• VIPINDI VYA ELIMU HASA KILIMO

    Tuna vipindi mbalimbali vinavyohamasisha jamii katika kilimo cha Korosho, ufuta na Mhogo. tunaendelea na jamii inafurahia uwepo wa vipindi kwa sababu wanakutana na wataalamu moja kwa moja

  • SAUTI ZA WANAJAMII HUSIKIKA

    Sauti ni muhimu hasa unapohudumia jamii ya vijijini, wasikilizaji hupenda kusikia sauti zao kwakua watu wao wanawafahamu, hivyo huwa kivutio kwako na ni rahisi jamii kuamini kuwa mpo pamoja nao

  • MICHEZO MBALIMBALI

    Afya ni sehemu ya vipindi vyetu kwenye radio, hii husaidia kuwapa fursa watu wanaopenda michezo kuwa pamoja na kubadirishana mawazo, michezo hujenga urafiki na undugu baina mwa jamii

  • WATOTO KATIKA RADIO

    Hupenda kushiriki na hujiona sehemu ya radio kwa kuwa huishi katika jamii, kipindi cha watoto kimekuwa kikifuatiliwa na watu wazima kwasababu kuu moja tu, watoto waishio vijijini huwa hawapewi kipaumbele kama tulivyofanya Jamii fm

  • SIKIKA KATIKA RADIO

    Kipengere hiki hutoa fursa kwa wanajamii wanaotuzunguka kuongea moja kwa moja na kueleza hoja zao ambazo baadae hufuatiliwa kwa undani

Waziri Ndejembi ataka mradi wa Gesi Ntorya ukamilike kwa wakati

 

Picha na Mchoro wa mradi wa uchimbaji na ujenzi wa bomba la Gesi asilia kutoka Ntorya kuelekea Bomba kuu la Madimba (Picha na Musa Mtepa)

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi wa bomba la gesi Ntorya–Madimba ifikapo Septemba 2026

Na Musa Mtepa

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa uchimbaji na ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Ntorya kwenda Madimba mkoani Mtwara kukamilisha mradi huo kwa wakati, ili kuendana na mahitaji ya Watanzania.

Rai hiyo ameitoa Februari 27, 2026, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa uchimbaji na usambazaji wa bomba la gesi asilia uliofanyika katika eneo la Ntorya, lililopo kijiji cha Namahyakati Barabarani, kata ya Nanguruwe, mkoani Mtwara.

Ndejembi amesema lengo la wizara ni kuhakikisha kuwa ifikapo Septemba 2026, visima hivyo vinaanza kuzalisha gesi na kuungwa katika bomba kuu la Madimba. Amesisitiza kuwa mkandarasi hana budi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

Sauti ya Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Aidha, Ndejembi amesema ili kufanikisha hilo kunahitajika usimamizi wa hali ya juu kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kuwepo eneo la mradi muda wote, ili wakati utakapofika mradi huo uweze kuanza kama ilivyopangwa.

Sauti ya 2 Deogratius Ndejembi, Waziri wa Nishati

Akizungumzia hali ya utekelezaji wa mradi huo, Mjiolojia Mwandamizi ambaye pia ni Meneja wa Mradi wa Ntorya kwa upande wa mkondo wa juu, Patrick Kabwe, amesema utekelezaji ulianza mwaka 2005 baada ya kusainiwa kwa mkataba kati ya TPDC, Ndovu Resources ya Uingereza pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa wakati huo.

Amesema mwaka 2010 walichimba kisima cha Ntorya namba moja na kufanikiwa kugundua gesi ambayo sasa inatarajiwa kuchimbwa na kuungwa katika bomba kuu la Madimba.

Sauti ya Patrick Kabwe, Meneja wa Mradi wa Ntorya

Akimkaribisha Waziri wa Nishati, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. James Mataragio, amesema kitalu cha gesi cha Ntorya ni kitalu kipya kitakachoongeza upatikanaji wa gesi, huku mahitaji yake yakiendelea kuongezeka siku hadi siku kutoka kwa wananchi.

Ameongeza kuwa Wizara ya Nishati kupitia TPDC imejipanga kuhakikisha inachimba na kuzalisha gesi ya kutosha kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kukidhi mahitaji ya viwanda na matumizi ya wananchi.

Sauti ya Dkt. James Mataragio, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati

Kukamilika kwa visima vitatu vya gesi vinavyochimbwa katika eneo la Ntorya — Ntorya namba moja, Ntorya namba mbili na Ntorya namba tatu — kunatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa takribani futi za ujazo milioni 60 kwa siku katika uzalishaji wa gesi nchini.

