DODOMA: SHILINGI TRILIONI 1 ZATENGWA KULIPA MADENI MBALIMBALI MWAKA WA FEDHA 2017/2018
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi ameeleza hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa miradi na ahadi mbalimbali za Serikali.
“Kati ya shilingi Trilioni 1 zilizotengwa kulipia madeni kwa mwaka huu wa fedha, shilingi Bilioni 896.3 zimeshalipwa kwa watoa huduma, wazabuni na watumishi wa Serikali,” alisema Dkt. Abbasi.
Amesema hesabu hiyo inajumuisha shilingi Bilioni 43 ambazo zimelipwa Februari, 2018 ikiwa ni malimbikizo ya wafanyakazi wa sekta ya Umma.
“Madeni mengine uhakiki unaendelea na yataendelea kulipwa siku zijazo na tutawajulisha,” alifafanua Dkt. Abbasi.
Vile vile amesema, Serikali katika kuwaondolea adha ya usafiri kwa wananchi wa maziwa makuu likiwemo Ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria. Kwa upande wa Ziwa Victoria, mkandarasi amepatikana na majadiliano ya mwisho na kusaini mkataba na kampuni ya STX ya Jamhuri ya Korea vitafanyika mwezi huu kwa ajili utengenezaji wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400.
Kwa upande wa Ziwa Tanganyika zabuni kwa ajili ya utengenezaji wa meli mpya ya abiria na mizigo itatangazwa mwezi huu. Meli hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo na italeta mapinduzi makubwa katika usafiri ziwani hilo.
Aidha Dkt. Abbasi amesema Julai mwaka huu nchi itapokea ndege kadhaa mpya ikiwemo Boeing Dreamliner na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kitaifa, Kimataifa na Kimkoa unaendelea kwa kasi kote nchini.
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
DODOMA: BASHE Akabidhi hoja binafsi kwa katibu wa BUNGE "kuchunguza matukio ya Mauaji na Utekaji Nchini"
Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe ameshindwa kuvumilia matukio mbalimbali yanayojitokeza katika ardhi ya Tanzania na mwisho ameamua kuandika barua yenye hoja binafsi kwa Katibu wa Bunge ili kuundwe kamati ya teule ya uchunguzi.
"Leo asubuhi (jana) nimewasilisha kwa Katibu wa Bunge barua ya kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kuunda Kamati teule ya Bunge kuchunguza matukio mbalimbali yanayoonesha kutishia umoja, usalama na mshikamano wa Taifa letu", amesema Bashe.
CHANZO: MPEKUZI HURU

MBEYA: Saba Watiwa Mbaroni Mbeya Kwa Mauaji ya Mlinzi Wa SUMA-JKT
#Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linawashikilia watu saba kwa matukio mbalimbali ya uhalifu, wakiwamo vijana watano wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya mlinzi wa SUMA-JKT.
Wanadaiwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumpora bunduki na kutokomea nayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa #Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema Februari 26, mwaka huu ya saa 1:30 jioni, vijana hao wakiwa na mapanga, walimvamia na kumshambulia mlinzi huyo, Chewe Wilson (34), akilinda kituo cha mafuta cha Manyanya kilichopo Uyole.
Aliwataja vijana hao ni Hamis Shaban (19) na Ibrahim Mbilinyi (22) wote wakazi wa Itezi, Stan Wema (21) mkazi wa Uyole, Bahati Laulend (22) mkazi wa Iduda na Sambaa Samson (32) mkazi wa Isyeseye.
Alisema vijana hao baada ya kumjeruhi wakidhani amekufa walimpora bunduki aina ya Shortgun, mali ya SUMA-JKT aliyokuwa anaitumia na kutokomea nayo.
Hata hivyo, alisema mlinzi huyo alikutwa na wasamaria wema akiwa hai na kukimbizwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufani ya Mbeya, lakini akafariki kesho yake kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata vijana hao na baada ya kupekuliwa walikutwa na bunduki hiyo waliyopora yenye namba za usajili 009009906-MP-18EM-M wakiwa wameificha nyumbani,” alisema Mpinga na kuongeza:
“Vilevile vijana hao wanaojiita ‘Doshaz’ walikutwa na mapanga matatu ambayo mojawapo lilitumika kumjeruhi Chewe na maganda matatu matupu ya risasi, tulipowahoji walikiri kuhusika na tukio hilo na tunatarajia kuwafikisha mahakamani upelelezi ukikamilika.”
