DAR ES SALAAM: WAZIRI NDALICHAKO, ANNA MAKONDA WATOA SOMO KWA WANAWAKE
Ikiwa leo Machi 8, 2018 ni kilele cha maadhimisho ya siku ya
wanawake duniani, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Stadi, Profesa
Joyce Ndalichako na Spika Mstaafu wa Bunge, Anna Makinda wametoa somo kwa
wanawake hapa nchini.
Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa
kuhusu masuala ya maendeleo endelevu ya Wanawake barani Afrika, Prof.
Ndalichako amewataka wanawake kufanya kazi kwa bidi ili waweze kuaminiwa na
jamii.
“Wito wangu ni kwamba tuendelee kufanya
kazi kwa bidii kwa sababu historia imemuweka mwanamke katika nafasi isiyo nzuri
kwa hiyo wanawake tukiendelea kufanya kazi kwa bidii mchango wetu kwa jamii
utaendelea kuonekana na kuthaminiwa na hivyo tunaweza tukawa tunapata nafasi
kubwa na nzuri ya kulitumikia taifa, hii historia ya kubaki nyuma tutaiondoa
wanawake wenyewe kwa kufanya kazi kwa bidi,” amesema.
Naye Makinda amewataka wanawake kujiamini
sambamba na kuwa na uthubutu huku akiwasihi kujitika katika utafutaji wa elimu
kwani ndiyo mkombozi wa maendeleo ya wanawake.
“Elimu ni kitu muhimu sana, wanawake wengi
elimu zao ni ndogo wananyanyasika wananyang’anywa mali sababu hawajui wanaenda
wapi, elimu yenyewe siyo ya utaniutani, wenyewe wanasoma lakini hawajui
wanasoma nini. Mkombozi wa mwanamke ni kupatikana elimu sahihi ya kuweza
kupambanua maisha yake na kujua haki zake ziko wapi na si kumdekeza sababu
ukimdekeza hatuwezi kufanya chochote,” amesema na kuongeza.
“Elimu inamfanya mwanamke athubutu, kama
huna elimu hijuamini ndiyo unatengeneza mazingira ya kupata mafanikio kwa
kupitia mtu, kusoma vizuri kujiamini, kuwa na uthubutu mwengine anataka kwenye
kazi apelekwe na mtu.”
Na Regina Mkonde
DAR ES SALAAM: Jaji Mkuu awataka hawa wajitathimini
Jaji Mkuu wa Tanzania, PROF. IBRAHIM
JUMA amewataka watendaji na wataalamu wa Mahakama, nchini kujitathmini na kuona
namna wanavyoweza kutoa msukumo wa maboresho wa Mahakama katika suala la kutoa
haki kwa wakati
Jaji PROF. JUMA amesema hayo Jijini ARUSHA wakati akifungua
Mkutano wa watendaji na wataalam wa Mahakama wenye lengo la kutathmini
utekelezaji wa mpango wa maboresho wa Mahakama nchini.
Jaji Mkuu huyo wa Tanzania amesema kuwa kuna tatizo la utoaji wa
taarifa muhimu kwa Wananchi kitika MAHAKAMA jambo linalowanyima wananchi haki
ya kufuatilia mashauri yao.
Pia Jaji Mkuu amewataka watendaji kufanya Tathmini na kuona
namna wanavyeweza kutoa msaada katika kufikia malengo yaliyokusidiwa na
Mahakama.
Msikilize hapa chini Jaji Mkuu akiongea zaidi.
DODOMA: DKT. KALEMANI AIAGIZA TPDC KUHARAKISHA UUNGANISHAJI WA GESI MAJUMBANI
Dkt. Kalemani aliyasema hayo tarehe 3 Machi, 2018 ofisini kwake mkoani Dodoma alipokutana na watendaji wa TPDC kwa lengo la kujadili suala la usambazaji wa Gesi asilia katika nyumba za Wananchi pamoja na bei watakayouziwa wananchi hao.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kalemani aliwataka TPDC kuunganisha nyumba kuanzia Hamsini ( 50) na kuendelea katika maeneo ya Mwenge na Mikocheni kwa kuwa tayari miundombinu ya Bomba la Gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani limepita maeneo hayo.
kuhusu suala la bei ya kuwauzia wateja, Dkt. Kalemani alisema kuwa Gesi hiyo itauzwa kwa Wananchi kwa pungufu ya 40% ya bei ya mitungi ya gesi itakayokuwa sokoni kwa wakati huo.