Baada ya uzinduzi huo, Waziri wa Nishati alitembelea eneo la Mnazi Bay, ambapo kuna uchimbaji wa kisima kipya ambacho kikikamilika kitaongeza takribani futi za ujazo milioni 45 za gesi asilia kwa siku. Kwa sasa, uzalishaji wa gesi kutoka Mnazi Bay ni takribani futi za ujazo milioni ni 90 – 100 za gesi asilia kwa siku (Million Standard Cubic Feet per Day) MMscf/d).

Share:

Soko la Embe nje ya nchi kufikia Dola Bilioni 75

 

Mwonekano wa Embe mbichi zikiwa zimedondoshwa mtini (Picha kwa msaada wa mtandao)

Mkurugenzi wa AGCOT na wizara ya kilimo wametaka wadau kukuza zao la embe, kuongeza tija, kuuza nje, na kuwapatia wakulima zana za kisasa ili kuongeza mapato na maendeleo ya kilimo

Na Musa Mtepa

Mkurugenzi Mkuu wa AGCOT, Geoffrey Kirenga, amewahimiza wadau wa kilimo kuendeleza na kuinua zao la embe katika soko la ndani na la kimataifa ili kuongeza kipato cha wakulima na kupunguza utegemezi wa zao la korosho pekee.

Akizungumza  Februari 18, 2026, baada ya Warsha ya Wadau wa Kilimo iliyolenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo kwa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara, iliyofanyika mjini Mtwara, Kirenga amesema kuna fursa kubwa katika uzalishaji wa embe kwa kuongeza thamani na kuuza nje ya nchi, hatua itakayoongeza mapato ya fedha za kigeni kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Sauti ya Geoffrey Kirenga, Mkurugenzi Mkuu wa AGCOT.

Kirenga ameeleza kuwa endapo zao la embe nchini litaendelezwa ipasavyo, soko lake Duniani linaweza kufikia zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 75 kwa mwaka, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 187.5 za Tanzania, kiasi kinachokadiriwa kuwa takribani mara tatu ya mapato yanayotokana na zao la korosho.

Sauti ya Geoffrey Kirenga, Mkurugenzi Mkuu wa AGCOT.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo katika Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Elizabeth Misokia, amesema shoroba za kilimo zimeanzishwa kwa lengo la kuweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta ya kilimo kupitia ongezeko la uzalishaji, ajira na mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wakulima ili waweze kunufaika kibiashara.

Sauti ya Bi. Elizabeth Misokia, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo

Aidha, Misokia amesema licha ya mipango thabiti inayotekelezwa na Serikali, bado wakulima wengi wanatumia zana duni kama majembe ya mkono. Hivyo, Serikali imejipanga kuwapatia wakulima zana za kisasa zikiwemo matrekta, elimu ya kilimo bora pamoja na mbegu bora ili kuongeza tija katika uzalishaji.

Sauti ya Bi. Elizabeth Misokia, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo

Akizungumzia changamoto ya kilimo kinachotegemea mvua, Misokia amesema Serikali inapanga kuboresha na kuongeza mabwawa ya maji, kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za maji, pamoja na kushirikiana na sekta binafsi ili kuwawezesha wakulima kuendesha kilimo cha kisasa chenye miundombinu rafiki kwa uzalishaji wa mwaka mzima.

Sauti ya Bi. Elizabeth Misokia, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo
Share:

SIDO Mtwara yawataka wajasiriamali kukuza biashara kidijitali

 

Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdalla Mwaipaya akizungumza wakati ya mafunzo ya uingezaji thamani uliofanyika february 24,2026 mjini Mtwara(Picha na Gregory Milanzi)

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewahimiza wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa na kutumia teknolojia, ikiwemo akili mnemba, kukuza biashara zao. Mafunzo hayo yaliandaliwa na SIDO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwawezesha kibiashara

Na Gregory Millanzi

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewataka wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuongeza kipato, pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kujitangaza na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Mwaipaya ameyasema hayo Februari 24, 2026, wakati akifungua semina ya utambuzi wa bidhaa, viwanda na matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence), iliyofanyika katika Ukumbi wa Benjamini Mkapa, Chuo Kikuu cha MUST Mtwara (zamani Chuo cha Ualimu TTC Kawaida).

Sauti ya Abdallah Mwaipaya – Mkuu wa Wilaya ya Mtwara

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mtwara, Merina Mkuchu, amesema lengo la semina hiyo ni kuwatambua wajasiriamali wa Manispaa ya Mtwara na kuwapatia elimu ya kufanya biashara kidijitali badala ya kufanya biashara kwa mazoea.

