Rais John Magufuli amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha wamiliki wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.SHINYANGA: Rais Mkuu Ataka Viwanda Viajiri Wazawa
Rais John Magufuli amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha wamiliki wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.
Ametoa agizo hilo leo Jumapili Machi 11,2018 akizindua kiwanda cha kufua vyuma cha Kahama Oil Mill mjini Kahama mkoani Shinyanga.
Rais amesema wananchi wazawa ndio waliompigia kura, hivyo wapewe kipaumbele cha ajira katika viwanda hivyo.
“Kama wewe ni waziri nimekuteua mimi, unaacha kuwaajiri wazawa walionipigia kura unaenda kuchukua watu wa nje hii hakubaliki,” amesema.
Rais Magufuli amesema, “Nitoe wito kwa mawaziri wangu na wakurugenzi, hakikisheni viwanda mnavyovianzisha nchini mnaajiri Watanzania, hawa ndio walionipigia kura.”
Amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanatumia malighafi za ndani kutengeneza bidhaa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
“Mwaka huu pamba nyingi imelimwa, Kahama Oil Mill pia mnatengeneza mafuta, hakuna haja ya kuagiza pamba kutoka nje wakati tuna pamba ya kutosha hapa,” amesema.
Kuhusu kiwanda cha chuma amesema malighafi inapatikana nchini, hivyo iwapo mkurugenzi wa Kahama Oil Mill anahitaji yupo tayari kumpa bure badala ya kuagiza nje.
Pia, amewataka Watanzania kununua bidhaa za ndani, huku akiwataka wamiliki wa viwanda kutengeneza zenye ubora ili kuhimili ushindani.
CHANZO: MPEKUZI
KUWANIA UONGOZI TLS KWAZUA KIZAAZAA
Mabadiliko ya kanuni za uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) zimewagonganisha viongozi wake na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) baada ya kudaiwa kuongezwa masharti yanayowanyima fursa watumishi wa umma na wanasiasa kuwania uongozi ndani ya chama hicho.
Kanuni hizo zimechapishwa juzi katika Gazeti la Serikali (GN) namba 116, jambo ambalo limekifanya chama hicho kuitisha kikao cha dharura kujadili mabadiliko hayo kwa maelezo kuwa hakikuyapitisha katika kikao cha baraza la uongozi.
Kipengele hicho kinacholalamikiwa na TLS ni cha (8)(e) kinachoeleza masharti ya mwanachama anayetaka kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho kuwa asiwe mtumishi wa umma, mbunge, diwani au kiongozi wa chama cha siasa kilichosajiliwa.
Pia, Rais wa TLS, Tundu Lissu aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu amedai kuwa saini yake imeghushiwa katika kanuni hizo inayoonyesha alisaini Februari 9.
Jana, Makamu Mwenyekiti wa TLS, Godwin Ngwilimi alisema, “Hiki kipengele hakikupitishwa katika kanuni za kikao cha baraza la uongozi ambazo zilikwenda kwa AG, lakini zimerudi kikiwa kimeongezwa, kwa nini aliweka muulize AG.”
Hata hivyo, alipotafutwa kwa simu kuzungumzia madai hayo, AG Dk Adelardus Kilangi alijibu kwa kifupi “sorry (samahani) sizungumzi katika magazeti.”
Kuhusu hatua ambazo TLS itachukua kutokana na utata huo, Ngwilimi alisema, “Kwanza tayari ishakuwa katika gazeti la Serikali, mimi siwezi kutoa uamuzi wangu, tumeitisha kikao cha dharura cha kujadili suala hilo. Hatujajua AG ametumia mamlaka gani kuweka hayo mabadiliko.”
Kuhusu madai ya Lissu kwamba saini yake imeghushiwa, Ngwilimi alisema saini hiyo haijaghushiwa kwani iliyotumika ni saini ya kielektroniki ambayo baada ya kikao cha baraza la uongozi kumaliza kupitisha kanuni, mmoja wa watumishi wa TLS aliiweka.
“Hata Lissu analijua hilo, lakini kwa kuwa kipengele hicho kimeongezwa ndiyo anasema imeghushiwa lakini kama isingeongezwa kipengele hicho sidhani kama angeongea, lakini hili nalo la saini ni moja ya mambo tutakayojadili kwenye kikao hicho cha dharura.”
Kwa upande wake, Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki na mwanasheria mkuu wa Chadema alisema, “Vita ya mwaka jana inaendelea...”