“Hii ni gesi yetu na Bomba ni la kwetu, vyote vinapatikana hapahapa nchini, ni vyema iuzwe kwa bei ya chini zaidi ya ile iliyopo sokoni kwa sasa, ili kila mwananchi aweze kumudu gharama zake pia itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kulinda misitu yetu,” alisema Dkt. Kalemani.
Dkt. Kalemani pia aliwaagiza TPDC kuendelea na taratibu za kuwaunganisha wananchi wa Mtwara na huduma ya Gesi asilia katika nyumba zao kama itakavyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni.
Aidha alilishauri Shirika hilo, kutumia wataalam wake wa ndani kupitia Shirika lake Tanzu la kulinda Miundombinu ya Gesi ( GASCO) ili kusambaza Gesi asilia kwenye nyumba za wananchi badala ya kutegemea wakandarasi ambao mchakato wa kuwapata unachukua muda mrefu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, alifafanua kuwa gharama za uunganishwaji wa huduma ya Gesi asilia katika nyumba za wananchi itategemea na ramani ya nyumba husika pamoja na umbali wa nyumba kutoka ilipopita miundombinu ya Bomba la gesi asilia linalotumika kusambaza gesi katika maeneo ya makazi.
Vilevile, Mhandisi Musomba aliweka wazi kuwa mfumo wa kusambaza Gesi asilia katika nyumba za wananchi utakuwa kama ule unaotumika kusambaza huduma ya maji, lakini ulipaji wa gharama za matumizi ya gesi hiyo utakuwa kama ule unaotumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lipa Umeme Kadri Unavyotumia ( LUKU) kwa maana kwamba kila mtumiaji atalipia huduma kadri atakavyokuwa akitumia.
Gesi itakayokuwa ikisambazwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ni ile inayozalishwa katika Visima vya Gesi vilivyopo katika Mkoa wa Lindi na Mtwara.
DODOMA: Bashe anena "Lolote Litakalonikuta ni Mipango ya Mungu"
Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe amewahakikishia
wananchi wa Tanzania kuwa hoja yake aliyoiwakilisha kwa Katibu wa Bunge kuwa
haiwezi kukwamishwa na jambo lolote kwa madai hakuna kisichojulikana
kinachoendelea kutoka katika nchi.
Bashe ametoa kauli hiyo jana (Machi 08, 2018) wakati
alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwa lengo la
kuelezea sababu zilizompelekea yeye kama Mbunge kuandika barua ya kutaka
kuundwe kwa kamati ya uchunguzi dhidi ya matukio mbalimbali yanayoonesha
kutishia umoja, usalama na mshikamano wa taifa la Tanzania.
"Madhumuni ya kikatiba ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) ni kuwasemea wananchi, kuwatetea kwa hiyo natimiza wajibu
wangu kama Mbunge sioni kama nitapoteza Ubunge wangu katika hili.
"Mimi ninaamini nitapoteza ubunge wangu
kwasababu zifuatazo, endapo nitashindwa kutimiza wajibu wangu ndani ya Bunge,
nikishindwa kutimiza wajibu wangu ndani ya Jimbo langu kwa maana nimeshindwa
kuisimamia serikali katika kuleta maendeleo, nimeshindwa kutimiza ahadi wakati
wa uchaguzi katika jimbo langu na mwisho wanaccm watakaposema kwenye mchakato
wa kidemokrasia wa kura kwamba Hussein wewe hapana.
