RC TELACK AHAMASISHA WANANCHI KUTOA TAARIFA SAHIHI UTAFITI WA MAPATO NA MATUMIZI YA KAYA BINAFSI
Telack ametoa rai hiyo leo Ijumaa Februari 23,2018 katika mkutano na
waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga akizungumzia Utafiti wa Mapato na
Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/2018.
Utafiti huo unaosimamiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaoendelea
nchini katika kata 796 utazifikia kaya 9,552 nchini ambapo kaya 408 zitafikiwa
katika kata 34 za mkoa wa Shinyanga.
Telack alisema njia pekee ya kufuatilia utekelezaji wa program za
maendeleo ni kufanya tafiti mbalimbali kama huu unaoendelea ambao unalenga
kutoa takwimu za hali ya umaskini na takwimu nyingine ili kuisaidia serikali na
wadau kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutimiza malengo ya kitaifa.
“Suala la ukusanyaji wa takwimu rasmi za serikali ni shirikishi na ni
wajibu wa kila mwananchi kutoa taarifa sahihi,natoa wito kwa viongozi kuanzia
ngazi ya mitaa,vitongoji,vijiji,kata,wilaya na mkoa kutoa ushirikiano wa karibu
kwa watafiti watakaozifikia kaya 408 zilichaguliwa katika mkoa wetu”,alisema
Telack.
“Utafiti huu wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa mwaka
2017/2018 unahitaji sana ushirikiano kutoka kwa wananchi wote hasa katika kaya
zilizochaguliwa kitaalamu kuwakilisha sampuli za kaya zilizopo mkoani
Shinyanga”,aliongeza.
Alibainisha kuwa kila kaya iliyobahatika kuchaguliwa itahojiwa kwa siku
14 mfululizo na mdadisi atakutana na mkuu wa kaya ambaye hatatakiwa
kubadilishwa ili kupata takwimu sahihi kwa ajili kupanga maendeleo ya
nchi.
Mkuu huyo wa mkoa alisema utafiti huo utasaidia kuweka msingi katika
kutambua viashiria vya msingi vya kiuchumi,ajira na ustawi wa jamii ambavyo
vitatakiwa kufuatiliwa kwa kipindi husika na kupata makadirio ya jumla ya
mwenendo wa matumizi ya kaya ili kuandaa fahirisi za bei.
Telack alizitaja kata 34 za mkoa wa Shinyanga zitakazofanyiwa utafiti
kuwa ni Ngokolo,Mwawaza,Ndala,Ndembezi,Songwa,Mwadui
Lohumbo,Kishapu,Mwakipoya,Lagana,Talaga,Didia,Mwakitolyo,Iselamagazi,Mwamala,Nyida
na Lyabusalu.
Kata zingine zitakazofikiwa ni Lyamidati, Lunguya, Chela, ,Jana, Isaka,
Chambo, Igunda, Sabasabini, Bulungwa, Ushetu, Ubagwe, Mondo, Nyahanga, Zongomera,
Nyihogo,Majengo na Kilago.
Kwa upande wake Meneja wa Takwimu (NBS) wa mkoa wa Shinyanga,
Evarist Tairo alisema huo ni utafiti wa saba tangu nchi ipate Uhuru na utasaidia
kwa kiasi kikubwa kupata takwimu halisi za mapato na matumizi ya kaya binafsi.
DK. KIGWANGALLA AAGIZA MBINU MPYA ITUMIKE KUDHIBITI WANAOCHIMBA MADINI
Dk. Kigwangalla ametoa agizo
hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea
eneo la chanzo hicho na
kukuta uharibifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaodaiwa kuchimba madini ya dhahabu katika eneo hilo la hifadhi kinyume cha sheria “Nimeagiza
watu wa TFS wajenge kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo hili, na waweke walinzi wetu wa kudumu hapa badala ya kutegemea kufanya patrol (doria) na kuondoka, kwasababu eneo hili wananchi wanaamini lina madini ya dhahabu kwahivo kila siku wataendelea kuja kujaribu kuvuna dhahabu kutoka hapa.
kukuta uharibifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaodaiwa kuchimba madini ya dhahabu katika eneo hilo la hifadhi kinyume cha sheria “Nimeagiza
watu wa TFS wajenge kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo hili, na waweke walinzi wetu wa kudumu hapa badala ya kutegemea kufanya patrol (doria) na kuondoka, kwasababu eneo hili wananchi wanaamini lina madini ya dhahabu kwahivo kila siku wataendelea kuja kujaribu kuvuna dhahabu kutoka hapa.