“Wanajua hawaniwezi kwenye sanduku la kura za mawakili... Mimi sijashiriki kikao au shughuli yoyote ya TLS tangu wanaoitwa ‘watu wasiojulikana’ waliponipiga risasi nyingi mwaka jana,” alisema Lissu.
“Nitasaini vipi kanuni za uchaguzi zilizopitishwa na kikao ambacho sikukiendesha wala kukihudhuria?”
Ngwilimi alipoelezwa kuhusu Lissu kupinga saini yake kutumika wakati hakuwapo kwenye kikao alisema “Hilo sasa siwezi kulisemea lakini muulize yeye ni mjumbe wa baraza la uongozi, alipowauliza walimjibu nini.”
Hata hivyo, Lissu alipoulizwa swali hilo alisema “Walifanya hivyo kwa idhini ya nani? Mimi sikuwepo kwenye kikao husika, sikushiriki kwenye kufanya maamuzi haya na sikusaini au kutoa idhini ya sahihi yangu kutumika kwenye maazimio ya kikao husika.
“Sahihi yangu imetumika huko nyuma kwenye kikao gani ambacho sikukihudhuria? Hakuna, kwa kadri ninavyofahamu hii ni hoja ya ajabu kabisa. Maana yake ni kwamba wanaweza kutumia sahihi yangu ya kielektroniki kutolea pesa benki na ikawa sawa tu.”
DODOMA: Waziri Kigwangalla Amsimamisha Kazi Mkuu Wa Kanda - Pori La Akiba Rukwa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amemsimamisha kazi mkuu wa kanda Pori la Akiba Rukwa lililopo wilayani Mlele mkoani Katavi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu, Dk Aloyce Nzuki iliyotolewa jana Machi 10,2018 inasema waziri amemsimamisha kazi Emmanuel Barabara ambaye pia ni mhifadhi wanyamapori mkuu.
Dk Kigwangalla amefikia uamuzi huo kutokana na taarifa za raia wema kuwa Barabara amekuwa akishirikiana na majangili kuhujumu rasilimali za misitu nchini.
Waziri Kigwangalla katika taarifa hiyo ameagiza iundwe kamati ya uchunguzi kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
Amesema iwapo mtuhumiwa atatiwa hatia, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma ili iwe fundisho kwa wengine.
“Tunatoa onyo kali kwa watumishi wa wizara wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu wa rasilimali za misitu, wanyamapori na mali kale. Tunawataka waache mara moja kwa kuwa hatutosita kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo, ikiwemo kufukuzwa kazi,” amesema.
Amewataka watumishi wa wizara kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na miongozo iliyowekwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya uhifadhi wa rasilimali za nchi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

DAR ES SALAAM: KUBENEA "DC HAPI KADANGANYA UMMA, NIMEONDOKA MWENYEWE OFISINI"
Akizungumza na wanahabari asubuhi ya leo Jumamosi Machi 10, 2018, Mhe. Kubenea amesema mkuu wa wilaya hiyo ameamua kutumia jina lake (Kubenea) ili kujipatia umaarufu maana taarifa ya mkuu wa wilaya imekuja ikiwa tayari yeye ameshahama kwenye ofisi hizo.
Katika hatua nyingine Mhe. Kubenea amewataka vijana walioaminiwa na Mhe. Rais, na kupewa madaraka, wasilewe madaraka hayo na kujiona wao miungu watu, huku akisema vyeo walivyonavyo kwasasa ni vya kupita tuu maana walikuwepo waliokuwa navyo kabla yao, hivyo wawatumikie wananchi kwa kuzingatia utawala wa sheria bila kuwabagua wapinzani.
Mhe. Kubenea amehitimisha mkutano wake na wanahabari kwa kumsihi Mhe. Rais Magufuli atazame yale yanayofanyika kwa majirani zetu Kenya, ambapo Rais Uhuru Kenyatta alikutana na mpinzani wake Raila Odinga, na kufanya mazungumzo naye kwa maslahi ya wakenya wote, hivyo kumuomba Rais Magufuli asiwachukulie wapinzani kama maadui, bali watu wanaompa changamoto ili kulisaidia taifa, na hivyo hanabudi kushirikiana nao.
CHANZO: DARMPYA
BERLIN: TANZANIA YAJITANGAZA KITALII UGHAIBUNI
Lengo la Maonesho hayo ni kutangaza fursa za utalii zilizopo nchini hapa Tanzania katika masoko mbalimbali ya utalii barani Ulaya na duniani kote.