Aliongeza kuwa vijana hao walieleza kuna mtu aliwatuma ili wakaibe bunduki hiyo kwa ahadi ya kupewa zawadi ya Sh. milioni tatu.
Katika tukio lingine, watu wawili akiwamo mzee wa miaka 60, wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kosa la kutengeneza bunduki ya kienyeji aina ya Shortgun pamoja na kukutwa na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengenezea silaha hiyo.
Mpinga aliwataja ni Mzee Fadhili Mayenga (60) na Mashaka Samuel (38), wote wakazi wa Kijiji cha Kambikatoto Wilaya ya Chunya.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Machi Jumamosi mchana kufuatia msako mkali uliofanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Kwa mujibu wa Mpinga, baada ya kukamatwa walipekuliwa na kukutwa na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengeneza silaha hiyo pamoja na risasi 25 za kienyeji ambazo hutumika kwenye silaha hiyo.
Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani muda wowote upelelezi utakapokuwa umekamilika.
CHANZO: MPEKUZI HURU
Zaidi ya Vibanda 600 vimeungua katika Ajali ya moto Mbagala
Soko la Kampochea lililopo Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam limeteketea kwa moto alfajiri ya leo Jumanne Machi 6, 2018 na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.Imeelezwa moto huo ulianza kuteketeza mabanda ya soko hilo saa 12 alfajiri huku uongozi ukitaja kuwa chanzo ni hitilafu ya umeme.
Mwenyekiti wa soko hilo, Mohamedy Njiwa amesema limekuwa likikumbwa na hitilafu za mara kwa mara licha ya kuripoti kwa mamlaka husika.
"Wiki mbili zilizopita hapa kulikuwa na hitilafu ya umeme, ulikuwa unakuja na kukata. Tanesco walikuja kufanya ukaguzi wakaeleza kuwa kuna hitilafu kwenye transfoma,"amesema.
Amesema mabanda yote 673 yaliyokuwapo eneo hilo yameungua kwa moto na kwamba, hasara ni kubwa.
Mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo, Chacha Mwang'wene amesema hajafanikiwa kuokoa chochote zaidi ya taarifa zake za biashara.
Msemaji wa Zimamoto Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Peter Mwambene amesema jeshi hilo lilijitahidi kudhibiti moto huo, lakini tatizo kubwa ni aina ya bidhaa zilizokuwamo.
"Soko hili lina mali ambazo zinachangia kusambaza moto kwa kasi sana kama mitumba ambayo ni rahisi kuteketea kwa moto,"amesema.
Pia, amesisitiza kuwapo kwa vifaa vya awali vya kuzimia moto ili kunusuru mali kwenye masoko mengine jijini hapa.
Hatahivyo, wafanyabiashara hao wameeleza nia yao ya kuendelea kulitumia soko hilo licha ya agizo la mkuu wa Wilaya ya Temeke kuwataka kuhamia masoko mengine.
CHANZO: MPEKUZI HURU
MTWARA: BIASHARA KATI YA INDIA NA MTWARA KUENDELEA KUIMARIKA
Ushirikiano
wa Kibiashara kati ya Tanzania na India umeendelea kuimarika kutokana na
kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa zinazouzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo
mbili. Hayo yalisemwa na Mheshimiwa Sandeep Arya, Balozi wa India nchini
Tanzania wakati wa Kongamano la Kukuza Biashara kati ya India na Mtwara
lililofanyika jana Jumamosi tarehe 3 Machi, 2018 katika Ukumbi wa NAF Hotel
Apartment, Mjini Mtwara.
Balozi Sandeep alisema asilimia
24 ya mauzo ya bidhaa za Tanzania nchi za nje kwa mwaka 2017 ziliuzwa nchini
India. Mwaka 2017 Tanzania iliuza nchini India bidhaa zenye thamani ya Dola za
Kimarekani 977.5 ambapo ilinunua bidhaa mbalimbali kutoka nchini India zenye
thamani ya Dola za Kimarekani 1,165.