Mkuchu ameongeza kuwa kwa sasa wanaandaa kanzidata ya kuwatambua wajasiriamali hao ili kuwaunganisha na wadau mbalimbali wanaofika Mtwara kutafuta washirika wa biashara. Pia, SIDO inaandaa kongani la viwanda katika kila wilaya kwa lengo la kuwaunganisha wajasiriamali na kukuza ushirikiano miongoni mwao.

Sauti ya Merina Mkuchu – Meneja SIDO Mkoa wa Mtwara

Naye Afisa Uhusiano kwa Umma kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Feisal Abdul, amewahimiza wajasiriamali kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Uendelezaji Ubunifu (Samia Fund), unaolenga kuwajengea uwezo na kuwapatia ruzuku za kuendeleza bunifu zao.

Sauti ya Feisal Abdul – Afisa Uhusiano COSTECH

Aidha, kampuni ya Scan Code imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wa Mtwara kuhusu matumizi ya Scan Code na akili mnemba katika kujitangaza na kupanua masoko ya biashara zao.

Abdulwahid Khamis, mkufunzi kutoka Scan Code, ameeleza faida za teknolojia hiyo na namna inavyoweza kuwasaidia wajasiriamali kuongeza wigo wa soko na mapato.

Sauti ya Abdulwahid Khamis – Mtaalamu wa Mafunzo kutoka Scan Code
Share:

Vijana Mtwara wahimizwa maadili kulinda amani nchini

 

Vijana wa Skauti wakiwa katika maandamano ya kuadhimisha siku ya Skauti Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Vijana wamehimizwa kutumia mitandao kwa maadili na kulinda amani wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani yaliyofanyika Mtwara , yakikumbuka miaka 160 ya Robert Stephenson Baden-Powell

Na Musa Mtepa

Vijana wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia maadili, tamaduni na mila za Kitanzania, na kuitumia kwa manufaa yao binafsi pamoja na taifa kwa ujumla. Pia wametakiwa kuachana na maudhui yanayoharibu maadili, utu, tunu za taifa, pamoja na yale yanayochochea uvunjifu wa amani.

Nasaha hizo zimetolewa leo Februari 22, 2026 na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara , ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Bi. Telack amewataka vijana kutumia teknolojia kwa hekima na busara, pamoja na kupambanua maudhui yanayopatikana kwenye mitandao ya kijamii, na kuachana na yale yote yanayoharibu imani za dini, maadili na tamaduni za Kitanzania.

Sauti ya Bi. Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Lindi

Aidha, Bi. Telack ameendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kuipenda na kuilinda amani iliyopo nchini kwa kuwa na uzalendo wa kweli kwa Tanzania. Alisema hakuna nchi nyingine kwao zaidi ya Tanzania, hivyo ni wajibu wa kila kijana kuhakikisha anailinda na kuipambania nchi yake.

Sauti ya Bi. Zainab Telack, Mkuu wa Mkoa wa Lindi

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Sarah Vanessa, mwakilishi wa Skauti Mkoa wa Mtwara, amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia Skauti bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo ufinyu wa bajeti ya kusaidia vijana wa skauti kutekeleza miradi ya uzalishaji mali, pamoja na ukosefu wa vifaa vya uokoaji kwa timu za maafa katika wilaya na mikoa.

Sauti ya Sarah Vanessa, Mwakilishi wa Skauti Mkoa wa Mtwara

Akitoa salamu kwa niaba ya Bodi ya Skauti Tanzania, mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ndugu Lazaro Mkeni, amesema wizara itaendelea kusimama pamoja na Chama cha Skauti Tanzania kuhakikisha misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho inalindwa na kuimarishwa. Ameongeza kuwa wizara ipo tayari kutoa msaada pale inapobidi ili kuhakikisha misingi hiyo inasimamiwa ipasavyo.

Sauti ya Lazaro Mkeni, Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Komredi Ibrahim Mjanaheri Ibrahim, amewapongeza waandaaji wa maadhimisho hayo,huku akitoa rai kwa vijana kuendelea kudumisha amani na kuachana na mtu yeyote anayetaka kuivuruga amani ya nchi.

Sauti ya Ibrahim Mjanaheri Ibrahim, Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara

Maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani Kitaifa kwa mwaka 2026 yamefanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Elimu Bunifu na Stadi za Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu ya Vijana.”

Maadhimisho hayo ni kumbukizi ya miaka 160 tangu kuzaliwa kwa mwanzilishi wa Skauti Duniani, Robert Stephenson Baden-Powell, mzaliwa wa Uingereza, aliyezaliwa Februari 22, 1857. Alianzisha Skauti mwaka 1907 na baadaye mwaka 1908 akaandika kitabu maarufu kiitwacho Scouting for Boys.