Maonesho hayo yalianza tarehe 7 mwezi huu na yanatarajiwa kufikia tamati hapo keshokutwa tarehe 11 Machi, 2018. Ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo umehusisha Sekta ya Umma na Sekta mbalimbali Binafsi.
Ambapo washiriki kutoka sekta ya umma ni pamoja na idara ya utalii kutoka wizara ya maliasili na utalii,bodi ya utalii Tanzania,shirika la hifadhi za taifa,mamlaka ya hifadhi Ngorongoro na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania.
Kwa upande mwingine sekta binafsi jumla ya kampuni zipatazo 60 zimeshiriki maonyesho hayo ikiwemo kampuni moja inayoshughulika na uratibu wa matukio (Events and Exhibitions management),kampuni tatu zinazoshughulika na usafiri wa anga,kampuni ishirini na saba(27) zinazoshughulika na huduma za malazi yaani hoteli,loji na kambi za utalii na kampuni ishirini na tisa(29) za Wakala wa biashara ya kusafirisha watalii.
Pamoja na shughuli za maonyesho hayo katibu mkuu Milanzi amefanya pia mikutano kadhaa na wadau wa utalii na washirika wa maendeleo waliopo nchini Ujerumani.
Sekta ya utalii inachangia wastani wa asilimia ishirini na tano(25%) ya fedha zote za kigeni zinazoingia nchini kwetu Tanzania huku ikichangia asilimia kumi na saba na nusu(17.5) ya pato la Taifa.
CHANZO: DARMPYA
KENYA: Kenyatta, Odinga wakutana Nairobi
Hii ni mara ya kwanza kwa wawili hao kukutana tangu walipotofautiana kuhusu uchaguzi mkuu uliokuwa na upinzani mkali wa Agosti 8, 2017 na wa marudio Oktoba 26 ambao Odinga alisusia.
Agenda ya kikao chao haikuwekwa wazi. Baada ya kikao chao Kenyatta na Odinga walitarajiwa kulihutubia taifa.
Seneta wa Siaya James Orengo, mshirika wa karibu wa Odinga aliliambia shirika la habari la Reuters akithibitisha kufanyika kikao hicho.
“Kinafanyika sasa, lakini tutatoa maelezo zaidi kitakapokuwa kimemalizika,” amesema.
Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu aliwaambia waandishi wa habari kwamba Odinga atakuwa wa kwanza kuhutubia na kisha Rais Kenyatta atatoa maoni yake.
Kikao cha viongozi hao kimefanyika siku ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson anatarajiwa kuwasili Nairobi akiwa katika ziara ya Afrika.
CHANZO: MWANCHI
DAR ES SALAAM: MAGONJWA YA FIGO YANAATHIRI ZAIDI WANAWAKE
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati akitoa tamko la siku ya Figo duniani ambapo huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi.
Kwa upande wa Tanzania Naibu Waziri huyo alisema ugonjwa huo umekuwa ukiongezeka na tafiti zilizofanya Kanda ya Kaskazini mwaka 2014, ulionyesha kuwa kati ya 7% – 15% ya Watanzania wana matatizo sugu ya figo na kwa asilimia kubwa yamekuwa yakichangiwa na magonjwa ya Shinikizo la Damu na Kisukari
Hata hivyo aliongeza kuwa kwa utafiti uliofanywa na Hospitali ya Kanda Bugando, umeonesha kuwa 83% ya Wagonjwa wa Kisukari wana matatizo sugu ya figo na kati ya hawa, 25% walikuwa wanahitaji huduma za usafishaji damu.
“Wagonjwa waliokuwa wanapatiwa huduma ya kusafisha damu kutokana na figo kushindwa kufanya kazi, ambao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) walikuwa 178. Kwa sasa idadi ya Wagonjwa hawa imeongezeka na kufikia 783.
Alisema Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa wagonjwa thelathini na tano(35) kwa mwaka nje ya nchi kwa ajili ya kupandikiza figo na idadi ya waliokwishapandikizwa figo na ambao wanafuatiliwa matibabu yao katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni takribani 204.“Gharama za kupandikiza figo nje ya nchi ni wastani wa fedha za Kitanzania milioni 75 hadi 77 kwa mtu mmoja,ikijumuisha upandikizaji,nauli na malazi”Alisema Dkt.Ndugulile
Dkt.Ndugulile alitoa wito kwa wananchi kubadili jinsi ya kuandaa vyakula nyumbani, mfano kwa kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula na kiasi cha mafuta kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza magonjwa shinikizo la damu (hypertension), kisukari na unene wa kupindukia, vile vile kuhamasisha familia kufanya mazoezi.Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya figo ya mwaka huu wa 2018 ni “FIGO NA AFYA YA WANAWAKE: WASHIRIKISHWE, WATHAMINIWE NA WAWEZESHWE”.