"Mimi ni muumini wa kiislamu ninaamini kila
binadamu umauti utamfika (kifo) na chochote kitakachonifika ni kile ambacho
amekipanga Mwenyezi Mungu lakini sina hofu yeyote kwasababu hili sio taifa la
namna hiyo.
"Nikiwa kama Hussein sidhani hii hoja kama
inakwenda kukwama kwasababu unapoikwamisha hoja unapaswa kusema unaikwamisha
kwa kutumia misingi gani kama watu wanaamini kwa kila kinachotokea ndani ya
ardhi ya Tanzania sioni kama itakwama.
"Bunge limeshafanya maamuzi mbalimbali juu ya
masuala mbalimbali katika rekodi ya nchi hii, kwa hiyo mimi nadhani ni muhimu
tukatoa fursa jambo hili lifike Bungeni na likifika huko kama litakataliwa basi
tujue ni kwasababu zipi na kama nilivyofanya kuwaambia watanzania ndivyo
hivyo nitarudi kuwaambia limekataliwa kwasababu zipi na hapo tutajadili hatua
za kufanya".
Kwa upande mwingine, Bashe amesema anasubiria majibu
ya barua aliyotuma kutoka kwa Katibu wa Bunge Pamoja na Katibu Chama cha
Mapinduzi (CCM) ambayo ameeleza dhamira na nia yake huku akisisitiza zaidi kuwa
jambo hilo hajalifanya kwa mihemuko (kukurupuka) bali amefanya kwa umakini wa
hali ya juu na utafiti wa kutosha.
DAR ES SALAAM: Mtuhumiwa wa Maandamano ya CHADEMA awadai polisi gari yake
Mfuasi wa CHADEMA, Ally Rajabu anayekabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anaomba arejeshewe gari lake ambalo lipo mikononi mwa polisi.
Ally Rajabu ni mshtakiwa wa 28 kati ya 31 wakiwemo watatu waliopigwa risasi na Polisi ambao ni wafuasi wa chama hicho wanaokabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali maeneo ya Kinondoni Mkwajuni Dar es Salaam.
Awali kabla ya kueleza hayo, Wakili wa Serikali Aldo Mkini, amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Naye Wakili wa utetezi, Alex Massaba amedai kuwa wateja wake wawili ni wagonjwa na wameshindwa kufika mahakamani hapo.
Baada ya kueleza hayo, mshtakiwa wa 28, Ally Rajabu ameieleza mahakama kuwa anaomba kurudishiwa gari lake ambalo linashikiriwa na Jeshi la Polisi tangu siku ya maandamano.
Hata hivyo, Hakimu Mashauri amesema kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuingilia masuala yaliyofanyika Polisi ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi April 4, 2018.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Thabitha Mkude, Khaji Lukwambe, Emmanuel Kimio, Mohamed Juma, Husein Mnimbo na wenzao kwa pamoja wanadaiwa kati ya February 16, 2018 maeneo ya Mkwajuni Kinondoni DSM walifanya mkusanyiko usio wa halali kinyume cha sheria.
CHANZO: MPEKUZI
CHANZO: MPEKUZI
DODOMA: Makamu wa Rais na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO wafanya mazungumzo kuhusu viwanda
Katika mkutano huo ambao ulikuwa na lengo ya kujadiliana masuala mbalimbali ya uendelezaji Viwanda nchini Tanzania.
Mkurugenzi huyo amemjulisha Makamu wa Rais kuwa Tanzania ni nchi ya nne kuitembelea tangia ateuliwe .
Aidha katika mazungumzo hayo Mkurugenzi wa UNIDO amesema anajua Tanzania ajenda yao kuu ni uanzishwaji wa Viwanda na alimhakikishia Makamu wa Rais kwamba UNIDO itajitahidi kusaidia ajenda hiyo.
“Kuna umuhimu wa kuzingatia sekta binafsi na viwanda vidogo na vya kati wakati wa uanzishwaji viwanda ili vijana na wanawake wapate ajira,” alisema Mkurungenzi Mkuu wa UNIDO.
Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong amesema pia suala la uanzishwaji na Uendelezaji wa Viwanda ni lazima lizingatie masuala ya upatikanaji wa nishati na mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha Mkurugenzi huyo alisifia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea ndani ya Serikali ya awamu ya tano na kusema UNIDO suala muhimu ni Utekelezaji.
Pia aliupongeza uongozi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na mashirikiano mazuri na Serikali.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alimhakikishia Mkurungenzi huyo wa UNIDO ushirikiano wa hali ya juu kutoka Serikalini na alimuomba kuipa Tanzania kipaumbele katika programu yake muhimu itakayochochea maendeleo ya Viwanda ya “Programmes For Country Partnership-PCP”.
Mwisho Kiongozi huyo aliishukuru Tanzania kwa mapokezi mazuri na programu nzuri walizompangia.
Viongozi wengine walioshiriki kwenye mazungumzo hayo ni Waziri wa Viwanda, Bishara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Philip Mgango pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Augustine Mahiga ambapo pia Waziri wa Viwanda , Biashara na Uwekezaji alitia saini pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO Bw. Li Yong
Tamko la Kusudio la kuanzisha (Declaration of Intention) Mpango wa UNIDO unaojulikana kama “Programmes For Country Partnership-PCP” ambapo Makamu wa Rais alishuhudia kusainiwa kwa Tamko hilo,kusainiwa kwa tamko hilo kutarahisisha mchakato wa wa kukamilika kwa uwasilishwaji wa ombi la Tanzania kuomba iingizwe katika Mpango Maalumu wa UNIDO ambao ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya Viwanda.
CHANZO: MPEKUZI
DAR ES SALAAM: Mvua yaleta maafa kwa Jeshi la Polisi
Mvua zilizoambatana na upepo mkali zilizonyesha usiku
wa jana zimeacha athari kubwa kwa Jeshi la Polisi kwa kuharibikiwa na
jengo lao la ofisi pamoja na kujeruhiwa askari mmoja.
Akizungumza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni, ACP Muliro Jumanne Muliro amekiri kutokea kwa
tukio hilo na kusema ofisi ndogo iliyopo ndani ya jengo la serikali ya Mtaa wa
Goba limeharibika kufuatia kuangukiwa na nguzo ya mnara wa simu kuangukia.
"Askari mmoja amejeruhiwa katika
ajali hiyo ila alifanikiwa kukimbizwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
matibabu", amesema Kamanda Muliro.
Mbali na tukio hilo, mvua zilizonyesha
usiku wa jana (Machi 07, 2018) zimeweza kuwaathiri pia baadhi ya jamii kwa
kuezua paa za nyumba zao na kusababisha kukosa makazi.
CHATO: Rais Magufuli kuzindua tawi la benki Chato Kesho
Rais John Magufuli kesho Machi 9, 2018 anatarajiwa kuzindua tawi la benki ya CRDB katika jengo jipya lililopo eneo la mlimani mjini Chato mkoani Geita.
Taarifa iliyotolewa leo na mkuu wa Wilaya ya Chato Shaban Ntarambe, inaeleza kuwa hafla ya uzinduzi wa tawi hilo itaanza saa mbili asubuhi katika eneo lilipo jengo jipya la benki hiyo.
Ntarambe amewataka wananchi wa Chato na maeneo ya jirani kujitokeza kumsikiliza rais na kushuhudia uzinduzi huo ambao unaendelea kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Baadhi ya wananchi wa mjini Chato wamepongeza juhudi zinazofanywa na wadau wa maendeleo kusogeza huduma karibu na wananchi na kusema Chato ya sasa sio kama ya zamani na kwamba, uwepo wa miundombinu hiyo inafungua maendeleo.
CHANZO: MPEKUZI
DODOMA: Makamu wa Rais atoa neno siku ya Wanawake duniani
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu amesema ana kila sababu ya kuzungumza japo kwa kifupi jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kuimarisha usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini.
