usafiri wa anga,kampuni ishirini na saba(27) zinazoshughulika na huduma za malazi yaani hoteli,loji na kambi za utalii na kampuni ishirini na tisa(29) za Wakala wa biashara ya kusafirisha watalii.
Pamoja na shughuli za maonyesho hayo katibu mkuu Milanzi amefanya pia mikutano kadhaa na wadau wa utalii na washirika wa maendeleo waliopo nchini Ujerumani.
Sekta ya utalii inachangia wastani wa asilimia ishirini na tano(25%) ya fedha zote za kigeni zinazoingia nchini kwetu Tanzania huku ikichangia asilimia kumi na saba na nusu(17.5) ya pato la Taifa.
CHANZO: DARMPYA