“Kwasababu sisi kazi yetu ni
kuhifadhi Maliasili ambayo tumepata kama urithi wa nchi yetu, niwahakikishie kwamba
tutaimarisha ulinzi kwa kuanzisha kituo cha ulinzi hapa ili askari wawe
wanabadilishana na kudhibiti kabisa uharibu ambao umekuwa ukifanyika, kwasababu maji
yanayotoka katika chanzo hiki yanakwenda kunywesha Muheza yenyewe na wilaya
wa Tanga, tukiharibu hapa yatakosekana maji safi na salama” alisema Dk.
Kigwangalla.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
wa Wakala huyo, Prof. Dos Santos Silayo alisema pamoja na eneo hilo kwa
sasa kuwa linalindwa na askari wa Suma JKT watahakikisha ulinzi
unakuwepo muda wote kwa kutekeleza agizo hilo la Waziri la kujenga kituo cha ulinzi
cha kudumu ili askari wawepo katika eneo hilo muda wote.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba
wananchi hawaingii ili tusiwe tunawashtukiza kuwakamata na kwachukulia
hatua, lazima tuwe watu wa kuzuia uhalifu usitokee, nia yetu ni kuwa na kituo
mara moja kama alivyoelekeza Mhe. Waziri na hili jambo tumelichukua kama
maelekezo na tutalitekeleza kwa nguvu kabisa,” alisema Prof. Dos Santos
Silayo.
Awali Dk. Kigwangalla
alitembelea kikundi cha wafugaji wa vipepeo katika Tarafa ya Amani ambao waliiomba
Serikali ifungulie vibali vya kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi, aliahidi
kuyafanyia kazi maombi yao huku akiwataka kutumia fursa ya ufugaji huo kama bidhaa ya
utalii kuwavutia watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani.
Akiwa mkoani Tanga alitembelea pia
Kituo cha Mambo ya Kale cha Mapango ya Amboni na kusema Wizara yake
itaboresha kituo hicho pamoja na vituo vingine vya Mambo ya Kale ili kupanua wigo wa vivutio
vya utalii nchini viweze kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.
Katika ziara hiyo ya siku moja
mkoani Tanga alitembelea pia shamba la miti ya Mitiki Longuza, Makumbusho ya
Shaban Robert na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Dodoma Yatekeleza kwa Vitendo Dhana Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda
Akizungumza
katika Kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt.
Binilith Mahenge amesema kuwa Mkoa huo umejipanga vyema kama Makao
Makuu ya Nchi kuhakikisha kuwa dhana ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda inatekelezwa
na wananchi wote kwa vitendo .
Akifafanua
zaidi Dkt. Mahenge amesema kuwa Dodoma ni mahali salama na kuna maeneo
yakutosha kwa ajili ya uwekezaji hivyo wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi
wanakaribishwa kuja kuwekeza.
“Dodoma
tayari tumeanza kutekeleza miradi inayochochea maendeleo ya uchumi wa viwanda
na tunaamini kuwa Dodoma itakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kiunganishi
cha mikoa yote nchini” Alisisitiza Dkt. Mahenge
Aliongeza
kuwa ni vyema Vijana wanaoishi Mkoani Dodoma wakajiunga katika kwenye
Vikundi ili wapatiwe ujuzi utakaowawezesha kujikwamua kiuchumi ikiwemo
kuanzisha viwanda vidogo na shughuli za uzalishaji kwa ujumla.
Pia
aliwaasa wanaotaka kujenga Mkoani Dodoma kuzingatia Mpango Mji
(Master Plan) kwa kuwa Serikali imeshapanga na
itasimiamia mpango mji uliopo kwa faida
ya wananchi wote.
Akitolea
mfano suala la kumiliki Ardhi Mkoani Dodoma Dkt. Mahenge alisema kuwa ni muhimu
kupitia Manispaa ili kuepuka utapeli na usumbufu unaoweza kujitokeza baadae
ikiwa taratibu hazitafuatwa katika kumiliki Ardhi.