CHANZO: AFYABLOH Na WAMJW. Dar es salaam.
MASASI:wasichana waonyesha vipaji kwa kusakata "volleyball"
Timu ya volleyball ya
watoto wa kike kutoka shule ya msingi na sekondari MKALAPA Kata ya NDANDA iliyopo
Halmashauri ya Wilaya ya MASASI wameadhimisha siku ya wanawake duniani kwa mchezo
wa volleyball.
Wakizungumza baada ya
mchezo huo, wamefurahi na kuiomba jamii
kutoa kipaumbele katika michezo inayohusisha jinsia ya kike.
Ikumbukwe kuwa timu ya watoto hao ni moja kati
ya timu ambazo zimeupa ushindi Mkoa wa MTWARA katika mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA,
hivyo watoto wa kike wakiwezeshwa wanaweza katika kujitelea maendeleo na kushiriki katika safari ya kuelekea uchumi wa
Viwanda kwa kutumia vipaji vyao.
WAKATI HUOHUO
Halmashauri
ya Wilaya ya MASASI imeadhimisha siku ya Wanawake duniani katika Kata ya NDANDA
huku Mambo MATATU ya kumwezesha mwanamke ili kushiriki kwa vitendo kuelekea
uchumi wa viwanda ifikapo 2025 ikiwemo kuwawezesha kielimu, kuwapa mitaji na
kuwashirikisha katika maamuzi yakisisitizwa.
Halmashauri ya wilaya ya
Masasi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi milioni 79,445,000
zimekopeshwa kwa vikundi 31 vya wanawake ikiwa ni mitaji ya kuendeleza biashara
zao na hivyo kuzalisha kwa tija ili kukuza uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla.
WAKATI HUOHUO
Halmashauri
ya Wilaya ya MASASI imeadhimisha siku ya Wanawake duniani katika Kata ya NDANDA
huku Mambo MATATU ya kumwezesha mwanamke ili kushiriki kwa vitendo kuelekea
uchumi wa viwanda ifikapo 2025 ikiwemo kuwawezesha kielimu, kuwapa mitaji na
kuwashirikisha katika maamuzi yakisisitizwa.
Halmashauri ya wilaya ya
Masasi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi milioni 79,445,000
zimekopeshwa kwa vikundi 31 vya wanawake ikiwa ni mitaji ya kuendeleza biashara
zao na hivyo kuzalisha kwa tija ili kukuza uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani mwaka 2018
unasema"KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA: TUIMARISHE USAWA WA KIJINSIA NA
UWEZESHAJI WANAWAKE VIJIJINI"
RUKWA: WAZIRI UMMY AWAONYA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WASIOTENGA FEDHA ZA UWEZESHAJI WANAWAKE
Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mkoa wa Rukwa ambapo amepokea changamoto kutoka kwa wanawake wengi kuhusu utoaji mdogo wa mikopo na wengine kutopata kabisa mikopo kutoka Halmashauri zao.
Ummy amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashuri zote nchini kutenga asimilia 4 kwa ajili ya wanawake na kutoa mikopo yenye tija itaakayoweza kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi na sio kurudi nyuma kiuchumi.
“Mikopo ya laki tatu haina tija toeni kikopo yenye tija itakayoendana na kauli mbiu ya kuelekea uchumi wa viwanda,”alisema Mhe. Ummy
Mhe. Ummy ameongeza kuwa ili kufikia azma ya Tanzania ya Viwanda basi Halmashauri hazina budi kujiwekea mikakati ya kutoa mikopo mikubwa itakayo wawezesha wanawake na wananchi kwa ujumla kufikia dhana hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kalembo Mhe. Julieth Binjula ameiomba Serikali kuendelea kuwawezesha wanawake kwa kuwapa elimu ya jinsi ya kutumia fedha na kuendesha miradi mbalimbali itakayo wakwamua kiuchumi.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Khalfan Haule amesisitiza wadau kushirikiana na Serikali pale ambapo wanaweza kuwawezesha wanawake sehemu walipo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kutoa mchangokatika kuchangia kujiletea maendeleo jumuishi.