Alisema mauzo ya bidhaa za Tanzania zilizouzwa India mwaka 2017
yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 38 ikinganishwa na mauzo ya mwaka 2016.
Hii ilitokana na
ongezeko la bidhaa zilizozalishwa nchini ambazo zilihitajika kwa wingi huko
India zikiwemo dhahabu, korosho n.k. Aidha, Balozi huyo alisema ili kuimarisha
biashara kati ya Tanzania na India, Serikali ya India imeondoa tozo za ushuru
kwa baadhi ya bidhaa zinazosafirishwa kutoka Tanzania kwenda India zikiwemo
korosho, mchele n.k na pia imefuta gharama za kibali cha kuingia India (Visa)
kwa wafanyabiashara kutoka Tanzania na kubaki 7,000 tu.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Chama cha
Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mtwara na Ubalozi wa India
nchini Tanzania.
Karim Faida – JAMII FM.
MTWARA: SERIKALI IMESEMA HAIJARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA BARABARA YA MTWARA MNIVATA
Waziri wa
Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Mh MAKAME MBALAWA amepozungumza na Wananchi wa
Kata ya Naliendele Jana Tarehe 4/3/2018 na kumtaka Mkandarasi anaejenga
Barabara hiyo kwa kiwango cha Lami kuharakisha ujenzi huo.
Waziri MBALAWA mesema"Haturidhishwi na kasi ya Ujenzi wa barabara hii yenye
Urefu wa Km 50 Kutoka Mtwara hadi Kijiji cha Mnivata kwa Thamani ya Tsh Bilioni
89.59 na ndio maana tunatembelea
mara kwa mara kumsukuma Mkandarasi huyu afanye kwa kasi tunayoitaka"
Akijibu maswali ya baadhi ya Wananchi waliouliza kuhusu Swala la
wenyeji kukosa Ajira ndogondogo na kupewa watu wa Mikoa mingine pamoja na
kukosa miundombinu itakayosaidia maji yasituwame katika eneo moja, Waziri huyo
amesema atayafanyia kazi kama Serikali.
Waziri Mbalawa aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara MH EVOD
MMANDA ambae nae alipata nafasi ya kuzungumza na Wananchi hao na kuwasihi
waendelee kushirikiana na Mkandarasi huyo ili barabara hiyo iweze kukamilika
kwa haraka.
Karim Faida-JAMII FM.
MTWARA: VIWANDA VYA UBANGUAJI LAZIMA WAPATE KOROSHO GHAFI
Waziri wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji
CHARLES MWIJAGE amevihakikishia Viwanda
vya Ubanguaji Korosho MTWARA vinapata malighafi hiyo mwaka mzima kuliko ilivyo
hivi sasa ambapo zaidi ya tani laki tatu za korosho ghafi zimesafirishwa nje ya
Nchi huku Viwanda hivyo vikifungwa kwa kukosa malighafi hiyo.
MWIJANGE
amesema hayo baada ya kutembelea Shirika linalohudumia viwanda vidogo vidogo
SIDO Mkoani hapa na kukuta kiwanda kinachotumiwa na wanawake
kubangua korosho kimefungwa kutokana na kukosa Korosho ghafI
Hata hivyo Waziri MWIJAGE amesema hilo
haliwezi kukubalika lazima utaratibu ufanyike ili sehemu ya Korosho
ghafi ibaki Nchini kulinda viwanda hivyo,
Akiwa mkoani MTWARA waziri
huyo amewakabidhi SUMA JKT kazi ya ujenzi wa Kiwanda cha
wajasiriamali kitakachojengwa katika ofisi za SIDO MTWARA,
Mwakilishi wa SUMA JKT Meja ATUPELE MWAMFUPE ambae ni Meneja wa Kanda ya Kusini
amesema watahakikisha watafanya kazi ndani ya muda miezi mitatu kazi itakuwa
imekamilika.
Maeneo mengine aliyotembelea na kituo cha
uwekezaji , Kiwanda cha kubangua korosho cha Cash nut pamoja na kiwanda cha
kuzalisha Cementi cha DANGOTE, na MTWARA CEMENT.