Katika
kuhakikisha kuwa Makao Makuu ya nchi yanakuwa katika mpangilio unaovutia tayari
Serikali imepima viwanja kwa ajili ya kujenga majengo ya Ofisi za Wizara ,
Taasisi na Balozi zote katika eneo maalum utakapojengwa mji wa Serikali.
Kipindi
cha TUNATEKELEZA kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na
kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO ambapo awamu hii inawashirikisha wakuu wa
Mikoa yote, baada ya awamu iliyotangulia kuwahusisha Mawaziri wote
na watendaji wengine wa Serikali.
UJUMBE WA RAIS WA POLAND WATUMA SALAMU ZA RAIS MAFUGULI KWA WAZIRI HARRISON MWAKYEMBE
Hayo
yamesemwa leo Ijumaa (Februari 23, 2018) Jijini Dar es Salaam na Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe wakati alipokuwa
Salamu za Rais wa Poland kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli.
Dkt.
Mwakyembe alisema hatua zote muhimu za ufunguzi wa Ubalozi huo, taratibu zote
muhimu kwa ajili ya ufunguzi Ofisi za Ubalozi huo tayari zimekamilika na
kuongeza kuwa kufunguliwa kwa ubalozi kutazidi kudumisha ushirikiano na urafiki
wa muda mrefu baina ya Tanzania na Poland pamoja na kuimarisha diplomasia ya
uchumi baina ya mataifa hayo.
“Serikali
ya Jamhuri ya Poland imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania, ambapo
matunda ya ushirikiano ni kwa Serikali yetu kupata wa mkopo wa masharti nafuu
uliofanikisha uanzishaji wa kiwanda kikubwa cha matrekta kibaha Mkoani Pwani”
alisema Dkt. Mwakyekmbe.
Kwa
upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Poland Krzysztof Szczerski
alisema ziara yake ya kuja nchini ni kuwasilisha salamu za Rais wa
Jamhuri ya Poland ambapo pamoja na mambo mengine Serikali ya nchi hiyo
imekusudia kuimarisha mahusiano yake ya kiuchumi na Tanzania.
Aliongeza
kuwaa katika kuendeleza jitihada zake za kuimarisha uhusiano wake na Tanzania,
Serikali ya Poland tayari inaendesha miradi mbalimbali ya uwekezaji nchini
ambapo Rais wa Poland ameahidi kuimarisha ushirikiano huo baina yake na Rais wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
“Niwewasilisha
salamu za Rais wa Jamhuri ya Poland ambapo pamoja na mambo mengine, amemualika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda nchini Poland kwa ajili ya ziara
maalum ya kiserikali” alisema Szczerski.
Makamu wa Rais Autaka Mkoa wa Simiyu Kuendeleza Mpango wa EQUIP-Tanzania
Makamu
wa Rais ametoa agizo hilo leo Mkoani Simiyu alipokuwa akiongea na viongozi na
watumishi wa Serikali wa Mkoa huo katika kikao cha majumuisho ya ziara
yake ya siku tano mkoani humo.
“Mpango
huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa Mkoa wa Simiyu, kutokana na kuongezeka kwa
kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya darasa la Saba
ambapo Mkoa umetoka kushika nafasi za mwisho Kitaifa hadi kufikia nafasi ya 11
mwaka 2017.
Amesema
mafanikio ya mpango huo yamekuwa makubwa, huku akishukuru shirika la DFID kwa
mchango wao mkubwa ikiwa ni pamoja na kutoa kiasi cha fedha shilingi Bilioni
1.3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule.
Aidha,
Mhe. Samia ameutaka uongozi wa mkoa huo kuhakikisha Mpango huo unaendelezwa
hata baada ya wafadhili hao kumaliza muda wao ili kuhakikisha kiwango cha elimu
kinaendelea kuboreka kila mwaka.
Mhe.
Samia amemuhakikishia Kiongozi Mkuu DFID-Tanzania Bibi Elizabert Arthy
kuwa nchi ya Uingereza itaendelea kufanya kazi na Serikali katika kuboresha
elimu nchini.