Baden-Powell alianza kwa kufanya kambi ya majaribio mwaka 1907 katika Kisiwa cha Brownsea, Uingereza, ambapo alitoa mafunzo kwa vijana yenye lengo la kuwafundisha uongozi, kujitegemea, uzalendo na huduma kwa jamii. Harakati hizo zilisambaa duniani kote, kama ambavyo leo zimeadhimishwa mkoani Mtwara na Tanzania kwa ujumla.

Share:

AGCOT yataka mageuzi ya kilimo mikoa ya Kusini

 

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi Zainab Telack akizungumza na wadau wa kilimo katika mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara (picha na Musa Mtepa)

“Kama tunaweza uzalisha zaidi ya bilioni 260 kwa zao moja, tunashindwa nini kutegemewa”

Na Musa Mtepa

Wadau wa kilimo wametakiwa kushirikiana kwa umoja katika kumsaidia mkulima kuzalisha kilimo chenye tija kwa kuwawezesha kulima kwa njia za kisasa, ikiwemo kuwapatia vitendea kazi bora vya kilimo.

Hayo yamesemwa Februari 20, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, wakati akifungua Warsha ya Wadau wa Kilimo ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo kwa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara, iliyofanyika mjini Mtwara.

Bi. Telack amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika zao la korosho, ambapo wakulima wamezalisha zaidi ya shilingi bilioni 260, yanaonesha kuwa inawezekana pia kuongeza uzalishaji wa mazao mengine endapo wakulima watawezeshwa kulima kisasa. Amesisitiza matumizi ya matrekta na zana bora za kilimo ili kuwawezesha wakulima kulima mashamba makubwa zaidi na kuongeza tija.

Sauti ya Bi Zainab Telack mkuu wa mkoa wa Lindi

Aidha, amewataka wakuu wa wilaya, wakuu wa idara za kilimo na sekta binafsi kutumia warsha hiyo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati imara ya utekelezaji wa mageuzi ya sekta ya kilimo kwa mikoa ya kusini na taifa kwa ujumla.

Sauti ya Bi Zainab Telack mkuu wa mkoa wa Lindi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa utaratibu wa Shoroba Tanzania (AGCOT), Geoffrey Kirenga, amesema lengo la warsha hiyo ni kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma pamoja na kuongeza ukaribu baina yao ili kukuza sekta ya kilimo.

Sauti ya Geoffrey Kirenga mkurugenzi wa AGCOT

Kirenga ameongeza kuwa katika warsha hiyo ameguswa na hoja zilizotolewa na sekta binafsi pamoja na viongozi wa halmashauri kwamba mwaka 2026 huenda malengo ya uzalishaji yasifikiwe kama ilivyotarajiwa kutokana na uhaba wa mbegu bora za ufuta. Amesema hali hiyo inaashiria kuongezeka kwa idadi ya wakulima wa zao hilo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Sauti ya Geoffrey Kirenga mkurugenzi wa AGCOT

Kwa upande wao, Mkuu wa Idara ya Kilimo Halmashauri ya Masasi, James Chitumbi, pamoja na Mkuu wa Idara ya Kilimo Halmashauri ya Nachingwea, Rafael Magetu, wamesema warsha hiyo imewapa manufaa makubwa, ikiwemo namna ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mbegu bora za mazao ya chakula na biashara kwa kuongeza juhudi za uzalishaji ili kufikia kilimo chenye tija.

Wakuu wa Idara ya Kilimo halmashauri ya Nachingwea na Masasi

Akifunga warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brig Jenerali ,Ahmed Abbas, ametoa wito kwa wakuu wa wilaya kwenda kujifunza mbinu za kilimo-biashara zinazotekelezwa mkoani Lindi ili kukuza kilimo mseto na biashara katika Mkoa wa Ruvuma.

Sauti ya Brig Ahmed Abbasi mkuu wa mkoa wa Ruvuma

Warsha hiyo ya siku moja imewakutanisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakuu wa idara za kilimo, sekta binafsi pamoja na wadau wa kilimo kutoka mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara. Lengo kuu lilikuwa kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo katika mikoa hiyo.

Share:

Sikiliza jamii FM Radio

🎧 Jamii FM Live

IDADI YA WASOMAJI

HABARI ZA HIVI PUNDE

Blog Archive

WAENDESHA WEBSITE

Contact Form



1 ] )[0]; $title = $recent_post['post_title']; $excerpt = wp_trim_words( $recent_post['post_content'], 20 ); $image = get_the_post_thumbnail_url( $recent_post['ID'], 'full' ); ?>