GREGORY MILLANZI- JAMII FM
DAR ES SALAAM: JOSEPH BUTIKU: UVCCM MLINDENI RAIS MAGUFULI
Mzee Butiku ameyasema hayo leo Jumapili Machi 4, 2018, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiwasilisha mada ya Uzalendo na Historia ya Taifa letu kwa Viongozi, ikiwa ni sehemu ya mafunzo maalumu ya uongozi kwaajili ya vijana wa umoja huo kwa ngazi ya kata, wilaya na mkoa inayoendelea jijini Dar es Salaam.
“Uamuzi wa Rais Magufuli wa kuhakikisha rasilimali za taifa letu haziendelei kunyonywa na wezi wa ndani na nje umemletea maadui wengi sana na nyinyi vijana mnayo dhamana kubwa ya kuhakikisha mnamlinda Rais wetu kufa na kupona” amesema Butiku.
Toka Rais Magufuli aingie madarakani na kuanza kusimamia rasilimali za nchi ili ziwanufaishe watanzania wote hasa maskini, kumekuwepo na vilio kutoka kwa wale ambao walikuwa wakinufaika na rasilimali hizo, huku wakifanya kila njia kuhakikisha wanakwamisha juhudi zake, jambo ambalo halijafanikiwa, na kwa mwenendo wa Rais Magufuli inaonekana dhahiri shahiri kuwa mipango ya kumkwamisha haitafainikiwa maana wananchi wengi wamekuwa wakimuunga mkono.
TAHLISO Yatoa Tamko Kuhusu Wanafunzi Wanaotaka Mwigulu Ajiuzulu Kwa Kifo Cha Akwilina
Ndugu waandishi wahabari tunawashukuru sana kwa kukubali wito wetu wakuja kujumuika pamoja nasisi.
Leo tarehe 3/3/2018 tumekutana na viongozi wa vyuo vikuu nchi nzima kwa ajili yakujadili changamoto zinazotukabili.
Kikao hiki ni cha TAHLISO Baraza Kuu (SENATE) kina husisha Maraisi wa serikali za wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini.
Tunatambua kwamba kuna kifo cha mwanafunzi mwenzetu Akwilina Akwilini,mwanafunzi wa chuo cha NIT kilichotokea mwezi wa pili. Tunawashukuru wanafunzi wenzetu kwa utulivu mkubwa na mshikamano waliouonesha tangu msiba ulipotokea, wakati wa kipindi cha majonzi hadi kufikia sasa.
Tunamshukuru Mhe.Raisi wa Jamuhuri ya Muunganowa Tanzania kwa kuingilia kati suala hili na kuagiza uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika kuhusika na kifo cha Akwilina Akwilini.
Vilevile tunaishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ukaribu waliouonesha katika kipindi chote cha msiba.
Tunaomba wanafunzi waendelee kuwa watulivu wakati maagizo ya Mh. Raisi yakitekelezwa.
Aidha tunapenda jamiii tambue kuwa TAHLISO ndio chombo kikuu cha kuwasemea wanafunzi wote nchi nzima Tanzania na sio kikundi kingine chochote kile.
Vipo vikundi vingi vimejitokeza na kutoa matamko mbalimbali baada ya kifo hiki kutokea, vikundi vingine vikaenda mbali Zaidi kwakuwataka baadhiya watendaji wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani kujiuzulu jambo ambalo linaashiria vikundi hivyo kuongozwa ama kutumika na makundi ya kisiasa, haiwezekani kutaka watendaji wa Serikali wajiuzulu wakati uchunguzi bado unafanyika na matokeo ya uchunguzi huo bado hayajatoka.
Jambo la kusikitisha Zaidi kuna baadhi ya vikundi vimejitangaza kwamba vinaungwa mkono na Maraisi wa Vyuo Vikuu jambo ambalo sio la kweli, Marais wote wa Vyuo Vikuu tuko hapa Dodoma tunaendelea na vikao vyetu vya kujadili changamoto zinazowakabili wanafunziwa Vyuo Vikuu.