Siku ya Wanawake Duniani 2018 kilele chake ni siku ya tarehe 8 Machi, 2018 na Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni‘‘KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA: TUIMARISHE USAWA WA JINSIA NA UWEZESHAJI WA WANAWAKE VIJIJINI”. Dhamira ya Wizara nikuona kila mdau mmoja mmoja anaelewa madhumuni ya kaulimbiu na kuchukua hatua kuchangia utekelezaji wa ujumbe mahususi wa kuwajumuisha wanawake wa vijijini katika maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.
CHANZO: DEWJBLOG
UNIDO TAYARI KUSAIDIA TANZANIA YA VIWANDA
Kauli hiyo imetolewa katika hafla ya
chakula cha mchana iliyoandaliwa na Sekta Binafsi kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO
Li Yong ambaye alikuwa katika ziara ya kwanza nchini Tanzania na pia ya kwanza
nje ya makao makuu ya Shirika hilo baada ya kuchaguliwa kwake kwa mara ya pili
mwaka jana.
Alisema katika hotuba yake kwamba moja ya
majukumu makubwa ya shirika hilo ni kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu
(SDGs) hasa lengo namba tisa la maendeleo na teknolojia
kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo.
Aidha alisema ili kufanikisha hilo
kumesisitizwa ushirikiano ambao ni lengo namba 17 la SDGs.
Alisema sekta binafsi ikishirikiana vyema
na serikali ndiyo inayoendesha uchumi hasa katika kutoa fursa za kazi kwani
asilimia 80 ya kazi kila mwaka hutolewa na sekta binafsi.
Alisema katika hotuba yake hiyo kwamba
amefurahishwa na malengo ya Tanzania na nia ya Shirika hilo kuona kwamba
malengo hayo kuelekea uchumi wa kati wa viwanda yanatekelezwa kwa kuangalia
vionjo muhimu.
Aidha alisema kwamba wataendelea
kushirikiana na sekta binafsi kupitia TSPF kuhakikisha kwamba wananchi
wanashirikishwa katika malengo ya maendeleo ili kuwa na malengo endelevu na
yanayozingatia mazingira.
Naye Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini-
TPSF Dr. Reginald Mengi akizungumza katika hafla hiyo aliitaka UNIDO kusaidia
kutengeneza utajiri nchini Tanzania.
Dr. Mengi alisema kwamba ziara ya kiongozi
huyo imekuja wakati muafaka, wakati ambapo Tanzania inaelekeza macho yake
katika uchumi wa kati na hivyo kuwa na nafasi ya kusaidia ndoto hiyo kufanikiwa.
Alisema wakati nchi nyingi zimekuwa
zikipiga maendeleo, zimekuwa na msingi dhaifu wa uchumi wa viwanda kutokana na
kusafirisha zaidi bidhaa ambazo hazijasindikwa au zinazotokana na uziduaji.
Alisema hali hiyo pamoja na kuipa utajiri
nchi imekuwa haitawanyi utajiri uliopo.
Alisema kutokana na hali hiyo, UNIDO ina
kazi kubwa ya kusaidia Tanzania kufikia lengo lake la viwanda hata kusaidia
kuanzishwa kwa maeneo ya viwanda (Industrial Park).
Aidha aliishukuru UNIDO kwa kuwezesha
sekta binafsi na serikali kukaa pamoja kupitia Baraza la Taifa la Biashara
ambako kunakuwa na mazungumzo yenye tija kuhusiana na maendeleo ya biashara na
uchumi nchini Tanzania.
Alifafanua kwamba UNIDO ina nafasi kubwa
ya kuisaidia Tanzania hasa katika mipango mikakati yake kwa kuunganisha sekta
binafsi na umma ili kuiharakisha Tanzania kuelekea uchumi wa kati wenye
kutegemea viwanda.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda pamoja na Kimataifa Dr Augustine
Mahiga, ambaye wizara yake ndiye ilimwalika Mkurugenzi mkuu huyo, pamoja na
kumshukuru kwa kuitikia wito huo aliitakabkusaidia kuchagiza maendeleo ya
viwanda.
Alisema kwamba viwanda vya Tanzania bado
vichanga na vinahitaji kusaidiwa na kupewa nguvu ya kuendelea mbele kwani
pamoja na uchanga wake mchango wake katika kuelekea uchumi wa kati ni mkubwa.
Awali kabla ya hafla ya chakula cha mchana
UNIDO ilitiliana saini na serikali ya Tanzania waraka wa kusaidia kuitoa
Tanzania katika mipango ya kitaifa kwenda kwenye mipango ya nchi na washirika
ili kufikia uchumi wa kati.
Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es
Salaam kati ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles
Mwijage pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, Li Yong huku yakishuhudiwa na
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.