Kwa
upande wake, Elizabeth Arthy amesema katika kuhakikisha wanapambana na hali ya
kuboresha elimu nchini tayari Mkoa wa Simiyu umepewa fedha kutoka DFID kiasi
cha shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameishukuru DFID kwa ufadhili wake kupitia
EQUIP-Tanzania ambapo ufaulu wa wanafunzi umeongezeka mkoani humo kutoka
asilimia 36 mwaka 2013 mpaka 68 mwaka 2017.
Katika
kipindi cha miaka Minne DFID imewekeza katika mpango wa kuinua ubora wa elimu
mkoani Simiyu kwa kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.
NAIBU WAZIRI WA MADINI AAGIZA KUTOLEWA MIKATABA YA WAFANYAKAZI MIGODINI
Mhe Biteko ametoa
agizo hilo Leo 23 Februari 2018 wakati alipotembelea eneo la uchimbaji wa makaa
ya mawe katika Kijiji na Kata ya Magamba, Wilayani Mbozi linalomilikiwa na
kampuni ya Magamba Coal Mine.
Alisema amejiridhisha
kuwa wafanyakazi wengi katika migodi mbalimbali nchini ukiwemo wa Magamba
hawana mikataba jambo ambalo linafifihisha uhakika wa ajira zao.
Aidha, Naibu Waziri
huyo wa Madini ametoa siku 14 kuanzia Leo 23 Februari 2018 mpaka 9 Machi 2018
kwa kampuni ya Magamba Coal Mine kuwa wamekamilisha taarifa ya utekelezaji wa
maelekekezo ya ukaguzi wa migodi yaliyotolewa kwao na Ofisi ya Madini kanda
hiyo.
Alisema kuwa endapo
watashindwa kufanya hivyo ni wazi kuwa watakuwa wamekiuka masharti ya leseni
zao na wajibu wao kwa jamii inayowazunguka na hivyo Wizara itawachukulia hatua
bila kuchelewa.
Sambamba na hayo pia
kampuni hiyo imetakiwa kuboresha na kuwa na mahusiano chanya na kijiji cha
Magamba na serikali kwa ujumla ikiwemo kusaidia kuboresha baadhi ya maeneo
ikiwemo sekta ya afya na elimu.
Naibu Waziri wa
Madini akiwa katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Songwe alisema kuwa serikali
imekusudia kurejesha uchumi fungamanishi kwa wananchi hivyo kampuni haziwezi
kuwa na uchumi imara kama zitasalia kuendesha migodi pasina utaratibu wa
kisheria.
LIGI KUU YA WANAWAKE YA SERENGETI PREMIUM LITE KUZINDULIWA RASMI NA WAZIRI MWAKYEMBE JUMAPILI
Mchezo
utakaotumiwa kuzindua ligi hiyo utazikutanisha timu za Kigoma Sisterz ya Kigoma
dhidi ya Simba ya Dar es Salaam.
Aidha
uzinduzi utaenda sanjari na mpango maalumu wa FIFA wa kuhamasisha soka la
Wanawake uliopewa jina la Live Your Goal ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dr.Harrison Mwakyembe.
Mbali
na mechi ya uzinduzi mechi nyingine za ligi hiyo ya Wanawake ya Serengeti
Premium Lite zinatarajia kuchezwa kesho kwenye viwanja tofauti.
Uwanja
wa Samora Panama FC watacheza dhidi ya Evergreen Queens ya Dar es Salaam saa 10
jioni,huko Mbweni JKT Queens watacheza dhidi ya Alliance saa 10 jioni,mabingwa
watetezi Mlandizi Queens wanasafiri mpaka Jamhuri Dodoma kucheza na Baobab
Queens.
Wakati
huohuo Kozi ya makocha wa kozi ya grassroots kwa watoto wenye umri wa miaka
6-12 Wasichana na Wavulana imeanza Jumatano kwenye Uwanja wa Lake
Tanganyika,Ujiji,Kigoma.
Waziri wa Elimu Aaahidi kumsomesha mdogo wake Akwilina
Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako ameahidi kumsomesha mdogo wake Akwilina Akwilini, Angela Akwilini ambaye kwa sasa anasoma kidato cha tatu.
Akizungumza leo Februari 23, 2018 baada ya mazishi ya Akwilina aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, 2018 eneo la Mkwajuni jijini Dar es Salaam, Profesa Ndalichako amesema atamsomesha Angela hadi Chuo Kikuu.