Tunatoa wito kwa vikundi vyote vinavyojihusisha nakutumia mwamvuliwa Marais wa Vyuo Vikuu kama kinga yao ili kuu hadaa Umma kwamba wanaungwa Mkono, vikundi hivyo viache tabia hiyo vinginevyo tutawachukulia hatua za kinidhamu.
TAHLISO tunasubiri matokeo ya Uchunguzi unaofanyika juu ya kifo cha Akwilina na tunaimani wahusika wote watachukuliwa hatua kali zakisheria.
Tunawaomba wanafunzi wote tuendelee kuwa watulivu wakati tukisubiri matokeo hayo na kujiepusha na maandamano na vitendo vyovyote vitakavyo sababisha uvunjifu wa Amani nakuleta mgawanyo miongoni mwa wanafunzi.
Hata hivyo namna bora yakufikisha hoja nikutumia njia ya majadiliano kama wasomi badala ya kutumia nguvu ama maandamano kwakutofuata taratibu na madhara yake ni kusababisha vuruguzi sizotakiwa na hatimaye kuhatarisha usalama na hivyo kuathiri jamii kwaujumla wake.
Vurugu zozote zitokanazo kwakutozingatia taratibu zinaweza kudhorotesha shughuli za kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Uchumiwa Taifa letu.
Vile vile zinapoteza mvuto kwawawekezaji wanje na wandani, ikiwemo shughuli za utalii nchini ambazo zinachangia pato la Taifa letu.
Athari za Vurugu na kukosekana kwa amani zipo wazi natunaziona kwa nchi nyingine zikiwemo baadhi ya nchi jirani zetu ambao wamekua wakimbizi nchini kwetu kila siku.
Tunaona kuwa kama wanataaluma tunajukumu kubwa la kuelimisha jamii na kuwamfano bora wakutumia njia za majadiliano katika kujenga hoja zetu ilizitatuliwe kuliko kutumia njia ya maandamano au vurugu zisizo na ulazimawowote.
Taasisi hii ndio yenye dhamana ya kutetea nakusimamia maslahi ya wanafunzi wote wa vyuo na vyuovikuu Tanzania na si vinginevyo.
………………………………….
GEORGE ALBERT MNALI
MWENYEKITI
TAHLISO
LINDI:::: Waziri Mkuu: Msiuze Ufuta Wenu Mashambani Pelekeni Minadani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa ufuta katika mikoa inayolima zao hilo nchini kuuza kwa kutumia njia ya minada na si mashambani.
Ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Nachihungo, Narungombe na Chikwale.
Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi amesema ili wakulima waweze kupata tija ni vema wakauza ufuta wao kwa kupitia minada kama inavyofanyika katika zao la korosho
“Usikubali kumuuzia mtu yeyote ufuta wako ukiwa shambani kwa sababu bei atakayonunulia ni ndogo kulinganisha na soko, naamini ufuta wote ukiuzwa katika minada mtaona faida.”
Kufuatia agizo hilo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue aandae utaratibu wa maeneo ya kukusanyia ufuta na kufanyia minada.
Amesema ufuta unaolimwa nchini ni bora na unapendwa sana duniani hivyo wasiwe na wasiwasi. Baadhi ya Mikoa inayolima ufuta kwa wingi ni Lindi, Pwani, Dodoma, Manyara, Kigoma na Singida.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema vijiji vote visivyokuwa na umeme nchini vikiwemo vya wilaya ya Ruangwa vitaunganishiwa katika REA awamu ya tatu.
Amesema wananchi waendelee kuwa na subira kwa sababu tayari mkandarasi ameshaanza kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji vingine vya wilaya hiyo na atafika kwenye maeneo yao.
Alibainisha kuwa mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli ni kuhakikisha wananchi wote nchini waunganishiwa nishati ya umeme kwenye majumba yao, hivyo waendelee kuwa na subira na kushirikiana na Serikali yao.
Kuhusu suala la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama alisema, “Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo vijiji vyote vitapata maji”.
Pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kote nchini kutunza vyanzo vya maji ili kuliepusha taifa kugeuka jangwa pia miradi inayoletwa na Serikali iwe endelevu.
CHANZO: MPEKUZI BLOG