Makamu wa Rais amesema kuwa serikali ina sera kuendeleza wanawake,huku akisema kuwa sheria ya ardhi za mwaka 1999 ambazo husimamia haki za wanawake katika kumiliki ardhi.
"Leo katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Mimi kama mwanamke na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nina kila sababu ya kuzungumza japo kwa kifupi jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kuimarisha usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini.
"Serikali inayo Sera ya kuendeleza Wanawake, Sheria za ardhi za mwaka 1999 ambazo husimamia haki za wanawake katika kumiliki ardhi.
"Sera ya elimu bure inayotekelezwa na serikali ya Awamu ya Tano imetoa fursa kwa watoto wengi wa kike kuandikishwa shuleni.
"Kuboreshwa kwa huduma za kijamii kama vile kujengwa zahanati na vituo vya afya na usambazaji wa maji vimempunguzia mwanamke usumbufu na hivyo kumpa muda wa kutosha kufanya shughuli za maendeleo.
"Usambazaji umeme vijijini kwa kiasi kikubwa umesaidia wanawake wengi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.
"Uwezeshaji wa Wanawake kwa kuwapatia asilimia 5 ya mapato ya halmashauri na asilimia 30 ya zabuni za halmashauri kumewawezesha wanawake wengi kufanya biashara na hatimaye kuwa na uhakika wa kipato .
"Serikali kuendelea kuhimiza taasisi za kifedha kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha wanawake wengi kunufaika na mikopo hiyo.
"Kurasimisha vikoba pamoja na kuwashawishi wanawake wengi zaidi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuweza kunufaika na mafao na mikopo itolewayo na taasisi hizo.
"Kauli Mbiu:Kuelekea Uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini."
IRINGA: Walichokisema Polisi baada ya kupatikana kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) aliyekuwa ametekwa
Jeshi la Polisi Mkoani Iringa limeeleza kuwa limefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Omari Nondo alikuwa ametekwa au la ili liweze kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire akiongea na waandishi wa habari ameeleza kuwa bado uchunguzi dhidi ya tukio hilo unaendelea ili waweze kubaini kama ni kweli ametekwa na kuwakamata wahusika kwa ajili ya kuwachukulia hatua zaidi za kisheria.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa alimefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli kama alikuwa ametekwa, na kama kweli alikuwa ametekwa tunaahidi kwamba sisi jeshi la polisi tukiwapata watuhumiwa sheria itachukua mkondo wake,” amesema Kamanda Bwire.
Kamanda Bwire ameongeza kuwa pamoja na kufanya uchunguzi, jeshi hilo linapeleleza zaidi ili kujiridhisha kama taarifa iliyotolewa ni ya uongo kwa nia ovu ya kuhamasisha wanafunzi nchini kuleta uvunjifu wa amani, na wakibaini hilo watamchukulia hatua kali za kisheria.
“Aidha tunaendelea kuchunguza kama ametoa tarifa za uongo kwa nia ovu, kwa lengo la kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake ili kuleta uvunjifu wa amani nchini. tutamshughulikia kama wahalifu wengine,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda bwire amesema kuwa Abdul anaonekana kuwa na afya njema na hana majeraha yoyote kuashiria kuwa alipigwa au kuteswa.
“Kwa sasa anaonekana hali yake ni nzuri, hana majeraha yoyote, hajapigwa ni mzima wa afya njema. hivyo basi Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi kupitia maeneo yote aliyopitia ili tuweze kujua nini kilichomsibu,” alisema Kamanda.
Vile vile aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi wakati wa uchunguzi dhidi ya tukio hilo ili waweze kubaini kilichotokea na wahusika waweze kufikishwa mahakamani.
Abdul Nondo (24) ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka wa tatu kitivo cha Siasa na Utawala, alisemekeana kupotea katika mazingira ya kutatanisha siku ya Jumanne majira ya kati ya saa 5 na 6 usiku jijini Dar es Salaam na kupatikana jana Jumatano akiwa Mkoani Iringa.