CHADEMA Wamjibu Msajilii wa Vyama vya Siasa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejibu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi inayowataka ndani ya siku tano kuwasilisha maelezo ya tuhuma za uvunjifu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na ya maadili ya vyama vya siasa kwa kufanya maandamano Februari 16, 2018.
Katika majibu yake, Chadema wamejibu hoja mbalimbali za msajili na kuhoji hatua alizochukua mpaka sasa kufuatia mfululizo wa matukio ya mauaji ya viongozi wa chama hicho.
Akizungumza leo Februari 23, 2018 na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho-Bara, John Mnyika amesema msajili kwenye barua yake anakituhumu Chadema kwa kukiuka kifungu cha 9(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Mnyika amefafanua kwamba kifungu hicho hakihusu vyama vyenye usajili wa kudumu bali vyama vya siasa vyenye usajili wa muda mfupi ambavyo vinaahidi kwamba vikipata usajili wa kudumu vitadumisha amani katika shughuli zao.
Mnyika amekosoa pia barua ya msajili ambaye anahoji ushiriki wa Chadema kwenye uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Ubungo wakati uchaguzi huo ulifanyika katika jimbo la Kinondoni, kuongeza kuwa hiyo inaonyesha kwamba msajili amekosa umakini katika majukumu yake.
"Tunaelewa kwamba msajili anasukumwa na Serikali. Dhamira yao ni kukifuta Chadema. Nawaambia tu jambo hilo hawaliwezi," amesema.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Kibamba amesema msajili amebainisha kwenye barua yake kwamba wamekiuka kanuni ya 6(1)(b) ya maadili ya vyama vya siasa ambayo inampa mamlaka ya kupokea malalamiko na kuzisikiliza pande mbili.
Akijibu jambo hilo Mnyika amesema msajili hajabainisha mlalamikaji ni nani katika malalamiko aliyoyapokea.
Chama hicho pia kimelaani mauaji ya diwani wake Kata ya Namala, Godfrey Luena na kutaka Polisi kufanya uchunguzi wa haraka na kumchukulia hatua za kisheria kila anayehusika.
"Katika Taifa letu kwa sasa, kuna vikundi vya watekaji, vikundi vya wauaji na vikundi vya watesaji. Ni wakati wa kujilinda kwa sababu kuna mashambulizi mengi sana," amesema Mnyika.
Walichoongea Rais Magufuli na Kenyatta Baada ya Kukutana Leo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wamewaagiza Mawaziri wa Tanzania na Kenya kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza katika biashara kati ya nchi hizi mbili.
Marais hao wametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 23 Februari, 2018 walipokutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Munyonyo mjini Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta wamesema wanataka kuona biashara kati ya Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.
“Kuna mambo madogomadogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogomadogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa” amesema Mhe. Rais Magufuli na kuungwa mkono na Mhe. Rais Kenyatta.
Wametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Mhe. Peter Munya.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit katika hoteli ya Munyonyo Mjini Kampala.
Baada ya Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki inaguswa na hali ya Sudani kusini na ametoa wito kwa pande zinazopingana kumaliza tofauti zao ili wananchi wa Sudani Kusini wajikite kujenga nchi yao.
“Nimemhakikishia Mhe. Rais Salva Kiir kuwa Tanzania ipo pamoja na Sudani Kusini na tunapenda tofauti zinazosababisha matatizo nchini mwake ziishe, sisi Tanzania tupo tayari kufanya biashara na Sudani Kusini, hata chakula kama wanahitaji tutawauzia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Salva Kiir Mayardit amesema Tanzania na Sudani Kusini zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba japo kuna vita nchini mwake Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaendelezwa na kukuzwa zaidi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Gaston Sindimwo.
Mhe. Gaston Sindimwo amemfikishia ujumbe wa Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza kuwa hali ya Burundi ni shwari na Mhe. Rais Magufuli amesema anafurahi kuona sasa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wamepata hifadhi Tanzania wameanza kurudi nchi kwao.
Mhe. Rais Magufuli pia amefanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni mratibu wa mazungumzo ya amani ya mgogoro wa Burundi aliyealikwa kuhudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hapa Kampala.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
23 Februari, 2018










